Ilipoishia Nzena (Kijiji Kilicholaaniwa) sehemu ya nne
Wakiwa wanaendelea kujibizana, walianza kusikia sauti ya Bi. Lugumi ikisema
“Kufaaaaa‼ kufaaaa‼” kila aliyeisikia sauti hii alianza kutetemeka huku damu nzito ikimtoka puani kisha walikufa papo hapo, hali ya taharuki iliingia na kufanya kila mmoja atawanyike anakokujua yeye mwenyewe. Sauti ya Bibi Lugumi ilizidi kusambaa, ilikua ni sauti ya kunong’ona iliyotoka kwa kuivuta sana.
SEHEMU YA TANO
Kelele za Wanakijiji ziliwashtua Mzee Miroshi na Zahoro wakiwa wamefungiwa ndani ya chumba kimoja nyumbani kwa Mzee Kova, Zahoro akamwambia Baba yake
“Ni lazima tujiokoe kutoka hapa Baba” alisema kisha alitafuta kitu kitakachomsaidia kuuvunja ule Mlango, macho yake makubwa yalikiona kipanda cha mbao kilichokua kimeegemezwa ukutani, akakichukua. Kilikua ni kipande kilichotokana na fanicha za
zamani, haraka akasogea mlangoni huku akimtazama Baba yake Mzee Miroshi ambaye tayari alikua ameshaishiwa nguvu huku akitoa hewa nzito
“Baba usijali tutatoka salama Hapa” alisema Zahoro, kisha alimsogeza kando Baba yake ili atakapouvunja mlango Baba yake asiathirwe na vipande vitakavyoruka. Akavuta nguvu kisha akaukita mlango kwa kutumia kipande cha mbao, mlango ukatikisika
Kelele zilizoendelea kusikika huko nje zilimpa nguvu Zahoro ya kuendelea kuuvunja Mlango ili waondoke kifungoni. Hapakua na Mlinzi hapo nje kwasababu taharuki ilikuwa imewasomba wote na kuiacha nyumba hiyo yenyewe.
Zahoro aliendelea kugonga mlango kwa nguvu zaidi, kila pigo liliufanya mlango kudhoofika. Jasho lilimtoka huku mikono yake ikianza kuuma, lakini hakuacha. Alijua kuwa muda ulikuwa hauko upande wao. Baada ya mapigo kadhaa, mlango ulianza kulegea na hatimaye kupasuka vipande vipande. Haraka akamshika baba yake mkono na kumsaidia kusimama.
“Twende Baba, hatuna muda!” alisema kwa sauti ya dharura. Zahoro alimsaidia Baba yake kutoka ndani ya chumba kisha wote walisimama huku macho yao yakijawa na Mshangao. Moshi mkubwa ulikua ukifuka Kijijini, Mlinzi mmoja wa kijiji ambaye aliachwa kwa ajili ya kuwalinda walimkuta akiwa amelala chini huku Damu nzito ikimtoka puani na Mdomoni.
Mzee Miroshi aligeuza shingo yake kwa uchovu akimtazama Zahoro ambaye aliguswa na Mtazamo wa Baba yake, macho yao yalipokutana kila mmoja alisubiria kusikia kutoka kwa mwenzake. Ghafla sauti ya muito wa simu ilisikika kutoka kwenye mfuko wa suruali wa Zahoro.
Mzee Miroshi alikaza macho ya Mshangao, hakuwahi kumwona Zahoro akiwa na simu hata siku moja. Zahoro alipepesa macho taratibu kumwonesha Baba yake kua alikua akiitumia simu hiyo kisiri, haraka aliitoa kutoka mfuko wa siri maarufu kama ‘Docho’
Ilikuwa ni simu ndogo sana. Mzee Miroshi akampa ishara Zahoro aipokee haraka – pengine wangepata msaada wa kutoka hapo kijijini. Zahoro aliweka simu sikioni, lakini kabla hajaongea chochote, alishtuka kuona kivuli kikisogea mbele yake.
Mzee Kova alikuwa amesimama hapo, uso wake ukiwa na uamuzi usiotikisika. Mikono yake ilikuwa thabiti, ikishikilia bunduki aina ya Gobole, ambayo sasa ilikuwa imeelekezwa moja kwa moja kwa Zahoro.
“Usithubutu kuendelea,” Mzee Kova alisema kwa sauti nzito, yenye mamlaka.
Zahoro alihisi mgongo wake ukilowa jasho, lakini akajitahidi kutokupoteza mwelekeo. Akatazama moja kwa moja machoni mwa Mzee Kova, akijaribu kutafuta dalili yoyote ya huruma. “Mzee Kova, hatutaki matatizo. Tunajaribu tu kuondoka hapa,” alisema kwa sauti tulivu lakini thabiti.
Mzee Kova hakutikisika. “Hamna pa kwenda. Mnafikiria mnaweza kutoroka baada ya yote yaliyotokea?” aliuliza huku akiimarisha mshiko wake kwenye Gobole.
Mzee Miroshi aliyekuwa kimya muda wote, alisogea mbele kidogo, akiinua mkono wake kwa ishara ya utulivu. “Mzee Kova, umetufahamu kwa miaka mingi. Unajua kuwa sisi si maadui zako. Tafadhali, tuache tuondoke.”
Mzee Kova akahamaki huku akihisi pengine Mzee Miroshi alikua anapanga njama ya kumzubaisha ili waondoke, akaikaza Gobole huku kidole kikiwa tayari kufyatua risasi, akawa anaiamisha Bunduki kutoka kwa Zahoro kuelekea kwa Mzee Kova
“Nipatie hiyo simu vinginevyo nitamuuwa Baba yako” alisema Mzee Kova kwa sauti iliyoashiria muda wowote anaweza kutenda ikiwa mzaha utatokea. Kwa jinsi Zahoro anavyompenda Baba yake, alimpatia ile simu Mzee Kova ambaye alikua makini sana.
Akamuuliza Zahoro
“Hakuna simu inayofanya kazi hapa Kijijini, simu yako imewezaje kuita?” Zahoro alijawa na hofu huku akitetemeka. Jasho la mgongo lilikua likimvuja
“Mzee Kova, Kijana wangu si adui yako. Alikua Mdogo wakati ule, tafadhari sana hurumia Maisha yake” alisema Mzee Miroshi, akapigwa na Mdomo wa gobole akaanguka chini.
“Hii Biashara haikuhusu kabisa Miroshi, kaa kimya.” Kisha akamgeukia Zahoro, akakaza Mikono yake kwenye Gobole huku akimtazama kwa jicho kali.
“Wewe kosa lako ni kuona laana ikiwa inaingia, nina uhakika unajua njia ya kutoka hapa Kijijini” alisema Mzee Kova, kelele za WanaKijiji ziliendelea kuongezeka, vilio na Moshi viliendelea kujaza taharuki.
Sauti ya Bibi Lugumi ilikua ikiendelea kusikika taratibu ikija nyumbani kwa Mzee Kova, kila mmoja aliisikia sauti hiyo, ni sauti nyemelezi isiyo na kelele. Sauti ya kunong’ona inayouwa Mamia ya Wanakijiji wa Kijiji cha Nzena. Mzee Kova akataka kufanya haraka ili sasa Zahoro aseme njia ya kutoka hapo Kijijini ili awe salama na Laana ambayo yeye ndiye aliyeisababisha kwa kumuuwa Masumbuko.
Zahoro alikua kimya akiisikia sauti hiyo iliyokua ikikaribia hapo, sauti hii ni ile sauti aliyoisikia ndotoni. Ni sauti iliyomsumbua, hakutaka kuisikia. Akaziba masikio yake
“Hutaki kusema si ndiyo? Sasa nakuuwa” akasema Mzee Kova, kitendo bila kuchelewa Mzee Miroshi akaivuta Miguu ya Mzee Kova ili Zahoro akimbie. Mzee Kova akaanguka, Gobole lake ikadondokea pembeni.
Ghafla wote wakasimama huku wakiangalia juu, kitendo kilichomshangaza sana Zahoro, akajiuliza maswali mengi huku akiwa ameziba masikio yake. Akashuhudia Damu zikianza kuwatoka. Hata dakika moja haikufika, walianguka chini na kuanza kutapatapa. Kwa macho yake Zahoro alishuhudia kivuli chenye taswira ya Bibi Lugumi aliyemwona ndotoni, alikua akitabasamu huku akiongea maneno yake ambayo Zahoro hakutaka kuyasikia kabisa
Macho yalimtoka pima Zahoro, alirudi nyuma huku akijibamiza ukutani. Alihisi hali isiyo ya kawaida, mwili ulikua mzito akitokwa na jasho jingi huku kile kivuli kikimtaka Zahoro atoe mikono yake Masikioni aisikie ile sauti ya ajabu inayouwa. Zahoro hakutaka kuisikia ile sauti hivyo alijitahidi sana kupambana
Kadili kivuli kilivyosogea ndivyo ambavyo alikua akipata maumivu makali ya kichwa, mwisho alipiga kelele yenye sauti kali ya kugumia. Pale pale alipoteza fahamu zake na kuanguka chini kama mzigo.
***
Nje Ya Kijiji.
Magari ya Ulinzi na Usalama yalikua eneo ambalo Kijiji cha Nzena kilikuwepo kabla ya kutoweka kwake. Bado ilibakia kua simulizi ya kushangaza kwa wengi. Waziri wa Maliasili alikua akifikiria kwa kina ni sayansi ya aina gani ambayo imekipoteza Kijiji kilichobeba rasilimali kubwa ya Madini, wafanya Biashara na wamiliki wa Migodi walikua wamepotelea humo.
Simu zilikua hazipatikani, akasogea kwa mmoja wa washauri wake akamwuliza
“Haihusiani na Uchawi?” aliuliza kwa sauti ambayo ilionesha wazi kuwa alikosa majibu ya kawaida. Aliongea akiwa anapandisha suruali yake nyeusi, akaweka koti lake vizuri. Huku nje ilikua ni saa Mbili asubuhi, jua lilikua limechomoza vyema sasa.
“Mh! Hili jambo ni gumu sana kulipatia majibu ya haraka, kupotea kwa Kijiji ni hadithi za kwenye vitabu vya kale lakini leo tumeshuhudia hili jambo la kushangaza” alijibu Mshauri wa Waziri, akaweka mawani yake vizuri halafu akaendelea
“Pengine tunaweza kupata Majibu kwa njia hiyo, hebu tuifanyie kazi” alisema, haraka Waziri akamjibu kwa sauti ya kishindo
“Atafutwe na afichwe kwa siri ili hili jambo liwe siri baina yetu.”
“Ondoa shaka Mkuu” akasema kisha akapiga simu mahali ili kuhitaji Mganga wa Kienyeji mwenye uwezo Mkubwa sana wa kuangalia mambo yasiyoonekana kwa macho ya kawaida.
Ilichukua takribani masaa mawili hadi kumpata na kumfikisha kwenye gari ya Waziri wa Maliasili. Gari hiyo ilikua kubwa yenye nafasi ya kutosha, Mganga akaelezwa ni jambo gani aliloitiwa hapo.
Yule Mganga akacheka kidogo kama ilivyo kawaida ya waganga, kisha akatulia na kuwaambia
“Niliona kuhusu Kijiji hiki, hakipo. Kukiona ni Mjaaliwa” alisema kwa kujiamini, kwa sauti ya upole sana iliyojaa huzuni. Waziri akashtuka kisha akamwuliza
“Unamaanisha nini?” alihoji akiwa ameshupaza shingo yake huku makunyanzi yakiwa yamefunga uso wake. Mganga akameza mate kidogo halafu akasema
“Kijiji hiki, kimepokea laana ya Miaka mingi kwa kifo cha Kijana Masumbuko aliyekua mlemavu wa ngozi. Tangu hapo Bibi yake alikilaani Kijiji hiki kisha alijichoma Moto na kufa, sasa ile laana imekifanya Kijiji hiki kupotelea kuzimu. Laiti kama mgepata japo nafasi ya kusikia sauti za vilio, mateso na maumivu wanayo kutana nayo mgelia machozi ya Damu.” Alisema kisha alisikitika kwa kichwa chake
“Hakuna anayeweza kwenda huko wala kutoka huko. Historia itafutika, Kijiji cha Nzena kimeshapotea. Msihangaike sababu hakuna atakayetoka hai na kurudi Duniani” alisema, Waziri na Mshauri wake walitazamana. Walielezwa kila kitu na hawakuwa na swali lolote lile, Mganga akarudishwa walipomtoa.
Ukimya ukatawala, kila mmoja alikaa kimya baada ya kujua kuwa hakuna chochote wanachoweza kukifanya ili kukipata Kijiji hicho tajiri. Agizo la Rais lilikua ni kuhakikisha wanapata ufumbuzi wa Kisayansi lakini hadi muda huo Sayansi haikutoa majibu, majibu pekee ambayo waliyapata ni ya kiganga.
Waziri akajitupa kitini huku akifumba macho yake, hakujua atamweleza vipi Rais wa Ganza, utajiri uliopotea kwenye Kijiji cha Nzena ni utajiri mwingi sana wa Madini.
Mara mlango wa gari ulifunguliwa haraka sana, Waziri na Mshauri walishtuka. Mtu mmoja kutoka kwenye timu yake alikuja ghafla na kumwambia kua kuna Mtu kutoka Kijiji cha Nzena amepiga simu. Macho yalimtoka Waziri wa Maliasili, ingewezekanaje kua simu itoke kuzimu? Alikua kama Mtu aliyezinduliwa kutoka usingizi wa Pono, akatupa swali moja ngangari
“Unasemaje?”
Nini Kitaendelea? Usikose SEHEMU YA TATU Hapa Hapa Kijiweni
JIUNGE NA KIJIWENI WHATSAPP CHANNEL Kwa Kugusa Hapa
Soma Riwaya Nyingine Za Kijiweni Kwa KUGUSA HAPA
Wewe kama MFANYABIASHARA.. Kuna wakati unatamani kuwafikia watu wengi zaidi na hujui wapi pa kuanzia , USIJALI kwani hapa ndipo ambapo MTAA UNAONGEA na tuko tayari kukusaidia kuwafikia watu wengi kwa BEI YA OFA
Njoo Utangaze Nasi Sasa Kwa Kutuambia Una TANGAZO Gani na unataka kutangaza kwa muda gani kwa kutuma ujumbe hapa WwhatsApp Kupitia Namba +255760871896
5 Comments
Good job 🔥🔥🔥🔥
Tamu
Aloooooo hii mambo ni 💥💥💥💥Afu nikukumbushe ni sehemu ya Sita ndo inafata na si sehemu ya tatu kama ulivosema
Bonge la move
Simulizi nzuri Sana sema imekuwa fupi