Ilipoishia sehemu ya Kumi na moja ya In the name of LOVE

Moyo Wangu na akili yangu vilikua tayari kusikia chochote kile hata kama  kitaniumiza kiasi gani lakini Ndiyo ukweli pekee niliouhitaji kuusikia ili  nifahamu mengi yaliyokua yakinitatiza.  

Nilikua kimya huku moyo Wangu ukinidunda, viti vilipoletwa tuliketi  kando ya kile chumba Kisha yule Mzee alishusha pumzi zake akaniuliza 

“Ulikua wapi Kijana?”  Endelea

SEHEMU YA KUMI NA MBILI

“Nilipata ajali Baba, ilikua mbaya. Nilikaa Hospitali kwa wiki tatu”  nilisema. 

“Wiki tatu?” 

“Ndiyo Baba” 

“Na hizo siku nyingine ulikua wapi Hadi Mdogo wako anafia humu ndani,  tunamzika kwa kushirikiana na Watu uliokua ukifanya nao kazi?” nilikaa  kimya, kuhusu kifo Cha Melisa nilikisikia, nilikumbushwa machungu  yaliyoanza kupoa moyoni mwangu, nikajiinamia huku chozi likianza  kunitoka. 

“Usilie, wewe ni Mwanaume. Lakini ni Kosa kubwa umefanya kumtelekeza  Mdogo wako hapa Hadi rafiki Yako Sudi alipofanya aliyoyafanya. Kwa  Miaka mitano nimekifunga hiki chumba nikiamini ungerudi hapa  kuchukua kumbukumbu za Mdogo wako” alisema Baba mwenye nyumba,  niliinua kichwa changu huku chozi likiendelea kunibubujika. 

Nilimtazama kwa macho yenye huzuni huku nikipeleka macho yangu ndani  ya chumba Cha Sudi, palikua patupu nikajiuliza hizo kumbukumbu  anazozisema zipo wapi. 

“Hizo kumbukumbu zipo wapi?” nilimuuliza, alikaa kimya kidogo Kisha  akaniambia kwa sauti ya Ubaba.  

“Kwa bahati mbaya nimezichoma moto asubuhi ya Leo, nilikata tamaa  niliamini usingelirudi hapa. Kijana kwa Miaka yote ulishindwa kurudi hapa 

kweli?” aliniuliza swali lile lile lililokua likichanganya akili yangu, nilijiuliza  ndani ya nafsi yangu 

“Miaka yote? Ni Miaka gani anaizungumzia huyu Baba?” aliponiona nipo  mawazoni alinigutua kwa kunishika bega akaniuliza tena 

“Ulikua wapi?” Nilivuta hewa kidogo Kisha nilifuta chozi langu halafu  nikamtazama yule Baba kwa macho yaliyojaa ukungu wa mchozi laini  nikamwambia kwa sauti ya kitetemeshi Cha kulia. 

“Kuna kitu hakipo sawa kwangu Baba, sijui kuhusu Miaka unayoisena.  Naona ghafla Kuna kitu sikikumbuki, ni wiki tatu tu naona Kila Mtu  anaizungumzia kuhusu Miaka mitano iliyopita na mwingine Miaka minne.  Nipo gizani Baba naomba unieleze ukweli, Mdogo wangu alifariki lini?”  

Nilikua ninalia kwa kuuumia, akili yangu ilifungwa gizani. Kila kitu katika  Maisha yangu kilianza upya kabisa, Yule Baba alinitazama Kisha  akaniambia 

“Nifuate” alinyanyuka na kuingia ndani ya kile chumba, moyo Wangu  ulizizima kwa upweke na maumivu. Chumba Cha Sudi kilibeba  kumbukumbu zenye kuniumiza sana, niliishi na Mdogo wangu humo lakini  kwa Simulizi alifia humo kwa kuuawa na Sudi Kisha Sudi akakimbia.  

Nilisimama huku miguu yangu ikiwa mizito sana kuingia ndani ya hicho  chumba, yule Baba alikua tayari ameingia akageuka na kunipa ishara kua  niingie, nilinyanyua Mguu wangu huku chozi likinibubujika. 

Kumbukumbu za Melisa zilipita machoni pangu mithiri ya filamu ya  maumivu. Mguu wangu ulikua baridi sana kama Mtu aliyepooza lakini  niliusukuma ili niingie ndani pengine ningeona kitu chenye kunikumbusha  kitu kuhusu Miaka inayotajwa. 

Niliingia ndani ya chumba Cha Sudi, kilikua vile vile, magazeti ya Michezo  yalikua yamebandikwa ukutani, nilitembea Hadi ukutani huku yule Baba  akiniangalia tu. Niliushika Ukuta, nikapapasa Yale magazeti, yalikua  yamejaa vumbi 

Moja ya gazeti liliandikwa tarehe, ilikua ni Miaka mitano iliyopita. Palikua  na kitanda kilichofunikwa shuka nyeupe, yule Baba akaniambia 

“Tulimkuta Mdogo wako akiwa ameharibika hapa” nilianza kulia,  akanituliza na kuniambia. 

“Nilikitunza chumba hiki niliamini ungerudi japo nilikata tamaa. Kijana, ni  Miaka mitano imepita, unapaswa kuwauliza Watu wako wa karibu ni kitu 

gani wanakuficha” Alisema yule Baba, chozi lilianza kunibubujika maana  hata hao Watu wa karibu hawakuweza kunieleza chochote kile 

“Baba, niliambiwa baada ya ajali akili yangu haijakaa sawa lakini nahisi  nilidanganywa. Hapa Kuna kitu ninafichwa” nilisema Kisha Niliketi  kitandani, yule Baba naye aliketi kitandani pia 

“Kijana, hii Dunia ni Uwanja wa Siri, Binadamu wanaweza kuficha Siri  Hadi wanaingia kaburini ilimradi tu Siri hiyo isiwe faida kwa mwingine.  Inawezekana katika hiyo Siri Kuna jambo muhimu ambalo hawataki ulijue,  Kitu pekee kinachoweza kukufanya uijue Siri unayofichwa nayo ni kuwa  mdadisi zaidi” alisema yule Baba, maneno yake yaliamsha Hali Fulani ya  Ujasiri ndani yangu, nilikubali maneno yake kua kama nitaendelea kulia  siwezi kufahamu chochote kuhusu Miaka mitano iliyopita. 

“Nenda kautafute ukweli kwa gharama yoyote ile, hakuna kitu kibaya katika  Maisha ya Binadamu kama kujipoteza. Usikubali kujipoteza, unapaswa  kupambana” alisema tena, maneno yake yalijaa hekima na busara kubwa  sana. 

Nilifuta chozi langu nikamwambia “Naenda kuutafuta ukweli ulio gizani  Baba” Kisha nilinyanyuka na kuondoka pale, nilimwacha yule Baba akiwa  amesimama Mlangoni akinitazama nikipotea kwenye Kuta za nyumba yake 

Jina Moja lililo kichwani kwangu ambalo niliamini linaweza kunipa majibu  ni Clara, ndiye Mtu pekee aliyekua kando yangu siku niliyorudisha fahamu  baada ya ile ajali. 

Nilimsimamisha dereva wa pikipiki, nilihitaji kurudi nyumbani kwa Clara.  Akili yangu haikutaka kutulia kabisa, ilikua ni Mishale ya Alhasiri, nilifika  nyumbani kwa Clara 

Moja kwa moja nilielekea Chumbani kwangu, Zaylisa alikua hajarudi.  Sikujali sana kuhusu yeye, nilichohitaji ni kufika chumbani kwa Clara  pengine alikua Mtu muhimu kwenye Maisha yangu niliyoyasahau, akili  yangu iliniambia hivyo maana asingeliweza kua pale wakati narudisha  fahamu tena akiwa na Mtoto wake Melisa 

Nilizunguka chumbani huku nikipanga mkakati wa namna gani nitaingia  chumbani kwa Clara, Mtu pekee ambaye angeniwezesha kuingia humo  alikua ni Matilda. 

Niliufungua mlango Kisha nilienda sebleni, nikamkuta Matilda akiwa  anaangalia filamu, nikamtazama kwa sekunde kadhaa Kisha nikafanya 

uamuzi wa kukielekea chumba Cha Clara, aliponiona naelekea huko  Matilda alinikimbilia 

Nilitikisa kitasa Cha mlango nikagundua mlango ulikua umefungwa kama  nilivyohisi mwanzo, sasa lile wazo la kumtumia Matilda lilitakiwa kufanya  kazi. 

“Nahitaji kuingia chumbani kwa Clara” nilisema nikimtazama Matilda kwa  jicho Kali, hata yeye alishangaa kwasababu sikuwahi kumtazama kwa jicho  lile, akameza funda zito la mate huku akipumua kwa nguvu, alishaanza  kuingiwa na woga lakini akaniambia 

“Dada amefunga mlango wake, kwanini unataka kufanya hivyo?”  

“Nina uhakika ndani ya hiki chumba Kuna kumbukumbu zangu, nataka  kujua Clara ni Nani kwangu, kitu gani ambacho hamkisemi nyinyi?”  niliuliza kwa Uchungu sana, niliona Wazi kua Watu wale walifanya  makusudi kunipoteza kifikra bila kunipa kumbukumbu yoyote ile. 

Matilda alirudi kidogo nyuma, alichokisikia kutoka kwangu alionesha Wazi  kua alikitarajia. Hata sura yake ilionesha kua alikua ni miongoni mwa Watu  walioamua kunificha kuhusu Maisha yangu yaliyopita 

“Matilda, Kuna kitu unakijua na hutaki kusema si Ndiyo? Mimi ni Nani  nataka kujua Matilda, kwanini najiona sijakamilika Kuna kitu gani  nimesahau, nataka kujua ni kitu gani muhimu nimekisahau?” niliuliza,  Matilda alikua akinitazama kwa Mshangao tu huku chozi lake  likimbubujika 

Nilisogea taratibu Kisha nilimwambia kwa sauti ya huzuni huku chozi  likinidondoka. 

“Nakuomba Matilda, lazima utakua unanifahamu vizuri. Niambie  nisichokifahamu, niambie nilichokisahau” nilisema, niliona jinsi ambavyo  sura yake ilivyokua ikionesha huruma juu yangu. Nilimshika mabegani  nikamwonba aniambie chochote hata kama kilijaa maumivu kiasi gani  lakini nilitaka kusikia ukweli, niliona chozi lilikua likimbubujika ni wazi  aliguswa sana na maneno yangu. 

“Akili yangu imekosa utulivu Matilda, Nilipopata ajali na kurejesha fahamu  nilimwona Clara pale Hospitalini, niambie yeye ni Nani kwenye Maisha  yangu?” nilimuuliza Matilda. Alikua akinitazama kwa jicho la huruma sana 

Matilda hakusema chochote kile japo sura yake ilionesha kua alifahamu  jambo fulani. 

Nilirudi chumbani kwangu nikiwa na huzuni sana, chozi lilikua  likinibubujika. Kilichokua moyoni mwangu ni kama Mzigo mzito  nilioshindwa kuubeba. Nilijivuta Hadi nikaketi kitandani, sikua na hamu ya  chochote isipokua kujua Siri ya Maiaka Mitano iliyopita. 

Usiku ulipoingia ulinikuta nikiwa nimejiinamia, chumba kilikua Giza  sababu sikuwasha taa yoyote ile. Nilianza kusikia sauti ya Matilda akigumia 

“Mwizi! Mwizi!” nilishtuka, haraka nikapapasia taa halafu nikafungua  mlango nikaelekea nje, Matilda alikua ameshafika getini. Kwa Kipindi hicho  nyumba ya Clara ilikua Haina Mlinzi 

Nilikimbilia getini nikamkuta Matilda akiwa analia, nilimuuliza kimetokea  nini, alikua analia akaniambia 

“Mwizi aliingia chumbani kwangu”  

“Sasa chumbani kwako alikuja kufanya nini?” nilimuuliza, aliendelea kulia  bila kusema chochote. Ilinifikirisha kidogo, mwizi kuingia chumba Cha  Msichana wa kazi ambaye Hana chochote kile. 

“Basi usilie Matilda kwani amefanikiwa kuiba chochote?”  “Sijui Mimi, ila nimemkuta chumbani kwangu akanisukuma na kukimbia”  “Uliiyona sura yake?” 

“Hapana alivaa kofia”  

“Basi twende ndani, hawezi kurudi tena. Mimi nipo nitakulinda” nilisema  kama Mwanaume. Nilimpeleka Matilda sebleni Kisha nilimpatia Maji ya  baridi anywe ili aondoe wenge. Alipomaliza kunywa Maji angalau akili yake  ilitulia akanieleza kwa uzuri 

“Basi Wacha tukaangalie kama Kuna chochote amechukua” nilisema. 

“Hapana Kaka, hakuchukua chochote hata usijali” alisema, lakini ndani ya  sauti yake nilihisi Kuna kitu hakikua sawa. Mara Mlango ulifunguliwa,  aliingia Zaylisa 

“Eeeh mmetulia wenyewe hapo mnapiga stori” alisema, haraka akili yangu  iliniambia napaswa kujifanya hakuna nilichokiona kuhusu yeye ili niweze  kumchunguza vizuri, nilitabasamu kidogo tu nikamwambia 

“Umepishana kidogo na mwizi” Nilisema, akashtuka  

“Mwizi?”

“Ndiyo, aliingia chumbani kwa Matilda lakini bahati nzuri hakuiba  chochote kile” Zaylisa akasogea taratibu Kisha akamshika bega Matilda 

“Pole Binti, pole sana iwe funzo siku nyingine usiache mlango Wazi sawa?”  alisema kwa sauti ya kujali iliyojaa Udada ndani yake. Matilda akaitikia kwa  kichwa Kisha akanyanyuka na kuondoka akaelekea chumbani kwake. 

Nilitabasamu kidogo, Zaylisa aliniangalia kwa jicho la mapenzi. Nikashusha  pumzi nikamuuliza 

“Za utokako?”  

“Ahh‼ hivyo hivyo Mpenzi, Hali ya Baba siyo nzuri sana yaani napata  wakati mgumu sana” alisema, kwa mara ya kwanza nilimwona Zaylisa  akiongea uwongo mbele yangu, nilihisi kuumia sana. Hakujua kua  niliifahamu Siri aliyoificha kua Mzee Paulo alifariki siku nyingi 

“Jamani, pole sana my love. Kua na Imani Baba Yako atapona”  

“Asante, Ndiyo maana napenda kua karibu Yako Jacob. Najihisi amani na  furaha sana niwapo kando Yako” alisema Kisha alilala begani kwangu. Nafsi  yangu ilizidi kutapa tapa, hakuna kitu kinaumiza moyo kama kugundua  Mtu unayemwamini na kumpenda anafanya mambo gizani, nilijiuliza  alikua ana lengo gani la kusema uwongo 

“Usijali, Mimi ni wako Zay. Basi twende ukaoge ili uweke mwili safi”  nilisema Kisha nilibeba mkoba wake, tukaongozana Hadi chumbani,  akabadilisha nguo akavalia taulo Kisha akaelekea Bafuni. Nilisubiria Hadi  pale nitakaposikia Maji yakimwagika  

Niliutazama Mkoba wake, simu yake ilikua humo. Nilipata wazo la  kuipekua simu yake maana mara nyingi alikua haweki Nywila. Taratibu na  kwa umakini mkubwa sana niliuchukua mkoba Kisha nikafungua zipu pole  pole bila kelele huku macho na masikio yangu vikiwa makini sana. 

Nilipomaliza kufungua zipu ya mkoba wake niliiyona simu yake. Nilishusha  pumzi zangu, huku nikiamini simu hiyo itanifungulia njia ya kujua ni  mpango gani wa Siri ambao Zaylisa alikua nao na huwenda alikua  anaifahamu Siri ya Miaka mitano nisiyoikumbuka na pengine hakutaka  nikumbuke. 

Basi niliichukua simu taratibu na kwa umakini, Kisha nilibonyeza mahali,  mwanga ukawaka. Nilijaribu kuifungua lakini ilidai Nywila yaani namba ya  siri, nilihisi kupandwa na hasira maana nisingeliweza kufanikiwa chochote  kile. Iliongeza Hali ya Wasiwasi kua alikua na mpango Fulani, kwanini  aweke namba ya siri bila kuniambia

Niliirudisha simu na kufunga zipu Kisha niliuweka mkoba pale pale  nilipoutoa halafu, nikatulia kitandani nikiendelea na tafakari, Kila  nilichofanya hakikunipa mwanga  

Zaylisa aliporudi kutoka Bafuni alikua mwingi wa tabasamu, alinitazama  kwa tabasamu Kisha alinifuata na kuanza kunipiga mabusu. Sikua na hisia  naye tena, ghafla tu hisia zilihama kwake licha ya Upendo mwingi niliowahi  kua nao kwake 

Tulifanya mapenzi huku nikijitahidi kuigiza kua nilikua na hisia Kali sana  juu yake, sikutaka aujue mpango wangu kama ambavyo nilihisi alikua  akiuficha mpango wake kwangu. 

Baada ya kumaliza alijilaza kifuani kwangu, alikua mwingi wa kubadilisha  stori za hapa na pale. Ilichochea wasiwasi wangu kua lipo jambo zipo  alilokua akilificha 

Basi, tulilala Hadi asubuhi kulipo pambazuka. Kama kawaida yake aliniaga  kua anaenda kumhudumia Baba yake Mgonjwa, nami nilikua mwepesi wa  kumruhusu ili nyuma nifanye Uchunguzi wangu. 

Nilimfuatilia tena nyuma nyuma kwa kutumia Bodaboda, safari zake zilikua  zile zile. Alipofika Mwenge aliingia kwenye gari nyeusi iliyopanda juu  iliyoonekana kua ya gharama sana Kisha walielekea kwenye ile Hoteli 

Nikapata wazo kua ndani ya Hoteli hiyo Kuna jambo Fulani ambalo yeye  pamoja na yule Mwanaume anayevaa kofia walikua wakilipanga au  kulifanya.  

Sikutaka kuendelea Kuchunguza zaidi, nilirudi nyumbani. Nilimwita  Matilda, Kuna kitu nilitaka kumuuliza, alipofika alinisalimia maana  nilipotoka sikuonana naye 

“Hivi ile siku ambayo Zaylisa na Clara walizozana ilikuaje? Naomba  usinifiche chochote” nilimuuliza kwa sauti kavu ambayo ilimfanya aone kua  sikutaka utani. 

“Dada Zay, alimwambia Dada Clara kua…..” alisema Kisha alisita,  nikamkazia macho yangu kwa ukali 

“Alimwambia hataruhusu Melisa awe karibu na wewe” nilishtuka sana,  kwanini aseme hivyo kwani Mimi na Mtoto Melisa tuna uhusiano gani?  

“Kwanini aseme hivyo?” nilimuuliza, nilikua makini kusubiria jibu la  Matilda.  

“Mimi sijui Kaka, niliyasikia hayo tu ndipo wewe ulipokuja” 

“Matilda sura Yako inaonesha una jambo la ziada la kuniambia, niambie  tuu tafadhali” nilisema kwa sauti ya Unyonge. 

“Kaka Mimi sijui chochote kile nakuapia”  

“Mimi ni Mtu mzima, ninapoitazama sura Yako naona inakusuta kwa  unachokisema. Matilda, usiwe Sehemu ya Watu wanaohitaji niishi gizani  Milele, naomba nikuulize. Mimi ni Nani kwa Clara, kwanini siku ile alikua  Hospitalini, Nina uhuasiano gani na yeye?”  

Matilda alinitazama, uso wake ulinyongea, chozi likaanza kumbubujika. 

“Samahani Kaka Jacob, siwezi kusema Kila kitu” alisema Matilda huku  chozi likitiririka machoni pake. Nilimshika mabega yake nikamwambia 

“Naelewa ni jinsi gani unajizuia kuniambia Matilda lakini huu ndio wakati  sahihi wa kunieleza, nateseka kwa kuishi kama kivuli kwenye Maisha  yangu” nilisema, Matilda alinishika mkono akanipeleka chumbani kwake  Kisha akaufunga mlango.  

Akafungua Begi Moja kubwa halafu akatoa picha Moja, akanipatia. Nilihisi  upepo Fulani ukikatiza usoni pangu, picha hiyo nilipiga Mimi, yeye na  Clara. 

Nilipomaliza kuangalia niligundua hakuna kilichobadilika kwangu kwani  Bado nilikua sikumbuki chochote hata hiyo picha sikukumbuka ilipigwa  lini.  

“Hii picha?” niliuliza huku mdomo Wangu ukiwa mzito lakini wenye  kuhitaji kuendelea kuongea, Matilda akadakia kwa hisia ya huzuni sana  huku chozi likimdondoka akaniambia 

“Hiyo Ndiyo siku ambayo ulikua na furaha kuliko siku yoyote uliyowahi  kuishi hapa Duniani Kaka Jacob” alisema kwa hisia Kali sana, jicho langu  Moja likaanza kudondosha chozi, picha ilikua ikining’inia mkononi huku  kope za macho yangu zikicheza kwa muwasho wa chozi.  

“Kwanini nilikua na furaha Matilda?” nilimwuliza Kisha niliitazama tena ile  picha, ni kweli nilionekana kua mwenye furaha sana, siyo Mimi tu hata  Matilda na Clara walionekana kua na furaha, picha ilisadiki maneno ya  Matilda lakini sikujua ni kwanini furaha ilitawala kiasi hicho.  

Matilda aliibana midomo yake kwa Uchungu huku akizuia sauti ya kilio  isimtoke, moyo Wangu ulikua ukidunda sababu nilijua jibu ambalo Matilda  angenipatia lingetoa mwanga halisi wa Kila swali nililokua nikijiuliza,  akasema

“Hiyo Ndiyo siku ambayo Melisa alizaliwa” alisema, chozi lilimtoka kama  alikua amewekwa pilipiki machoni mwake, nilitazama tena ile picha Kisha  nilimtazama yeye. 

“Nilikuwepo siku ambayo Melisa alizaliwa?” 

“Ndiyo” 

“Hiyo Miaka mitano iliyopita?” 

“Ndiyo, Kaka Jacob wewe ni Mume wa Dada Clara pia ndiye Baba wa  Melisa” alifunguka Matilda, ni kama alikua amerusha bomu la anga. Lilitua  chini na kupasua Kila kitu, nilistaajabu sana lakini sikukumbuka chochote  Bado  

Macho yalinitoka, nilirudi nyuma hatua ndogo ndogo. Japo nilihitaji  kuambiwa ukweli lakini sikutegemea kusikia nilichokisikia, niligeuka na  kutembea taratibu kama Mtu aliyechoka sana, nilitembea na kutoka mle  chumbani. Nilifika sebleni nikiwa hoi, chozi na jasho vilikua vikishindana  kumwagika kama Maji. 

Nilisimama mbele ya sofa huku Bado nikiwa kwenye Butwaa.  

“Huo ndio ukweli Kaka Jacob” niliisikia sauti ya Matilda nyuma yangu,  haikua sauti ya kawaida Bali ilijaa kilio. Niligeuka na kumtazama Kisha  nikamkazia sauti nikamwambia 

“Wewe ni mwongo Matilda, unajua kua unasema uwongo. Sijawahi  kuyaishi hayo Maisha, sikuwepo na wala hakijapita hicho kipindi Cha  Miaka mitano” nilisema, Kisha akanipa picha nyingine 

Niliitazama huku chozi likidondokea kwenye ile picha, ilikua ni picha  tuliyopiga kanisani Mimi na Clara siku ya ndoa, nilikua nimevalia suti  nyeusi, Clara alikua amevalia gauni jeupe na shela. Nilizidi kuchoka, majibu  ya maswali yangu niliyapata kikatili sana 

“Sasa kwanini sikumbuki, kwanini Clara hakusema chochote?” nilipaza  sauti, nilikua katika Hali mbaya sana kisaikolojia, niliambiwa vitu vyenye  ushahidi lakini sikukumbuka chochote kile. 

Matilda akanisogelea huku akifuta chozi lake akaniambia 

“Daktari alisema usikumbushwe Bali asubirie Hadi utakapokumbuka  mwenyewe. Hiyo Ndiyo sababu ya kwanini hakusema chochote, Ndiyo  maana alimleta Zaylisa tena kwenye Maisha Yako. Wewe ni Msomi, wewe ni  Mtendaji Mkuu wa kampuni zote za Dada Clara” alisema Matilda, nilihisi  mwili ulikua ukitetemeka kwa uzito wa maneno ya Matilda.

“Kwahiyo nilimpenda Clara?”  

“Ndiyo, mlikua na furaha kwa Miaka mitano mliyoishi pamoja kama Mume  na Mke. Furaha yenu ilikatishwa Usiku ule ulipopata ajali, ilikua ni siku ya  Kumbukumbu ya Kuzaliwa kwa Melisa, ulipata mtikisiko wa Ubongo na  kupelekea kupoteza kumbukumbu zako.” Aliposema Kauli hii nilihisi  maumivu makali sana ya kichwa huku nikiona baadhi ya picha zikipita  kwenye ufahamu wangu  

Nilianza kuona baadhi ya kumbukumbu, nilishikilia kichwa changu na  kujikuta nikiwa nimeanguka sakafuni, nilipoteza fahamu.  

Matilda alihangaika na Mimi, akanipeleka Hospitali.  

Ukweli unaoumiza. 

Masaa Matatu baadaye nilipata fahamu, nilijikuta nipo kitandani. Macho  yalikua mazito yakitokwa na Machozi, nilikumbuka niliwahi kuamka kama  hivi na kumwona Clara na Melisa mbele yangu, safari hii ilikua tofauti 

Matilda alikua ameketi kando amejiinami, hakujua kua nilikua nimeamka.  Nilipovuta hewa nzito ndipo aliposikia na kunitazama. 

Alitoa tabasamu lenye huzuni ndani yake huku chozi jepesi likimtoka,  aliniangalia Kisha akaniuliza 

“Unajisikiaje Kaka Jacob?” chozi lilinidondoka nikiwa ninamtazama,  niliamka nikiwa Jacob niliyetimia. Kumbukumbu zangu zote zilikua  zimerudi. Nilikumbuka Kila kitu kuanzia kifo Cha Mdogo wangu kipenzi  Melisa, kifo Cha Mama yangu, nilimkumbuka Clara na Mtoto Wangu  Melisa 

Nilitikisa kichwa kuashiria kua nilikua sawa, lakini Matilda akataka kutoka  kwa ajili ya kwenda kumwita Daktari, nilimzuia kwa kumshika mkono  Kisha nikamwambia 

“Nipo salama Matilda, nakushukuru sana” nilisema, Matilda aliketi taratibu  huku akiniangalia kwa kunishangaa  

“Ndiyo, nimekumbuka Kila kitu kuhusu Mimi” nilisema kwa sauti ya  taratibu iliyosindikizwa na huzuni. Matilda aliachia tabasamu huku chozi  likiendelea kumbubujika.

“Usilie Matilda, Kila kitu kitakua sawa. Umewasiliana na Clara na kujua  yupo wapi?” nilimuuliza, akafuta chozi lake Kisha kwa sauti iliyojaa kubana  kwa mafua aliniambia 

“Kaka, nimejaribu sana lakini simpati. Sijui yupo wapi, natamani awe hapa  na wewe akifurahia kumbukumbu zako” Alisema Matilda, alionesha Wazi  kua alikua amejawa na Upendo sana juu yetu, aliyabeba matatizo yetu  kama matatizo yake, hakua tu Msichana wa kazi Bali ndugu aliyetimia. 

“Nakuomba Matilda, usimwambie yeyote kua kumbukumbu zangu zipo  sawa” nilisema, aliitikia kwa kutumia kichwa chake Kisha aliniambia 

“Mimi ni mtiifu kwako Kaka, sitathubutu. Nitajifanya kama vile sijui  chochote kile” basi nilitabasamu, nikafuta chozi lililobakia machoni pangu.  

Nilihisi nimeshusha mzigo mzito mabegani kwangu, nilihitaji kujua mambo  mawili, ni wapi alipo Clara na Mwanangu Melisa lakini pia nilihitaji kujua  kuhusu Zaylisa, alikua na mpango gani kwenye Maisha yangu. 

Baadaye jioni niliruhusiwa kurudi Nyumbani, baada ya kushuka kwenye  Bajaji nilisimama na kuitazama nyumba ya Clara, nilikumbuka Maisha  mazuri tuliyoyaishi kwa Miaka mitano iliyopita. Kila Kuta ilikua na historia  nzuri ya Upendo 

Nilihisi kusikia sauti za Kicheko Cha Clara na Mtoto wetu Melisa, Kila  nilichokitazama kilinipa kumbukumbu zisizofutika Maishani mwangu.  Matilda alinielelewa akanishika bega kua nisiwe na wasiwasi. 

Tulipoingia ndani ya Uzio, nilitazama Kila kitu. Kulikua na kumbukumbu  nyingi sana, macho yangu hayakuacha kulitazama eneo ka maegesho, hapo  palikua na gari tatu lakini Moja ilikua imefunikwa kwa turubai ikionekana  kua ilikua haitumiki. 

Nilisogea pole pole huku Matilda akiwa nyuma yangu, nilipepesa macho  taratibu huku upepo wa pole pole ukiwa unanipiga, nilisogea na kufungua  turubai. Nililiona gari langu ambalo nilikua nikilitumia, nililipapasa  taratibu huku nikigusa vumbi jepesi 

Chozi lilinitoka, gari Hilo lilikua na kumbukumbu ya ajali yangu,  halikutengenezwa Bali lilikua vile vile kama ambavyo nilipata nalo ajali,  lilikua na mbonyeo upande wa Kushoto huku vioo vikiwa vimevunjika. 

“Kaka Jacob” aliniita Matilda, aliguswa sana na Mimi. 

Niligeuka kumtazama

“Najua ni jinsi gani umeumia Kaka, lakini Kila kitu kwenye hii Dunia  hutokea kwasababu. Namshukuru Mungu umerudisha kumbukumbu zako  muhimu” alisema, niliitikia kwa kutumia kichwa kwani kinywa changu  kilikua kizito sana hakikuweza kutoa neno lolote lile 

Matilda akalifunika tena lile gari sababu tulikubaliana kua Kila Siri itabakia  kama ilivyo. Nilipoingia ndani nilizidi kukumbuka kuhusu Familia yangu,  Kila hatua niliyopiga ilinipa kumbukumbu nzito sana. 

Sikua na swali la kuuliza sababu majibu yote yalikua Wazi, nilikitazama  chumba Cha Clara, ndicho chumba chetu lakini napaswa kuishi kama  sikifahamu chumba hicho, ulikua ni uamuzi mgumu sana lakini wenye  maana. Basi nilikipita chumba kama sikijui Kisha nilielekea Chumbani  kwangu na kujilaza kitandani huku macho yangu yakitazama Dali. 

Usiku, Zaylisa alirudi kama kawaida yake akijifanya alikua bize sana na  kumuuguza Baba yake, aliniletea stori nyingi huku akiamini Mimi nilikua  Bado sijapata kumbukumbu zangu, akaingia bafuni kuoga Kisha akarudi  tukaketi na kuanza kuzungumza. 

Safari hii nilimtazama kwa jicho la tofauti sana, sio mapenzi Bali umakini  wa kujua alikua na mpango gani na huyo Mtu anayejiita ‘Mzee wa  MIPANGO’  

“Kidogo sasa hivi Hali ya Baba inaendelea kuimarika. Hua najisikia vibaya  sana kukuacha mpweke Mpenzi wangu” alisema Zaylisa kwa sauti iliyojaa  Ulaghai, niliikumbuka sauti hii ilikua ikimtoka Kila siku lakini nilikua  gizani sikuweza kuitambua.  

Kila nilivyomtazama nilihisi alikua ana Maisha ya tofauti sana kwa Miaka  mitano iliyopita, sikujua ni Maisha ya namna gani lakini hayakua Yale  niliyomwacha nayo wakati ule. Niliishia kutabasamu kana kwamba nilikua  Jacob yule aliyekua akimchezea, hata chembe ya Upendo haikuwepo.  Moyoni mwangu 

“Pole sana, Mungu atamfanyia wepesi ataimalika zaidi” nilisema huku  nikimtazama, japo tulikua tumekaa tunaongea lakini niliona alikua bize  sana na simu yake. Akanipa mwanya mzuri sana wa kuitazama upya sura  yake. 

**

Zilipita siku Nne, hakuna aliyempata Clara kwenye simu. Mwanzo  ilionekana kua kawaida lakini tulianza kupata hofu, Kila mara Simu ya  Mezani ilipoita ilitufanya tuwehuke sana. 

“Au ni kawaida yake?” aliuliza Zaylisa, tulikua tumekaa sebleni. Niligeuka  kumtazama, moyoni mwangu nilijua kabisa haikua kawaida kwa Clara,  niliishi naye Miaka mitano ya furaha na amani, ni Mke wangu wa Ndoa.  Nilipandwa na hasira lakini niliificha  

“Mh! Nitajuaje wakati Mimi hapa si mwenyeji Mpenzi, lakini hata Matilda  anamshangaa inaonesha sio kawaida” nilisema, alitabasamu kidogo tu  

“Lakini Jacob, unajua yeye hataki wewe uendelee kuwa hapa hasa na Mimi  hivyo usiwaze sana kuhusu yeye sababu huwezi kujua akirudi atakua na  mpango gani dhidi yetu” alisema Kisha alinisogelea akasema tena 

“Niangalie Mimi, unanijua na nimekubali kuachana na Mume wangu  kwasababu Yako wewe Jacob, Clara asiitumie fimbo ya kukusaidia  kukuchapia” Nilitikisa kichwa kukubaliana na Zaylisa huku nikiwa  nayaelewa maneno yake kua yalijaa mizizi ya Uwongo, sura yake ilionesha  kua alikua akiifahamu Siri ya Miaka Mitano iliyopita lakini swali  nililojiuliza nikiwa ninamtazama 

“Kwanini Clara alikubali kumleta tena kwenye Maisha yangu ikiwa alikua  anajua Mimi ni Mume wake, waliongea nini?” Majibu ya maswali yote  yalikua kwa Clara ambaye Hadi sasa hatujui yupo wapi na anafanya nini. 

“Ni kweli, sasa tutafanya nini Mpenzi ili kuhakikisha huyu Clara hatuchapi  tena? Unajua tatizo Sina mahali pa kukupeleka, Hali yangu kiuchumi  unaijua Zaylisa” nilisema kwa Uchungu sana kama vile nilikua mbele ya  Kamera nikiifuata Script iliyoandikwa na Mwandishi Nguli. Hata moyo  Wangu uliniambia kua kama nikigeukia Uigizaji basi nitaweza kuigiza  vizuri sana. 

Nilikua nikimtazama kwa uhakika wa uthabiti wa kumaanisha, sikuruhusu  hata chembe ya Uwongo ijulikane. Mara akapita Matilda akielekea jikoni,  Zaylisa akamwita Matilda kama Kijakazi tu 

“Nimekutuma unileteee juisi Hadi sasa haujaleta, una dharau sana wewe  Mtoto” alisema Zaylisa, hii Tabia sikuwahi kuiona kwake isipokua wakati  huu aliporudi kwenye Maisha yangu upya. Nilimtazama Matilda kwa jicho  la hasira Kisha nikamwambia 

“Acha dharau Mdogo wangu haya Maisha tu, kipi kinakufanya uoneshe  dharau wakati wewe ni Msichana wa kazi tu. Lete juisi hapa” nilikaza sauti 

Kisha nilimkonyeza jicho Matilda, sikutaka Kuonesha Wazi nipo Upande  wake nilijiegemeza Upande wa Zaylisa ili kuivuna Imani yake kwangu. 

“Samahani, nilisahau hata hivyo naenda kukuchukulia” alisema Matilda  kwa adabu sana Kisha aliondoka zake pale. 

“Jacob, unanifanya nazidi kukupenda maana licha ya kua hauna mamlaka  hapa ila unasimama na Mimi” alisema. 

“Usijali Kipenzi, nisiposimama na wewe nitasimama na Nani tena maana  Sina familia nyingine zaidi Yako wewe” nilimwambia Zaylisa na ikaonekana  kumpatia furaha sana 

Basi, Baada ya dakika Moja juisi ilikua tayari na Matilda aliileta ikiwa  kwenye glasi ndefu Pana, kama nilivyokwambia nyumba ya Clara ni  nyumba ya kitajiri hivyo hata vyombo vyake vilikua vya thamani sana.  Wakati anampatia kwa bahati mbaya akateleza na kumwagikia Juisi  kwenye gauni la Zaylisa 

Taharuki ikatokea, hasira ikampanda sana Zaylisa akatamani kumpiga  Matilda lakini sikuruhusu litokee nikaingilia kati, nikamtandika Kofi Mimi  Matilda, halikua Kofi sawa na lile ambalo Zaylisa angempiga 

“Mshenzi sana wewe, kwakua umelazimishwa kuleta Juisi ndio unafanya  hivi si Ndiyo?” nilisema kwa kufoka Hadi misuli ya shingo ilinitoka,  nilifanya kwa ajili ya kumwaminisha Zaylisa kua nilikua Upande wake  muda wote na hakuna nilichokumbuka. Matilda alidondosha chozi huku  akiomba msamaha 

“Nenda ukatupe vipande vya glasi Kisha uje ufute hapa haraka sana”  nilisema, haraka Matilda aliokota vipande vya glasi akaondoka.  Nilimgeukia Zaylisa kwa jicho la kujali nikamshika magebani  nikamwambia 

“Pole Babe, yule mshenzi sana amefanya makusudi ila dawa yake ipo jikoni.  Hizi dharau zimefika mwisho sasa” Nilisema huku Zaylisa akipepesa macho  yake aliyobandika kope, alikua na hasira sana akaniambia 

“Nimechukia sana Jacob, hizi ni dharau na siyo Bure huyu ametumwa na  Bosi wake, sasa nitamwonesha” alisema kwa hasira akiwa anatetemeka  sana. 

“Usijali, nenda kabadilishe nguo zako” nilisema, aliondoka zake kwa hasira  akaelekea chumbani, ile nageuka na Matilda alikua akifika. Nusura chozi  linitoke nilimwangalia kwa huruma, sikupenda kumpiga Kofi ila nilifanya  vile ili kumkinga na hasira ya Zaylisa. 

MWISHO

JIUNGE NA KIJIWENI WHATSAPP CHANNEL Kwa Kugusa Hapa 

Soma Riwaya Nyingine Za Kijiweni Kwa KUGUSA HAPA

Wewe kama MFANYABIASHARA.. Kuna wakati unatamani kuwafikia watu wengi zaidi na hujui wapi pa kuanzia , USIJALI kwani hapa ndipo ambapo MTAA UNAONGEA na tuko tayari kukusaidia kuwafikia watu wengi kwa BEI YA OFA

Njoo Utangaze Nasi Sasa Kwa Kutuambia Una TANGAZO Gani na unataka kutangaza kwa muda gani kwa kutuma ujumbe hapa WwhatsApp Kupitia Namba +255760871896 

Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love 

2 Comments

Leave A Reply

Exit mobile version