Ilipoishia Kimya (Nzena-Kijiji Kilicholaaniwa) – 05

Lakini walijua wazi… safari ya kuelekea Patiosa haikuwa tena ya kutafuta msaada.  Ilikuwa safari ya maisha au kifo. Kutupwa kwa miale ya moto ni ishara ya Ujio wa  askari zaidi eneo Hilo, palikua Giza huku taa kadhaa zilizobebwa na askari  zikijitahidi kupambana na Hali hiyo ya Giza  

Anna akamwambia Zahoro.

“Hatuwezi kufia hapa Zahoro, Moana anatusubiria. Hatma ya Maisha yetu Ipo  hapa sasa hivi, ikiwa tutashindwa kujinasua hapa tutakua tumepoteza Kila kitu”  alisema Anna huku akitetemeka kwa baridi.  Endelea

SEHEMU YA SITA

“Tunapaswa kua makini zaidi ya wakati wowote ule Maishani” alisema Zahoro Kisha walitazamana na kukubaliana kua wanapaswa kufanya jambo ili kua salama. 

Filimbi zilizidi kusikika eneo lote la Mto, palizingirwa ndani ya muda mfupi sana.  Razaro na Anna walianza kuzamia na kuogelea pole pole kutoka eneo Hilo  kuelekea upande mwingine ambao walihisi pangelikua salama kwao.  

Ilikua ni safari iliyojaa mateso na hofu, wakizidi kupiga mbizi za Kimya kimya  ndani ya Maji. Kitu pekee kilichowasaidia kilikua ni mazoezi waliyonayo kwa  Miaka yote ya kuishi ndani ya Kijiji Cha Nzena.  

Baadhi ya tochi zilipenya kwa ukali Hadi ndani ya Maji na kusababisha miale ya  mwanga ndani ya Maji, ilikua ni hatari kwao kwasababu baadhi ya mitumbwi  ilikua ikikaribia walipo. Taratibu Zahoro alimvuta Anna chini zaidi ya Maji  wakajificha nyuma ya mwamba mmoja 

Pumzi zao zilikua zinaendelea kupukutika mithiri ya Mti uliokauka ghafla,  walijikuta wakiwa katika wakati mgumu zaidi ya mwanzo. Kutoka ndani ya Maji  ilikua ni sawa na kuyachoma moto Maisha Yao ya thamani, ilikua ni sawa na  kukubali kumpoteza Mtoto wao Moana. 

Waliendelea kujibana hapo chini ya Maji huku wakizidi kupata wakati mgumu wa  kupumua. Mara ghafla Giza nene likatanda Majini, Zahoro na Anna waliona hiyo  ilikua ni ishara ya wao kutoka majini kwasababu mwanga wa tochi uliopotea  uliashiria askari walikua wamesogea eneo lingine. 

Zahoro aliibuka kwanza kama mzuka akitiririsha Maji mwilini, macho yake  yakipepesa kwa haraka alikutana na Upanga machoni pake. Alijikuta mtegoni huku  mitumbwi ikiwa imelizunguka eneo Hilo kimya sana kama eneo ambalo lilikua  tupu 

Mara Anna naye aliibuka, alikutana na tochi Kali ikimmulika, hatimaye wote  wawili walikamatwa. Waliingizwa kwenye Mtumbwi Kisha safari ya kuelekea Mji  wa Patiosa ilianza wakiwa chini ya Ulinzi wa Askari wengi wenye mapanga.

Mfalme Selasi alikua amechanganikiwa sana, maneno ya Segebuka yalikua  yakizunguka kichwani kwake, Mtoto Moana alikua amefungwa mahali ndani ya  chumba. Aligoma kuongea chochote kile licha ya vitisho ambavyo alipewa,  zilipofika taarifa kua walikua wamewakamata Watu wawili ndani mto, zilimpa  angalau ahueni na kutamani kuwaona Watu hao. 

Safari ya zaidi ya dakika 45 Hadi kuufikia Mji wa Patiosa, Mji hatari unaoishi kwa  kumwaga Damu pamoja na Uchawi wa Mfalme Selasi. Malango yalifunguliwa  Kisha Askari waliingia wakiwa wanawasukuma Anna na Zahoro, ilikua ndiyo  mara ya Kwanza kwa Zahoro anakutana na Watu wa Jamii tofauti na Jamii yake  kwa muda mrefu, akili yake ikamwambia kua ule Mji aliouota ndotoni ulikua  Ndiyo huo. 

Kila hatua aliyoipiga ilimkumbusha kuhusu ndoto yake, kuanzia Ukuta Hadi  Lango kuu la kuingilia. Palikua kimya sana kama vile ni Mji uliotelekezwa bila  Watu, taratibu walisukumwa Hadi ndani kwa Mfalme Selasi. 

Anna alikua akiufahamu vyema Mji huu kwasababu aliishi hapa kwa Maisha ya  makuzi yake, aliishi kama Mtoto wa Mfalme Kisha kufukuzwa kama Ombaomba  baada ya Kifo Cha Baba Yao. Kila Kuta ilijaa historia Yao, Kila sakafu ilikuwa na  maana kwake, alijikuta akidondosha chozi. 

Zahoro alimtazama Anna, hakujua ni kwanini alikua akilia ila kwa hakika aliamini  Kuna Siri iliyojificha juu ya Mji huu. Nje waliona Watu waliosurubiwa wakiwa  wananing’inia kama nyama iliyobanikwa. Miale ya moto iliyoleta mwanga ndani  ilikua mikononi mwa Askari 

Razaro alikua wa kwanza kuvusha Mguu wake kuelekea eneo la Ufalme, Anna  alipofika hapo aliigusa ardhi ya mlango kwa kutumia mkono wa kulia Kisha  alisema 

“Ardhi itaamua ni Damu ipi itamwagika hapa” alisema kwa kujiamini sana huku  akiendelea kukububujisha chozi lake lililojaa hisia ya Maumivu na kumbukumbu  za zamani kuhusu Ufalme wa Mji wa Patiosa. Akasukumwa Hadi ndani Kisha  wote wawili walijikuta wakiwa mbele ya Mwanaume mmoja mwenye jicho Moja  aliyevalia nguo za Kifalme, Naam‼ huyu ndiye Mfalme Selasi

Sura yake haikua ngeni machoni mwa Anna, lakini kwa Zahoro pia japo hakuwahi  kufika kimwili ndani ya Mji huu lakini akili na maono yake yalikua yameshawahi  kufika hapa kupitia ndoto. Alipomwona Mfalme Selasi akamwambia 

“Nilikuona, ni wewe” alisema huku akilengwa na mchozi wa furaha na maumivu.  Ndoto yake juu ya Mfalme Selasi ilibeba Tumaini la kurejea Duniani. Mfalme  Selasi akamtazama Segebuka kama ishara ya kuwaangalia walio mbele kama ndio  hao ambao wametajwa kwenye maono. 

Segebuka alisimama na Kisha alisogea mbele akiwa amevalia mavazi ya Kiganga.  Macho yake yalikua kwa Anna, alimtazama sana Kisha akakenua meno yake na  kusema 

“Hii ni Damu ya Ufalme wa Patiosa, hii ni Damu ya Munis” alisema Kisha  alimgeukia Mfalme Selasi ambaye alipandwa na hasira. 

Mfalme Selasi alisogea Kisha akamwuliza Anna. 

“Mlikua wawili Mapacha wakati nawafukuza hapa, mwenzako yupo wapi?” alihoji  kwa hasira, Uso wa Mfalme Selasi ulikua umekunjamana kwa shauri la uzee.  Zahoro alimtazama Anna, moyoni alihisi Siri aliyokua akiificha Anna ilikua  ikikaribia kufichuka. 

Anna naye alimtazama Zahoro kwa jicho la aibu ya kuficha Siri ya kuishi ndani ya  Mji wa Patiosa, siku zote hakuwahi kusema kuhusu kuufahamu Mji wa Patiosa.  

“Mwenzako Yuko wapi?” aliuliza tena kwa hasira Mfalme Selasi. Anna aligeuka  Kisha akamtazama Mfalme Selasi na kumjibu 

“Alishafariki Miaka Mingi” alijibu kwa mkato, Kisha Bado alipeleka macho kwa  Zahoro aliyejawa na Mshangao. 

“Kwahiyo umekuja kumkomboa Binti yako au umekuja kupora kiti Cha Ufalme  wa Baba Yako Munis?” aliuliza kwa tabasamu la dhihaka Mfalme Selasi, sauti  iliyotoka kwa mikwaruzo kiasi ikiambatana na kukohoa kidogo. Walinzi walikua  wamezunguka eneo Hilo kwa ajili ya Ulinzi Usiku huo. 

Anna alijitingisha kidogo kwasababu alikua amekandamizwa na Walinzi. 

“Binti yangu yupo wapi?” aliuliza Zahoro kwa hasira sana huku akijitingisha bila  mafanikio. 

“Ooh! Kumbe alizaa na wewe, hii ni Hadithi ya kusisimua sana. Enhee wewe ni  Nani?” aliuliza Mfalme kwa dhihaka zaidi huku akiwa ameiweka mikono yake  nyuma. 

“Mimi ndiye hatma Yako, Mimi ni kifo chako. Utaanguka kabla ya kutuangusha  sisi” Maneno haya yalimchukiza sana Mfalme Selasi, akahamaki na kumtandika  Kofi Zahoro. 

“Segebuka, huyu ni Nani?” aliuliza Mfalme, alihitaji macho ya Kiganga  kumtazama Zahoro. 

Segebuka akamtazama sana Zahoro Kisha akamgeukia Mfalme na kumwambia 

“Amebeba Hatma ngumu yenye maono, ni Mtu wa ndoto zenye maana. Anaona  yajayo kupitia ndoto, lipo aliloliona” alisema Segebuka kwa heshima. Majibu haya  yalimpa wasiwasi sana Mfalme Selasi, alihisi kutimia kwa maneno ya Segebuka jambo ambalo hakutaka litokee kamwe 

“Nitawachinja wote kwa mikono yangu, nitaimaliza Damu yenu na hakuna kizazi  kitaishi kwa Damu yenu” alisema kwa hasira sana Kisha alirejea kuketi kwenye  kiti Cha kifalme. Sura yake ilipoteza Nuru nzuri, ilijawa na hasira na ghadhabu  

“Wafungeni, kesho nitawachinja kwa mikono yangu mbele ya Halaiki ya Watu  Wangu wote wa Patiosa, wataarifiwe” alitoa maagizo, mara Moja, Anna na Zahoro walienda kufungiwa kwenye chumba kimoja. Nje yake walinzi wawili waliojazia  miili Yao walikua wakiwalinda Usiku kucha. 

Anna alijua kua Zahoro alikua na maswali mengi kichwani, alianza kwa  kumwomba Msamaha. 

“Najua umesikia mengi Zahoro, mengi ambayo nina uhakika Kuna baadhi uliyaona  kwenye ndoto na hukutaka kusema, yote ni kweli” alisema kwa sauti iliyopoa  wakiwa wameketi sakafuni wakiegemea Ukuta. 

“Yupo wapi?” aliuliza Zahoro, akimaanisha Alice. 

“Kila mahali, atakuja hapa kukusaidia kutimiza Malengo Yako” alisema Anna,  hapakua na Siri ilibidi afunguke tu. Taratibu maongezi yaliendelea

“Ni yeye?” aliuliza, maswali yaliyojaa mafumbo sana. Anna alitikisa kichwa chake  huku chozi likianza kumbubujika, ulikua ni wakati wa kusema ukweli kwa hisia ya  ndani iliyojaa maumivu na hasira pamoja na Siri ya Maisha. 

“Lini ulianza kugundua na kufanya kua Siri?”  

“zahoro”  

“Lini Anna?, Nimepoteza Kila kitu kabla Yako, ulipokuja nilipoteza vilivyobakia  huku ukijua fika kua uliubeba ukweli moyoni, uliruhusu Watu wafe isipokua Mimi  pekee kwasababu unajua Mimi ni njia” alisema Zahoro huku akibubujisha chozi,  chumba kiligeuka kua Sehemu ya majonzi na maumivu ya kihisia. 

Palikua na hewa nzito iliyofanya sauti zao kubakia ndani ya chumba Cha Gereza  bila kutoka nje. Chumba chenye mwanga hafifu kilikua kikisikia Siri nzito ambayo  hata Mfalme hakupaswa kuisikia kuhusu Alice. 

“Nisamehe Zahoro, nilipogundua nilikua nimechelewa. Sikutaka kuharibu mpango  wako hivyo nilijua siku Moja nitakueleza ukweli, sikutaka uusikie ukweli kutoka  kwa Mtu mwingine, najua nimekuumiza na pengine umeondoa Imani juu yangu.” 

“Wewe ni msaliti Anna, ulitutumbukiza shimoni Kisha ulijifanya unatusaidia.  Nilikua gizani Hadi siku ambayo nilishambuliwa na Adui Kimya, ile Ndiyo siku  ambayo niligundua ukweli. Aliponionesha sura yake mbaya nilipokua  nimejeruhiwa Mguu, alidondosha kitu Fulani. Nilipokiokota niligundua kilikua ni  kipande kilichokosekana kwenye kidani chako, Usiku mmoja ukiwa umelala  niliunganisha. Kilipokubali kuunganika na kidani chako niligundua kua ulikua na  mahusiano naye” alisema Zahoro kwa sauti ya maumivu sana 

“Tokea siku ile niliacha kumwogopa kwa maana nilijua hawezi kunidhuru tena,  nilijua usingeliruhusu Hilo litokee kwasababu Mimi ni ufunguo wa wewe kufika  Duniani.”  

“zahoro siwezi kukuzuia kufikiria unachotaka ila ninaweza kukueleza Sehemu ya  usichokijua. Mimi na Alice ni Sehemu ya Ufalme wa Patiosa, Baba yetu alikua  mtawala hapa lakini yeye na Mama waliuawa na Watu kutoka Duniani, waliondoka  na Pete ya Baba yetu kwa makusudi. Kuanzia hapo Maisha yalibadilika,  Tulifukuzwa hapa na ndipo nilipotengana na Alice kwa miaka Mingi sana ya Hapa 

Kuzimu. Mimi sikuwahi kufika Duniani tofauti na nilivyokwambia Mwanzo”  alisema Anna Kisha alifuta chozi lake na kuweka sawa sauti yake Kisha aliendelea 

“Ikiwa kutoniamini kutakupa amani nipo tayari, lengo langu lilikua ni kulipa  Kisasi Kisha kuchukua Pete na kuirudisha huku. Alice siyo Mtu Mbaya isipokua  amepata nguvu za ajabu, ili aendelee kuishi ilikua ni lazima atekeleze laana, Ndiyo  maana alikua Sehemu ya laana yenu iliyowaleta huku. Hakupenda kuyafanya yote  aliyoyafanya Zahoro.” Alisema Anna, ukimya ulitawala kwa muda mrefu Kisha  baadaye kwa sauti ya kupona Anna alimwambia Zahoro. 

“Nina ombi Moja TU kwako, mchukue Moana, hastahili kuishi huku. Yeye siyo  mali ya huku, lakini Nina ombi zaidi. Nisaidie kufika Dunia kwa ajili ya kulipa  Kisasi na kuchukua Pete ya Baba” alisema Anna, maneno yake yaliusakafisha  moyo wa Zahoro. Yaliondoka na hasira ya Zahoro, angefanya nini wakati  ameelezwa ukweli mchungu. 

“Tumesha Chelewa, tayari tupo kizuizini Anna na hatuwezi kuchomoka hapa  tukiwa hai tena.” Alisema Zahoro 

“Usijali, Alice hawezi kutuacha hapa tuangamie. Atakuja kutupigania, subiri  utaona” alisema Anna, maneno yake ya matumaini yalitamatisha maongezi yao  Kisha kimya kingi kilitawala. 

Upande wa pili Mfalme Selasi alichukua farasi Usiku huo huo akiwa na Mlinzi  wake mmoja. 

Waliondoka Patiosa wakaelekea mbali zaidi na hapo, walipofika mahali ambapo  Mfalme alikusudia. Alimwambia Mlinzi wake amsubirie hapo kwani ana jambo la  Siri anahitaji kulifanya Usiku huo. Akamwacha Mlinzi pamoja na farasi wake  Kisha akaingia Msituni zaidi. Eneo lililojaa ukimya na Giza nene, lenye miti  iliyofungamana, eneo la kutisha ambalo Binadamu wa kawaida asingeliweza  kufikiria hata kulisogelea lakini Mfalme Selasi aliingia humo bila woga. 

Alijipenyeza Hadi ndani zaidi alishusha makorongo kadhaa kabla ya kuvuka  bwawa dogo na kutokea eneo lenye Mti mmoja mkubwa sana wenye Pango lenye  mwanga kama wa taa hivi. Hapo alitokea Mtu mmoja aliyefunika uso wake Kisha 

akampatia Mfalme Selasi mfuko mdogo, baada ya kumpatia wakazungumza  maneno ya Siri Kisha Mtu huyo alirejea pangoni Kisha Giza likatanda pale. 

Mfalme Selasi alipomaliza kuwasiliana na Mtu wa Siri alivuka Bwawa Kisha  alirudi kule alikomwacha Mlinzi wake Kisha safari ya kurejea Patiosa ilianza kwa  ukimya.  

Hawakuzungumza Hadi walipofika Mji wa Patiosa, wakafunguliwa lango kuu  Kisha Mfalme akarejea Patiosa Usiku huo. Moja kwa Moja alielekea chumbani  kwake kwa Siri, halafu akauweka ule mfuko juu ya meza ndogo Kisha akaketi 

Akatabasamu kidogo kabla ya kufungua ule mfuko, kilichomo ndani yake kilikua  ni Bastola ya Kisasa yenye rangi ya Dhahabu. Kwa teknolojia ya Kuzimu  pasingelikua rahisi kwa Mtu kutengeneza Bastola ile ya Dhahabu. Hapana shaka  safari yake ya kuonana na Mtu wa Siri ilikua na mahusiano na Dunia halisi,  kwamba Mtu aliyempatia ile Bastola alitokea Duniani. Lakini iliwezekanaje? Ni  Nani aliweza kufika Kuzimu ikiwa Mlango wa Kuzimu ulifungwa Miaka Mingi  baada ya GGB na Steve Mbasa kumwua Mfalme na kuiba Pete? Hebu tusonge  mbele 

** 

Asubuhi ilifika, Jua lilichomoza, Mji wote wa Patiosa ulikua umefunikwa kwa  Nuru ya mwanga. Hata chumba Cha Gerezani ambalo Anna na Zahoro walifungiwa kiliingia Mwanga. Ni siku nyingine tena ndani ya Mji wa Damu wa  Patiosa 

Walianza kusikia kelele nyingi huko nje, kwakua walikua wageni hawakufahamu  palikua na nini lakini Anna alitambua. Akamwambia Zahoro  

“Hizo kelele ni ishara kua Leo ni siku ya Umwagaji Damu ndani ya Mji. Huu ni  utaratibu mbaya sana wa Mfalme Selasi, ameugeuza Mji kua Sehemu chafu”  alisema, mara walikuja askari, malango ya Gerezani yalifunguliwa 

Walichukuliwa pamoja na wafungwa wengine wakapelekewa Hadi eneo Moja  ambalo lilijengwa mahususi kwa ajili ya Umwagaji Damu. Eneo Hilo lilikua na kiti  Cha Enzi Cha Mfalme pamoja na wasaidizi wake 

Walipofika shangwe liliibuka kwa Wananchi waliamini kua kumwaga Damu  kutawasaidia Mji wao kuendelea kua na nguvu zaidi. Miongoni mwa Walioletwa 

mbele ya Mfalme alikuwepo Mtoto Moana. Chozi lilimtoka Anna alipomwona  Moana akiwa amefungwa minyororo. 

“Moana” aliita Anna kwa sauti ya Juu, Moana alimtazama Mama yake Kisha  alimpa tabasamu la matumaini. 

Mfalme akawaambia walinzi kua Watu watatu watakua wa mwisho kuuawa  Asubuhi hiyo, Watu hao ni Moana, Anna na Zahoro. Walitengwa huku  wakishuhudia namna Watu wengine wakiuawa kwa kuchinjwa kama Kuku Kisha  Damu kutiwa kwenye chombo maalumu kwa ajili ya sadaka. 

Nini Kitaendelea? Usikose sehemu ya SABA

JIUNGE NA KIJIWENI WHATSAPP CHANNEL Kwa Kugusa Hapa 

Soma Riwaya Nyingine Za Kijiweni Kwa KUGUSA HAPA

Wewe kama MFANYABIASHARA.. Kuna wakati unatamani kuwafikia watu wengi zaidi na hujui wapi pa kuanzia , USIJALI kwani hapa ndipo ambapo MTAA UNAONGEA na tuko tayari kukusaidia kuwafikia watu wengi kwa BEI YA OFA

Njoo Utangaze Nasi Sasa Kwa Kutuambia Una TANGAZO Gani na unataka kutangaza kwa muda gani kwa kutuma ujumbe hapa WwhatsApp Kupitia Namba +255760871896 

Nzena xx Nzena xx Nzena xx Nzena xx Nzena xx Nzena xx Nzena xx Nzena xx Nzena xx Nzena xx Nzena xx 

 

Leave A Reply

Exit mobile version