Ilipoishia Kimya (Nzena-Kijiji Kilicholaaniwa) – 01 

Hapakua na sauti yoyote iliyosikika, hapakua na Ndege wala wadudu waliopiga  kelele. Ghafla Zahoro alisimama, akatoa ishara kwa Anna kusimama pia 

Sauti ya ajabu ilianza kusikika kama kuna kitu kikubwa kinakaribia kutokea juu.  Zahoro, aliyekuwa ni mtu wa tahadhari, hakutaka kugeuka haraka. Badala yake,  alivuta hisia zake kwa umakini zaidi. Taratibu, aligeuka na kutazama juu— palikuwa na nyoka mkubwa mweusi aliyekuwa akishuka kwa taratibu, kwa mtindo  wa kuvizia.  

Endelea

SEHEMU YA PILI

Mlilio wa ajabu wa nyoka huyo ulizidi kuongezeka. Kwa tahadhari kubwa, Zahoro alianza kuuchomoa upanga wake aliouweka nyuma ya kiuno. Alijua fika kuwa  yule nyoka alikuwa mwindaji hatari. Taratibu, nyoka alianza kuishusha shingo  yake, akielekea kwao.

Ghafla, kwa kasi ya ajabu, Anna alichomoa upanga wake na kukata kichwa cha  nyoka huyo kwa kishindo. 

“Tukimbie!” alisikika Anna akipiga kelele kwa sauti ya juu. Hakukuwa na siri tena  kuhusu adui yao—Kimya. 

Papo hapo, nuru nyekundu ikaja kwa kasi ya ajabu kutoka nyuma yao. Zahoro alimwongoza Anna mbele, na wote wakaanza kukimbia kwa kasi kuelekea mtoni.  Nuru hiyo haikuacha—iliendelea kuwafuata kwa kasi isiyo ya kawaida. 

Mara ghafla, wote walisimama. Ile nuru nyekundu ilikuwa tayari mbele yao. Wote  walibaki kimya, wakifunika macho yao kwa kutumia vitambaa vyeusi. 

Taswira ya jicho Moja kubwa ilionekana kwenye ule mwanga mwekundu, hakuna  walichokiona kwasababu walikua wamefunga macho Yao.  

“Mko wapi?” ilisikika sauti iliyotoka kwa kunong’ona pole pole. Ilizidi  kuwaonesha kua walikua kwenye hatari kubwa sana. Kwa mbali pia walikua  wakiisikia sauti ya Maji ya Mto yakitiririka, lile jicho lilizidi kusogea huku  likiwatazama kama masanamu yaliyo tengwa. Moana alikua ametulia tulii  Mgongoni kwa Anna, yeye alikua amefundishwa Kila kitu kuhusu Adui Yao  aitwaye KIMYA. 

Upepo wa taratibu uliendelea kuvuma na kusukuma majani, sauti ilizidi kuuliza.  Ilikua ni sauti ya Kike Iliyo hatari zaidi tena ilitoka kwa vitisho vikubwa sana 

“Nataka niwaone, mko wapi?” iliendelea kuuliza, ilikua ni sauti yenye nguvu za  ajabu, ilisikika zaidi kwenye vichwa vyao. Walisimama kama askari, wakiwa  kimya kuliko kawaida. 

Walijizuia hata kupumua kwa nguvu maana Adui Yao aliweza kusikia sauti Kisha  macho Ndiyo huona. Anapokutazama usoni, basi safari ya Maisha Yako huishia  hapo

Zilipita dakika tano za ukimya Kisha lile jicho lilijifunga, papo hapo ule mwanga  mwekundu nao ulitoweka. Kisha Hali ya Ukimya iliendelea, Angalau sasa  walishusha pumzi zao, wakaondoa vitambaa usoni mwao. Hali ilionekana kua  shwari, kwa mbali kidogo sauti ya kutiririka kwa Maji ilisikika 

Zahoro akamwuliza Anna kwa ishara kama alikua yupo salama, Anna aliitikia pia  kwa kutumia ishara ya kichwa, Kisha safari Yao iliendelea kwa kuuruka kidogo  mwili wa nyoka mkubwa. Walitembea taratibu sana na kwa tahadhari kubwa, sasa  walikua na kiu ya kuufikia Mto ambao waliamini ungewapeleka mbali zaidi kuliko  kutembea kwa Miguu. 

Jua lilipofika utosini liliwakuta wakiwa wamesimama wakiutazama Mto mbele  Yao, walikua wakitabasamu kwa Uchungu. Bado palikua kimya sana. Zahoro akampa Anna ishara kua wamsubirie hapo, taratibu alishuka Hadi Mtoni, Kisha  aligeuka na kumtazama Anna pamoja na Mtoto. 

Kimya kilikua kimetawala sana, aliyatumia macho yake kuangaza huku na kule  kwa tahadhari zaidi lakini pia alihitaji kutafuta kitu ambacho kingeweza  kuwasafirisha. Aliangaza zaidi na zaidi Kisha aliuwona Mtumbwi mmoja  uliojificha kwenye miti midogo kando ya Mto, alisogea hapo haraka Kisha  aliupapasa Mtumbwi kwa kutumia vidole vyake. 

Chozi lilimtoka, alitamani asiamini kama alikua amepata usafiri. Aliuvuta taratibu  Hadi kwenye Ukingo wa Mto. Aliutazama ulikua ni Mtumbwi uliokaribia kuoza  lakini angalau ungeweza kuwasogeza mbali kidogo, aligeuka kumtazama Anna. 

Anna hakuwepo eneo alilomwacha, mara ya Kwanza alihisi labda macho yake  yalimdanganya lakini alipoangalia vizuri palikua patupu. Moyo ulianza kumwenda  mbio, haraka Alikimbilia juu alipomwacha Anna na Mtoto. 

Alimkuta Anna akiwa ameshikiliwa na Mwanaume Mmoja mweusi, mnene  mwenye tumbo kubwa. Alikua ameshikilia kisu Kisha alimpa ishara Zahoro asifanye chochote vinginevyo angemuuwa Anna. Mikono ya Zahoro ilitetemeka  kwa hasira, alitamani kupambana lakini eneo Hilo lilipaswa kua Kimya zaidi.  Akamuuliza yule Mwanaume kwa sauti ya kunong’ona  

“Unataka nini?” swali hili lilijibiwa na Kicheko Cha Mwanaume huyo, Kicheko  Cha chini chini kilichojaa daharau za kutosha.

“Nataka mfe badala yetu, Kisha sisi tuondoke hapa kwa kutumia Ule Mtumbwi  kule chini” aliposema hivi, Zahoro aligeuka. Akamwona Mwanaume mwingine  aliyevalia nguo zilizo loa Damu akiuburuza Mtumbwi ndani ya Maji.  

“Washenzi….” Alisema kwa hasira ya chini Zahoro, ule Mtumbwi Ndiyo tumaini  pekee kwao. Aligundua kua huwenda Kuna Watu wengi walionasa kwa Miaka  Mingi kama wao.  

“Sawa, unataka tufanye nini?” aliuliza Zahoro kwa sauti ile ile ya chini lakini  iliyojaa hasira isiyovumilika, alikunja mikono yake lakini hakuwa na la kufanya. 

“Sawa. Nataka msimame hapa juu mpige kelele, wakati sisi tunaondoka na  Mtumbwi” alisema yule Mwanaume, lengo lake likiwa zisikike kelele ili Adui  Kimya akisikia basi apoteze muda kuwadhuru akina Zahoro ili wao waondoke  hapo. Wakati anaongea hivi, kule chini mwenzie alikua akimsubiria.  

Anna alikua akitetemeka, Mtoto alikuwa Mgongoni Kisha yule Mwanaume  akawaambia 

“Nitamchukua Mtoto, msipofanya hivyo basi sisi na Mtoto tutakufa. Lakini mkitii,  Mtoto ataishi nasi” alisema kwa dharau tena kwa sauti ile ile ya chini, hapakua na  chaguo Bali kuwasikiliza. 

“Mpatie” alisema Zahoro, Anna alibubujisha machozi. Hakutegemea kama  angetengana na Moana kwa staili hii katili sana. Alimshusha Moana taratibu huku  akiwa anatokwa na machozi 

“Utakua salama Moana” Anna alimwambia Moana aliyekua Bado angali na  kitambaa usoni pake kumkinga na Macho ya Adui Kimya.  

“Mama‼” aliita Moana kwa sauti ya chini, haraka yule Mwanaume akamkwapua  Moana kutoka chini, akamwekea kisu kidogo shingoni Kisha akasema 

“Fuateni nitakacho kisema” alisema kwa tahadhari sana, Kisha aliachia tabasamu.  Hakuonekana kua Mtu mwema kabisa na wala Zahoro hakumtambua Mtu huyo  kama alitoka Kijijini kwao Nzena lakini pengine labda ni miongoni mwa wageni  waliopotea na Kijiji.

Taratibu alishuka na Moana Hadi chini, Kisha aligeuka na kuwatazama akawapa  ishara ya tusi kwa kutumia kidole, chozi lilimbubujika sana Anna. Kilio Cha ndani  Cha Kiume kilimshika Zahoro. 

Moana alikua ni zaidi ya Mtoto kwao, walimfundisha Ujasiri, walimpa mbinu  nyingi za kukabiliana na Adui Yao Kimya. Hawakua na namna ya kufanya  isipokua kufanya kama walivyoambiwa ili kumlinda Moana. Hata wao waliamini  upande wa pili wa Mto huo kulikua na Maisha ya Watu wengine, pengine palikua  salama zaidi ya hapo walipo. 

Walimsindikiza Mwanaume yule Hadi alipopanda kwenye Mtumbwi, Kisha  walianza kuyakata Maji ya Mto taratibu kuondoka hapo huku chozi la huzuni na  maumivu likiwa linamtoka Moana. Bado alikua na kitambaa usoni lakini aliweza  kupata hisia Kali ya maumivu isiyostahimilika. 

Kelele za Kasia zilianza kusababisha Hali ya Upepo wa ajabu sana huku mwanga  mwekundu ukija kwa Kasi kutokea Msituni. Anna akamwambia Zahoro  

“Lazima tumsaidie Moana, hawezi kufa machoni mwetu” alisema kwa hasira huku  akiwa anabubujisha chozi lake, akawa wa kwanza kupanda juu ya Jiwe kubwa,  akahakikisha Buti zake zikikamata vizuri. Kisha alimeza funda zito la mate akiwa  anatazama Mtumbwi uliokua ukizidi kusonga mbele kwa Kasi sana. 

Razaro naye akapanda juu ya jiwe, kazi ikawa Moja tu kuhakikisha Moana  anaondoka salama japo na Watu ambao hata wao hawawajui kabisa. Iliwalazimu  kupiga kelele ili ule mwanga mwekundu usiufikie Mtumbwi, walipiga yowe. Ule  Mwanga pamoja na Upepo vilisimama mahali Kisha vikageuza uelekeo na kuanza  kuwafuata wao. 

Wakaruka kutoka juu ya jiwe Kisha wakazama Msituni na kuanza kukimbia kwa  Kasi sana, waliamua kurejea kule pangoni. Mahali ambako waliishi kwa Usalama  kwa Miaka Mingi. Walikua ni Watu wa mazoezi waliozoea Maisha ya Hela heka,  ikawa mfukuzano wa Kasi sana baina Yao na ule Mwanga.  

Walipoona ule mwanga unakaribia kuwafikia, waliamua kujificha nyuma ya jiwe  Moja. Walikua kimya huku wakiwa wameshajifunga vitambaa usoni mwao,  walihakikisha hawawezi kuona mbele. Upepo mkali ulisogea taratibu Hadi walipo,  matawi ya Miti yalikua yakichezacheza kwa Kasi kutokana na ule Upepo.

Walibana pumzi zao vizuri, walianza kuisikia sauti ya Mwanamke. Sauti  iliyowauliza 

“Mko wapi?” ilikua ni ile sauti ya ajabu ya kunong’ona. Ikiambatana na Kicheko  Cha chini chini. 

“Nawaona” iliendelea sauti hiyo huku Zahoro akiwa amejikausha kimya, ile sauti  Ikawa inakuja karibu na walipo kwa juu, Zahoro akampa ishara Anna kua  wanapaswa kutengana kwa muda ikiwezekana wakutane pangoni. Mwanga ulizidi  kusogea huku Upepo ukiwa unakaribia walipokua wamejificha. 

JIUNGE NA KIJIWENI WHATSAPP CHANNEL Kwa Kugusa Hapa 

Soma Riwaya Nyingine Za Kijiweni Kwa KUGUSA HAPA

Wewe kama MFANYABIASHARA.. Kuna wakati unatamani kuwafikia watu wengi zaidi na hujui wapi pa kuanzia , USIJALI kwani hapa ndipo ambapo MTAA UNAONGEA na tuko tayari kukusaidia kuwafikia watu wengi kwa BEI YA OFA

Njoo Utangaze Nasi Sasa Kwa Kutuambia Una TANGAZO Gani na unataka kutangaza kwa muda gani kwa kutuma ujumbe hapa WwhatsApp Kupitia Namba +255760871896 

1 Comment

Leave A Reply

Exit mobile version