Ilipoishia Nzena (Kijiji Kilicholaaniwa) sehemu ya tano 

Waziri akajitupa kitini huku akifumba macho yake, hakujua atamweleza vipi Rais wa  Ganza, utajiri uliopotea kwenye Kijiji cha Nzena ni utajiri mwingi sana wa Madini. 

Mara mlango wa gari ulifunguliwa haraka sana, Waziri na Mshauri walishtuka. Mtu  mmoja kutoka kwenye timu yake alikuja ghafla na kumwambia kua kuna Mtu kutoka  Kijiji cha Nzena amepiga simu. Macho yalimtoka Waziri wa Maliasili, ingewezekanaje  kua simu itoke kuzimu? Alikua kama Mtu aliyezinduliwa kutoka usingizi wa Pono,  akatupa swali moja ngangari 

“Unasemaje?”  

SEHEMU YA SITA

“Ndio Mkuu, tumepokea simu sasa hivi kutoka Kijiji cha Nzena”  

“Ha! Ha! Hebu acha ndoto za Asubuhi, mmefikia wapi kwenye utafiti?” Aliuliza Waziri  akihisi huwenda Mtu huyo alikua akiingiza utani. Lakini alipoitazama sura ya huyo Mtu  aligundua msisitizo, akasikika tena akikazia

“Sio utani Mkuu, ni simu ya Mkazi wa Nzena” alisema, Waziri aliona jambo hilo lilikua  siyo la mzaha, akajisogeza kidogo karibu na huyo Mtu akamwuliza 

“Inawezekanaje?” 

“Mkuu hakuna anayejua, sababu simu nyingi zilipigwa kwa kufuata anuani, hakuna  simu iliyoita isipokua simu moja. Kisha simu hiyo ikapiga”  

“Hebu nieleze, alisema nini?” 

“Tulichokisikia ni kelele za kuomba msaada, anasema hakuna anayeweza kutoka wala  kuingia ndani ya Kijiji. Inaonesha kipo lakini ni ngumu kwa akili ya kawaida” alisema,  Waziri akamtazama mshauri wake na wote wakajikuta wakiyakubali maneno ya yule  Mganga kua Kijiji hicho kwasasa kinapokea laana ya kifo na Mauwaji ya Kutisha. 

Akashusha pumzi zake kisha akaongozana na mtoa taarifa hadi eneo ambalo Lina  mtambo wa kupiga na kupokea simu. Taarifa ile ikathibitishwa na wataalam wengine,  japo wengi wao hawakuwa na imani sana lakini iliwalazimu kukubali, simu hiyo  haikuonesha eneo ilipopigwa. 

Wakajaribu kupiga tena lakini simu hiyo haikupatikana. 

“Shit‼ hakikisha mnampata huyo Mtu na atoe taarifa ya Kijiji kipo wapi na nini  kinaendelea.” Alisema kwa msisitizo Waziri wa Maliasili kisha alirejea ndani ya gari. 

** 

Ndani ya Kijiji Cha Nzena. 

Zahoro alikua amerudisha fahamu, alikua amejiegemeza ukutani akiwa amekaa. Alikua  kwenye maumivu makali ya kichwa, mkononi alikua ameshikilia simu yake ndogo  akijaribu kupiga huku na kule.  

Chozi lilikua likimbubujika, mwili wa Baba yake Mzee Miroshi ulikua ukituama nzi.  Mara simu yake aliyokua akiipiga iliita na kupokelewa haraka sana, akababahika  kuongea. Akasikia sauti ikimuuliza 

“Upo Nzena?”  

“Ndiyo, tunakufaaa. Mtusaidie” alisema huku akiwa analia, upande wa pili ukamwambia 

“Usilie, hebu tueleze nini kinaendelea. Mko wapi, Unaongea na Waziri wa Maliasili  Majula Majula” ulisema Upande wa pili, simu ilipokelewa na kitengo cha Waziri walio  nje ya Kijiji wakiendelea kutafuta namna Kijiji hicho kilivyopotea. 

“Tupo Kijijini Nzena lakini hatuwezi kutoka. Watu wanakufa kwasababu ya Laana”  alisema, hapo hapo simu hiyo ilikatika. Aipojaribu Kupiga, simu haikuita. 

Alilia sana Zahoro, hakujua ni namna gani anaweza kuondoka Kijijini hapo, macho yake  yalikua yakishuhudia moshi Mkali uliokua ukifuka Kijijini hapo. Kelele ziliendelea  kupaa za kuomba msaada, lakini kichwani pake Zahoro alijua fika kua kuisikiliza sauti  ya Bibi Lugumi ndiyo sababu ya vifo vya Watu.

Akanyanyuka na kufikiria aingilie wapi ili aanze kuwaeleza Watu kua wazibe masikio  yao ili wawe hai.  

Taratibu Zahoro aliondoka nyumbani kwa Mzee Kova huku akimwacha Baba yake akiwa  amesha fariki. Chozi lilikua likimbubujika, alitembea akiwa ameziba masikio kwa  kutumia mikono yake. Maiti zilikua zimetapakaa Kila mahali alipokua akipita. 

Miguu yake isiyo na kiatu ilikua ikifanya safari isiyo na uhakika, uharibifu mkubwa  ilikua umetokea Kijijini, mifugo ilikua imekufa kama jinsi ambavyo Watu walikuwa  wamekufa. Kila mwili ulikua umetapakaa Damu 

Alipata kichefu chefu na kujihisi kama Mtu anayetaka kutapika, akajikuta akitapika  huku akipepesuka kama mlevi Hadi eneo la Migomba, akapiga magoti na kuendelea  kutapika huku akihisi nguvu ilikua imemwisha. 

Alipoinua kichwa chake ili anyanyuke alimwona Msichana mmoja wa miaka 17,  Msichana huyo alikua ametapakaa masizi usoni, alikua akimtazama Zahoro kwa hofu  sana huku akiwa anarudi nyuma taratibu akihitaji kukimbia. Zahoro akagundua haraka  kua Msichana huyo alikua akiogopa. 

Zahoro akamwambia yule Msichana kwa sauti ya utaratibu. 

“Usikimbie, Mimi siyo Mtu mbaya tafadhali” alisema huku akiwa amenyooshea mkono  mmoja na mwingine akiwa ameshikilia eneo la kifua ili kumwaminisha zaidi Msichana  huyo mrefu, aliyesuka mabutu lakini akiwa amevalia gauni lenye maua ya bluu.  Msichana huyo alisimama baada ya kusikia maneno ya Zahoro, macho yake Msichana  huyo hayakuonekana kama alikua akimfahamu Zahoro. 

“Mimi ni Muhanga kama wewe, Naitwa Zahoro” hatimaye akajitambulisha Zahoro huku  akinyanyuka na kusimama. Macho Yao yalikua yakitazama kimkakati sana, Bado  Msichana alihitaji uhakika zaidi kua Zahoro hakua Mtu mbaya. 

“Unaweza kuzungumza?” aliuliza Zahoro maana Msichana huyo aliyekauka mdomo  wake hakuufungua mdomo huo. Akaitikia kwa kutumia kichwa chake kua anaweza  kuzungumza. 

“Sura Yako ni ngeni, huonekani kama mkaazi wa Nzena” alisema Zahoro, yule Msichana  hatimaye akafungua mdomo wake huku chozi likimbubujika, midomo ilikua ikitetemeka 

“Ndiyo, Mimi nimetokea Mjini. Nilikuja kwa Shangazi yangu, sijui nipo wapi kwasasa  maana ni mgeni. Nimepotezana na Shangazi yangu” Chozi lilikua likimbubujika, sura  yake ilionesha maumivu ya kihisia ambayo Binti huyo alikua nayo.  

“Usijali, Bado upo Kijijini. Unasikia hebu sogea” alisema Zahoro huku akianza kusikia  sauti ya Bibi Lugumi, sauti ambayo inauwa. Akamwambia yule Msichana kwa haraka 

“Kamwe usiisikilize hiyo sauti, ziba masikio yako!” Zahoro alipaza sauti kwa nguvu.  Msichana huyo, akiwa amechanganyikiwa, akatizama huku na kule, macho yake yakiwa  na hofu iliyojaa machozi. Alilia kwa kwikwi, mwili wake ukitetemeka kwa hofu  isiyoelezeka.

“Ziba masikio, usiisikie!” Zahoro alipaza tena sauti, lakini bado msichana huyo  alizunguka kama mtu aliyekosa mwelekeo, kama aliyekuwa tayari ametekwa na sauti ya  Bi. Lugumi. Hatua chache tu zilimfanya kuwa karibu na Zahoro, aliposimama karibu  naye, bila kufikiria, Zahoro alimshika kwa nguvu na kumpiga kibao usoni. Msichana  huyo alishtuka, macho yake yakikosa mwelekeo wa awali. Wenge liliondoka taratibu. 

“Ziba masikio yako!” Zahoro alirudia kwa msisitizo. Msichana huyo alifanya kama  alivyosema. Sauti ya Bi. Lugumi ikapita, ikiambatana na kimbunga cha majani makavu  na vumbi lililopeperuka juu ya ardhi. Zahoro alisubiri kwa tahadhari hadi upepo huo  ulipopotea, akapumua kwa nguvu na kuondoa mikono masikioni mwake. Kisha,  akamshika msichana yule na kuondoa mikono yake pia. 

“Haya yote unayoyaona hapa kijijini ni matokeo ya laana ya miaka mingi,” Zahoro  alisema kwa sauti nzito, macho yake yakikagua mazingira yaliyojaa maiti na damu  iliyomwagika ovyo. 

Msichana huyo alishindwa kusema neno, mwili wake ukiwa dhaifu kwa hofu. Giza  lilianza kuingia, hewa ikawa nzito na baridi ikaanza kupenya. Zahoro alimshika mkono  na kumwongoza hadi kwenye nyumba ya karibu. Ndani, waliwasha kibatari kidogo na  kujikunyata kila mmoja pembezoni mwake kama makinda ya ndege yaliyoachwa na  mama yao. 

Kimya kilitawala. Wadudu wa usiku pekee ndio waliotoa sauti ya chinichini. Zahoro  alipumua kwa kina, akamtazama msichana huyo kwa mara ya kwanza kwa makini.  “Unaitwa nani?” aliuliza, sauti yake ikiwa na mshikamano wa uchovu na tahadhari. 

Msichana alinyanyua macho yake taratibu. Kivuli cha huzuni kilikuwa kimetanda usoni  pake. Alijua maisha yake yameingia katika giza lisilojulikana. Mtu pekee aliyekuwa naye  kwa sasa ni Zahoro. 

“Upendo,” alijibu kwa sauti ndogo, akipepesa macho yake. Tabasamu dhaifu, lisilo na  maana, liliganda usoni mwake kwa sekunde chache kabla halijazimika kabisa. 

Baridi ilikuwa kali. Zahoro alitazama kibatari, mwali wake ukitingishika kwa upepo  mdogo uliopenya kupitia nyufa za ukuta. “Maisha yetu kwa sasa ni mfano wa hiki  kibatari,” alisema kwa sauti ya mawazo. “Kosa dogo, mwanga unazimika, nasi  tunapotea.”

Alitulia kwa muda, kisha akaendelea kwa sauti iliyokuwa na maumivu mazito. “Kwenye  dunia hii ya ghafla, nimempoteza mtu aliyenipambania maisha yangu yote. Baba yangu  amekufa mbele ya macho yangu.” Machozi mepesi yakamtoka lakini alijifuta haraka. 

Moyo wa Upendo uliingiwa na baridi ya huzuni. Alimwonea huruma Zahoro kwa namna  isiyoelezeka. 

“Sijui hatma ya maisha yetu hapa, Upendo,” Zahoro alisema, sauti yake ikiwa nzito na  polepole. “Hakuna anayeweza kuingia wala kutoka kijijini.” 

Upendo aliinamisha kichwa chake, akavuta pumzi kwa tabu. “Kama hatuwezi kutoka  hapa, basi kwa nini tunapambana kuishi?” aliuliza kwa sauti ya kutapatapa, akimtazama  Zahoro kwa macho yenye ukungu wa machozi yaliyokuwa karibu kudondoka. 

“Kwasababu hatuwezi kufa kama kuku,” Zahoro alijibu kwa msisitizo. “Tunapokea laana  isiyo yetu. Hatuhusiki kwenye dhambi hii.” 

Kimya kikarejea. Upendo akajiegemeza kwenye kona ya chumba, mwili wake ukawa  dhaifu. Hatimaye, alifumba macho yake na kuanza kukoroma polepole kwa uchovu. 

Zahoro alimtazama kwa muda mrefu. Alipohakikisha amelala, alichukua kibatari na  kuingia chumba kingine kutafuta nguo ya kumfunika. Bahati nzuri, alipata nguo nzito  na akarudi kumfunika Upendo. Kisha, akajiegemeza kwenye kona yake, akifanya uamuzi  wa kukesha usiku huo. Kama sauti ya Bi. Lugumi ingerudi tena, alitaka kuhakikisha  kuwa angeweza kumwamsha na kumlinda Upendo kwa gharama yoyote. 

** 

Uchovu ulimwelemea bila kujua, macho yake yakafumba taratibu, na usingizi mzito  ukamchukua. Ndoto ikaanza kumvaa kwa kasi, dunia ya giza na maangamizi ikajitokeza  akilini mwake. 

Alijiona akitembea katikati ya kijiji, lakini hakikuwa kile alichokijua. Kila nyumba  ilikuwa imejaa damu, miili ya watu waliokatwa vipande ikining’inia kwenye kuta, macho  yao yakiwa wazi bila uhai. Kilio cha maumivu kilisikika mbali, lakini hakukuwa na  aliyebaki kuweza kusaidia. 

Ghafla, akajikuta ameshika kisu, mikono yake ikiwa imelowa damu. Aliangalia chini— Upendo alikuwa amelala mbele yake, kifua chake kikiwa kimechomwa na kile kisu. 

Macho yake yalikuwa wazi, yakimkodolea kwa masikitiko na hofu. Alitaka kupiga kelele,  lakini sauti haikutoka. 

Sauti nzito, yenye mwangwi, ilianza kuzunguka kichwani mwake, sauti ya Bi. Lugumi.  “Huwezi kuukwepa ukweli, Zahoro… Laana ni yako sasa.” 

Nini Kitaendelea? Usikose SEHEMU YA TATU Hapa Hapa Kijiweni

JIUNGE NA KIJIWENI WHATSAPP CHANNEL Kwa Kugusa Hapa 

Soma Riwaya Nyingine Za Kijiweni Kwa KUGUSA HAPA

Wewe kama MFANYABIASHARA.. Kuna wakati unatamani kuwafikia watu wengi zaidi na hujui wapi pa kuanzia , USIJALI kwani hapa ndipo ambapo MTAA UNAONGEA na tuko tayari kukusaidia kuwafikia watu wengi kwa BEI YA OFA

Njoo Utangaze Nasi Sasa Kwa Kutuambia Una TANGAZO Gani na unataka kutangaza kwa muda gani kwa kutuma ujumbe hapa WwhatsApp Kupitia Namba +255760871896 

10 Comments

Leave A Reply

Exit mobile version