Ilipoishia Nyumba Juu Ya Kaburi 09

Basi nilikata tamaa, chozi lilinibubujika. Nikajikuta nikipandwa na hasira sana, nikasema kwa  mara ya mwisho kwa sauti kubwa ya hasira huku chozi likinibubujika 

“Fungukaaa‼!” ghafla tu nililiona lile shimo la ajabu likifunguka nyuma yangu, palikua panatoa  mvuke na joto kwa mbali, rangi nyekundu ilikua imelizunguka shimo lile, nilichungulia ndani ya  shimo maana sikuwahi kuingia hivyo nilikua sijui chochote kile hata kunaonekanaje nilikua sijui. 

Nilitumia muda mrefu nikiliangalia tu, kisha niliisikia sauti nzito ikiuliza kutoka ndani ya shimo. Endelea

SEHEMU YA KUMI

“Kwanini umenifungua?” nilishtuka nusura nikimbie, shimo lilikua likiongea. Nilijiuliza nijibu  nini, Nani ananiuliza ni shimo au yule jini. Nilimeza funda zito la mate huku vipele vidogo  vidogo vya hofu vikianza kunitoka.

“Mimi….mi-mimi naaa…” nilibabaika sana nikiwa napepesa macho yangu, kila nilochofikiria  kukisema niliona kama nitakosea, niliendelea kubabaika. Cha ajabu niliulizwa tena kwa kutajwa  kabisa jina langu 

“Kwanini umenifungua Celin?” hapa nilishindwa hata kujizuia nilionesha ni namna gani mimi  nilikua mwoga, nilishtuka kiasi kwamba hata mate yaligoma kupita kooni, kifua changu kilijaa  upepo huku miguu yangu ikiwa inatetemeka. Nguvu ziliniisha kabisa. 

Nilihema kuliko kawaida, kisha lile shimo lilijifunga likatoweka baada ya Mimi kukaa kimya.  Nilishikilia moyo wangu, nilijikuta nikikaa chini taratibu huku nikiendelea kuhema. Nilimeza  funda kubwa la mate kisha nikajiuliza 

“Nilipaswa kuingia au kujibu?” Nilikohoa mara moja kisha niliutazama ule ukuta ambao  ulifanya lile pango la ajabu likafunguka. Nilimkumbuka Mama yangu, Baba, Caren na Zena,  wote walikua wahanga wa hii nyumba ya ajabu yenye kaburi. Niliingiwa na shahuku ya  kumaliza tatizo kabisa, basi nikasema tena kwa Ujasiri sana 

“Fungukaaa‼” Nilisema kwa nguvu hadi vipele vya msisimko vilinitoka. 

Safari hii sauti yangu moja tu ilifanya lile shimo lifunguke, sikushtuka kama ilivyokua mara ya  kwanza. Niligeuka na kulitazama, nilimwomba Mungu maana nilihitaji kushuka chini ndani ya  lile kaburi la ajabu ili niipate nafsi ya Sabra. 

Nilitembea taribu hatua kama tatu hivi kisha nilifika mbele ya shimo, nikachungulia lakini  hakuna nilichoambulia ambacho kingenipa uelekeo sahihi. Sikuitaka ile sauti iniulize ninataka  nini, tayari moyo na akili yangu vilijua nahitaji nini zaidi. 

Niliingiza mguu mmoja kisha nikaingiza mwingine, ndani yake palikua na harufu kali ya udi.  Niliuzamisha mwili mzima, ghafla tu nikajikuta ndani ya shimo lenye giza la kutosha, tofauti na  mwanzo nilipoona mwanga ndani ya shimo lakini palikua giza kabisa. Hakuna nilichokiona  mbele wala nyuma yangu, giza nene lilikua limelifunika shimo lote. 

Nilisimama huku nikiangaza kama naweza kuona eneo la kutokea lakini haikua hivyo,  nilijiingiza shimoni bila kujua nawezaje kutoka. Palikua kimya sana, udi uliendelea kunukia,  nilisimama nisijuwe naelekea wapi. Mara nilisikia sauti ya yule Bibi Kizee, alikua akiimba  nyimbo zake nisizo zielewa.

Niliingiwa na hofu lakini niligundua kama vile alikua na pirika zake, kivumbi kilikua ni namna  ya kuyafanya macho yangu yaone angalau nipate pa kuanzia, nilimsikia tena akitafuna huku  akitoa miguno ya kufurahia alichokua anakula, vishindo vya kucheza pia nilivisikia. 

Sauti yake haikua karibu sana na Mimi, nilichagua kupapasa kwa kutumia mkono wangu wa  kushoto ambao ndio nilikua nautumia sana, niliendelea kupapasa huku nikipiga hatua fulani  ndogo ndogo za kuvizia. Kadiri nilivyozidi kwenda mbele nilianza kuhisi mwanga kidogo,  nikapepesa macho yangu halafu nikaendelea mbele taratibu sana.  

Sikutegemea kama kule chini kulikua na nafasi kubwa kiasi kile, niliweza kupiga hatua za  kutosha kuifuata ile sauti ya yule jini, hapakua pa kawaida kabisa maana kadili nilivyosonga  nilihisi kuna vitu vinaota kwenye mwili wangu mithiri ya manyoya hivi. Nilisisimka sana, hofu  iliendelea kunisumbua lakini sikutaka kukoma nilijiambia kama kufa ni bora nife kuliko  kushuhudia Wazazi wangu wakiwa wameharibikiwa. 

Niliendelea kutembea huku ile hali ya kuota manyoya ikizidi kuendelea hadi nilianza kuhisi  nimekua kiumbe cha ajabu sana, ule mwanga ulizidi kujaa machoni pangu kiasi kwamba nilianza  sasa kupata nuru ya kuona mbele. Nilichokua nakiona kilizidi kunitia hofu, palikua na mafuvu  mengi chini, panya walikuwa wakiingia kwenye mafuvu na kutoka. Sikutaka hofu iendelee  kunitawala maana nilijua kama hofu itanitawala basi sitaweza kukamilisha kazi ya kuipata nafsi  ya Sabra. 

Pole pole, nilianza sasa kuisikia ile sauti ya Mwanamke anayeimba. Safari hii niliisikia kwa  ukaribu zaidi, ilionekana ilitoka eneo ambalo niliisikia sauti ya yule jini, niliendelea kusonga  taratibu nikiwa makini sana. Sikutaka hata kujiangalia maana nilijua nikifanya hivyo nitajiogopa  kwa jinsi ambavyo mwili wangu ulikua umeota manyoya madogo madogo.  

Nilifika sehemu moja, palikua na mlango ambao ulikua haujafungwa vizuri, upenyo mdogo  uliobakia ndio uliokua ukinipa nuru. Ndani palionekana kua na taa kali sana, sauti ya kuimba na  sauti ya kutafuna vilikua vinaendelea kusikika. Nilisimama kidogo kabla ya kufanya uamuzi wa  kuchungulia ndani

Nilimwona Mwanamke mmoja aliyevalia gauni jekundu, alikua amekaa chini akiimba huku  chozi likimtoka. Alikua anatoa chozi la damu machoni mwake, kwa haraka haraka nilitafsri kua  huwenda alikua akimwimbia huyu Jini Bibi Kizee, nilitaka kuona ni nani aliyekua mbele yake.  

Niliuingiza mwili wangu nusu ndani ya kile chumba, nikafanikiwa kumwona yule Bibi kizee  akiwa kwenye umbo la kawaida kabisa kama lile analonitokeaga nalo, alikua akifurahia nyama  aliyoishikilia mkononi lakini pia alikua akicheza cheza ikionesha namna ambavyo ile nyimbo  ilikua ikimburudisha. 

Ndipo nilipo yaaminu maneno ya yule Mwanaume kua ndani ya nyumba yetu palikua na kaburi  ambalo alizikwa yeye pamoja na Dada yake, haitoshi niliamini kua Dada yake Sabra alikua  akitumikishwa na jini huyo ndiyo maana alikua akiimba huku akiwa analia. Ndani palikua na  mwanga mkali kiasi kwamba hata sisimizi angeweza kuonekana kirahisi sana. Kiumbe chochote  ambacho kingeingia ndani ya chumba kingeonekana haraka sana. 

Sabra alikua akiimba huku akionesha kama vile alihisi mlangoni palikua na Mtu, shingo na  macho yake vilikua mlangoni mara kwa mara huku akiendelea kuimba na kumburudisha yule  Bibi kizee.  

Mara nyingi alikua akipepesa macho yake yaliyokua yakitiririsha chozi, alikua akiniangalia kisha  akimwangalia Bibi Kizee, sura yake ilionesha mateso makali aliyokua akiyapitia, alikosa nuru  kabisa. Lakini alionesha kunishangaa maana ilikua ndiyo mara ya kwanza Mimi na yeye  tunaonana halafu isitoshe pale chini palikua ni eneo hatari sana kwa Binadamu wa kawaida kama  Mimi. 

Nilikua na uhakika kabisa kua ndiye ninayepaswa kuondoka naye ili akakutane na Kaka yake  waunganishe nguvu zao kwa ajili ya kumwangamiza Bibi Kizee. Wakati naendelea kufikiria nini  cha kufanya nilimsikia Bibi Kizee akisema 

“Inatosha” alisema kwa sauti kavu iliyojaa amri, kisha naye aliacha kula alichokua anakula.  Akavuta harufu kwa kutumia pua yake ndefu kama vile alihisi uwepo wa Binadamu. 

Alianza kuimba yeye kwa kuguna guna huku akitikisa kichwa chake, halafu akaweka mikono  yake mgongoni mwake akaanza mwendo wa kuja mlangoni, Sabra akanipa ishara kwa kutikisa 

kichwa chake, papo hapo nikajua napaswa kufanya nini. Nikarudi nyuma haraka haraka halafu  nikabana sehemu. 

Ni hatua chache tu kutoka mlangoni, alipofika nje aligeuka alipotoka kisha akasema  

“Fungaaa‼” Mara moja ule mlango ukafunga kisha akaondoka zake, sikutaka kutingisha hata  pumzi zangu, nilizibana vizuri sana hadi pale nilipomsikia akisema Fungukaa akiliamlisha lile  shimo nikajua alikua anaondoka. 

Basi haraka nikafika pale mlangoni, japo palikua na giza la kutosha lakini hisia zangu  ziliniongoza vyema hadi nilipofika mlangoni. Mlango ulikua umefungwa, nilipapasa huku  nikiusukuma kuona labda utaweza kufunguka. Nilijaribu mara kadhaa bila mafanikio hatimaye  niliona ni bora nimwite kwa jina lake 

“Sabra” nilimwita nikiwa nategemea pengine angesogea mlangoni na kunipa msaada wa  kuufungua. 

“Wewe ni Nani?” Niliisikia hii sauti ya kike ya Sabra, ilitoka kwa upole sana. Ilijaa mshangao  mkubwa wa kuona Binadamu akiwa ndani ya lile kaburi.  

“Mimi ni Celin, Kaka yako amenituma” nilimjibu. Pakawa kimya sana, wastani wa dakika moja  hivi nikamsikia tena 

“Kaka yangu? Wewe ni Nani hasa na umewezaje kufika huku?” Aliniuliza, nilikua na uhakika  wa jambo moja, alikua amepoteza tumaini, alishaamini kua nafsi yake ingekua utumwani daima.  Hakutegemea kusikia kua kaka yake bado anamhagaikia. 

“Haji?” Aliuliza kwa Mshangao zaidi. 

“Ndiyo, ni yeye. Amenituma kukutoa ndani ya kaburi. Kwa pamoja mtaweza kumuangamiza  huyu jini ambaye amekua akifanya mauwaji kila uchwao tena kwa Watu wasio na hatia,  nimepoteza Wazazi wangu kwasababu yake” niligongelea msumari wa mwisho 

Alikaa kimya kwa sekunde kadhaa kisha akasema.

“Sijui kama itawezekana, nimedhohofika vya kutosha. Sijioni nikiwa nina nguvu” alisema, sauti  yake ilibadilika kidogo. Aliongea kwa huzuni. Chozi lilikaribia kunitoka, maneno yake yalijaa  hatma isiyo na matumaini. 

“Haijalishi Sabra, ni lazima utoke humu ili ukaungane na Kaka yako kwenye Maisha mengine.  Hauwezi kua Mtumwa Daima” nilijikuta nikianza kumshawishi niondoke naye japo nilikua sijui  uhatari mkubwa uliopo mbele yangu.  

“Celin, upo sehemu iliyojaa hatari kubwa sana. Hiki kiumbe kina nguvu za ajabu sana sijui kama  unaweza ukatoka ukiwa hai”  

“Haijalishi Sabra,nikifa kwenye mapambano itakua haki yangu kuliko kuishi kwa furaha  iliyokandamizwa na upweke na mateso. Natafuta haki ya kifo cha Mama yangu pamoja na haki  ya Baba yangu” nilisema kwa Ujasiri, kiukweli nilikua nimefika mwisho wa hofu yangu.  

“Sawa, fungua unitoe” alisema, nilikumbuka namna yule Bibi Kizee alivyoufunga huu mlango  kwa kusema tu Funga. Nikakumbuka namna hata lile shimo la ajabu linavyofunguka kwa  kuliamrisha, basi nikajiweka sawa ili niseme 

“Fungukaaa‼” Nilisema kwa ujasiri na Mamlaka makubwa sana, mara mlango ulifunguka.  Ndani palikua pana nuru ya ajabu inayowaka na kufanya pawe na Mwanga mkali. Palijaa  mafuvu ya vichwa vya Watu, macho yangu yalikutana na macho ya Sabra. Alichokua amekisema  ndicho nilichokiona kwenye sura yake, alikua amechoka na kukata tamaa. 

“Twende Sabra” nilisema kisha nilimpa mkono, aliutazama sana Mkono wangu kwa sekunde  chache za kuhesabu. Hakunipatia mkono wake, sikujali nilichotaka ni kuondoka naye. Basi  tuliongozana akiwa anatembea kwa kuchoka choka hivi. 

Hakutaka nimguse kabisa, hata alipoonekana kua amechoka anaelekea kuanguka, tulisogea  taratibu na alikua akizijua njia za mule ndani ya lile kaburi kubwa la ajabu, akawa ananiambia  kila kitu kinachohusiana na njia za mule kwa kila hatua ambayo tuliipiga. 

Alikua anajua kila kitu hata lilipo lile shimo la kutokea ndani ya lile kaburi, kuna namna  nilijiuliza maswali mengi inawezekanaje Mtu anayejua pa kutokea na asitoroke siku zote hizo? 

Nilipotezea suala hili, nikaweka nguvu zaidi kuhakikisha tunaondoka tukiwa salama kabisa.  Akaniambia 

“Natamani sana kumwona Kaka yangu, ni muda mrefu nimeishi nikiwa mpweke” alisema  maneno yaliyonigusa moja kwa moja. 

Nilitabasamu kidogo maana aliongea maneno yaliyojaa tumaini na kiu ndani yake, binafsi  sikujua tunawezaje kutoka maana ndani ya kaburi ni udongo, hakuna simenti hivyo hata mahali  pa kutokea sikupajua. 

Akapaza sauti akasema 

“Fungukaa‼” Haikuchukua hata sekunde nyingi, shimo likajitengeneza. Mwanga wa chumba cha  stoo ukaonekana. Nikageuka kumtazama, nilikua na swali la kumuuliza lakini niliona ni bora  tukitoka nimuulize. Tukafanikiwa kutoka salama ndani ya lile shimo, tukawa tumefika stoo.  Kumtoa Sabra ndani ya lile Kaburi ilikua rahisi kuliko hata kaka yake alivyoniambia kitu  ambacho kilinipa maswali mengi yasiyo na majibu.  

Mara lile shimo likatoweka. Alikua anahema sana kama Mtu aliyechoka, alikua amedhohofu  mno hadi nilimwonea huruma ila nilimuuliza 

“Kwanini haukutoka siku zote hizo ikiwa unajua kila kitu?”  

Nilikua na kiu sana ya kutaka kujua, alinitazama akanijibu haraka 

“Kila jambo na wakati wake Celin” lilikua ni jibu fupi jepesi ambalo halikua chakula kizuri cha  fikra zangu. Akanitazama kisha akaniuliza 

“Umevaa nini mkononi?” Swali lake lilinishtua kidogo na kuanza kunipa hofu maana kule chini  alikataa kabisa kumgusa. Nilijiuliza kwanini alikataa ikiwa yeye ni nafsi salama kama ya Kaka  yake ambaye ndiye aliyenipatia ile shanga. 

Nilimeza funda la mate, nikatabasamu kidogo nikampa jibu bila kusema Uwongo 

“Huu ni ulinzi amenipatia Kaka yako, ni kinga dhidi ya yule jini” nilimjibu, nilimwona  akitafakari jambo halafu mdomo wake ukawa mzito kama vile alitaka kusema jambo alafu  akaghaili.

“Twende anaweza kutukuta hapa” akasema kisha nikaongoza mbele maana mimi ndiye  ninayejua nini cha kufanya. Nilikua tayari nimempata Sabra ila sikujua ni namna gani nitaweza  kumpata Kaka yake ili waunganishe nguvu zao na kupambana na kile kiumbe.  

Tulitoka ndani hadi nje kabisa ya nyumba, palikua kimya lakini hali ya kusisimka mwili ilikua  ikinianza. Hisia hii iliniambia kua lile jini lilikua karibu na Mimi, nilihisi kuchanganikiwa maana  tayari nilikua nimefanikiwa kumtoa Sabra mle kaburini hivyo kama atatukuta basi ataniuwa.  

Barabara ilikua tupu, sikujua nifanye nini lakini kwa haraka haraka nilifikiria niondoke na Sabra kutoka pale kwenda mbali kidogo mahali ambapo yule Kaka yake angeliweza kututokea  nikamkabidhi mdogo wake. 

Tulitembea taratibu tukiiacha nyumba yetu nyuma, sikutaka tuelekee upande ule wa nyumba  jirani ya yule Mzee, tulisonga mbele kwa hatua nyingi za kutosha, hadi tulipofika mbali kiasi  chake. Tulisimama, palikua kimya hakuna mazungumzo, niliangaza huku na kule kuona  huwenda angetokea lakini alikua kimya 

“Yupo wapi Haji?” Aliniuliza, sikua na jibu la moja kwa moja la kumpa maana Haji sikujua  nawezaje kumwita akatokea maana alikua kama Mzimu fulani hivi wa ajabu ambao ungeweza  kutokea popote pale. Mahali tulipokua tumesimama palikua na miti mikubwa miwili, mmoja  ulikua upande wa pili na mwingine ni upande tuliokua tumesimama Mimi na Sabra. 

Tulisimama kwa dakika kama tano hivi nikiwa sielewi nafanya nini, kwakua Haji ni nafsi basi  atakua ametuona lakini kwanini hatokei kumchukua Dada yake? Nilijiuliza swali hili nikiwa sina  jibu la moja kwa moja. Niliangaza huku na kule bila mafanikio, nikakata tamaa bila kujua  nitaenda wapi na Sabra. 

Alikua akiniuliza mara kwa mara mahali alipo Kaka yake, hata pale nilipompa mgongo  nilipogeuka alikua akinitazama sana lakini alikua hataki nimguse kabisa kitu ambacho kilikua  kinanishangaza kila dakika. Mara nilianza kuhisi kama vile nilikua napigwa na vitu mgongoni  mwangu, sikutaka kugeuka moja kwa moja. Hapo mwili ulikua unazidi kusisimka sana.

Akili yangu iliwaza mara moja kua pengine yule Bibi Kizee alikua ndiye anayenipiga na vitu  mithiri ya vidude vidogo vidogo ambavyo haviumizi lakini baadaye akili yangu ikanambia  huwenda nilipaswa kugeuka taratibu ili nijuwe ni Nani aliyekua akinishtua kwa nyuma na  kwanini alifanya kua siri. 

Niligeuza shingo kitaalam sana sidhani hata kama Sabra aliweza kung’amua, nilifanya kama  nageuka hivi. Ndipo nilipomwona Haji Kaka yake Sabra, akanipa ishara ya kunitaka nikae  kimya. 

Sikujua ni kwanini alitaka nikae kimya, nikawa nazugazuga kama naangalia huku na kule  kumtafuta Kaka yake Sabra, nikawa naendelea na ule mchezo, nageuka kwa siri siri. Baadaye  akawa ananiambia kwa ishara akimaanisha kua niliyekua nimesimama naye alikua siyo Dada  yake Sabra. Jicho lilinitoka, msisimko ulizidi kuongezeka, mwili ulikosa nguvu ghafla  nikatamani nipate mahali nikae. 

Sasa nikawa naunganisha mambo kadhaa na moja wapo ni kitendo cha kukataa nisimguse, hapo  nikapata picha halisi sasa kua niliyetoka naye kaburini kwa kufikiria ni Sabra alikua ni yule Bibi  Kizee aliyejivika sura ya Sabra. Nilimeza funza zito la mate huku macho yakiwa yamenitoka,  japo nilijawa na hofu lakini sikutaka kumpa mwanya wa kugundua kua nimemshtukia. 

“Huyo Haji anakuja saa ngapi jamani, siwezi kusubiria kumwona maana niliamini siwezi  kumwona tena” alisema Bibi kizee mwenye sura ya sabra, nilimtazama nikaachia katabasamu  nikamwambia 

“Atakuja muda sio mrefu, mimi sijui namna ya kumwita” 

“Oooh‼”  

Bado alikua akinikwepa, alikua hataki nimguse hata kwa bahati mbaya, alikua anapiga hatua za  kunikwepa. Nilishajua hawezi kunidhuru kwasababu ya ule ushanga niliopewa na Haji. Sikujua  nini Haji angefanya maana Bi Kizee alikua makini kunitazama kila hatua ninayoipiga, nilielewa  lengo lake lilikua ni kupiga ndege wawili kwa jiwe moja.

Bado Haji alikua akinipa ishara za siri nigeuke, pengine alikua na mpango fulani ila sasa Bibi  Kizee alikua hanipi huo muda, alikua makini zaidi na Mimi. Nilijaribu kugeuza jicho la kuiba  lakini sikufanikiwa kumfikia Haji, ikabidi nimwambie Bibi Kizee 

“Ninahisi Mkojo, nahitaji kujisaidia” nilimwambia nikiwa nina mtazama, nilihitaji nafasi  muhimu zaidi kupata wazo la Haji maana aliyekua mbele yangu alikua siyo Sabra bali ni Jini. 

“Haina shida, Mimi nitasimama hapa kumsubiria Haji. Usikawie” alinijibu, nilihisi nilikua  nimeukaribia ushindi. Nyuma yangu palikua na pori dogo lenye mti mkubwa ambao Haji alikua  amejificha, nikajifanya kuangaza huku na kule kisha nikakimbilia pori dogo ambalo ningekutana  na Haji. 

Lakini wakati natoka nililiona tabasamu la Bi Kizee, nikajua sasa huwenda amejua kua nilikua  nimemshtukia. Nilipofika nyuma ya ule Mti nilimkuta Haji, upepo ulikua ukivuma kiasi kwamba  maua yalikua yakituangukia. Haji aliniambia haraka haraka 

“Yule Bibi amejua kua umejua, anaweza akaucheza mchezo lakini hawezi kushinda. Chukua hii  kamba, hakikisha unamfunga popote kwenye mwili wake” alinipa kamba ndogo nyekundu kama  zile wanazovaa wahindi mkononi. 

Akanipa ishara ya kuondoka, kweli niliondoka pale na kurudi barabarani. Nilipofika nilikuta  peupe. Yule Bibi Kizee hakuwepo pale barabarani, niliangaza huku na kule pengine ningemwona. 

Macho yangu yalikua kodo kila mahali, nilihesabu idadi ya gari zinazopita bila mafanikio.  Hatimaye nilipogeuza shingo yangu nilimwona akija akitokea upande wa pili wa barabara.  Maswali hayakuniisha sababu nilikua sina uhakika kama alikua amegundua jambo au laa. Ila  moyo wangu ulinieleza mengi juu yake, nilihisi aligundua jambo kama alivyonieleza Haji.  Nilipaswa kua muigizaji nguli japo yeye ana nguvu za kutambua mambo kwa haraka kutokana  na uwezo wake wa Kijini. 

Alipofika nilipo, nilimtazama usoni pake. Alikua na haya fulani iliyoficha jambo. “Bado hujaonana naye?” 

“Nani?” 

“Ulisema Haji!” 

“Aaah ndiyo, samahani hiki kichwa kinafikiria sana.” Nilisema huku nikifikiria zaidi namna ya  kumfunga kamba yule jini, niliishikilia ile kamba kwa nguvu mkononi nikiwa nimeificha vizuri. 

“Mimi nafikiria turudi kule ndani, pengine anaweza kuja kule. Kumsubiria hapa ni kama  tunapoteza muda” alisema, machale yalinicheza kua alikua na lengo la kuniingiza mtegoni. 

“Aaah‼ Alisema hawezi kuingia mle sababu anamwogopa yule Jini, Mimi naona angalau tuketi  chini ya ule Mti kwa kitambo fulani. Huwenda anaweza kuja” naye aligeuka kuutazama mti huo,  ulikua Mti mkubwa uliomea vizuri kijani cha kutosha na matawi makubwa yaliyopeba majani  mapana. Alinitazama kisha akajibu 

“Hakuna shida, kama tunaweza kufanya hivyo. “ Nilisubiria atangulie mbele ili nimfunge ile  kamba haraka, kweli aliongoza mbele nami nikawa nyuma ya mgongo wake. Alikua mwingi wa  mazungumzo yasiyo isha, ndani yake alionesha alikua akimtaka sana Haji sababu nilishampa siri  pasipo kujua kua yeye ni jini, ile siri ya nafsi mbili kuungana na kummaliza yeye. 

Alikua akiutupa sana mkono wake wa kulia, alikua akitembea kwa kujiachia achia kama siyo  yule aliyedhohofika. Macho yangu yalikuwa hayatulii, mapigo ya moyo yalinienda mbio. Kila  hatua niliyoipiga ilikua ikitoa sauti ya kunikumbusha wajibu wangu wa kumfunga ile kamba  lakini nilijawa na hofu sana. 

Hadi tunafika chini ya Mti sikuweza kumfunga. Tulipokaa chini akaniuliza 

“Umekunja ngumi muda wote huumii?” Aliniuliza huku akiutazama mkono wangu wa kulia  ambao niliishikilia ile kamba, nilitabasamu kuondoa ngoma juani. Nilikua nawaza mambo  mawili 

Pale Mtini ni mahali nilipomwacha Haji, vipi kama atamwona? Swali la pili nilijiuliza nitamjibu  nini? 

“Aaah‼ Nimezoea siwezi kuumia, wala usihofu” Nilipomjibu hakusema chochote, alipeleka  macho yake barabarani. Kumfunga ile kamba ilikua kazi ngumu sana, aliketi hatua moja kutoka  kwangu pia alikua akigutuka mara kwa mara na kunitazama kama Mtu aliyejiandaa zaidi, hii  ilinipa hofu sana.

Hakuruhusu nimsogelee sababu hakutaka kugusana nami akihofia kupata madhara sababu ya ule  Ushanga wa ulinzi niliopewa na Haji. Kimya kilitawala, hisia ilizidi kuniambia kua atanigeuka  endapo nitaonesha dalili zote kua nimegundua siri yake. 

Kuna nyakati alinitazama kama vile alikua anataka kuniambia amegundua kila kitu lakini  nilimkatisha kwa kuzungumza, sauti za magari zilikua zikisikika kwa kuvuma.  

“Una hakika Haji atakuja?” Akaniuliza, alijawa na shahuku sana sababu aliona muda ulikua  ukienda.  

“Naamini hilo litafanyika, cha msingi ni kuendelea kusubiria”  

“Tutasubiria hadi saa ngapi Celin?” 

“Sijui lakini hakuna kitakacho haribika, cha muhimu ni kwamba nimekutoa kwenye mateso ya  yule jini mshenzi” nilisema kwa kujikaza ili angalau kumwaminisha kua hakuna kilichojulikana  kuhusu yeye. Alitoa tabasamu tu wala hakusema neno lingine 

Muda ulivyozidi kwenda nilianza kuingiwa na hofu sana, maana alinionesha dalili kua  angenidhuru. Kuna muda akawa anazungusha sana macho yake kisha akasimama nikamuuliza 

“Kuna nini?” Nilimuuliza nikiwa nimesimama pia, alinitazama tu kisha aliketi bila kusema  chochote kile. Aliufanya moyo wangu udunde sana, hofu ilizidi kuongezeka. Mwili ulikua  ukisisimka sana. 

Alikua kama mbwa, alikua akinusa harufu sana. Akapiga hatua kama mbili hivi, akawa  amesimama mbele yangu akiwa amenipa mgongo. Harufu ya kifo ilianza kukita pua zangu,  damu yangu ilizunguka haraka, mapigo ya moyo yalizidi kuongezeka. 

Silaha pekee niliyonayo ilikua ni ile kamba nyekundu niliyopewa na Haji, sikujua baada ya  kumfunga kingetokea nini lakini nilipaswa kuamini kua ilikua ni silaha muhimu sana, niliona  wazi kua alikua akihangaika kunusa jambo, nikaukunjua mkono wangu. Kiganjani nilikua na ile  kamba, safari hii nilijiambia 

“Liwalo na liwe, ni kheri nife kuliko kuuishi Uwoga” 

Nilivuta pumzi zangu katika hali ya kujiandaa, nilijiapiza kisha nilifanya uamuzi wa kumfuata  kwa kasi kisha nikaushika mkono wake, kitendo cha kumshika alibadilika na kua Kiumbe  chenye sura mbaya iliyoungua. Macho yalimtoka kisha alipiga ukunga kama tembo anayemtafuta Mtoto wake. Sikujali sababu hakuna nisichokiona kutoka kwake, nilimfunga ile  kamba halafu nikasogea pembeni 

Akabadilika kabisa kutoka kwenye sura ya Sabra hadi kua Bibi Kizee mwenye sura mbaya sana.  Kitendo cha kumwacha kilimfanya aache kupiga ukunga, aliuinua mkono wake kisha akaiangalie  ile kamba halafu akaniambia 

“Hii vita haitakuja kufika mwisho Celin, kama unafikiria utashinda basi ndiyo kwanza vita hii  imeanza” alikua akisema huku akinifuata, nilikua ninarudi nyuma nyuma lakini kadili alivyokua  akinifuata niliona alikua akibadilika viungo vyake na kua sanamu kavu la kufinyangwa. 

Akawa ameganda akiwa anapiga hatua kuja nilipo kisha akaniambia 

“Siku nikiwa huru Dunia yako itapiga yowe Celin, hakuna Mtu atakusaidia” kisha alipomaliza  aliganda kila kiungo chake na kua sanamu. Nilichoka kwa hofu nikajikuta nikianguka na kukaa  chini. Chozi lilikua likitoka, sanamu lake lilikua hapo mbele yangu 

Mara alikuja Haji, alinitazama huku chozi likiwa linambubujika. Akaniambia “Ni muda wa kumkomboa Sabra, twende kwenu”  

“Vipi kuhusu hilo sanamu?” 

“Utalivunja kisha utatenganisha udongo wake, udongo mwingine uchome moto kisha mwingine  utupe Baharini, hawezi kamwe kurudi Duniani” alisema Haji, sikutaka kumwambia alichokisema  Bibi Kizee 

Basi, kwa uwezo wake wa kimiujiza tulitoweka pale pamoja na lile sanamu. Tukajikuta ndani ya  nyumba yetu. Kila kitu kilibadilika kuanzia hewa na hata mimea ilionekana kua na nuru  kuashiria ukombozi. Tulipofika kwenye korido tuliiacha sanamu kisha tuliingia stoo pamoja,  kitendo cha kuingia tu shimo lilijitengeneza kisha lilituuliza 

“Mnataka niwafayie nini?” Tulitazamana halafu Haji akasema

“Tunamtaka Sabra kutoka kwako” pakawa kimya kisha ikaja harufu kali ya marashi, Sabra akatoka ndani ya lile shimo, alipomwona Kaka yake alimfuata na kumkumbatia kwa nguvu.  Ilinifanya nitabasamu 

“Celin, asante kwa msaada na ujasiri ulionao. Nimempata Sabr, tunakutakia Maisha Mema  rafiki” alisema Haji kisha walitoweka sikujua hata walielekea wapi, lile shimo liliniuliza 

“Unataka nifanye nini tena?” Nikalitazama kisha nikasema 

“Funga na usifunguke Daima Milele, usiwe njia ya kufika chini” baada ya kusema lile shimo  lilitoweka kabisa, nikatoka stoo kisha nikaenda kwenye korido, nikalichukua sanamu kisha  nikaenda nalo nje 

Nikalivunja vunja, nikatemganisha udongo kisha nikauchoma moto. Mwingine nikaenda kuutupa  Baharini, nikawa nimemaliza kazi nzito ya kuliangamiza lile jini, nikaenda Gerezani kumueleza  Baba yangu. Alifurahi kisha akaniambia 

“Mama yako atakua amepumzika salama, hata Mimi sina wasiwasi na adhabu yangu sasa. Nenda  ukatimize ndoto zako za kua Msanifu Celin” alisema Baba, tokea siku hii nilianza Maisha mapya  ndani ya nyumba yetu, palijaa tumaini, amani ya kutosha. Sikusikia mauzauza wala Mazonge ya  aina yoyote ile, kilichobakia ni kutimiza ndoto ya kua Msanifu. 

Nataka kuwashuri mnaonunua Nyumba au viwanja kua makini sana sababu nyumba zingine zina  maagano mabaya ya kichawi, viwanja vingine ni makaburi ya zamani. Nyumba nyingi zipo juu ya  Makaburi. 

MWISHO 

MNATAKA SIMULIZI IJAYO IWE YA NAMNA GANI? MAPENZI AU UJASUSI? COMMENTS ZIWE NYINGI SASA NIIACHIE MAPEMA MAANA KAKA MKUBWA AMEREJEA NA SIMULIZI ZA KUTOSHA

JIUNGE NA KIJIWENI WHATSAPP CHANNEL Kwa Kugusa Hapa 

Soma Riwaya Nyingine Za Kijiweni Kwa KUGUSA HAPA

Wewe kama MFANYABIASHARA.. Kuna wakati unatamani kuwafikia watu wengi zaidi na hujui wapi pa kuanzia , USIJALI kwani hapa ndipo ambapo MTAA UNAONGEA na tuko tayari kukusaidia kuwafikia watu wengi kwa BEI YA OFA

Njoo Utangaze Nasi Sasa Kwa Kutuambia Una TANGAZO Gani na unataka kutangaza kwa muda gani kwa kutuma ujumbe hapa WwhatsApp Kupitia Namba +255760871896 

Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx

 

Leave A Reply

Exit mobile version