Niliomba niletewe Binti yangu pale Gerezani, Mama Sofia alimleta Moyo. Nilimkumbatia Mwanangu hadi nikahisi faraja iliyo pitiliza.
“Umeongea na Wakili vizuri?” aliniuliza Mama Sofia, nilimtazama na kumwambia
“Ndio”
“Matumaini yangu utakuwa huru Veronica” Alisema, Muda ulipoisha Mama Sofia aliondoka na binti yangu aliyeitwa Moyo.
Nilibakia pale kwenye kiza, Maaskari walinichukua na kunirudisha kwenye chumba changu! Nilikuwa nikiishi kwenye chumba cha peke yangu kutokana na kesi ya mauwaji iliyokuwa ikinikabili, Moyoni nilijisema kuwa
“Sipaswi kuwa huru” niliketi kwenye pembe ya kile chumba kilichojaa wadudu wadogo wadogo, chini kulikuwa na maji yaliyomwagika, niliyamwaga mwenyewe kwasababu sikupenda kula. Kuna wakati niliwahi kumwambia Askari aliyekuwa akinihudumia kuwa
“Niletee sumu nife, sipendi kuendelea kukaa hapa”
“Veronica, Bado hii kesi ni mbichi sana. Subiria hukumu yako , Kama Mahakama ikikukuta hauna hatia? unataka kufa ili binti yako alie kwa uchungu?” aliniuliza
“Usiwaze kufa, hakuna anayeijua kesho yako” alisema na kuondoka zake.
Sikuona umuhimu wa kuendelea kuwa hai tena nikiwa pale gerezani kama Mahabusu niliyekuwa nasubiria siku ya hukumu ya kesi yangu ya Mauwaji
“Ni kweli umemuuwa Mama yako Mzazi?” yule Wakili alirudi tena kuutaka ushahidi ili ajuwe namna ya kunitetea, Wakili huyu aliajiliwa na Mama Sofia ambaye alikuwa jirani yangu mwema, alipenda kuniona nikishinda ile kesi
“Nikikwambia nilimuuwa utaiambia nini Mahakama? Utaidanganya kuwa sijauwa?”
“Ukiniambia ukweli nitajua jinsi ya kukuweka huru Veronica”
“Uhuru sio kitu ninachokitaka kwasasa, naitaka haki tu” nilisema kisha nilikaa kimya sikutaka kuendelea kuzungumza nae hadi Muda ulipoisha nilirudishwa tena kwenye kile chumba.
Yule Wakili alimpelekea taarifa Mama Sofia, Mama huyu alikuwa tajiri sana. Alikuwa jirani yangu kule Mbezi Luis nilipokuwa ninaishi
“Ninavyomjuwa Veronica hawezi kumuuwa Mama yake Mzazi Jacob” alisema akimuelekeza yule Wakili..
“Veronica ni mpole, mcheshi na mtaratibu sana…kusema amemuuwa Mama yake hilo haliwezekani kabisa”
“Unafikiria nitafanya nini na hataki kuzungumza kabisa, amekaa kimya?”
“Veronica sema ukweli, angalia ulivyodhohofu…Mwanao analia na kukuulizia utarudi lini, hivi ni kweli hutaki kuishi tena na binti yako Moyo?” Mama Sofia aliongea Baada ya kunitembelea, ni kweli nilikuwa nimekondeana sana, Mwili ulidhohofu mno, Afya yangu ilikuwa mbaya!
Mawazo yalipelekea nidhohofike namna ile, kingine ni mazingira ya pale ambayo hayakuwa rafiki kabisa kwangu!
“Mahakama itatenda haki kwangu Mama Sofia, Mungu ndiye anayejua kilichojificha” nilisema kwasababu sikupenda kabisa kuzungumzia jambo lile lililotikisa vichwa vya Watu wengi sana.
“Kwanini hutaki kusema kama kweli umeuwa au haujauwa Veronica?” Alihoji lakini sikumpa majibu kila alipokuja yeye au Wakili wa ile kesi.
Tukio hili lilitokea Mwaka 2009, lilizua gumzo kubwa, hakuna aliyeamini kama kweli Nimemuuwa Mama yangu. Ni kweli nilikuwa nimemuuwa Mama yangu Mzazi na chanzo cha tukio hili alikuwa ni Mume wangu aliyitwa Jonas.
Baada ya siku 21 nilirudishwa tena Mahakamani ili kusikiliza kesi yangu iliyojaza waandishi wa habari, kurasa zote za Magazeti zilipambwa kwa picha yangu na maelezo juu ya tukio langu la Mauwaji.
Hakimu alinitazama kabla ya kuanza ile kesi, jicho lake lilijaa huruma ambayo niliweza kuiona pindi nilipogongana nae macho, nilimuona akitoa kitambaa chake na kufuta chozi lililokuwa likimbubujika. Mahakama ilizizima kusikiliza atasema nini, niliweza kuzisikia pumzi zangu nilipokuwa nikihema ilitokana na ukimya uliotawala pale Mahakamani.
Nilipotazama pembeni nilimuona Mwanangu Moyo, aliniangalia na kutabasamu na kunifanya na Mimi nitabasamu.
Kila Mtu alikuwa kimya, wengine wakinitazama Mimi na wengine wakiwa wanamtazama Hakimu aliyekuwa amejiinamia kwa zaidi ya dakika 10, sikujua alikuwa akifikiria nini.
“Veronica!” aliniita yule Hakimu mwenye umri mkubwa, alivua miwani yake na kunitazama tena
“Abee!”
“Uko tayari kusema ukweli?” aliniuliza, nilikaa kimya kwa dakika moja kisha nilimpa jibu
“Ndio”
“Ilikuwaje ukamuuwa Mama yako Mzazi?” alihoji tena, nilimtazama Mama Sofia ambaye alinipa ishara niwe jasiri niseme.
Alitamani kusikia nikikanusha kuwa sijamuuwa Mama yangu, Watu wote wakawa bize kunitazama, waandishi wa Habari walitega karamu zao kwenye karatasi ili wapate cha kuandika kwenye Magazeti yao.
Nilianza kwa kigugumizi, pale pale chozi lilianza kunibubujika, midomo yangu ilikuwa ikitetemeka
“Nisamehe Mwanangu Moyo” nilisema huku nikiwa ninalia, niliendelea
“Ni kweli nimemuuwa Mama yangu Mzazi” kauli hii iliwashtua wengi, Hakimu alionekana kuvunjika moyo kabisa aliinamisha kichwa chake chini huku akijifuta Machozi.
Nilianza kueleza kilichotokea, Naitwa Veronica Moyo, najua wengi mmeshtushwa kusikia nimemuuwa Mama yangu, baada ya kueleza haya naomba Mahakama inihukumu kifo.
MIAKA MINGI KABLA YA TUKIO
Nilipofika chuoni kusomea masuala ya Utalii nilikutana na Mwanaume aliyeitwa Jonas, nilitokea Kumpenda nae pia alinipenda sana lakini hofu yangu ilikuwa kwenye maumbile yangu, nilihofia kumwambia Jonas kuwa nimekeketwa na huo ukawa udhaifu wangu katika Maisha yangu.
Kila nilipo kumbuka juu ya kile kitendo cha kukeketwa nilijisikia vibaya sana lakini kwa kipindi chote hicho nilikuwa bado sijawahi kukutana na Mwanaume na kufanya nae mapenzi.
Jonas ni binadamu mwenye hisia kama Wanaume wengine alionekana kuanza kukata tamaa kila nilipompa visingizio kuwa nipo kwenye siku zangu, naogopa Mimba au tutafanya tukimaliza chuo.
Nilimsikia rafiki yangu aliyeitwa Konzo akisema kuwa naenda kumpoteza Jonas siku za usoni kwani hawezi kukaa bila kusex na mimi
“Ooh! amekwambia hivyo?”
“Ndio, anataka kujua ni kwanini humpi tendo…Mwaka wa pili sasa”
“Sikia Konzo, naogopa Jonas atanikimbia akishakula tunda langu”
“Hofu yako haina msingi, haishawishi kabisa Veronica au wewe ni msichana bado?” Aliniuliza, sikuwahi kumwambia kuwa mimi ni Bikra nikaona ni vema nimwambie
“Ndio, mimi ni Bikra na sijawahi kushiriki tendo na Mwanaume” “Unasema kweli? Jonas anajua?”
“Hajui konzo na sitaki ajue kwasasa, acha iwe siri baina yetu” Nilimueleza hivyo, kitendo cha kukeketwa kilinifanya nikose kujiamini kwasababu niliwahi kusoma majarida kadhaa yanayozungumzia suala hilo kwa Wanaume, wengi wakisema Wanaume hawapendi Wanawake waliokeketwa kwa madai kuwa sio Watamu.
“Sawa nitaitunza Veronica na sitamwambia Mtu hapa Chuoni” Alisema na kunifurahisha Konzo, siri ya kukeketwa ikabakia kwenye nafsi yangu!
Nilipomwambia Mama yangu Mzazi aliniambia kuwa nikiona Mwanaume anasema hapendi Mwanamke aliyekeketwa basi Mwanaume huyo hajui nini maana ya Mapenzi wala radha ya tendo haijui vizuri
“Mama! mbona wataalam wanathibitisha kuwa kukeketwa kunamfanya Mwanamke akose radha halisi?”
“Mtaalam gani huyo anayeshindana na mababu wa Kabila letu? Sayansi inakupoteza Mwanangu” Maneno ya Mama yaliniweka njia panda kwa kipindi kirefu hasa baada ya kuvunja ungo
Niliishi na Mawazo ya aina mbili, Sikujua nimfuate nani kati ya Mama yangu au Wataalam walioandika majarida yale. Nikasema ipo siku nitaujua ukweli ingawa sikutaka kumpoteza Jonas, Mwanaume mzuri wa sura, alitokea kwenye maisha bora sana, Mcheshi na mkarimu. Alinisaidia Mambo mengi sana tukiwa chuoni.
Alinipa robo ya pesa alizotumiwa na Wazazi wake wakati Mama yangu Mzazi akinihimiza kuishi kulingana na mazingira, hakuwa na uwezo wa kunisomesha
“Veronica Mwanangu! Nenda kasome huko lakini tambua kuwa Maisha ni magumu mno, nitakachopata nitakituma kwako na nikikosa ishi kulingana na mazingira” alisema Mama nikiwa ninaenda kujiunga na Chuo Jijini Dar kutokea Arusha.
“Sawa Mama! nitatimiza malengo yangu na ya kwako, nitaishi kama ulivyoniagiza” Jinsi alivyonilea ilikuwa ni rahisi sana kukubaliana na hali zozote za kimaisha, Baba yangu alitutelekeza nikiwa mdogo, Kwa mujibu wa Mama alisema kuwa Baba alikimbia madeni yaliyokuwa yakimuandama.
Pale chuoni kwetu wengi walinifahamu, na msemo ulikuwa ukitamba sana ni ‘Tazama Pisi kali ya Arusha ile’ ulikuwa ni msemo uliopendwa, nilikuwa mzuri, macho makubwa yakukonyeza, shepu ilikuwa ya kawaida tu lakini ilitosha kunifanya nikamilike sana, Mapedeshee waliokuja kutafuta Wanawake wazuri pale chuoni hawakuacha kunisumbua kila wakati waliwatuma rafiki zangu akiwemo Konzo
“Una bahati sana Veronica, mabosi wanakuulizia wewe tu” alisema rafiki yangu Konzo, alinichekesha mno
“Sasa Bahati au usumbufu? ni kheri wewe unaishi upendavyo kuliko mie ”
“Ningekuwa ndio wewe! ningeshapata gari maana Mabosi wako tayari kukupatia upendacho” Nilitamani sana Maisha mazuri lakini ile siri ya kukeketwa niliogopa itasambaa pale chuoni ndio maana nilihakikisha namkataa kila aliyenitongoza.
“Huyu Mwanamke anaringa sana hapa chuoni sijui anajikuta nani yaani” Ni miongoni mwa kauli nilizowahi kuzisikia kutoka kwa Baadhi ya Wanaume walionikataa, niliona ni bora waseme naringa kuliko ile siri ifahamike kwenye hadhara.
Jonas alifanya kila mtego ili nifanye nae tendo lakini nilikuwa makini kuhakikisha namaliza kwanza chuo ili hata kama akijua mbele ya safari sitapata aibu kama ambayo nitaipata nikiwa bado chuoni, alinitoa Out kila mara.
Konzo aliniletea majarida mbalimbali ili nijifunze jinsi Mwanamke anavyotolewa usichana akiamini naogopa kufanya hivyo, aliniletea hadi video za ngono ili nishawishike! Ndio, zilinihamasisha sana na hofu yangu ikawa pale pale
“Nimefanya jitihada zote Veronica, kinachokukwamisha ni usichana wako huo, unakosa madili ya pesa”
“Imeshakuwa Bwana Konzo, acha iwe hivyo hivyo wakati ukifika nitapata hayo madili”
“Tatizo lako wewe ni mbishi sana Veronica, jaribu usiseme tu wakati…unaogopa utafikiria unataka kutolewa uhai?”
“Ha! ha! ha!”
Nilimzoea Konzo, siku moja Mwalimu Kasase aliniita ofisini kwake, alikuwa ni miongoni mwa Watu waliokuwa wakinitongoza pale chuoni, nilipofika aliulizia kuhusu jibu lake nilimwambia aendelee kusubiria, alinielewa.
Basi Maisha ya Chuo yalikuwa matamu na ya kukera kwa wakati mmoja, kuna wakati nilisikia raha sana lakini wakati mwingine nilikereka, likizo ilipofika nilirudi Arusha nikiwa msichana bado yaani Bikira. Pale nyumbani nilimkuta Mjomba yaani Kaka yake Mama aliyeitwa Sanga.
“Eeh! Veronica umekuwa Mkubwa hivi?” aliponiona aliniuliza, niliishia kucheka tu maana ukubwa wa Mtu unaonekana kupitia kwa wengine, mimi nilijiona nipo vile vile
“Huyu Mtoto kafanana sana na Baba yake”
“Sana, hasa anavyotembea kama anarudi vile”
“Ha!ha!ha!” Mama aliingiza utani wake kwa kilugha cha kwetu, tukawa tunacheka lakini Mjomba akionekana kama kunishangaa sana hadi nikawa naona aibu
“Msindikize Mjomba wako Kanisani” Alisema Mama baada ya siku mbili za kuwa Arusha
“Ina maana Anko Sanga hakujui kanisani Mama? siku zote hizo alizokaa”
“Mpeleke bwana!! Hakuwa na Mtu wa kumsindikiza huko, ukirudi utayarishe chakula cha Usiku”
Basi, tuliingia kwenye gari lake tukaanza safari ya kuelekea kanisani kwetu, palikuwa na umbali kiasi, mwendo wa Kilomita 15 hadi kufika huko, palikuwa karibu na nje ya Mji wa Arusha kulikuwa na hilo kanisa la Mzungu ambalo tangia nikiwa mdogo nilikuwa nikisali hapo hadi nakuwa mkubwa.
“Kumbe ni mbali hivi?” aliniuliza tukiwa tumebakisha takribani Kilomita 4, Kwa mbali mlima kilimanjaro ulikuwa ukionekana kwa uzuri sana, tulipishana na magari ya Watalii waliokuwa wakielekea huko
“Umeshawahi kwenda kufanya utalii?” aliniuliza tena, nilitabasamu tu kwani sikuwahi hata kuusogelea ule mlima japo nilizaliwa Arusha.
“Hapana Anko sijawahi kufanya utalii, ule mlima nauona kwa mbali tuu” Mjomba alicheka sana akaniuliza kama ningependa twende huko mlimani
“Ndio napenda”
“Nitaongea na Mama yako” alisema kisha tuliendelea na safari ya kuelekea Kanisani, tulipofika nilimuacha akanipatia pesa kama Elfu 50 hivi kisha akaniambia nisimwambie Mama Maana ataichukua
“Sitamwambia Anko”
“Haya natumaini mapishi yako yatakuwa Bul bul leo Veronica”
“Ha!ha!ha!” nilikuwa napenda sana kucheka nilikuwa siwezi kununa yaani, nilifurahi kisha nilipanda daladala na kurejea Nyumbani.
Nini Kitaendelea? Usikose SEHEMU YA PILI
JIUNGE NA KIJIWENI WHATSAPP CHANNEL Kwa Kugusa Hapa
Soma Riwaya Nyingine Za Kijiweni Kwa KUGUSA HAPA
Wewe kama MFANYABIASHARA.. Kuna wakati unatamani kuwafikia watu wengi zaidi na hujui wapi pa kuanzia , USIJALI kwani hapa ndipo ambapo MTAA UNAONGEA na tuko tayari kukusaidia kuwafikia watu wengi kwa BEI YA OFA
Njoo Utangaze Nasi Sasa Kwa Kutuambia Una TANGAZO Gani na unataka kutangaza kwa muda gani kwa kutuma ujumbe hapa WwhatsApp Kupitia Namba +255760871896
1 Comment
Woow inakujakuja vikee 🧐