Niliomba niletewe Binti yangu pale Gerezani, Mama Sofia  alimleta Moyo. Nilimkumbatia Mwanangu hadi nikahisi faraja  iliyo pitiliza. 

“Umeongea na Wakili vizuri?” aliniuliza Mama Sofia,  nilimtazama na kumwambia 

“Ndio” 

“Matumaini yangu utakuwa huru Veronica” Alisema, Muda  ulipoisha Mama Sofia aliondoka na binti yangu aliyeitwa Moyo. 

Nilibakia pale kwenye kiza, Maaskari walinichukua na  kunirudisha kwenye chumba changu! Nilikuwa nikiishi kwenye  chumba cha peke yangu kutokana na kesi ya mauwaji iliyokuwa  ikinikabili, Moyoni nilijisema kuwa 

“Sipaswi kuwa huru” niliketi kwenye pembe ya kile chumba  kilichojaa wadudu wadogo wadogo, chini kulikuwa na maji  yaliyomwagika, niliyamwaga mwenyewe kwasababu sikupenda kula.  Kuna wakati niliwahi kumwambia Askari aliyekuwa akinihudumia  kuwa 

“Niletee sumu nife, sipendi kuendelea kukaa hapa” 

“Veronica, Bado hii kesi ni mbichi sana. Subiria hukumu yako  , Kama Mahakama ikikukuta hauna hatia? unataka kufa ili binti  yako alie kwa uchungu?” aliniuliza 

“Usiwaze kufa, hakuna anayeijua kesho yako” alisema na  kuondoka zake. 

Sikuona umuhimu wa kuendelea kuwa hai tena nikiwa pale  gerezani kama Mahabusu niliyekuwa nasubiria siku ya hukumu ya  kesi yangu ya Mauwaji

“Ni kweli umemuuwa Mama yako Mzazi?” yule Wakili alirudi tena  kuutaka ushahidi ili ajuwe namna ya kunitetea, Wakili huyu  aliajiliwa na Mama Sofia ambaye alikuwa jirani yangu mwema,  alipenda kuniona nikishinda ile kesi 

“Nikikwambia nilimuuwa utaiambia nini Mahakama? Utaidanganya  kuwa sijauwa?” 

“Ukiniambia ukweli nitajua jinsi ya kukuweka huru Veronica” 

“Uhuru sio kitu ninachokitaka kwasasa, naitaka haki tu”  nilisema kisha nilikaa kimya sikutaka kuendelea kuzungumza  nae hadi Muda ulipoisha nilirudishwa tena kwenye kile chumba. 

Yule Wakili alimpelekea taarifa Mama Sofia, Mama huyu alikuwa  tajiri sana. Alikuwa jirani yangu kule Mbezi Luis nilipokuwa  ninaishi 

“Ninavyomjuwa Veronica hawezi kumuuwa Mama yake Mzazi Jacob”  alisema akimuelekeza yule Wakili.. 

“Veronica ni mpole, mcheshi na mtaratibu sana…kusema  amemuuwa Mama yake hilo haliwezekani kabisa” 

“Unafikiria nitafanya nini na hataki kuzungumza kabisa,  amekaa kimya?” 

“Veronica sema ukweli, angalia ulivyodhohofu…Mwanao analia  na kukuulizia utarudi lini, hivi ni kweli hutaki kuishi tena  na binti yako Moyo?” Mama Sofia aliongea Baada ya  kunitembelea, ni kweli nilikuwa nimekondeana sana, Mwili  ulidhohofu mno, Afya yangu ilikuwa mbaya! 

Mawazo yalipelekea nidhohofike namna ile, kingine ni  mazingira ya pale ambayo hayakuwa rafiki kabisa kwangu! 

“Mahakama itatenda haki kwangu Mama Sofia, Mungu ndiye  anayejua kilichojificha” nilisema kwasababu sikupenda kabisa  kuzungumzia jambo lile lililotikisa vichwa vya Watu wengi  sana. 

“Kwanini hutaki kusema kama kweli umeuwa au haujauwa  Veronica?” Alihoji lakini sikumpa majibu kila alipokuja yeye  au Wakili wa ile kesi. 

Tukio hili lilitokea Mwaka 2009, lilizua gumzo kubwa, hakuna  aliyeamini kama kweli Nimemuuwa Mama yangu. Ni kweli nilikuwa  nimemuuwa Mama yangu Mzazi na chanzo cha tukio hili alikuwa  ni Mume wangu aliyitwa Jonas.

Baada ya siku 21 nilirudishwa tena Mahakamani ili kusikiliza  kesi yangu iliyojaza waandishi wa habari, kurasa zote za  Magazeti zilipambwa kwa picha yangu na maelezo juu ya tukio  langu la Mauwaji. 

Hakimu alinitazama kabla ya kuanza ile kesi, jicho lake  lilijaa huruma ambayo niliweza kuiona pindi nilipogongana nae  macho, nilimuona akitoa kitambaa chake na kufuta chozi  lililokuwa likimbubujika. Mahakama ilizizima kusikiliza  atasema nini, niliweza kuzisikia pumzi zangu nilipokuwa  nikihema ilitokana na ukimya uliotawala pale Mahakamani. 

Nilipotazama pembeni nilimuona Mwanangu Moyo, aliniangalia na  kutabasamu na kunifanya na Mimi nitabasamu. 

Kila Mtu alikuwa kimya, wengine wakinitazama Mimi na wengine  wakiwa wanamtazama Hakimu aliyekuwa amejiinamia kwa zaidi ya  dakika 10, sikujua alikuwa akifikiria nini. 

“Veronica!” aliniita yule Hakimu mwenye umri mkubwa, alivua  miwani yake na kunitazama tena 

“Abee!” 

“Uko tayari kusema ukweli?” aliniuliza, nilikaa kimya kwa  dakika moja kisha nilimpa jibu 

“Ndio” 

“Ilikuwaje ukamuuwa Mama yako Mzazi?” alihoji tena,  nilimtazama Mama Sofia ambaye alinipa ishara niwe jasiri  niseme. 

Alitamani kusikia nikikanusha kuwa sijamuuwa Mama yangu, Watu  wote wakawa bize kunitazama, waandishi wa Habari walitega  karamu zao kwenye karatasi ili wapate cha kuandika kwenye  Magazeti yao. 

Nilianza kwa kigugumizi, pale pale chozi lilianza  kunibubujika, midomo yangu ilikuwa ikitetemeka 

“Nisamehe Mwanangu Moyo” nilisema huku nikiwa ninalia,  niliendelea 

“Ni kweli nimemuuwa Mama yangu Mzazi” kauli hii iliwashtua  wengi, Hakimu alionekana kuvunjika moyo kabisa aliinamisha  kichwa chake chini huku akijifuta Machozi.

Nilianza kueleza kilichotokea, Naitwa Veronica Moyo, najua  wengi mmeshtushwa kusikia nimemuuwa Mama yangu, baada ya  kueleza haya naomba Mahakama inihukumu kifo. 

MIAKA MINGI KABLA YA TUKIO 

Nilipofika chuoni kusomea masuala ya Utalii nilikutana na  Mwanaume aliyeitwa Jonas, nilitokea Kumpenda nae pia  alinipenda sana lakini hofu yangu ilikuwa kwenye maumbile  yangu, nilihofia kumwambia Jonas kuwa nimekeketwa na huo  ukawa udhaifu wangu katika Maisha yangu. 

Kila nilipo kumbuka juu ya kile kitendo cha kukeketwa  nilijisikia vibaya sana lakini kwa kipindi chote hicho  nilikuwa bado sijawahi kukutana na Mwanaume na kufanya nae  mapenzi. 

Jonas ni binadamu mwenye hisia kama Wanaume wengine  alionekana kuanza kukata tamaa kila nilipompa visingizio kuwa  nipo kwenye siku zangu, naogopa Mimba au tutafanya tukimaliza  chuo. 

Nilimsikia rafiki yangu aliyeitwa Konzo akisema kuwa naenda  kumpoteza Jonas siku za usoni kwani hawezi kukaa bila kusex  na mimi 

“Ooh! amekwambia hivyo?” 

“Ndio, anataka kujua ni kwanini humpi tendo…Mwaka wa pili  sasa” 

“Sikia Konzo, naogopa Jonas atanikimbia akishakula tunda  langu” 

“Hofu yako haina msingi, haishawishi kabisa Veronica au wewe  ni msichana bado?” Aliniuliza, sikuwahi kumwambia kuwa mimi  ni Bikra nikaona ni vema nimwambie 

“Ndio, mimi ni Bikra na sijawahi kushiriki tendo na Mwanaume” “Unasema kweli? Jonas anajua?” 

“Hajui konzo na sitaki ajue kwasasa, acha iwe siri baina  yetu” Nilimueleza hivyo, kitendo cha kukeketwa kilinifanya  nikose kujiamini kwasababu niliwahi kusoma majarida kadhaa  yanayozungumzia suala hilo kwa Wanaume, wengi wakisema  Wanaume hawapendi Wanawake waliokeketwa kwa madai kuwa sio  Watamu.

“Sawa nitaitunza Veronica na sitamwambia Mtu hapa Chuoni”  Alisema na kunifurahisha Konzo, siri ya kukeketwa ikabakia  kwenye nafsi yangu! 

Nilipomwambia Mama yangu Mzazi aliniambia kuwa nikiona  Mwanaume anasema hapendi Mwanamke aliyekeketwa basi Mwanaume  huyo hajui nini maana ya Mapenzi wala radha ya tendo haijui  vizuri 

“Mama! mbona wataalam wanathibitisha kuwa kukeketwa  kunamfanya Mwanamke akose radha halisi?” 

“Mtaalam gani huyo anayeshindana na mababu wa Kabila letu?  Sayansi inakupoteza Mwanangu” Maneno ya Mama yaliniweka njia  panda kwa kipindi kirefu hasa baada ya kuvunja ungo 

Niliishi na Mawazo ya aina mbili, Sikujua nimfuate nani kati  ya Mama yangu au Wataalam walioandika majarida yale. Nikasema  ipo siku nitaujua ukweli ingawa sikutaka kumpoteza Jonas,  Mwanaume mzuri wa sura, alitokea kwenye maisha bora sana,  Mcheshi na mkarimu. Alinisaidia Mambo mengi sana tukiwa  chuoni. 

Alinipa robo ya pesa alizotumiwa na Wazazi wake wakati Mama  yangu Mzazi akinihimiza kuishi kulingana na mazingira, hakuwa  na uwezo wa kunisomesha 

“Veronica Mwanangu! Nenda kasome huko lakini tambua kuwa  Maisha ni magumu mno, nitakachopata nitakituma kwako na  nikikosa ishi kulingana na mazingira” alisema Mama nikiwa  ninaenda kujiunga na Chuo Jijini Dar kutokea Arusha. 

“Sawa Mama! nitatimiza malengo yangu na ya kwako, nitaishi  kama ulivyoniagiza” Jinsi alivyonilea ilikuwa ni rahisi sana  kukubaliana na hali zozote za kimaisha, Baba yangu  alitutelekeza nikiwa mdogo, Kwa mujibu wa Mama alisema kuwa  Baba alikimbia madeni yaliyokuwa yakimuandama. 

Pale chuoni kwetu wengi walinifahamu, na msemo ulikuwa  ukitamba sana ni ‘Tazama Pisi kali ya Arusha ile’ ulikuwa ni  msemo uliopendwa, nilikuwa mzuri, macho makubwa yakukonyeza,  shepu ilikuwa ya kawaida tu lakini ilitosha kunifanya  nikamilike sana, Mapedeshee waliokuja kutafuta Wanawake  wazuri pale chuoni hawakuacha kunisumbua kila wakati  waliwatuma rafiki zangu akiwemo Konzo 

“Una bahati sana Veronica, mabosi wanakuulizia wewe tu”  alisema rafiki yangu Konzo, alinichekesha mno

“Sasa Bahati au usumbufu? ni kheri wewe unaishi upendavyo  kuliko mie ” 

“Ningekuwa ndio wewe! ningeshapata gari maana Mabosi wako  tayari kukupatia upendacho” Nilitamani sana Maisha mazuri  lakini ile siri ya kukeketwa niliogopa itasambaa pale chuoni  ndio maana nilihakikisha namkataa kila aliyenitongoza. 

“Huyu Mwanamke anaringa sana hapa chuoni sijui anajikuta nani  yaani” Ni miongoni mwa kauli nilizowahi kuzisikia kutoka kwa  Baadhi ya Wanaume walionikataa, niliona ni bora waseme  naringa kuliko ile siri ifahamike kwenye hadhara. 

Jonas alifanya kila mtego ili nifanye nae tendo lakini  nilikuwa makini kuhakikisha namaliza kwanza chuo ili hata  kama akijua mbele ya safari sitapata aibu kama ambayo  nitaipata nikiwa bado chuoni, alinitoa Out kila mara. 

Konzo aliniletea majarida mbalimbali ili nijifunze jinsi  Mwanamke anavyotolewa usichana akiamini naogopa kufanya  hivyo, aliniletea hadi video za ngono ili nishawishike! Ndio,  zilinihamasisha sana na hofu yangu ikawa pale pale 

“Nimefanya jitihada zote Veronica, kinachokukwamisha ni  usichana wako huo, unakosa madili ya pesa” 

“Imeshakuwa Bwana Konzo, acha iwe hivyo hivyo wakati ukifika  nitapata hayo madili” 

“Tatizo lako wewe ni mbishi sana Veronica, jaribu usiseme tu  wakati…unaogopa utafikiria unataka kutolewa uhai?” 

“Ha! ha! ha!” 

Nilimzoea Konzo, siku moja Mwalimu Kasase aliniita ofisini  kwake, alikuwa ni miongoni mwa Watu waliokuwa wakinitongoza  pale chuoni, nilipofika aliulizia kuhusu jibu lake  nilimwambia aendelee kusubiria, alinielewa. 

Basi Maisha ya Chuo yalikuwa matamu na ya kukera kwa wakati  mmoja, kuna wakati nilisikia raha sana lakini wakati mwingine  nilikereka, likizo ilipofika nilirudi Arusha nikiwa msichana  bado yaani Bikira. Pale nyumbani nilimkuta Mjomba yaani Kaka  yake Mama aliyeitwa Sanga. 

“Eeh! Veronica umekuwa Mkubwa hivi?” aliponiona aliniuliza,  niliishia kucheka tu maana ukubwa wa Mtu unaonekana kupitia  kwa wengine, mimi nilijiona nipo vile vile 

“Huyu Mtoto kafanana sana na Baba yake”

“Sana, hasa anavyotembea kama anarudi vile” 

“Ha!ha!ha!” Mama aliingiza utani wake kwa kilugha cha kwetu,  tukawa tunacheka lakini Mjomba akionekana kama kunishangaa  sana hadi nikawa naona aibu 

“Msindikize Mjomba wako Kanisani” Alisema Mama baada ya siku  mbili za kuwa Arusha 

“Ina maana Anko Sanga hakujui kanisani Mama? siku zote hizo  alizokaa” 

“Mpeleke bwana!! Hakuwa na Mtu wa kumsindikiza huko, ukirudi  utayarishe chakula cha Usiku” 

Basi, tuliingia kwenye gari lake tukaanza safari ya kuelekea  kanisani kwetu, palikuwa na umbali kiasi, mwendo wa Kilomita  15 hadi kufika huko, palikuwa karibu na nje ya Mji wa Arusha  kulikuwa na hilo kanisa la Mzungu ambalo tangia nikiwa mdogo  nilikuwa nikisali hapo hadi nakuwa mkubwa. 

“Kumbe ni mbali hivi?” aliniuliza tukiwa tumebakisha  takribani Kilomita 4, Kwa mbali mlima kilimanjaro ulikuwa  ukionekana kwa uzuri sana, tulipishana na magari ya Watalii  waliokuwa wakielekea huko 

“Umeshawahi kwenda kufanya utalii?” aliniuliza tena,  nilitabasamu tu kwani sikuwahi hata kuusogelea ule mlima japo  nilizaliwa Arusha. 

“Hapana Anko sijawahi kufanya utalii, ule mlima nauona kwa  mbali tuu” Mjomba alicheka sana akaniuliza kama ningependa  twende huko mlimani 

“Ndio napenda” 

“Nitaongea na Mama yako” alisema kisha tuliendelea na safari  ya kuelekea Kanisani, tulipofika nilimuacha akanipatia pesa  kama Elfu 50 hivi kisha akaniambia nisimwambie Mama Maana  ataichukua 

“Sitamwambia Anko” 

“Haya natumaini mapishi yako yatakuwa Bul bul leo Veronica” 

“Ha!ha!ha!” nilikuwa napenda sana kucheka nilikuwa siwezi  kununa yaani, nilifurahi kisha nilipanda daladala na kurejea  Nyumbani.

 Nini Kitaendelea? Usikose SEHEMU YA PILI 

JIUNGE NA KIJIWENI WHATSAPP CHANNEL Kwa Kugusa Hapa 

Soma Riwaya Nyingine Za Kijiweni Kwa KUGUSA HAPA

Wewe kama MFANYABIASHARA.. Kuna wakati unatamani kuwafikia watu wengi zaidi na hujui wapi pa kuanzia , USIJALI kwani hapa ndipo ambapo MTAA UNAONGEA na tuko tayari kukusaidia kuwafikia watu wengi kwa BEI YA OFA

Njoo Utangaze Nasi Sasa Kwa Kutuambia Una TANGAZO Gani na unataka kutangaza kwa muda gani kwa kutuma ujumbe hapa WwhatsApp Kupitia Namba +255760871896 

Leave A Reply

Exit mobile version