Ilipoishia sehemu ya saba ya In the name of LOVE
“Nampeleka Mtoto Arusha, kesho nitarudi. Ubaki salama” alisema Kisha aligeuka na kuondoka hapo huku Melisa akigeuka geuka mara kwa mara kuniangalia, sikujua ni kwanini alikua akiniangalia sana lakini hisia zilinianbia nilikua na uhusiano wa Maisha yaliyopita na Mtoto yule.
Nilirudi chumbani, nilianza kujihisi huzuni kiasi. Nilimtazama Zaylisa aliyekua amelala, nilijiinamia huku kichwa kikiwaka moto kwa mawazo lukuki, nilitamani kujua kitu ambacho nilihisi kilikua muhimu kukijua lakini sikujua nitafanya nini. Nilishusha tu pumzi zangu, Usingizi ulikua umeshaisha. Endelea
SEHEMU YA NANE
Saa ya ukutani iliniambia kua ilikua ni saa 12 asubuhi, nilivaa fulana Kisha nilitoka chumbani nikaelekea jikoni, nilihisi kuhitaji kitu Cha kupasha tumbo moto kidogo. Nilipofika jikoni nilikutana na Msichana wa kazi, aliponiona alinywea sana
Haikua mara ya kwanza kua hivyo pindi anionapo, nilimtazama kidogo nikagundua ni mwenye wasiwasi Fulani uliojaa Siri. Basi nilimsogelea karibu, nikapata kuuona ule uwoga na hofu ya Siri fulani, alipoteza kujiamini kabisa
Nilimuuliza “Haujambo?”
“Sijambo shikamoo” alisalimia kwa wasiwasi. Nilimkazia macho yangu, akainamia chini.
“Kwanini Kila unionapo unakua ni mwenye wasiwasi?” nilimuuliza, sijui nilijihisi vipi lakini nilihisi kiu kubwa ya kupata majibu ya maswali mengi yaliyoingia kichwani pangu.
Alikaa kimya huku akipata tabu, alipoteza Hali ya utulivu kabisa.
“Baby” niliisikia sauti nyuma yangu, sauti ya Zaylisa ilikatisha zoezi langu. Nilitabasamu Kisha niligeuka
“Naam‼” alinisogelea Kisha aliniuliza “Kwanini upo hapa ukaniacha peke yangu chumbani Baby”
“Nilihitaji kitu Cha moto Cha kuingiza tumboni, istoshe nilikuacha umelala sikutaka kukusumbua”
“Hapanaa‼ hauwezi kunisumbua Mpenzi, Mimi ni wako” alisema Zaylisa, yule Msichana wa kazi akaondoka pale jikoni.
“Haya niambie nikuandalie nini?”
“Chai, weka limao na asali”
“Basi?”
“Ndiyo babe” sura zetu zilijaa tabasamu kubwa sana, basi Zay alianza kuniandalia chai. Nikatoka nikaelekea chumbani
Nilichohitaji kufanya wakati ule kilikua ni kuingia bafuni kwa ajili ya kuoga Maji ili nikitoka nipate chai niliyoagiza. Wakati naelekea bafuni, simu ya Zaylisa ilianza kuita
Nilijishauri mara mbili, nimpelekee au nioge. Nilifikiria huwenda ilikua simu muhimu asubuhi ile, niliona ni Bora nimpelekee jikoni, basi nilikata shauri nikaielekea ile simu
Wakati naifikia ilikua inakata, lakini niliona ni Bora niipeleke tu kama ni simu muhimu ili awahi kuwasiliana na Mtu huyo, niliichukua nikawa natoka chumbani, ukaingia Ujumbe
Sijui ni kitu gani kilinifanya niangalie kioo, kumbe ilikua haijafungwa kwa nywila. Meseji ilijionesha pale juu, Meseji hiyo ilitoka kwa Mtu aliyemsevu kama Mzee wa Mipango.
“Zay nakupigia simu hupokei. Nakusistiza usijisahau, upo huko kwa mpango maalum” Nilishtuka kidogo, nilijikuta nikipotea kiakili kidogo
Nilisimama huku nikichezesha macho yangu huku na kule kama nilikua natafuta kitu kilichopotea, niligeuza shingo yangu kuelekea chini huku akili yangu ikiniambia kua ujumbe ule ulikua na maana zaidi ya ulivyoandikwa, niliufungua Hadi ndani ya Boksi la jumbe.
Niliurudia kuusoma tena, hakuna kilichobadilika. Hapakua na Meseji nyingine kutoka kwa Mtu huyo, pengine walikua wakiwasiliana zaidi kwa kupigiana simu au zilikua zinafutwa.
Moyo ulinienda mbio kidogo, meseji ilikua na Fumbo gumu sana. Nilitafakari kwa dakika tatu bila Majibu, niliurudia mstari aliposema “Upo huko kwa mpango maalum”
Nilijiuliza “ Upo huko Ina maana ni hapa, sasa kama ni hapa amekuja kwa mpango gani wakati ni Mpenzi wangu au ulikua ni ujumbe usio wake.?”
Nilishusha pumzi zangu, kwakua simu ilikua mkononi niliona niufute ule ujumbe maana asije ona kua nimefungua simu yake, sikutaka kuichunguza tena ile simu, niliirudisha nilipoitoa
Ilianza kuita tena, huku mpigaji akiwa yule yule Mzee wa Mipango. Nikaelekea Bafuni kuoga, Nilioga nikiwa ninaiwaza sana ile simu, sijui hata kwanini nilipata wasiwasi Fulani
Nilipomaliza kuoga nilitoka bafuni, macho yangu yalikua na shahuku sana, Moja kwa moja yalielekea kitandani, Bado simu ya Zaylisa ilikua hapo. Wakati najifuta Maji mwilini, simu ilianza kuita tena
“Kwanini huyu Mtu anapiga sana simu?” nilijiuliza, mara Mlango ulifunguliwa haraka, Zaylisa alielekea Moja kwa moja kuchukua simu yake. Nilimdadisi kwa umakini sana nikijifanya naendelea kujifuta Maji kama vile nilikua sijui chochote.
“Imeita muda mrefu” nilisema, alinitazama kidogo huku akionekana kua na wasiwasi Fulani usoni pake baada ya kuona ni Nani aliyekua akimpgia. Kisha akaachia tabasamu la kuzuga, tabasamu nililo ligundua haraka sana kua halikutoka moyoni pake
“Dakika Moja baby, naongea na Baba” alisema Kisha aliondoka chumbani, moyo Wangu uliripuka kwa mshituko. Nilijiuliza kama alikua Baba yake, kwanini aliingiwa na wasiwasi au ndio kusema aliyepiga safari hii hakua yule Mzee wa Mipango?
Aliniacha njia panda, akili yangu iligawanyika vipavipande nisijue kipi ni sahihi na kipi si sahihi. Nilifunika kombe ili mwanaharamu apite lakini akili yangu iliniambia napaswa kumchunguza Zaylisa
Haikuchukua hata dakika tano alirudi akiwa mnyonge sana, nilishtuka kumwona akitembea pole pole huku sura yake ikionekana kutokua sawa. Nilimsogelea na kumwuliza
“Upo sawa?” alinitazama kwa jicho lililojaa huzuni sana Hadi nilishtuka huku nikijiuliza alikua ameambiwa nini na aliyempigia simu.
“Babe‼”
“Baba..” alisema Kisha aliketi kitandani, Nami Niliketi.
“Baba amefanya nini?”
“Jacob, Hali ya Baba siyo nzuri. Nimepigiwa simu na Mama, natakiwa kwenda”
“Pole sana, basi Wacha tuongozane” nilisema huku nikiweka taulo pembeni ili nipake mafuta na kuvaa nguo.
“Hapana, siku nyingine Jacob. Kwa Leo Wacha Mimi niende kwanza, taratibu atakufahamu sawa Mpenzi wangu?” alisema, ilinibidi niwe Mpole ukizingatia ni kweli Wazazi wake walikua hawanifahamu.
Nilihisi Kuna uwongo usio dhahiri lakini sikuweza kuuthibitisha, Niliketi kitandani nikimtazama Zaylisa akijiandaa haraka haraka lakini uso wake ulikua na ukakasi mwingi sana, alikua akinitazama Kila dakika. Alipomaliza kujiandaa alinisogelea na kunipa busu Kisha akaniaga
“Bye Babe” niliitikia kwa kutikisa kichwa changu, nahisi aligundua kua sijafurahia.
“Basi nisindikize Hadi getini my love” nilitabasamu kidogo, tukatoka Hadi getini. Alikua tayari ameshaita taxi akaingia na kuondoka zake huku nikimsindikiza kwa kutumia macho yangu pekee. Nilishusha pumzi zangu baada ya gari kupotea machoni pangu, mkono mmoja ukiwa umeshikilia geti na mwingine ukiwa Mfukoni
Moyo Wangu uliingiwa na Hali ya Wasiwasi sana. Nilirudi ndani taratibu nikaketi kwenye Bembea Moja ndani ya Bustani kando ya Eneo la maegesho.
Nilihitaji kutulia zaidi na kuwaza mambo mengi yaliyokua yamepita. Dakika tano zilipita nikiendelea kufikiria, ghafla nilikatishwa na sauti ya kugongwa kwa geti, niliuangalia mlango wa kuingilia ndani hapakua na dalili ya Msichana Wakazi kutoka, nikaona ni Bora nikafungue
Nilipofungua nilimwona Msichana mmoja, alisimama kwa matege ya kurudi nyuma, alikua na nywele ndefu nyeusi zilizoshuka Hadi mabegani. Alikua amevalia mawani nyeupe huku midomo yake ikiwa imekolea ‘Lipstiki’ nyekundu.
Alikua akitabasamu baada ya kuniona, haraka niligundua alikua hajanifananisha na yeyote isipokua Mimi nilikua ni Mtu aliye mtarajia.
‘‘Habari Bosi Jacob” alisema huku akili yangu ikiniambia kua Kuna Siri kwenye jina la Bosi, yeye hakua Mtu wa kwanza kunita jina Hilo lakini sikuacha kujiuliza ilikua ni Siri gani nzito iliyojificha? Niliachia tabasamu la kusita, huku nikimpa sura isiyo tabirika.
“Nimeleta mzigo uliopaswa kuupokea siku uliyopata ajali” alisema, Kisha alielekea kwenye gari akatoka na boksi dogo Jekundu. Nilikua katika Bumbuwazi, Kisha alinipatia Boksi na kuniambia
“Nakutakia mapumziko Mema pia nakuombea urejee kazini haraka kuliko ilivyopangwa” aliondoka aliniacha nikiwa kimya kama Bubu, mkononi nilikua na Boksi Jekundu
Macho yangu yalilizunguka Boksi na kugundua palikua pameandikwa jina langu MR. JACOB.
Nilihisi kua nilishawahi kuyaishi Maisha Fulani niliyoyasahau, kumbukumbu zangu zote zilinianbia kua Mimi Jacob ni Kijana masikini asiye na kazi lakini kwanini Watu walikua wakiniheshimu kama Mtu mkubwa mwenye utajiri.
Nilikua nimesimama huku Boksi likiwa mkononi mwangu, nilipepesa macho yangu huku nikitafuta kumbukumbu ambazo sikua nazo, lakini akili yangu iliniambia huwenda ndani ya Boksi Kuna kitu muhimu sana, nilifanya haraka nikaingia ndani, Moja kwa moja Hadi chumbani kwangu
Nililiweka lile Boksi kitandani, nilijishika kiuno huku nikiendelea kupambana na Giza nene kichwani kwangu. Niliinama na kulishika tena, hamu ya kufungua na kuona kitu kilichomo ndani ya Boksi ilinijia, taratibu nilianza kulifungua huku moyo Wangu ukiwa unadunda sana
Mara mlango uligongwa, nilijiuliza ni Nani anayegonga wakati Clara na Zaylisa hawakuwepo nyumbani, kitu Cha kwanza nilipata wazo la kuhifadhia Boksi, nikaliweka chini ya Uvungu wa Kitanda Kisha nikaelekea mlangoni
Nilipofungua mlango nilikutana na sura ya Msichana wa kazi. Aliponiona alinitazama sana kama Mtu ambaye alikua anataka kusema kitu lakini alikua akiogopa kufanya hivyo.
“Hey‼” nilimshitua, kweli alikua mbali kifikra.
“Abee‼ samahani, Dada Clara anataka kuongea nawe, simu iko hewani sebleni” alisema, nilimtazama kidogo. Sikutaka kumwuliza chochote tena
Nilielekea Sebleni nikimwacha Msichana nyuma yangu, kweli nilikuta simu iko hewani, niliiweka simu sikioni
“Jacob, nilitaka kukujulisha kua nimefika salama Arusha.” Niliisikia sauti ya Clara.
“Sawa” nilimjibu kwa Mkato Kisha nilisikiliza kama alikua na jambo la kusema tena.
“Haya, kesho nitarudi. Uwe na siku njema” alisema, sikuitikia Bali nilikata simu. Kuna kitu kuhusu Clara kilikua moyoni mwangu, kitu hicho kilijificha
lakini kilianza kuonekana taratibu, kitu chenyewe ni chuki ndogo. Nilipomaliza, niliirudisha kisikilizio eneo husika Kisha nikageuka nilikutana na Yule Msichana wa kazi anayeitwa Matilda, alikua akinitazama na ilionesha alikua akisikiliza maongezi yetu.
Nilimvuka na kuelekea Chumbani kwangu. Nikaufungua na kufunga mlango kwa nguvu sana, Hali ya hasira ilinijaa hasa nilipokumbuka maneno ya Zaylisa kua Clara hapendi kuniona pale kwake.
Nilikumbuka kuhusu Boksi nililolisukumiza Uvunguni, basi niliinama na kuanza kupapasa pale nilipoamini lile Boksi lilikua limetulia lakini sikulipata. Niliinama na kuchungulia, palikua peupe, Boksi halikuwepo mahala pale
Ilinishangaza sana, Nani atakua amelichukua na kwanini alichukue.
“Au Matilda atakua amelichukua? Kama amelichukua atakua amelionaje, kwanini alichukue?” nilishusha pumzi, harufu ya utata ilikua imejaa puani kwangu
Jasho lilianza kunitoka kama Mtu aliyekua chumba Cha joto, haraka nilielekea kugonga chumbani kwa Matilda. Nilikua nahitaji majibu ya maswali yangu
Alipofungua mlango alinitazama kama vile alikua akiniona kwa mara ya kwanza. Nilimtazama kwa sekunde kadhaa bila kusema chochote kile Kisha nilimuuliza kwa sauti kavu iliyokua imejaa mamlaka sana
“Umechukua Boksi chumbani kwangu?” swali hili liliambatana na kufunga ndita zangu, sikutaka mzaha kwasababu niliamini lile Boksi lilikua na Fumbo kuhusu Mimi, akili yangu iliniambia Kuna Sehemu ya Maisha yangu ilikua imeondoka. Alinitumbulia macho kama vile alikua hajasikia nilichomuuliza, nilimsogelea huku nikiwa nimemtolea macho ya hasira
“Boksi ulilolichukua chumbani kwangu lipo wapi?”
“Boksi?” aliniuliza huku mdomo wake mwekundu wenye upana kiasi ukijiminya kwa kukosa neno la kuongeza
“Ndiyo” nilisema kwa hasira Hadi chembe za mate zilimrukia usoni, alimeza funda zito la mate nililiona likipita kooni pake kama Nyoka aliyemeza panya mnene, jasho likianza kumtoka huku hofu na wasiwasi vikimtawala.
“Naongea na wewe Matilda, umechukua Boksi” nilimshitua tena baada ya kuona akili yake ilikua imelala kwa tafakari ya kina, alipepesa kope za
macho yake, huku akizungusha macho kama kinyonga. Alipata kigugumizi Cha sekunde kadhaa Kisha alikuja na jibu kavu huku akiondoa wasiwasi aliouonesha awali.
“Sijui hata unauliza kuhusu Boksi gani, Mimi sielewi” sikuacha kumtazama, niliona kuendelea kumuuliza ningepoteza muda mwingi zaidi. Niliondoka nikimwacha amening’inia mlangoni kama konda wa daladala anayedaiwa chenji.
Nilifunga mlango kwa nguvu, sauti ya kuubamiza ikavuma kuashiria nilitumia nguvu nyingi kuufunga. Nilijiuliza lile Boksi lilikua na kitu gani kilichokua maalum, kitu ambacho yule Mtu alidai nilipaswa kupokea siku niliyopata ajali.
“ Alisema nilipaswa kupokea Boksi siku niliyopata ajali? Mbona ile siku nakumbuka nilienda nyumbani kwao Zaylisa, hapa katikati Kuna Siri gani kuhusu Mimi, kwanini Watu wananipa heshima Mimi masikini nisiye na chochote?” nilijiuliza huku nikibadilisha mikao pale chumbani.
Ghafla tu, wazo la kumpigia simu Zaylisa lilinijia, nilihitaji kujua kama alikua amefika kwa Baba yake. Nilipopiga niliambiwa simu ya Zaylisa ilikua haipatikani, nilipatwa na hasira sana
Niliketi nikitafakari zaidi, hamu ya kuendelea kua ndani iliniisha. Niliona ni Bora niende mgahawani ambako nilikua nikifanya kazi, japo nilikua nimefukuzwa lakini niliamini huko ningepata mwanga zaidi wa Maisha yangu
Niliondoka, nikaita Taxi. Safari ya kuelekea mgahawani ilianza. Nafsi yangu ilikua kwenye Giza nene, hapakua na mwanga mithiri ya Handaki.
Nini Kitaendelea? Usikose sehemu ya TISA
JIUNGE NA KIJIWENI WHATSAPP CHANNEL Kwa Kugusa Hapa
Soma Riwaya Nyingine Za Kijiweni Kwa KUGUSA HAPA
Wewe kama MFANYABIASHARA.. Kuna wakati unatamani kuwafikia watu wengi zaidi na hujui wapi pa kuanzia , USIJALI kwani hapa ndipo ambapo MTAA UNAONGEA na tuko tayari kukusaidia kuwafikia watu wengi kwa BEI YA OFA
Njoo Utangaze Nasi Sasa Kwa Kutuambia Una TANGAZO Gani na unataka kutangaza kwa muda gani kwa kutuma ujumbe hapa WwhatsApp Kupitia Namba +255760871896
Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love
4 Comments
https://shorturl.fm/sFDZF
https://shorturl.fm/kY1h4
Fupi sana
Toa na ya 9 Kaka story tanu kweli