Ilipoishia sehemu ya pili ya In the name of LOVE
“Sikumbuki chochote Clara, natamani nikumbuke ili nijuwe tunapoelekea”
“Hofu ondoa, Kila kitu kinahitaji muda kukifahamu. Jipe muda zaidi, usikimbie sana Bali taratibu utakumbuka hatua kwa hatua J” ilikua ni safari ya wastani wa saa nzima, Hadi tulipofika mtaani.
“Gari haiwezi kufika Hadi kule, hivyo tutatembea” alisema Clara, tuliacha gari mahali Kisha tulishuka na kuanza kutembea. Tulikatisha maeneo kadhaa, nilimwona Clara akinitazama sana ili kuona kama nilikua nikiikumbuka mitaa hiyo, sikukumbuka kabisa. Endelea
SEHEMU YA TATU
“Melisa anaishi hii nyumba, hata wewe uliishi hapa kabla ya Hadithi mpya kuhusu Maisha Yako Jacob” tulisimama mbele ya nyumba Moja iliyopakwa rangi nyekundu. Ilikua ni nyumba ya kawaida ya Mtaani, palionekana kutulia sana.
“Unapakumbuka hapa?” aliniuliza, niliitazama sana nyumba ile lakini sikuweza kukumbuka chochote kile, upepo Mdogo ulikua ukivuma
“Hapana”
“Mimi nilifika mara ya kwanza ilikua ni siku ile Mdogo wako Melisa alipokuja mgahawani kukuita. Niliguswa na kutaka kujua kilitokea nini ukawa Ndiyo mwanzo wa kuingia kwenye Maisha Yako” alisema Clara, chozi likinitoka. Sikupakumbuka, nyumba yenyewe ilionekana kama yenye kufanyiwa Ukarabati. Wakati tunaongea mara alikuja Mzee Mmoja, alikua amevalia Msuli na tisheti, alikuja Moja kwa moja kwangu kama vile alikua akinifahamu Hadi nilishtuka sana.
“Wewe Kima umekuja kufanya nini hapa?” alipaza sauti huku akininyooshea Kidole. Sikujua nimjibu nini nilibakia nikiwa ninamtazama tu, mapigo ya Moyo yalianza kwenda Mbio, nilimtazama Clara Kisha niliruhusu macho yangu kumtazama tena yule Mzee.
“Niliwaambia msije tena hapa, hii nyumba haiwahusu, siyo wewe wala huyo Mshenzi mwenzako. Mama yenu alikimbia Urithi sasa unakuja hapa kufanya nini tena” alizidi kuniporomoshea maneno makali yaliyoniumiza sana japo nilikua sielewi alikua akimaanisha nini.
“Samahani Baba, Jacob hakumbuki chochote. Alipata ajali, nimemleta ili amwone Mdogo wake Melisa” alidakia Clara, Yule Mzee akamtazama Clara kwa hasira Kisha akasema
“Anhaa kumbe ni wewe Binti, nimekukumbuka. Wakati ule ulitaka usawa kama huu lakini wakati huu huambulii kitu, uliweza wakati wa mazishi ya Mama Yao tu. Jacob na Melisa niliwafukuza hapa, sasa mnakuja kumwangalia Melisa gani? Muulize huyo Mbwa akwambie alipo mpeleka Mdogo wake” nilishtuka na kushangaa sana, hata Clara aligeuka kunitazama. Ilionesha Clara hakufahamu mengi baada ya Kifo Cha Mama
“Huyu ni Nani?” nilimuuliza Clara, akamtazama yule Mzee Kisha akarejesha macho kwangu.
“Huyu ni Mjomba wako, Kaka wa Mama Yako”
“Sema nilikua Kaka wa Mama yake. Kwanza msifanye mambo kua magumu, hebu tokeni hapa haraka kabla sijapandisha mashetani ya Kwetu” Yule Mzee akang’aka. Nilichukia sana, nikaondoka kwa hasira.
“Jacob, subiri” alisema Clara, nilitembea haraka Hadi kule tulikoacha gari. Chozi lilikua linanibubujika. Hapakua na tumaini la kumpata Melisa kwa haraka
“Jacob usitumie hasira tafadhali. Haya mambo yanahitaji Ujasiri” alisema.
“Ujasiri gani unaousema Clara, yule Mzee anatoa lugha Kali na matusi, haonekani kua Mtu mzuri kwangu. Kama ni kweli yeye ni Kaka wa Mama yangu basi hatukuwahi kuelewana naye, ningekua na kumbukumbu zake sijui kama tungefika huku, ilianza kama ndoto lakini inaenda kua kweli sasa, kumpata Melisa ni Mtihani, Mimi sijui nilikompeleka” nilisema kwa kujihukumu, chozi likinibubujika nikiwa nimeegemea Bodi ya gari
“Jacob, pale ndipo nilipowaacha wewe na Mdogo wako baada ya Mazishi ya Mama yenu. Sikurudi tena Hadi nilipokugonga na gari, sikujua kama
Mlifukuzwa Masikini” alisema Clara huku sura yake ilijaa majuto na huzuni, nilipomtazama niligundua alikua kwenye maumivu sana ya kihisia.
“Haina maana tena Clara, sijui alipo. Sikumbuki tulienda wapi, Ina maana sikua na rafiki, kwanini tusiende mgahawani uliposema kua nilikua nafanya kazi?” Nilimuuliza, nikaona uso ang’avu kwa Clara kama Mtu aliyekumbushwa alichokisahau.
“Ndiyo, tunaweza kupata fununu huko. Hebu twende” tuliingia kwenye gari, safari ya Mgahawani ilianza kwa Kasi sana. Nilijilazimisha kukumbuka nilipomwacha Melisa lakini ilikua ngumu niliishia kupata maumivu ya Kichwa. Clara akajitahidi kunisihi sana kua nisitumie nguvu kubwa na hasira kukumbuka
Tulikua kimya Hadi tunafika mgahawani, Clara akaniambia Mgahawa huo ndipo tulipokutana Mimi na yeye, niliuangalia lakini sikupata kumbukumbu yoyote ile, sikukumbuka kama niliwahi kufika hapo na kufanya kazi. Ulikua ni Mgahawa wa Kisasa wenye hadhi ya juu sana
Tulishuka kwenye gari, Kisha tulielekea ndani ya Mgahawa. Mtu wa kwanza kutuona alikua ni Mwanamke mmoja mwenye Sare za wafanyakazi wa Mgahawa. Akatabasamu Kisha akaniita
“Jacob”
Nilimtazama kama Mtu aliyekua akilia, sikujua nitabasamu au nishangae. “Nam‼” nikaitikia huku nikisukumwa na kiu ya kujua alipo Melisa kwanza. “Ulikua wapi?” aliponiuliza sikujua Cha kumjibu, nilimtazama Clara.
Mara akapita Mtu mwingine akiwa amevalia suti, akatabasamu na kunikumbatia akionesha ni Mtu muhimu kwangu, nilianza kuhisi pengine ndiye rafiki yangu ambaye angetupatia fununu na kujua mahali alipo Melisa.
“Naomba tukae kwanza” alisema Clara, yule Mwanamke aliondoka zake. Mimi, Clara na yule jamaa tukapata muda wa kuongea, akaanza kusema
“Jacob huonekani kua sawa, ni kama Mtu aliyehama sana kifikra, halafu ulikua wapi siku zote hizo?” aliuliza yule Jamaa, hakujua chochote kile.
“Alipata ajali, amepoteza kumbukumbu. Yupo hapa kujikumbuka, kujua mengi kuhusu Yeye” alijibua Clara, Hali hii ilimshangaza sana yule
Mwanaume. Akanitazama huku akiiuliza nafsi yake kama alichoambiwa kilikua kweli.
“Ndiyo, sikukumbuki wewe. Sikumbuki chochote. Najiona kama Mtu mgeni hapa Duniani, miezi mitatu iliyopita ilibadilisha Kila kitu” Nilisema, niliona namna yule Mwanaume alivyosikitika
“Pole sana Jacob, angalau uko Mzima.”
“Asante, wewe ulikua rafiki yangu? Kama ni hivyo naomba unipe majibu ya Maswali yangu tafadhali” nilisema huku nikilengwa na Mchozi.
“Hapana, Mimi nilikua meneja wako. Hata hivyo hapa ulishafukuzwa kazi, rafiki Yako alikua Sudi” niliposikia kuhusu rafiki, nilishtuka nikajua sasa huyo Sudi atakua na Majibu.
“Yupo wapi huyo Sudi?” niliuliza, akanitazama Kisha akasema.
“Bahati mbaya, Sudi alikimbia na hajulikani alipo. Chumbani kwake ilikutwa maiti ikiwa na mikwaruzo shingoni, kwa mujibu wa Polisi ni kua Maiti huyo alibakwa na Sudi Kisha kuuliwa” alisema, nilishusha pumzi zangu, niliuwona Mlima mrefu sana Hadi kujitambua
“Sasa nataka kujua niliishi wapi?”
“Mara ya mwisho nilisikia ulikua ukiishi kwa Sudi.”
“Kwa Sudi?”
“Ndiyo, pole sana Jacob. Maiti ile ilikua ya Mdogo wako Melisa” Moyo Wangu ulilipuka mithiri ya Volkano, kusikia Mdogo wangu Melisa ndiye aliyebakwa na kuuawa kulifanya nishtuke sana, nilihema bila kujizuia, nilihisi hata Presha yangu ilikua imepanda, koo langu lilikauka mate.
Taratibu chozi lilianza kunidondoka kwa Uchungu sana, japo sikukumbuka hata sura ya Melisa lakini alikua Ndiyo tumaini pekee kwangu. Kilichoniumiza zaidi ni kuona rafiki yangu mkubwa ndiye aliyekatisha uhai wa mdogo wangu kwa kumbaka na kumwua. Nilihisi kufa-kufa, chozi lilibubujika jingi kwa mfululizo.
Niligeuka kumtazama Clara, niliona naye alikua akidondosha chozi. Alikua akiumizwa sana, alinifuta chozi kwa kutumia kitambaa Chake Kisha akaniambia
“Pole sana Jacob, taswira imebadilika tena. Najiona ni mwenye hatia kuu, siwezi kuukwepa huu msalaba. Kama siyo Mimi kukugonga na gari basi hata mdogo wako Melisa asingelitendewa Unyama kama huu, hakustahili
kabisa” alisema huku akidondosha chozi pia, sikumtazama Clara kama ambavyo yeye alikua akijiona. Kwangu alikua ni Mwanamke asiye na hatia, sikuweza kumjibu chochote nikamuuliza yule jamaa
“Unapafahamu alipozikwa Mdogo wangu?” alinitazama, macho yake yalitambua Uchungu ulio moyoni mwangu, akapepesa macho yake kidogo halafu akaniambia
“Ndiyo, amezikwa Makaburi ya Kinondoni. Naweza kuwapa Mtu akawapeleka huko, sisi tuliubeba Msiba wa Mdogo wako sababu hapakua na Mtu mwingine aliyejitokeza. Tulimzika” aliongea maneno mengine yaliyonipa Uchungu zaidi, niliona ni jinsi gani mdogo wangu alivyokosa Mtu muhimu wa Kumzika. Nilijiuliza ni jinsi gani alinilaani bila kujua mahali nilipo, sijui alitaja jina langu wakati anakufa au aliacha laana?
Nilimeza mate ya maumivu sana, nilipoteza Mtu pekee aliyeko upande Wangu.
“Sawa, naomba nikalione Kaburi lake” nilimwambia. Yule Meneja akanitazama tena, Kisha akatoa simu yake na kunionesha picha ya Melisa Kisha akaniambia
“Huyo ndiye Melisa, Jacob. Unapaswa kukumbuka Kila kitu. Usiwe mtumwa” Nilimtazama Melisa, akiwa anatabasamu. Picha hiyo nilipiga nikiwa naye, tulionekana kua wenye furaha sana. Nilitabasamu kwa maumivu makali sana ya Moyo Wangu.
Bahati mbaya sikuweza kukumbuka hata chembe ya Maisha tuliyoishi Mimi na Mdogo wangu Melisa. Akili yangu ilitapatapa lakini sikuambulia chochote, nilimrudishia ile simu Kisha akawa amemwita Mtu wa pale Mgahawani ili atupeleke Kinondoni
Tuliondoka pale Hadi Makaburi ya Kinondoni kwa ajili ya kuzuru Kaburi la Mdogo wangu. Clara alikua bega kwa bega na Mimi Hadi Kinondoni, yule Mtu akatupeleka Moja kwa moja Hadi lilipo Kaburi
Lilionekana ni Kaburi lililofukiwa siku chache tu maana udongo wake Bado ulikua mwepesi. Laiti kama ningelirudisha fahamu na kupona mapema, pengine ningewahi kumwokoa Melisa Jamani.
Nilipiga goti nikiwa ninalia huku mwili ukinisisimka sana, Melisa aliondoka bila kupenda. Sudi alikatisha uhai wake, niliambiwa kua nilikua na urafiki wa kushibana sana na Sudi lakini ndiye aliyemuuwa Mdogo wangu Kisha kukimbia.
Nililia sana kama Mtoto mdogo, Clara alikua akinituliza Kila sekunde iliyoondoka. Nilihisi Uchungu sana, ni Bora hata ningekufa kwenye ajali ili nisijuwe chochote kile kilichoendelea Kwa Mdogo wangu Melisa
“Jacob, inatosha. Turudi nyumbani sasa, umelia sana leo imetosha, hatuwezi kurudisha muda nyuma. Mpango wa Mungu umetimia” alisema Clara huku akinivuta kwa kushirikiana na Mtu aliyetuonesha Kaburi la Melisa. Waliniondoa kwa nguvu nikiwa ninalia, wakanirudisha kwenye gari
“Kaka Asante sana, hii hapa pesa itakusaidia kurudi Mgahawani, sisi tunaelekea nyumbani” Clara aliongea, akampatia pesa yule Jamaa.
“Poleni sana, namwonea huruma sana Jacob. Ni Mtu mzuri sana pengine hakustahili yote haya” yalimtoka yule Jamaa, akasinya ile pesa akaondoka zake taratibu. Tuliondoka tukarejea nyumbani kwa Clara, sikua na mahali
pengine pa kwenda tena. Kila kitu kilikua kipya kwangu kama Mtoto Mchanga.
******
Siku zilisonga mbele, taratibu ule Uchungu ulianza kuondoka. Clara alihakikisha Kila baada ya Siku kadhaa naonana na Daktari wa akili ili kuona namna ya kunisaidia kurejesha kumbukumbu zangu. Nilikua nimetenganishwa na Jacob wa zamani, nilimfahamu Jacob wa sasa pekee.
Siku Moja Jioni, Clara aliniambia kua anahitaji kuongea na Mimi. Tulitoka na kwenda nje ya Mji, mahali Fulani pazuri sana. Palikua na Mgahawa mdogo lakini wenye hadhi ya juu, pesa haikua tatizo kwa Clara kwani alikua na uwezo mkubwa kifedha, alikua akiendesha biashara zake kubwa
Tulipofika hapo, aliagiza chakula. Ilikua jioni imeingia, kagiza ka kuchombeza kalikua kanaingia taratibu, taa nzuri zilikua zimewashwa.
Mara zote alikua akinitazama sana usoni Hadi nilianza kujihisi aibu kidogo lakini sikukubali kupotezwa. Baada ya kupiga mvinyo kidogo, alianza kuniambia
“Jacob, ni Miezi sita sasa. Nimekuita hapa kwa ajili ya mambo mawili” alisema kidogo Kisha aliachia tabasamu la kuniondoa shaka maana alihisi jambo ndani yangu. Nilianza kuhisi pengine alihitaji kuniambia niondoke kwake
“Umekua familia yangu, sikuwahi kukueleza chochote kile kuhusu Familia yangu” alisema Kisha alishusha pumzi kidogo halafu akaendelea “Mimi Sina Baba wala Mama, Sina ndugu wa aina yoyote ile. Niliokotwa na kulelewa kwenye vituo vya kulea Watoto Yatima, nilikulia huko na kusoma Hadi nikawa mkubwa, Sina ndugu wa kulalamika kwake hivyo nayajua Maumivu ya kuishi bila ndugu….Nisamehe kwa kua sababu ya wewe kuishi Kama Mimi” alisema huku chozi likimdondoka
Alinishangaza kidogo, sikuwahi kufikiria kua Hana ndugu yeyote maana ni jambo ambalo hakuwahi kunieleza kabisa. Iliniumiza sana “Clara usijali, yaliyotokea yameshatokea. Hakuna tunachoweza kufanya kurejesha chochote kile. Nilishakusamehe na Sina kinyongo kabisa halafu pole sana kwa uliyoyapitia, sikuwahi kufikiria kabisa”
“Umenisamehe kutoka Moyoni Jacob?”
“Shaka ondoa Clara”
“Ahsante sana”
“Usijali karibu” nilimpa tabasamu la kumwakikishia kua nilimsamehe kwa kila kitu.
“Jacob, siwezi kuendelea kuficha hili jambo. Limekua moyoni mwangu tokea siku ya kwanza nilipokuona kule Mgahawani, najua hukumbuki chochote kile. Naomba ujue Leo kua Nakupenda sana” Nilihisi mwili ukizizima, kama taa za mwili Ndiyo zilishtuliwa na kuwashwa kwa mara ya kwanza.
Nilimtazama Clara kama Mtu aliyepigwa na Bumbuwazi, neno nakupenda lilipenya Hadi ndani ya Moyo Wangu. Nilihisi kua neno kama hili niliwahi kuambiwa lakini sikukumbuka niliambiwa na Nani, wapi. Sikukwepesha macho yangu, nilimtazama sana Clara bila kusema chochote kile
“Najua hukutegemea kama ningelisema hili lakini Jacob” akasema Kisha akanishika kiganga Cha mkono Wangu na kuniambia
“Naomba uwe Mume wangu” alizidi kunisisimua mwili Wangu, nilimeza funda zito la mate nilimtazama kwa Mshangao, sikujua nifurahi au niulize maswali.
“Tafadhali Jacob” alisema Huku chozi likimbubujika, alionesha hisia zake zilikua za kweli na zilitoka ndani ya Uvungu wa Moyo wake, siku zote alikua mwema kwangu. Nilisimama pole pole huku nikimtazama, Uso wake ulionesha Mashaka, naye alisimama
Haraka nilizunguka na kumkumbatia kwa nguvu sana, nilihisi utulivu sana moyoni mwangu. Nilihisi kupata furaha isiyoelezeka, japo sikuwahi kua na hisia naye lakini maneno yake yaliibua hisia ya haraka sana.
“Jacob, nipo tayari kukupa Kila kitu changu ilimradi tu uwe Mume wangu. Maisha bila Mtu wa kumpenda ni sawa na Bure” alisema akiwa amejilaza kifuani.
“Clara….Nimehisi kupona ghafla kutoka kwenye Upweke, siku zote nilijihisi kama Mtu nisiye na pakwenda, niliyepoteza Kila kitu. Lakini uwepo wako mbele yangu ulikua na maana sana lakini Leo umekua na maana zaidi” nilimsikia Clara akilia kwa furaha.
Ukurasa mpya wa Maisha yangu na Clara ulianza jioni ile, Kila kitu kuhusu Mimi na yeye kilianza upya. Upendo, furaha tele vilitufuata Kila Kona, hatimaye Clara alipata Ujauzito baada ya Miezi kadhaa kupita. Tulipanga taratibu za ndoa, Kila kitu kilienda sawa
Tulifunga ndoa kubwa yenye gharama sana, ilikua ndoa haswa. Furaha yetu ilikua kupata Mtoto ndani ya ndoa, hatimaye Mimi na Clara tulikua Mume na Mke. Tuliendelea kulea Ujauzito Hadi pale alipojifungua Mtoto wa Kike, tulimpa jina la Melisa ili kumuenzi Mdogo wangu Melisa
Kila nilipomtazama Mwanangu Melisa nilijiona nikiwa nimepata bahati ya kuishi tena na Mdogo wangu.
“Hatimaye umempata Melisa wako Jacob” alisema Clara, alinifanya nitabasamu sana.
“Asante kwa kunipa nafasi ya kuishi tena na Melisa Wangu” nilisema. Clara alinitafutia Mwalimu na kunifundisha masuala ya Usimamizi wa Biashara, alikua akinifundisha nyumbani, alitokea Moja ya vyuo Bora sana Nchini.
Nilipokea masomo Kila siku, aliniandaa kuja kusimamia Biashara zake zote. Baada ya kuhitimu ulikua Ndiyo muda sahihi wa kuchukua umiliki na Usimamizi wa Biashara zote kama Mume wake, Kila kitu kilienda sawa nikawa ndiye Msimamizi Mkuu wa Biashara zote za Clara
Alikua na Makampuni zaidi ya Matatu Nchini. Nilifanya kazi kwa Bidii sana, Siku zilienda, Miaka ikasonga mbele.
CHUKUA ZAWADI YAKO KUTOKA KWA ADMIN wa Kijiweni Kwa Kugusa HAPA
Miaka mitano ilipita, Melisa alikua Mkubwa. Biashara ilikua kubwa zaidi, tangu kunipa Usimamizi Kila kitu kilibadilika hata yeye mwenyewe Clara aliona matunda ya kuniamini.
Siku Moja, mvua ilikua ikinyesha Mji mzima. Siku hiyo ilikua ni siku ya Kumbukumbu ya Kuzaliwa kwa Mtoto wetu Melisa. Nilihitaji kumaliza vikao mapema ili nirudi nyumbani kwa ajili ya Kusherehekea Siku hiyo pamoja na Familia yangu.
Hadi mishale ya Saa 12 jioni nilikua Bado sijamaliza. Nikazungumza na Melisa kupitia simu nilimwomba kua asherehekee na Mama yake kwani nilibanwa sana na kazi, lakini yeye alikubali kunisubiria Hadi nitakaporudi
Kusema ukweli, Melisa alikua na Upendo sana na Mimi pengine kuliko hata na Mama yake, siku zote alinisubiria Hadi niliporudi.
Basi, niliongeza Kasi ya kufanya kazi. Saa Moja Usiku, nilikua tayari kwa ajili ya kurudi nyumbani, nikiwa ndani ya gari nilipiga simu kwa Clara, nikazungumza na Melisa kwa njia ya video, alionekana ni mwenye furaha sana kunisubiria.
Basi, niliendesha gari kwa mwendo wa kawaida sana maana mvua ilikua ikinyesha tena haikua mvua ndogo ilikua kubwa sana. Nilipofika maeneo ya Morocco, taa za upande wa gari zinazotoka Mjini zilikua zimeruhusu, Mimi nilikua mbele zaidi, wakati tayari nimeshaingia katikati ya Barabara palitokea gari Moja ndogo nyeusi iliyotokea Kinondoni na kuingia mazima Barabarani.
Wakati natahamaki nikajikuta nimegongwa ubavuni, wenge zito likaniandama. Nilipojiangalia vizuri nilikua nikitokwa na Damu nyingi kichwani, nilihisi kupoteza uono mara ghafla hata fahamu zangu ziliniondoka.
Nini Kitaendelea? Usikose sehemu ya PILI
JIUNGE NA KIJIWENI WHATSAPP CHANNEL Kwa Kugusa Hapa
Soma Riwaya Nyingine Za Kijiweni Kwa KUGUSA HAPA
Wewe kama MFANYABIASHARA.. Kuna wakati unatamani kuwafikia watu wengi zaidi na hujui wapi pa kuanzia , USIJALI kwani hapa ndipo ambapo MTAA UNAONGEA na tuko tayari kukusaidia kuwafikia watu wengi kwa BEI YA OFA
Njoo Utangaze Nasi Sasa Kwa Kutuambia Una TANGAZO Gani na unataka kutangaza kwa muda gani kwa kutuma ujumbe hapa WwhatsApp Kupitia Namba +255760871896
Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love
3 Comments
https://shorturl.fm/xSZw0
https://shorturl.fm/oIYMW
https://shorturl.fm/dAqa1