“Jacob, nataka kuujua Msimamo wako kwangu. Utaniowa lini?” Aliuliza  Zaylisa, Nilishusha pumzi zangu. Nikageuka huku na kule kama Kuna Mtu alikua anatusikiliza pale Mgahawani. Nilikua nimevalia sare zangu za kazi  ya Uhudumu wa Mgahawa.  

“Zaylisa, naomba univumilie Hadi Mama yangu apone. Unajua fika  anaumwa, Mimi Ndiyo tegemezi. Halafu isitoshe Mpenzi wangu kwasasa  kipato changu kipo chini unafikiria Wazazi wako watanielewa?”  Nilimuuliza, kiukweli nilikua napitia kipindi kigumu Cha kifedha 

“Hadi lini Jacob?” aliniuliza huku akianza kutokwa na Machozi, macho  yake yalijaa Upendo sana lakini nilihisi Kuna jambo lililokua likimsumbua 

“Mpenzi nivumilie tu, najua unavyojisikia lakini haiwezi kuchukua muda  mrefu nitakua nimejipata” Ghafla Zaylisa aliondoka akiwa anakimbia huku  akionekana kama analia, sikuweza kumsimamisha sababu ulikua ni muda  wa kazi na sikutaka Mtu yeyote ajuwe kinachoendelea. 

Nilijaribu kumpigia simu lakini hakupokea, niliumia sana. Sikutaka kua  chanzo Cha Zaylisa kulia, mara zote alikua akinihimiza kwenda kwao  kujitambulisha lakini nilijawa na hofu. 

Familia Yao ilikua na uwezo kifedha, Mimi nilikua masikini ninayeishi  kumlea Mama yangu mgonjwa. Basi nilishusha pumzi Kisha nikaendelea na  kazi huku nikiwa mnyonge sana.  

*** 

Usiku baada ya Muda wa kazi kwisha nilijiandaa kwa ajili ya kuondoka.  Lakini ghafla alikuja Mdogo Wangu Melisa, alikuja mbio kama Mtu  anayefukuzwa, alishindwa hata kuongea huku akisema. 

“Kaka, Mamaaa!” 

“Mama amefanya nini Melisa?” nilimuuliza huku mapigo ya Moyo Wangu  yakianza kwenda Mbio, hisia mbaya iliniingia. Nilihisi Kuna jambo lisilo la  kawaida lilikua limetokea, hisia mbaya iliendelea kunipanda. Haraka  nikamwambia rafiki yangu Sudi kua naelekea nyumbani.

Tuliondoka mbio pale kuelekea Nyumbani, kutoka kazini kwangu Hadi  nyumbani siyo mbali sana. Tulipofika, nilihisi mwili Wangu ulikua  unaishiwa nguvu baada ya kumwona Mama akiwa ananing’inia kwenye  Kamba. Macho yalinitoka 

“Mamaa‼” nilimwita, alikua ameshajinyonga chumbani kwake. Nilifanya  haraka kufungua nikiamini pengine nitaweza kuokoa uhai wake.  

Basi nikaita Bajaji haraka, tukampeleka Mama Hospitali. Nilimtazama  Mdogo wangu akiwa analia, iliniuma sana, tumaini la Mama kua hai lilikua  dogo sana.  

Tuliketi Sehemu ya kumsubiria daktari aliyeingia chumbani, nilimkumbatia  mdogo wangu Melisa, roho iliniuma sana. Zilipita dakika kumi na tano,  daktari alitoka Kisha alisimama mbele yetu 

“Mnifuate” alisema yule Daktari, haraka tulimfuata kuelekea kwenye  chumba kimoja. Alitukaribisha vizuri sana huku akiachia tabasamu kana  kwamba alikua na habari njema ya kutuambia kuhusu Hali ya Mama yetu. 

“Nyie ni Nani yake?” aliuliza. Tulitazamana Mimi na Melisa, tulihisi amani  ndani yetu.  

“Watoto wake” nilijibu Kisha nilimwuliza 

“Hali yake ipoje Dokta, ni mzima?” Daktari akabadilisha uso wake,  akaondoa tumaini mioyoni mwetu, sura yake ikaonesha kua Kuna asilimia sifuri ya Uhai wa Mama yetu.  

“Poleni, amefariki” alisema.  

“Mamaa!” aligumia Melisa, pale pale alipoteza fahamu. Tulianza  kuhangaika na Hali ya Melisa, akakimbizwa wodini haraka. Chozi lilikua  likinibubujika bila kukoma, hapakua na Mtu kando yangu wa kuhisi  maumivu yangu, Niliketi peke yangu nikiweweseka, sikujua nilishike lipi niliache lipi 

Moyo Wangu uligawanyika, upande mmoja alikuwepo kwa Meliza na  Upande mwingine alikuwepo kwa Marehemu Mama yangu. Dunia ilikua  nzito, ilishuka kichwani kwangu 

Chozi lilikua likinibubujika, siku yangu iliharibika dakika za jioni kabisa.  

Nilijiinamia, nilikosa tumaini. Ghafla nilihisi kuguswa begani, nilishtuka.  Niliinua kichwa changu ili nimtazame aliyenishika

Macho yangu yalikutana na sura ya Mwanamke mmoja, sikukumbuka kama  niliwahi kumwona popote katika Maisha yangu, sikumfahamu lakini sura  yake ilionesha kunitambua na kuguswa na ninayoyapitia. Nilifuta chozi  langu Kisha nilijiweka tayari kumsikiliza 

“Pole..” sauti yake ya kwanza ilinifanya nizidi kudondosha chozi, alikua ni  Mtu wa kwanza kunitia moyo. Niliitikia kwa kichwa, mdomo Wangu ulikua  mzito, ulikua ukitetemeka tu. 

“Naitwa Clara, sijui kama unanikumbuka” nilitikisa kichwa changu  kuashiria kua nilikua simkumbuki  

“Usijali, kimetokea nini? Ulitoka mgahawani mbio, niliguswa sana. Hata  hivyo Mimi ni mteja uliyenihudumia kwenye meza namba 6” Niliitikia kwa  kichwa huku chozi likinibubujika, sikuweza kusema chochote zaidi ya kulia.  Akaniweka kifuani pake, alionesha kunijali sana. Nililia Hadi nililala  kifuani kwake, akaja kunishtua saa Sita Usiku 

Melisa alikua amesharejesha fahamu, daktari alitupatia utaratibu wa jinsi  ya kuuchukua mwili wa Mama. Gharama zote za Hospitali akazilipa Clara 

“Asante sana Clara” nilimshukuru, sijui ningetoa wapi pesa za matibabu ya  Melisa pamoja na gharama za kutoa Mwili wa Mama. 

“Usijali, tutakua pamoja Hadi mwisho Jacob. Mungu alipanga iwe hivi”  alisema. Tukaurudisha mwili wa Mama nyumbani, tulipofika tulikuta  ndugu wengine wakiwa wamefika hapo, Mjomba Masawe alikua  amesimama Mlangoni Kisha akaniuliza swali 

“Hukuona umuhimu wa kutupigia simu Hadi tumetaarifiwa na Majirani?”  alikua amekasirika, mara zote yeye ni mkorofi sana. 

“Anko, ningewezaje? Nilikua nimechanganikiwa sana. Samahani” nilisema,  Clara aliniangalia kwa jicho lenye maswali mengi sana. Basi akatupisha  tukaingiza maiti ndani, taratibu na mipango ya mazishi ikaanza 

Hakuna aliyenishirikisha kwa lolote, walikaa vikao vyao vya Siri na  kupanga taratibu zote. Sikujali sana sababu hata Mama alipokua hai  walikua ni Watu wenye Hila zao, hawakutaka sisi tuishi kwenye nyumba  Yao ya Urithi, walipigania kuiuza ila Mama ndiye aliyekua kizuizi chao. 

Siku iliyofuata, mazishi ya Mama yalifanyika. Baadaye kikao Cha familia  kiliketi 

Walikubaliana kwa Kauli Moja kua Mimi na Melisa tuondoke, wanauza  nyumba Yao. Hatukua na mahali pa kwenda. Nilimtia moyo Melisa, 

tulikusanya Kila kilicho chetu, hatukujua tungeenda wapi, hatukujua  tungeishi vipi lakini tulijipa moyo kua Kila kitu kitakua sawa 

Tulienda kwa Sudi maana ndiye Mtu pekee ambaye ningeweza kwenda  kwake na kutarajia msaada, ni rafiki pekee niliye naye. Sudi alitupokea  vizuri tu lakini palikua na kikwazo kimoja, tutawezaje kukaa wote watatu  chumba kimoja, Melisa ni Mwanamke angalau Angekua Mwanaume 

“Kaka, tusaidie kwa siku kadhaa wakati Mimi nahangaika nijue nampeleka  wapi Melisa” nilimwambia Sudi, akamtazama Melisa Kisha akakubali.  

Tulianza Maisha mapya nyumbani kwa Sudi, siku iliyofuata nilimtafuta  Zaylisa maana tokea ile siku hatukuwasiliana tena. Simu ya Zaylisa ilikua  haipatikani, ilianza kunipa Mashaka. Hapakuwahi kutokea siku Zaylisa  asipatikane kwa simu, nilijiuliza huwenda alikua amepata tatizo maana  sikumwona hata kwenye Mazishi ya Mama. 

Tuliondoka na Sudi kuelekea kazini, nilifanya kazi Hadi mida ya Mchana.  Baadaye niliitwa na Bosi, nilitegemea kusikia akinipa pole lakini Hali ilikua  ya tofauti kabisa, alinieleza kua hawezi kuendelea na Mimi kwamba  amepata Mtu mwingine.  

“Bosi, kwanini ni ghafla?”  

“Jacob, siku zote Shilingi Ina pande mbili. Huu ni upande mwingine ambao  ulikua hauutazami” alisema, nilihema. Sikutegemea kabisa kama  ningeikosa kazi bila sababu ya Msingi tena ndani ya Siku chache tu za  Matatizo ya kufiwa na Mama yangu. 

Miguu yangu ilikufa ganzi, mwili mzima ulikua ukiweweseka lakini maneno  ya Bosi yalikua kama msumali wa mwisho uliogongwa moyoni mwangu,  kilichoniumza zaidi ni Maisha tunayoishi 

“Asante Bosi..” Nilisema, Kisha niligeuka na kuondoka zangu, sikuamini  kama nilikua nikiziacha Kuta nilizozizoea, Watu niliowazoea hata kelele na  usumbufu wa wateja ambao nilishauzoea.  

Sudi alipoiona sura yangu alijua nilikua nimezongwa na mawazo, nilipoteza  Nuru. Niliona nimepoteza thamani juu ya uso wa Dunia, nilihisi uzito wa  Mzigo mwingine mzito nilioubeba 

“Jacob…Mbona una huzuni?” aliniuliza Sudi, nilishusha pumzi huku  nikizuia chozi lisinitoke mbele yake. Nikajikaza Kiume lakini moyo Wangu  ulijenga ufa.

“Moshi mweusi Sudi, nimepoteza tena Mimi” nilisema, ule Ujasiri ulianza  kuondoka niliangusha kilio mbele ya Sudi, chozi likinitiririka.  

“Una maanisha nini?” 

“Sina kazi tena, nimefukuzwa. Sijui nimeambukizwa mkosi gani Sudi, sijui  wengine wamemfanyia nini Mungu ambacho Mimi sifanyi” 

“Shii! Bro, nenda nyumbani, tutaongea zaidi huko” alisema Sudi,  niliondoka kazini taratibu. Macho yangu yalikua yakiyatazama mazingira  ya Mgahawa kwa mara ya mwisho, nilitembea kama Mtu aliyepoteza Kila  kitu.  

Nilipofika nyumbani kwa Sudi, nilimkuta Melisa akiwa ameketi kwenye  kochi dogo, aliponiona aligundua haraka sana kua siko sawa, alinifuata na  kunikumbatia. Sikusita kulia tena mbele yake, nilikosa ule Ujasiri wa  Kiume mbele yake 

Tuliketi nikamsimulia kilichotokea, niliona jinsi hata moyo wake  ulivyosononeka 

“Ulifanikiwa kumpata Wifi kwenye simu?” aliniuliza baada ya kumaliza  kumsimulia kuhusu kazi. Kiukweli Hadi muda huo simu ya Zaylisa ilikua  haipatikani, sikujua kama alipatwa na tatizo au aliamua kuzima simu yake,  kwa jinsi nilivyokua namfahamu isingelikua rahisi akae siku zote hizo bila  kuwasiliana na Mimi. 

“Melisa, Usijali. Naenda kwao sasa hivi nikazijue mbivu na Mbichi. Usijali  Mdogo wangu, Kila kitu kitakua sawa. Nitampata pia nitapata kazi nzuri  itakayobadilisha Maisha yetu” nilisema, angalau nilifamfanya atabasamu  kidogo, nikamfuta chozi lake 

“Vipi ulikula?” 

“Ndiyo Kaka, nimebakiza kwa ajili Yako”  

“Usijali, nikirudi nitakula sawa?” 

“Sawa, unaenda sasa hivi eeeh?” 

“Ndiyo, angalau nikimwona nitajisikia ahueni. Ubaki salama” nilisema  Kisha niliondoka.  

** 

Nilipofika nyumbani kwao Zaylisa ilikua ni mishale ya jua la utosi lililokua  likikimbia haraka, jasho lilikua likinitoka maana nilitembea kwa umbali 

mrefu. Nilishtuka kuona palikua na magari mengi, pia Watu walikua wengi.  Ilinifanya nijiulize maswali mengi yasiyo na Majibu 

“Kuna nini? Itakua amepatwa na Tatizo gani, au labda amefiwa na Wazazi  wake, au…?” kabla hata sijamaliza kutafakari nilimwona Mtu mmoja akija  upande Wangu akitokea nyumbani kwao Zaylisa. Niliona ni Bora  nimuulize, nilimsimamisha Kisha nilimsalimia kwa sauti ya kiungwana  sana, baadaye nikamuuliza 

“Samahani Kaka, pale Kuna nini mbona naona Kuna Watu wengi?”  akanitazama Kisha naye akageuka kuangalia tena kama vile hakutokea  huko, Kisha akaniuliza 

“Wewe ni ngeni hapa mtaani?” nikajichekesha chekesha kidogo Kisha  nikamjibu 

“Ndiyo, nilikua napita tu.” 

“Kuna harusi” 

“Harusi?” 

“Ndiyo, vipi umeshtuka Mzee?” 

“Nani anaolewa?” 

“Mtoto wa Mwenye nyumba anaolewa, anaitwa Zaylisa” alisema Kisha  aliondoka zake, hakujua alikua ameupasua moyo Wangu kiasi gani, hakujua  alikua ameuunguza moyo Wangu kwa kiasi gani. Chozi la pole pole lilianza  kunitoka, nilihisi kuishiwa nguvu.

Nini Kitaendelea? Usikose sehemu ya PILI

JIUNGE NA KIJIWENI WHATSAPP CHANNEL Kwa Kugusa Hapa 

Soma Riwaya Nyingine Za Kijiweni Kwa KUGUSA HAPA

Wewe kama MFANYABIASHARA.. Kuna wakati unatamani kuwafikia watu wengi zaidi na hujui wapi pa kuanzia , USIJALI kwani hapa ndipo ambapo MTAA UNAONGEA na tuko tayari kukusaidia kuwafikia watu wengi kwa BEI YA OFA

Njoo Utangaze Nasi Sasa Kwa Kutuambia Una TANGAZO Gani na unataka kutangaza kwa muda gani kwa kutuma ujumbe hapa WwhatsApp Kupitia Namba +255760871896 

Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx 

Exit mobile version