Ilipoishia sehemu ya nane ya In the name of LOVE
Ghafla tu, wazo la kumpigia simu Zaylisa lilinijia, nilihitaji kujua kama alikua amefika kwa Baba yake. Nilipopiga niliambiwa simu ya Zaylisa ilikua haipatikani, nilipatwa na hasira sana
Niliketi nikitafakari zaidi, hamu ya kuendelea kua ndani iliniisha. Niliona ni Bora niende mgahawani ambako nilikua nikifanya kazi, japo nilikua nimefukuzwa lakini niliamini huko ningepata mwanga zaidi wa Maisha yangu
Niliondoka, nikaita Taxi. Safari ya kuelekea mgahawani ilianza. Nafsi yangu ilikua kwenye Giza nene, hapakua na mwanga mithiri ya Handaki. Endelea
SEHEMU YA TISA
Nilimkumbuka rafiki yangu Sudi, Nilitamani sana kuonana naye maana tokea nilipofukuzwa kazi wiki chache zilizopita sikuonana naye tena, nilikua na uhakika kua alishiriki mazishi ya Mdogo wangu Melisa. Nilitaka kujua mengi sana kutoka kwake, basi Taxi ilitembea taratibu Hadi ilipofika Mgahawani.
Nilimlipa pesa dereva Kisha aliondoka zake, aliniacha nikiwa nimesimama mbele ya Mgahawa. Nilikua nimevalia suruali ya kaki yenye mifuko mikubwa, ilikua fupi, chini nilivalia sendozi nyeusi huku juu nikiwa na tisheti nyeupe
Nilitabasamu kidogo maana Mgahawa huo ulikua na kumbukumbu ya safari ndefu ya Maisha yangu. Ilinijia kumbukumbu ya Siku ambayo nilizungumza na Zaylisa Kuhusu kumuowa. Nilikumbuka siku hiyo Ndiyo siku ambayo Mama yangu alifariki kwa kujinyonga, lile tabasamu liligeuka kua huzuni nyepesi, chozi kidogo lilinilenga lakini sikuruhusu lidondoke
Macho yangu yalikua yakichemka ukali wa fukuto la chozi huku kope zangu zikicheza haraka haraka, nilivuta hewa nzito ili kufungua zaidi pua zangu.
Muda huo jua lilikua likianza kua Kali kidogo, nilitoa kitambaa na kufuta jasho pamoja na matone madogo ya machozi yaliyoganda kwenye kope zangu.
Halafu niliutazama zaidi Mgahawa, wakati huo Meneja alikua akikatiza kwenye kiunga, aliniona nikiwa nimesimama. Taratibu alisogea Hadi karibu na Mimi, nilipomwona nilitabasamu
Lakini yeye alitoa tabasamu la Mshangao kama vile alikua akijiuliza maswali mengi yasiyo na Majibu.
“Ooh Jacob” aliita kwa sauti ya Wasiwasi kidogo. Kisha alisogea zaidi “Ni Mimi hapa Meneja wangu” nilisema, nilizidi kumfanya anishangae.
“Karibu tu” alinikaribisha huku akinipa ishara kua niingie Mgahawani, tuliongozana huku nikiangalia huku na kule lakini sikufanikiwa kumwona hata Mfanyakazi mmoja niliyemfahamu, Kila Mfanyakazi alikua mpya machoni pangu kitu ambacho kilinishangaza
Nilihisi kutembea kwenye sakafu isiyonifahamu Mimi, niliona wakiwa wanahudumia Wateja tofauti tofauti, hata mpangilio wa meza, pazia na mapambo ulikua wa tofauti sana kama vile ulipitia muda mrefu nisioukumbuka
Nilitembea nyuma ya Meneja huku nikiwa na maswali mengi sana, macho yangu yalikua yakishuhudia vitu vingi vilivyonipa maswali mengi.
Tulielekea Moja kwa moja kwenye ofisi ya Meneja, alinikaribisha tena Kisha aliketi kitini huku akinitazama kwa Udadisi sana. Nilitabasamu kidogo huku nikiyapa nafasi macho yangu kubarizi ofisi ya Meneja, ilikua ni ofisi tofauti na ofisi niliyoifahamu
“Karibu sana Jacob” alinikaribisha tena, alikua ni Mtu wa kurudia maneno.
“Nimesha karibia Meneja wangu, wiki chache tu Kila kitu kimebadilika. Naona una sura ngeni Kila Kona ya Mgahawa, sioni wale Watu niliowafahamu” nilisema, Kauli hii ilimfanya anitazame kwa jicho la tofauti kidogo, alizidi kuonekana ni mwenye maswali mengi ya kuniuliza.
“Aah! Kwani Jacob…” alisema kwa kusitasita, nikamwahi
“Bosi usijali, najua ulinifukuza. Nimekuja hapa Nina maswali kadhaa, hata hivyo sikupanga kuonana nawe, nilikuja kwa ajili ya Sudi. Unajua nilipata ajali siku Moja baada ya kunifukuza hapa, angalau sasa najisikia nafuu” nilisema, niliuwona Msongo wa maswali ambao Meneja alikua akipambana nao
“Jacob upo sawa?” aliniuliza.
“Ndiyo Meneja wangu, vipi Sudi amefika kazini Leo?” niliuliza. “Sudi?”
“Ndiyo, maana sikumwona baada ya ajali. Hata hivyo nimempoteza Mdogo wangu Melisa sijui kama unalifahamu Hilo?” nilimuuliza, akameza funda
zito la mate huku akiniangalia kwa jicho la wasiwasi. Alianza kuwa mwoga na wala sikujua ni kwanini
Nilijitazama labda nilikua na kitu kilichoanza kumpa hofu lakini sikuona. “Aah Unajua Sudi….aaah‼” alijiuma uma, nikamuuliza tena “Au naye ulimfukuza?”
“Aaah‼ Ndiyo, aliacha kazi mwenyewe hivyo sikujua hata alielekea wapi” alinijibu, nilishusha pumzi zangu
“Basi sawa, nilikuja kumtazama yeye tu. Maana nimeshauriwa na Daktari kua siruhusiwi kutumia simu hivyo nimeshindwa kufanya mawasiliano naye” nilisema Kisha nilinyanyuka, naye alinyanyuka huku akinitazama sana
“Jacob, upo sawa?” aliniuliza swali lile lile, nilijua pengine alisikia kua nilipata ajali na labda alikua akijali kuhusu afya yangu.
“Usijali nipo sawa, Wacha nikamwangalie anapoishi” nilisema Kisha niliondoka pale ofisini, kitu pekee nilichotaka ni kuonana na Sudi maana ni Mtu pekee ambaye angeliweza kuniambia mambo mengi nisiyoyaelewa katika Maisha yangu baada ya ile ajali.
Kutoka pale Mgahawani Hadi anapoishi Sudi palikua na Umbali kiasi, wastani wa dakika kama ishirini na tano kwa usafiri. Nilitumia usafiri wa Bajaji, kichwa kilianza kuniuma kwa mbali lakini niliona ni Bora niende kwa Sudi ili kufahamu mengi nisiyoyajua kuhusu Mimi.
Nilijiona ni Mtu niliye gizani, wiki chache za ajali zilibadilisha mambo mengi sana. Sikua na tofauti na kitabu kilichopoteza baadhi ya kurasa kwa kuungua na Moto, tumaini pekee lilikua ni Sudi.
Tulipofika, nilimpa hela dereva Kisha pole pole nilitembea kutoka Barabarani kuelekea mtaani, ndani huko ambako hata Bajaji lisingeliweza kupita kirahisi. Mitaa ile haikua mipya kwangu, nilikua naifahamu vizuri sana.
Basi nilitembea kwa dakika kama mbili hivi, nilihisi kiu ya Maji tena ya Baridi, niliona Duka nikaingia nikanunua Maji Kisha nikanywa na kusonga mbele Hadi nilipofika anapoishi Sudi. Ilikua ni nyumba ya uswahilini yenye geti dogo Jekundu, niligonga na kusubiria lifunguliwe
Mara nilisikia sauti ya kufunguliwa Kisha nilimwona Mwanamke mmoja mfupi mweusi, aliyejifunga kilemba chekundu, alivalia Dera la rangi ya kahawia
“Karibu” alisema, sura yake ilikua ngeni machoni pangu ila sikutaka kulijadili Hilo sababu wapangaji hasa nyumba za Mijini huama Kila kukicha. Nilitabasamu kidogo maana Ndiyo ilikua Haiba yangu kubwa
“Ahsante, samahani. Namuulizia Sudi, sijui nimemkuta?” alistaajabu kwa kuguna kidogo Kisha akaniambia
“Mh! Kaka yangu Mimi ni mgeni tu hapa, nimehamia juzi. Simjui huyo Sudi labda uingie kama unakifahamu chumba chake” alisema, basi niliingia nikiwa nyuma yake Hadi eneo la Uwani, maana Sudi alikua akiishi chumba Cha Uwani.
Chumba chake kilikua kimefungwa kufuli kubwa, nilishusha pumzi maana nilijua atakua ametoka na kwa jinsi alivyofunga basi alikua mbali na nyumbani.
“Chumba chake ni kile pale lakini kimefungwa” nilimwonesha yule Mwanamke.
“Kwani mbona nilisikia kua kile chumba kina Siri” alisema, kidogo nilishtuka.
“Siri, una maanisha nini?”
“Mh! Samahani , nimesikia kile chumba hakipangishwi. Huu ni mwaka wa Tano sasa” alisema, nilijikuta nikicheka maana kwa ninavyofahamu nilikua nikiishi mle Mimi, Sudi na Mdogo wangu Melisa tena ni wiki kadhaa tu zilizopita.
“Hebu acha utani Bwana, kile chumba anaishi rafiki yangu Sudi. Labda tu ulisikia vibaya” nilisema lakini sura ya yule Mwanamke haikubadilika Bali iliendelea kuonesha kua alichokisema alikimaanisha
“Kaka yangu, Mimi nimeelezwa na Mwenye nyumba maana lengo langu lilikua nipange kile chumba. Niliambiwa kua ndani ya kile chumba alifia Msichana tena aliuawa na huyo unayemsema sijui ni Sudi kama sikosei
Kisha akakimbia, tangu hapo hakuna aliyeishi tena hivyo mwenye nyumba aliamua kukifunga.” Alisema kwa sauti ya Msistizo, nilijikuta nikiishiwa nguvu Hadi nilipepesuka. Kizungu-zungu kiliniandama Hadi Niliketi juu ya ndoo
“Kwani huyo Sudi wewe ni Nani Yako?” aliniuliza, nilimeza funda zito la mate. Nilihisi kuzidi kupagawa, nilichokisikia ni kama kilikua kwenye filamu au vitabu vya Riwaya. Ingewezekana vipi kifungwe kwa Miaka mitano kisa Sudi alifanya Mauwaji wakati Meneja aliniambia aliacha kazi, kama angelikua amefanya tukio Hilo ningejua sababu Mimi ni rafiki yake.
Jasho lilikua likinitoka, nilimuuliza yule Mwanamke aliyekua mbele yangu “Huyo Msichana aliyemuuwa alikua ni Nani?”
“Nitajuaje Mimi, hata hivyo sikupaswa kuyasema yote haya. Hujajibu, huyo Sudi ni Nani Yako?”
“Rafiki yangu, Ona Dada yangu. Mimi nilipata ajali wiki chache zilizopita, nilimwacha Mdogo wangu na Sudi, unaposema chumba hakitumiki kwa Miaka mitano sasa nastaajabu. Ni ndoto ya aina gani hii?” nilisema, mara Simu ya yule Mwanamke iliita.
“Mume wangu ananipigia, hicho ndicho nilichokisikia na wala Sina Cha ziada” aliondoka akiwa anaongea na simu, aliniacha nikiwa nimekaa juu ya ndoo, nilitamani kuamini lakini uhalisia ulinikataza.
Nilipata wazo la kurudi Mgahawani kwa meneja, niliamini sasa ni yeye ndiye anayeweza kufumbua Fumbo hili, nilinyanyuka taratibu kama Mgonjwa. Nilitembea kwa kujiburuza huku jasho likinitoka, nilikua nimechanganyikiwa sana. Kila kitabu nilichofungua ili nifahamu mengi kilikua na mapungufu ya kurasa muhimu, sasa nilirudi Mgahawani
Nilielekea Moja kwa moja Hadi ofisini kwa Meneja, nilimkuta akiwa anaendelea na majukimu yake. Aliponiona alinyanyuka kitini na kunitazama kwa Mshangao, alionekana kama Mtu aliyetarajia kua ningerudi kwake
Nilikua navuja jasho, nilichoka sana. Nikaketi nikiwa kimya sana, shingo yangu ilikua ikiangalia chini, Jasho lilidondokea kwenye Suruali yangu
“Jacob” aliita Meneja, taratibu nilinyanyuka kichwa changu nilimtazama, alinitazama bila kusema chochote kile.
“Naishi Dunia ipi?” nilimuuliza, aliinamia chini. Alionesha kujutia kwa jambo Fulani ambalo hakuniambia nilipofika kwa mara ya kwanza kumuulizia Sudi.
“Jacob, samahani”
“Samahani ya Nini?” nilimuuliza, alipoanza kunyanyuka Mdomo wake ghafla alikatishwa na sauti ya kufunguliwa kwa Mlango, Nami nilishtuka.
Niligeuka haraka kutazama mlangoni, Zaylisa alikua mbele ya macho yangu. Nilimtazama kwa kustaajabu sana, aliwezaje kujua nilipo?
“Jacob” aliniita kwa sauti ya taratibu, Kisha alimtazama Meneja.
“Nitakueleza Kila kitu, naomba turudi nyumbani” alisema, nilijawa na tumaini
Kitu pekee nilichohitaji ni kujua mengi yaliyokua yakizunguka kichwani kwangu, Basi. Mimi na Zaylisa tuliondoka pale Ofisini kwa meneja bila kusikia chochote Cha umuhimu kutoka kwa Meneja, ni kama Zaylisa alikua amekatisha mazungumzo yetu lakini kwakua alikua ameniambia atanieleza Kila kitu ilikua rahisi kwangu kukubali.
Tulitumia usafiri wa Taxi Hadi nyumbani kwa Clara, palikua kimya sana hakuna aliyezungumza na mwenzake. Palitulia kimya mithiri ya Usiku wa Giza nene, nilitembea taratibu huku kichwa changu kikiwa kimejaa maswali mengi, nyuma yangu nilikua nikizisikia hatua za Zaylisa, kiatu chake kirefu Cha kuchongoka kilikua kinamtoka sauti ya ‘KO! KO!’
Nilitekenya kitasa huku mkono mmoja ukiwa nyuma ya kiuno changu, nilielekea Kuketi kwenye sofa kama Mtu aliyepoteza tumaini, Zaylisa naye aliingia Kisha aliufunga mlango. Pole pole naye alisogea kando yangu Kisha akafungua kinywa chake kwa sauti ya utulivu sana
“Jacob” aliniita, niligeuza shingo nikamtazama. Alikua amebana midomo yake Kisha akanishika bega taratibu, mguso wa kunituliza
“Pole, najua una maswali mengi lakini nitayajibu” alisema Kisha alinyanyuka, nilikua namtazama kama Mtu aliyekua na mengi niliyokua nikiyatafuta. Kisha aliekea kwenye friji, akatoa Maji ya baridi akayamimina kwenye glasi, akarudisha jicho kwangu
Halafu pole pole akaja nilipokua nimekaa, naye akakaa na kuniambia
“Tafadhali kunywa kwanza haya Maji Mpenzi wangu Kisha nitazungumza nawe” nilimtazama nikiwa kimya, sura yangu ilikua na uchovu mwingi. Akanipatia glasi, nikatumia mkono Wangu wa kushoto kupeleka glasi kinywani Kisha nikaruhusu koo langu kupitisha Maji ya baridi
Nilipiga funda Nne za nguvu, kweli nilijisikia utulivu. Zaylisa akaichukua glasi kutoka kwangu na kuiweka juu ya meza ya halafu akanitazama huku akitabasamu.
“Ulijuaje kama nilikua pale?” nilimuuliza kwa sauti ya umakini, Kisha nilimtumbulia macho.
“Jacob, najua una maswali mengi sana. Nitajibu Moja baada ya jingine” alisema Zaylisa
“Nataka kujua, Mimi ni Nani Zaylisa? Kwanini Kila kitu kimebadilika ndani ya wiki chache tu?” nilimuuliza maswali mawili yaliyomfanya apumue kwa kina kabla ya kuitumia sauti yake tulivu kunijibu.
“Wewe ni Jacob wangu, yule yule niliyempenda na ninayempenda. Jacob, baada ya ajali Kuna kitu hakipo sawa kwako” alisema Kisha alisita kuendelea, nikamuuliza
“Hicho kimefanya Kila kitu kibadilike? Sudi alimuuwa Mdogo wangu na siyo kama ulivyoniambia kua Melisa alikufa kwa mshituko?”
“Hapana, Melisa alikufa kwa Mshituko Jacob. Nilikuwepo kwenye Mazishi, Jacob Bado haujapona vizuri unapaswa kutuliza akili Kisha Kila kitu kitakua sawa. Kila unachokiona hakipo kama unavyofikiria, jipe muda Kisha ukipona utaona mambo yanaenda inavyotakiwa” alisema Zaylisa, hakukata kiu ya maswali yangu. Ni kweli nilipata mtikisiko wa Ubongo kidogo kutokana na ajali lakini Bado akili yangu ilikua sawa Kwani nilikua natambua lakini nilihisi Kuna Sehemu ya Maisha yangu ilikua imerukwa.
Chozi lilinidondoka taratibu, upande mmoja wa akili yangu uliniambia kua nilikua ninaishi kwenye Dunia iliyojaa siri na Giza lakini upande mwingine uliniambia kua nilikua Pengine akili yangu ilikua inapitia changamoto kidogo
“Lakini Zaylisa, ni kwanini Watu huniita Bosi? Mimi ni Nani hasa, kitu gani sikijui kuhusu Mimi?” nilimuuliza, hakunipa jibu, alinisogeza na kunilaza kifuani pake huku akipapasa nywele zangu taratibu.
**
SURA YA 8
(Mpango wa Siri)
Jioni ilipoingia ilinikuta nikiwa nimeketi valandani, nilikua nabarizi kidogo huku nikipigwa na jua jepesi lililokua likielekea kuzama. Kila nilichokiona mbele yangu kilikua kina rangi nyekundu ya jua, upepo ulikua ukivuma taratibu sana
Palikua kimya, nilihitaji ukimya huo ili kunituliza akili yangu iliyokua ikipotea mara kwa mara. Nilikua nimekunja Nne nikiwa nimeketi kwenye kiti Cha nyavu kilichonipa utulivu, nilivalia singlendi nyeupe na Suruali nyepesi
Alikuja Zaylisa, alikua ameshikilia sahani yenye matunda. Nilipomwona nilimwonesha tabasamu, naye alinirudishia tabasamu
Zaylisa ni Mwanamke mzuri sana ambaye Kila Mwanaume alihitaji kua naye, tabasamu lake lilikua tiba isiyoonekana ya Moyo Wangu. Nilimtazama kidogo Kisha alisema
“Usiwaze sana kuhusu Dunia Yako Jacob. Kila kitu kitakua sawa” alisema huku akivuta kiti na Kuketi.
“Karibu matunda Mpenzi” alisema tena, alinipatia sahani yenye matunda pamoja na Uma. Nilichoma kipande Cha tiki Maji Kisha nilikitia Mdomoni na kukitafuna pole pole
“Asante My love. Uwepo wako ni tulizo tosha kwangu” nilisema huku nikimalizia kutafuna, akanishika mkono akaniambia
“Nitakua na wewe Maisha yangu yote Jacob, sitakuachilia hata kama penzi letu litapitia njia yenye Milima na mabonde” maneno yake yalinifanya nitabasamu tu, Kila Mwanaume hutulizwa kwa Maneno mazuri na matamu kama haya
“Lakini Zay, Bado nahisi Kuna kurasa ya Maisha yangu imeondolewa kwenye kitabu changu” nilisema, Zaylisa alinisugua mkono Wangu taratibu akaniambia
“Najua na ninakuelewa, unavyojihisi kwasasa hata Mimi najisikia vibaya Jacob. Kamwe sitakua sawa Hadi pale nitakapo hakikisha upo sawa”
Licha ya maneno mazuri na ya matumaini kutoka kwa Zaylisa Bado nilikua na wasiwasi kuhusu Mimi. Nilifikiria kuhusu ile Bahasha, sikujua ilikua imepotelea wapi?
Kama Matilda hakuichukua sasa Nani mwingine aichukue, kwanini ipotee ina nini ndani yake? Nilijiuliza yote lakini mwisho nilijiuliza kuhusu Mtu ambaye Zaylisa alikua amempigia simu asubuhi ‘MZEE WA MIPANGO’
“Babe” nilishtuliwa na Zaylisa baada ya kuona nilikua nimezama mawazoni, nilishtuka Kisha niliigiza kama vile nilikua sawa tu. Kabla hajasema neno lingine mara Simu yake iliita, haraka aliangalia ni Nani alikua akimpigia
Ghafla sura yake ilipoteza uchangamfu, akaonekana kua na wasiwasi.
“Samahani naongea Na simu” alisema Kisha aliondoka pale akaelekea ndani, sikutaka kujishughulisha sana. Niliendelea kula matunda
Haikuchukua muda mrefu, Zaylisa alirudi akiwa na furaha.
“Kulikoni mbona unafurahia sana, halafu hujanambia kuhusu Hali ya Baba Yako” nilimuuliza.
“Kumbe haikua inshu kubwa sana Mpenzi, Presha ilipanda kidogo. Ah! Mama yangu naye akalikuza sana” alisema huku naye akichukua kipande Cha tunda kwa kutumia mkono wake Kisha akaliweka Mdomoni.
“Na vipi kuhusu hiyo simu, una furaha sana”
“Eeh! Mama alikua akinipa mrejesho kuhusu Hali Baba” alisema Zaylisa. Niliguna tu Kisha niliendelea kula matunda.
Siku iliyofuata asubuhi mapema, Zaylisa aliniaga kua anaenda kumjulia Hali Baba yake, tukakumbushana kua ilikua ni siku ya Clara kurudi kutoka Arusha.
Nini Kitaendelea? Usikose sehemu ya KUMI
JIUNGE NA KIJIWENI WHATSAPP CHANNEL Kwa Kugusa Hapa
Soma Riwaya Nyingine Za Kijiweni Kwa KUGUSA HAPA
Wewe kama MFANYABIASHARA.. Kuna wakati unatamani kuwafikia watu wengi zaidi na hujui wapi pa kuanzia , USIJALI kwani hapa ndipo ambapo MTAA UNAONGEA na tuko tayari kukusaidia kuwafikia watu wengi kwa BEI YA OFA
Njoo Utangaze Nasi Sasa Kwa Kutuambia Una TANGAZO Gani na unataka kutangaza kwa muda gani kwa kutuma ujumbe hapa WwhatsApp Kupitia Namba +255760871896
Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love
2 Comments
https://shorturl.fm/I3jXn
vpj4ud