Ilipoishia Nzena (Kijiji Kilicholaaniwa) sehemu ya pili
Alipiga magoti na kujiinamia huku chozi likimtoka Zahoro, yeye na Baba yake pekee ndiyo ambao walikua wa kwanza kutambua kua laana ya Kifo cha Masumbuko iliyotolewa na Bibi Lugumi ilikua imeanza kufanya kazi, lakini ni yeye pekee ndiye aliyegundua kua hakuna anayeweza kuondoka hapo Kijijini kuanzia muda ambao aliiota Laana ile na kuisikia sauti ya laana ya Bibi Lugumi
Akiwa hapo anatokwa na mchozi, mara alivamiwa na walinzi wa Kijiji waliotumwa na Mzee Kova kumkamata. Dunia yake ilijaa mishangao sana, akawauliza kwa sauti ya upole huku chozi likimtoka.
SEHEMU YA TATU
“Kwanini mnahangaika na Mimi, sina ubaya. Mmemkamata na Baba yangu pia?” tayari alikua ameshasimamishwa, hakujibiwa chochote isipokua alisogezwa mbele ya nyumba ya Mzee Kova kisha mlinzi mmoja akatumwa kuelekea mazishini kumwita Mzee huyo mwenye mamlaka makubwa kuliko hata viongozi wa Kiserikali wa Kijiji cha Nzena.
Alifungwa kamba huku walinzi wakiendelea kumshikilia, Zahoro akawaambia
“Kijiji chetu kimelaaniwa, hakuna atakayetoka wala atakayeingia. Tutakufa kama Kuku kwenye ardhi yetu na hakuna atakayejiokoa” alisema huku mwili ukimsisimka kutokana na uzito wa Maneno hayo, chozi lilizidi kumbubujika.
Wale walinzi walimtazama Tu Zahoro bila kusema chochote kile, sauti ya Mzee Miroshi ilizidi kusikika pia.
Haikuchukua hata nusu saa, msafara wa Wazee wa Kijiji watano ulifika hapo. Mzee Kova alionekana kua na hamu ya kuzungumza na Zahoro. Alipewa kiti kisha aliketi mbele ya Zahoro akamtazama kidogo kisha akamwuliza
“Ni wewe uliyesema Kijiji hiki kina laana?” alimwuliza kwa sauti ya ukakamavu iliyotoka taratibu, huku jicho jekundu likiwa linamtazana Zahoro, Wazee wengine wakiwa wamemzunguka Kijana huyo.
“Sio Mimi, bali aliyetoa laana. Tumelaaniwa kwa makosa ya Watu wachache walioamini wanajua kila kitu. Hakuna atakayeweza kuingia wala kutoka Kijijini kuanzia sasa” alisema kwa kujiamini sana Zahoro sababu alikua na uhakika na anachokisema.
Wazee wote waliangusha vicheko vya dhihaka, ilionekana kua ni jambo lisilowezekana lakini Zahoro akawaambia
“Kifo cha Masumbuko na Bibi yake ni laana kwetu. Tutakufa sote” alisema kwa kushupaza shingo na sauti yake, akanaswa kibao na Mzee Kova ambaye alionesha kukerwa na kauli ya Zahoro. Kisha akawaambia Walinzi
“Wawili waende haraka Kijiji jirani, mrudi hapa na taarifa njema. Kisha atauawa huyu Mpuuzi na Baba yake” alisema kisha walinzi wawili walianza safari kwa kutumia Baiskeli, kutoka hapo kuelekea Kijiji jirani ni mwendo wa nusu saa kwa kutumia Baiskeli.
Mzee Kova na wazee wengine walisubiria huku Zahoro akipigwa na jua lililokua likianza kua kali, muda ulienda. Macho ya Wazee wote yalikua yakiitazama njia waliyoondoka nayo wale walinzi. Haikuchukua hata dakika 20 Watu hao walirejea wakitokea njia nyingine
Kila mmoja wao alitoa simulizi ya kutatanisha iliyoamsha hasira ya Mzee Kova, iliamsha hisia ya tofauti kwa Wazee wengine ambao macho yao waliyapeleka kwa Zahoro aliyekua akitabasamu licha kufungwa huku akipitia mateso.
Kisha Mzee Kova akawauliza tena kwa msisitizo huku akiwakazia macho, kwa jinsi ambavyo alikua akiogopwa isingelikua rahisi wale Walinzi kusema Uwongo.
“Tumeshindwa kufika kijiji jirani, kila tulivyokanyaga pederi tulijikuta bado tupo Kijiji Mkuu” Mzee Kova alipepesa macho yake kisha aligeuka kumtazama Zahoro halafu akarejea kuwatazama Walinzi wale halafu akawaambia
“Nendeni mkamfunge Zahoro pamoja na Baba yake chumbani, kisha mniitie Mtimbe sasa hivi” alisema kwa hasira sana, palikua kimya sana isipokua sauti yake, Mtimbe ndiye Mganga wa Kijiji cha Nzena, ndiye aliyemuuwa Masumbuko Usiku ule na kufanya tambiko.
Haraka maagizo yake yalitekelezwa ndani ya muda mfupi, Mganga Mtimbe alikua mbele ya macho yake wakiwa wote wameketi kwenye Baraza lake hapo nyumbani kwake Mzee Kova.
“Bila shaka umeshaipata habari si ndiyo?” alianza Mzee Kova huku mshipa wa kichwa ukiwa umemtoka. Mtimbe akauliza kwa utiifu sana
“Habari ipi hiyo?”
“Laana iliyotamkwa na Bibi Lugumi”
“Imefanya nini?”
“Usiulize kama Mtoto mdogo usiye na maono Mtimbe” akahamaki Mzee Kova kisha akaweka utuo na kuendelea
“Nilitegemea ungekua wa kwanza kuona kisha tukaidhibiti, umezidiwa uwezo na kijana mdogo wa hapa Kijijini. Ni hivi, hakuna anayeweza kutoka wala kuingia Kijijini, hii misiba ya mpigo ni kwasababu ya laana hiyo” Maneno ya Mzee Kova yalimnyong’onyeza Mtimbe, alionekana kulegea mwili mzima huku kijasho kikimtoka
“Mkuu ngoja nilifanyie kazi hilo mara moja”
“Sema unahitaji nini?”
“Ngoja niangalie ukubwa wake kisha tuone tunahitaji nini haraka, wacha nikimbilie nyumbani kuchukua kila kitu” alisema huku akisimama na kuondoka kwa kukimbia, aliacha taharuki kubwa sana miongoni mwa Wazee, hadi kufikia muda huo ni wachache walioigundua laana hiyo hapo Kijijini Nzena.
**
Ikulu ya Rais.
Rais Besigwe alikua ameketi kitini akitabasamu, mbele yake alikua ameketi waziri wa Ardhi. Kicheko kilimtoka Rais Besigwe kisha akamtolea sauti Waziri aliyejiinamia
“Kijiji kupotea?”
“Ndiyo, Mkuu. Kiasi chote cha madini kimebakia kua hadithi ya kusimulia vizazi vyote. Migodi imepotea na utajiri mwingi wa Nchi, hata ile ardhi tupu iliyobakia yenye pori dogo hakuna tena madini” alielezea Waziri huku akimtazama Rais kwa macho yake
madogo yenye kope fupi. Mikono ya Waziri ilijaa utii mezani, huku Rais akimtazama Waziri kwa jicho lisilo na uhakika wa nini alikua nataka kukisema tena. Sura ya Rais ilijaa maswali na umakini hasa baada ya Waziri kurudia alichokisema Mwanzo.
“Siwezi kuamini, Nahitaji kuelekea huko Mashariki” alisema Rais, mara moja Waziri aliondoka hapo akiwa anajua kua Rais hakuweza kumwamini.
Siku iliyofuata, ndege maalum ya Rais Besigwe iliota mbawa kutoka Mji Mkuu wa Nchi ya Ganza kuelekea kusini mwa Nchi hiyo, hamu na shahuku yake ilikua kutomasa alichokisikia. Kila aliyesikia safari ya Rais huyo alijisemea kua Rais alikua Tomaso. Ndani ya ndege aliambatana na Waziri wa Ardhi na Mali kale, pamoja na jopo la Walinzi
Hali ya usalama iliimarishwa hadi kufika kwake na kukanyaga Ardhi iliyokua ikizungumzwa zaidi Duniani. Kwa kutumia magari walianza safari kutoka wilayani kuelekea Kijiji cha Nzena. Masaa mawili yalitosha kuwafikisha huko
Rais alioneshwa mahali hapo kwa kutumia vidole na ramani, kwanza alichuchumaa na kuchota mchanga kisha akasema
“Hakika sikuona kila kitu, leo Mungu ametuonesha na kuturudisha enzi za Mitume” kisha alisimama na kuagiza mchanga aliouchota upelekwe Ikulu Kama ukumbusho. Aliporejea Ikulu alihutubia Taifa kwa kutoa taarifa kamili ambayo mwanzo ilidhaniwa kua ilikua ni uvumi tu. Kisa cha Kijiji cha Nzena kikachukua sura mpya.
**
Kijijini Nzena.
Muda ulizidi kwenda, jua lilizidi kutua na kua kali sana kuashiria kua Mchana ulikua umeshaingia. Mzee Kova na Wazee wengine walikua wakimsubiria Mganga Mtimbe.
“Kwanini usitume Mtu kumkagua?” aliuliza Mzee Kisugu. Mzee Kova akamtazama Mzee Kisugu kisha akamgeukia mlinzi mmoja wa Kijiji akamwambia
“Nenda uje na Mtimbe haraka” alisema, kisha haraka Mlinzi mmoja alichukua Baiskeli na kuelekea nyumbani kwa Mganga Mtimbe. Palikua na umbali kiasi lakini si wa kuchukua nusu saa haujafika.
Mlinzi alipofika aliteremka kutoka juu ya Baiskeli akiitazama nyumba ya Mtimbe iliyojengwa kwa udongo na kuezekwa kwa nyasi kavu mpya. Palikua Kimya, haikumtia hofu, badala yake alisogea mlangoni na kumwita kwa jina lake
Aliita kwa dakika mbili za bila kupokelewa, kisha aliilaza basikeli chini, akazunguka nyuma ya nyumba akiamini huwenda alikua huko. Alipofika nyuma alikutana na habari mpya ya kuipeleka kwa Mzee kova. Mganga Mtimbe alikua akining’inia kwenye kamba juu ya Mti mkubwa ulio nyuma ya nyumba yake karibu na choo.
Moyo wa Mlinzi ulianza kumwenda mbio akiutazama mwili wa Mtimbe aliyejinyonga huku Mkononi akiwa ameshikilia kipande kikubwa cha karatasi.
Akili na hisia ya Mlinzi vyote vilikubaliana kua asogee hapo kuangalia zaidi, aliangaza huku na kule, hapakuonekana kua na dalili ya ujio wa Mtu yeyote yule. Basi, mlinzi alisogea taratibu hadi alipoufikia mwili huo.
Macho yake aliyapeleka usoni kwa Mtimbe, povu lilikua likimtoka huku macho yake yakiwa yamemtoka pia. Aligeuza shingo yake haraka kutazama pembeni huku hali ya kichefu chefu ikianza kumshika. Mlinzi akahisi hali ya kutaka kutapika, lakini shahuku yake kubwa ilikua ni kuchukua ile karatasi aliyoishika Mtimbe.
Haraka aliivuta kisha alitoka ‘nduki’ kurudi alipokua ameiacha Baiskeli yake. Alipofika hapo alianza kutapika, alishangaa kuona alikua akitapika damu. Hali ya kumwogofya ilizidi kuongezeka, alikua akihema sana.
Akaona ni bora aangalie kilichoandikwa kwenye karatasi hiyo aliyoichukua kwa Mtimbe, alikutana na maandishi Yaliyoandikwa kwa wino mwekundu, yakisema
“MWISHO UMEFIKA” , alitulia kiasi akiwa amesimama huku akihisi kuna jambo lilikua likifanyika mwilini mwake. Mlinzi huyo, alihisi eneo la sikio, kisha puani. Alipopeleka kidole alikutana na damu nyeusi iliyokua ikitoka kwa mabonge mabonge.
Hali ya hofu ilianza kumzidia Mlinzi, alihisi hali ya kuchanganikiwa akajikuta akipiga yowe huku akikimbia kurejea nyumbani kwa Mzee Kova kupeleka taarifa ngumu. Hakukumbuka kuhusu baiskeli yake, mkononi alishikilia karatasi. Alikimbia sana kiasi kwamba alihisi kuchoka, kila aliyemwona alimshangaa sana.
Alipofika njia panda ya kuelekea nyumbani kwa Mzee Kova alianguka. Mahali hapo palikua na Watu wawili, Mke na Mume waliokua wamebeba kuni kichwani. Waliona ni bora wampe msaada, haraka walimkimbilia, walipomfikia walimkuta akiwa amepoa kabisa.
Mume alimtazama Mke wake kwa Mshangao, wote walitazamana huku wakigeuza macho yao na kumtazama mlinzi aliyekua amelala kifudi fudi akiwa ameificha sura yake.
“Tumsaidie?” aliuliza Mume, Mke alimtazama Mume wake kisha akatikisa kichwa kuashiria kua wamsaidie. Taratibu, Mume alimgeuza Mlinzi. Aliona namna ambavyo damu ilikua imetapakaa usoni, wote kwa pamoja waliiona karatasi ambayo yule Mlinzi alikua ameishikilia
Mara moja yule Mume aliichukua ile karatasi na kuanza kuisoma, akakutana na neno lile lile “ MWISHO UMEFIKA’’
Baada ya kuisoma ile karatasi alijikuta akitafakari bila kusema chochote kisha akamtazama Mke wake ambaye aliingiwa na wasiwasi kutokana na ukimya wa Mume wake.
“Mbona upo kimya, umekutana na nini?” aliuliza yule Mke huku uso wake ukiwa umejawa na Mshangao Mkubwa sana. Mume wake akampatia ile karatasi Mke wake bila kusema chochote kile huku akimtazama yule Mlinzi aliyelala chini akiwa hapumui.
Mke alipoisoma ile karatasi aligeuza macho kumtazama Mume wake kisha kwa mshangao akamwambia
“Mume wangu unatokwa na Damu puani” alisema akiwa anarudi nyuma taratibu, Mume wake akapeleka kidole puani. Alikua akitetemeka akikiangalia kidole chake kilichotapakaa damu. Kisha alimtazama Mke wake, aliiyona damu pia puani kwa Mke
wake. Akamnyooshea kidole kumwambia kua anatokwa na damu, naye Mke alipopeleka kidole puani aliiyona damu mbichi.
Nini Kitaendelea? Usikose SEHEMU YA TATU Hapa Hapa Kijiweni
JIUNGE NA KIJIWENI WHATSAPP CHANNEL Kwa Kugusa Hapa
Soma Riwaya Nyingine Za Kijiweni Kwa KUGUSA HAPA
Wewe kama MFANYABIASHARA.. Kuna wakati unatamani kuwafikia watu wengi zaidi na hujui wapi pa kuanzia , USIJALI kwani hapa ndipo ambapo MTAA UNAONGEA na tuko tayari kukusaidia kuwafikia watu wengi kwa BEI YA OFA
Njoo Utangaze Nasi Sasa Kwa Kutuambia Una TANGAZO Gani na unataka kutangaza kwa muda gani kwa kutuma ujumbe hapa WwhatsApp Kupitia Namba +255760871896
13 Comments
Duh! Mpaka nimeogopa
Yaan Ukis0ma karatasi t umekwish😅💔🙌
Aiseee mzigo ni wa moto ila fupi jmn
Mh mbona inafanana copyright n mobie ya kizungu inaitwa witch revenge kila kitu we umebdlish kdg san il hayo damu karts na vingn ving vinafanana na hyo movie
This is so funny…. The end is coming 😁😁
Drive sales and watch your affiliate earnings soar! https://shorturl.fm/ruwJK
Join our affiliate community and start earning instantly! https://shorturl.fm/DR071
Partner with us and enjoy recurring commission payouts! https://shorturl.fm/2WDAH
Promote our products—get paid for every sale you generate! https://shorturl.fm/221q4
Promote our products—get paid for every sale you generate! https://shorturl.fm/221q4
Tap into unlimited earnings—sign up for our affiliate program! https://shorturl.fm/jFw9m
Share our products and watch your earnings grow—join our affiliate program! https://shorturl.fm/0wkCq
9jzmxm