Utangulizi

“Fungua” Wadudu wa Usiku walikua wanalia, sauti kavu iliyojaa ubabe ilisikika ikisema  huku ikiambatana na kishindo kizito cha Kugonga Mlango.  

“Mnataka nini?” Sauti iliyotoka ndani ilijaa hofu sana, ilikua ni sauti ya Kizee iliyotoka  kwa udhaifu mno. 

“Tunamtaka Masumbuko, hatuwezi kuishi na laana hapa Kijijini” sauti ile ile ilisikika  tena ikizidi kuwatia hofu, Bibi Kizee aligeuka akiwa ameshikilia kibatari, nyuma yake  alikua amesimama Kijana wa Kiume wa Miaka 16 Mwenye ulemavu wa ngozi ( Albino ).  Kijana huyo ndiye Masumbuko, chozi lilikua likimbubujika 

“Kama haufungui tunauvunja huu mlango Bibi Lugumi” ilisema tena ile sauti, Bibi  Lugumi akasogea taratibu hadi aliposimama Masumbuko akamwambia 

“Sina chaguo, sijui naweza kukuokoa vipi leo” alisema huku uso wake ukiwa  umesimikwa huzuni iliyo kuu. Alimshika Masumbuko mkono akamwambia tena 

“Kama leo utakua ndiyo mwisho wako, basi utakua ni mwisho wangu pia” alipomaliza  kusema alisogea hadi mlangoni kisha akasema 

“Mnataka kufanya kosa kubwa litakalo wagharimu vizazi na vizazi.” Kabla hata  hajamalizia kuzungumza tayari mlango ulikua umeshavunjwa. Tochi kali ilimmulika  Masumbuko aliyekua akitetemeka 

“Huyu hapa” alisema Mwanaume mmoja, wanaume wengine wawili wakaingia na  kumkamata Masumbuko wakatoka naye ndani. Masikini, kijana huyu alikua akimwaga  chozi kila sekunde iliyopotea, alilia kwa uchungu akiwaambia 

“Kama Mimi ni laana hapa Kijijini, basi mniache nihame” alisema kwa kupaza sauti  huku akijaribu angalau kutaka kujinasua kwa kutumia nguvu zake lakini alidhibitiwa na  wale Wanaume Wawili walioshiba miili yao vyema. 

Bibi Lugumi akatoka ndani huku akiwasihi wale Wanaume 

“Msiitende hii dhambi, kamwe haitaondoka vizazi na vizazi. Ni bora mkamwacha  aondoke Kijijini” alisema kwa sauti iliyokua imetawaliwa na Kilio, ulikua ni Usiku wa  Manane. 

“Huyu ni lazima auawe ili kuukata huu mzizi, Kijiji kinakumbana na majanga mengi  tokea huyu Kijana aliporejea hapa Kijijini. Hii laana ilianzia kwa Mama yake, hatutaki  hii damu iendelee tena” alisema Mwanaume mmoja, kisha waliondoka na Masumbuko, 

walitokomea Gizani huku Bibi Lugumi akipaza sauti akiwataka wasimuuwe Masumbuko  kwani kwa Kufanya hivyo Kijiji chao kitapata Laana isiyofutika. 

Hakuna aliyemsikiliza Bibi Lugumi, walimwona ni Kikongwe asiye na Mpango kabisa,  walimdharau na wala hawakujali kuhusu kilio chake. Alikaa chini gizani akilia kwa  kusaga meno  

Usiku ule, Masumbuko alifikishwa kwa viongozi wa Kijiji ambao waliagiza Masumbuko  akamatwe. Viongozi hao walikua wamekusanyika karibu na Msitu mmoja wa Kijiji  ambao hutumika zaidi kwa ajili ya matambiko. Hapo palikuwa na wazee kadhaa, pia  Mganga wa Kienyeji ambaye akawaambia 

“Sasa laana itatokomea kusikojulikana, mtaishi kama zamani. Mtavuna, mtavua samaki,  mtachimba Madini. Nipeni kisu, mleteni huyo Kijana” alisema akiwa amekaa kwenye  Kigoda, mahali hapo palikua pamezungukwa na Miti mikubwa mithiri ya Mibuyu 

Haraka Msumbuko alisogezwa mbele ya Mganga, akamtazama Kijana huyo kisha  akasema tena 

“Kifo chako ndiyo ukombozi wa Kijiji cha Nzena” akatoa ishara kua alazwe kama Kuku  kisha achinjwe, damu iwekwe kwenye chungu. Masumbuko hakuacha kuleta purukushani huku akiwaambia wamwache aondoke Kijijini hapo lakini sauti yake ilikua  kama kilio cha Samaki ndani ya Maji. 

Upanga uliwekwa sawa kisha ulitua kwenye shingo ya Kijana huyu, damu nzito  ilimwagika. Wote walishuhudia Masumbuko akitapatapa katika hali ya kupoteza Uhai.  Wale Wanaume walimdhibiti vyema sana hadi pale roho ya Kijana huyu ilipouacha  mwili wake. 

Yule Mganga alifurahi sana, damu nyingi ilipatikana kisha akaichanganya na dawa zake  akawaambia kua wakamwage damu hiyo kila mahali ambapo palikua hapatoi mavuno  kama ilivyokua siku za awali. 

** 

Bibi Lugumi, alipigwa na Baridi. Nafsi yake iliingia unyonge sana kisha akarejea ndani,  alihisi upweke wa ajabu sana, chozi jepesi lilikua likimtoka. Ilikua ni ishara kua  Masumbuko alikua ameuawa 

Alilia kwa kwikwi, chozi liliendelea kumdondoka. Aliyakumbuka maisha ya Masumbuko  lakini hakuwa na uwezo wa kubadilisha chochote, ghafla aliacha kulia, roho ya Ujasiri  ikamvaa. Akasema 

“Roho ya Masumbuko itawalilia kila sekunde, Kuanzia sasa nakilaani Kijiji hiki na vizazi  vyake. Kifo kitawaandama, hakuna atakayeingia wala kutoka Nzena kuanzia sasa, Kijiji  hiki kitajulikana Dunia nzima” alipomaliza kusema alikitupa kibatari kinachowaka  kwenye kitanda cha kamba, kitanda hicho kikadaka moto.  

Bibi Lugumi alifia kwenye ule moto. Usiku huo, ulikua mwanzo wa Maisha mapya ndani  ya Kijiji cha Nzena kinachopatikana Mashariki ya Nchi ya Ganza.

Baada ya Miezi mitatu kupita, Maisha ya Kijiji cha Nzena yalikua yametawaliwa na  Baraka nyingi hadi baadhi yao walikufuru. Mavuno ya samaki yaliongezeka mara dufu,  wavuvi walivua samaki wengi kuliko wakati wowote ule, Madini yalipatikana kwa wingi. Kila mmoja aliamini laana ilikua imeondoka, kifo cha Masumbuko kilisafisha laana zote  Kijijini hapo. 

Maisha yaliendelea ndani ya Kijiji hiki kilichovutia wengi, Miaka mingi ilipita huku hali  ya Maisha ikionekana kwenda vizuri zaidi.  

Usiku mmoja, ndani ya nyumba moja Ndogo ya nyasi. Zahoro alikua amelala, huyu ni  Kijana wa Miaka 22. Yeye ni Mtoto wa Mkulima, alikua akiishi na Baba yake pekee  baada ya Mama yake kufariki Miaka mingi akiwa bado Mdogo. 

Jasho lilikua likimtoka Zahoro, alikua akigeuza shingo huku na kule huku akigugumia.  Baba yake aitwaye Mzee Miroshi aligutuka kutoka Usingizini na kuketi kitako huku  akisikia namna Kijana wake alivyokua akigugumia. 

Ulikua ni Usiku wa Manane, Mzee Miroshi taratibu alinyanyuka kutoka Kitandani,  alimeza funda la mate kidogo kabla ya kuanza safari fupi ya kukielekea chumba cha  Zahoro, alipofika mlangoni kwa Zahoro alifunua pazia huku akiwa ameshikilia Kibatari.  Alimwona Zahoro namna alivyokua akiweweseka huku akiwa ameloa jasho mwili  mzima. 

Kilichomfanya Mzee Miroshi asimame mlangoni ni maneno ambayo Zahoro alikua  akiyazumgumza. 

“Usitulaani, tusamehe. Usilaani kizazi chetu Bibi Lugumi” aliyarudia haya maneno kwa  zaidi ya mara kumi, ndipo Mzee Miroshi alipomwamsha Zahoro. 

Alishtuka na kuketi kitako huku akiwa anahema sana kama Mtu aliyekua akikimbia. 

“Usiwe na wasiwasi tulia Zahoro” alisema Mzee Miroshi huku akikuna ndevu zake  zilizojaa mvi nyeupe, alipepesa macho yake. 

“Baba” aliita Zahoro, Mzee Miroshi alimtazama Zahoro bila kusema chochote huku sura  yake ikionesha utayari wa kumsikia.  

“Naogopa Mimi” alisema Zahoro, alijisogeza mwilini mwa Baba yake na kumkumbatia,  haikua hali ya kawaida kwa Mzee Miroshi. Alijua ni kitu gani alichokua akikiota  Mwanaye sababu alimsikia akiweweseka. 

Alimeza tena funda zito la mate huku akimpiga piga Zahoro Mgongoni katika hali ya  kumfanya ajisikie kupoa. 

Nini Kitaendelea? Usikose SEHEMU YA PILI Hapa Hapa Kijiweni

 

JIUNGE NA KIJIWENI WHATSAPP CHANNEL Kwa Kugusa Hapa 

Soma Riwaya Nyingine Za Kijiweni Kwa KUGUSA HAPA

Wewe kama MFANYABIASHARA.. Kuna wakati unatamani kuwafikia watu wengi zaidi na hujui wapi pa kuanzia , USIJALI kwani hapa ndipo ambapo MTAA UNAONGEA na tuko tayari kukusaidia kuwafikia watu wengi kwa BEI YA OFA

Njoo Utangaze Nasi Sasa Kwa Kutuambia Una TANGAZO Gani na unataka kutangaza kwa muda gani kwa kutuma ujumbe hapa WwhatsApp Kupitia Namba +255760871896 

15 Comments

  1. ni nzuri sana sema ilibidi miaka isipite ming,i iwe michache baada ya kile kifo cha bibi, ili watu katika kijiji wakumbuke kwa urahisi chanzo.

Leave A Reply

Exit mobile version