Ilipoishia Mama Niachie Mume Wangu Sehemu Ya Saba
Ile simu ilikuwa ndogo tu yaani ya kitochi, hivyo ilikuwa ngumu kwangu japo kupata namba za Jonas wala za marafiki zangu niliosoma nao kama Konzo, Siku moja alirudi akiwa amelewa, alikuwa na Mwanamke mmoja ambaye jinsi alivyozungumza alikuwa hajalewa kabisa.
Siku zote kila alipoleta Mtu alikuwa akinifungia chumbani na kustarehe chumba Kingine, nikiwa mle chumbani nilipata harufu ya Sigara alafu nikasikia sauti ya Mwanamke akiongea kuwa
“Nalala huku huku asubuhi anipe changu, kalewa chakali” nilisikia sauti hii niliita . Endelea
SEHEMU YA SABA
“Dada! Dada!” ilikuwa majira ya usiku sana kama saa saba hivi, nilisikia ukimya baada ya kuita alafu nikaanza kusikia sauti ya kiatu kuja nilipo.
“Nani anaita?” aliuliza yule Mdada, pale pale Mtoto akaanza kulia
“Ni mimi hapa, Naitwa Veronica”
“Nikusaidie nini?”
“Naomba nifungulie tafadhari nina shida kidogo” “Nakufungulia vipi kwani umeingiaje humo”
“Nitakuelezea, naomba unifungulie tafadhari” Yule Mdada alinifungulia maana alikuwa akifunga kwa nje kwa kutumia komeo za kisasa!
“Ahsante sana Dada”
“Vipi huyo Mtoto ni wa kwako?”
“Ndio wa kwangu”
“Sasa ilikuaje ukajifungia humo tena, kama nisingepita huku ingekuwaje?”
“Mimi ni msichana wa kazi, nina shida ya simu” Ilibidi nimdanganye yule mdada ambaye alinipa tumaini la kunisikiliza, nilitamani kumwambia anitoroshe usiku ule lakini niliogopa kuhusu Afya ya Mtoto wangu na ile baridi ya Usiku niliona nitahatarisha zaidi Maisha yake.
“Hii hapa” alinipatia Simu yake kubwa na ndicho nilichokitaka, haraka haraka niliingia facebook nikamtafuta Konzo, nikamtumia meseji iliyoambatana na namba yangu!
“Ahsante!” nilimpatia simu yake baada ya kufuta meseji niliyoituma
“Usimueleze Anko Sanga tafadhari, nifungie kwa nje” nilisema na kurudi ndani, hapana shaka yule mdada alinisikiliza na kuelewa nilichotaka, kilichobakia kwangu ni dua na sala ili Konzo azione meseji zangu.
Asubuhi, yule mdada alikuja kuniaga akaondoka zake. Masaa mawili baadaye Anko Sanga alinifungulia, ndio hivyo niliishi kama Mtumwa kwenye maisha yangu. Mtoto alipoumwa alimchukua na kwenda nae Hospitali, chakula na vitu vingine alivifanya mwenyewe, Jukumu langu likawa kupika, kula na kumpa penzi.
Kama bahati tu baada ya siku tatu Konzo alinipigia, sikuamini kabisa. Nilizungumza nae na kumueleza hali halisi ya maisha yangu kwa kipindi kile, alisikitika sana pia hakuamini kama Mama yangu alikuwa akinitumikisha namna ile, akaniambia atamtafuta Jonas ili azungumze nae, kwakuwa Anko Sanga aliiunganisha ile simu na simu yake alifanikiwa kujua nilikuwa nikiongea na Mtu. Ilipokata alinipigia na kunifokea sana.
Aliporudi aliichukua ile simu na kuniambia sitaweza kuongea na yeyote yule, Akanipa na mkwara mzito kuwa endapo nitaenda kinyume atamuua Mtoto wangu!
Kwa kipindi hiki sikumsikia wala kumuona Mama yangu kabisa, nikawa mfungwa kwenye nyumba ya Anko Sanga.
Upande wa Konzo alifanya jitihada za kumtafuta Jonas akamuelezea changamoto nilizokuwa nazipitia, pamoja na hasira za Jonas alijikuta akinionea huruma, akasafiri kuja Arusha kunitafuta.
Kibaya zaidi ni kuwa Mama alihama pale alipokuwa anaishi hivyo alipoenda pale aliambiwa kuwa mwenye ile nyumba aliuza na kuondoka pale Arusha.
Yule jirani alipomuona Jonas alimsimulia kilichotokea kwa upande wa Mama maana hakujuwa kilichotokea upande wangu, kipindi yale mambo yanatendeka pale alikuwa Hospitali kutokana na kuanguka ghafla
“Kuhusu Veronica sijui alipo, labda Mama yake ameondoka naye” “Na Mjomba wake unaweza ukapafahamu anapoishi?”
“Kiukweli sijui anaishi wapi Kaka yangu!” Jonas alikuwa kwenye nyakati ngumu za kunipata mimi.
Baada ya Anko Sanga kuichukua ile simu haikupatikana tena, Jonas alipojaribu kuipiga ile namba aliyopewa na Konzo haikuita kabisa
Ilikua ngumu kwa Jonas kupafahamu nilipokuwa ninaishi, Mtoto wangu aliendelea kukua hatimae miaka miwili ilipita, Moyo alianza kuongea na kukimbia, hakupata nafasi ya kucheza wala kujumuika na watu wengine, alinifahamu mimi na Anko Sanga Pekee, kila nilipomtazama Mwanangu niliiona kabisa taswira ya Jonas, alifanana sana na Baba yake!
“Utakua huru Moyo” nilimwambia Mwanangu nikiwa ninalia wakati huo akiwa amelala, hata kama angelikuwa macho asingeliweza kutambua nilichomwambia, miaka miwili haikitosha kuwa na ufahamu kwake.
Nilimpiga busu la upendo binti yangu kisha nilimlaza, Anko Sanga alipoingia alinikuta nikiwa namfunika vizuri maana baridi la Arusha wakati huo lilikuwa juu sana.
“Nakuhitaji Chumbani” Alisema, nilijuwa tu alikua akihitaji penzi ili azidi kupata pesa
“Nakuja” Nilimjibu, alikua akimchukia sana binti yangu baada ya kugundua kuwa ujauzito haukua wake maana mwanzo alikuwa akidai kuwa Mimba ni yake lakini alipozaliwa Moyo akiwa na sura ya Jonas alianza kumchukia.
Siku moja aliniambia tumtenge Mtoto kwenye chumba kingine, tena wakati huo Moyo akiwa na mwaka mmoja tuu, ilikua ngumu kwangu lakini ililazimika kuwa hivyo japo roho iliniuma kumuacha Mtoto wangu kwenye chumba kingine.
Basi, baada ya kumaliza kumlaza Moyo nilienda chumbani kwa Anko Sanga, wakati huu tukiwa Mke na Mume, niliufunga ule Mlango vizuri kisha funguo niliondoka nayo, nilikuwa nikihofia sana juu ya Usalama wa binti yangu maana Anko Sanga alikuwa hamtaki pale nyumbani.
Nilimkuta akiwa amekasirika, alinitaka nikae kitandani nami nilifanya hivyo, nilishamzoea na hasira zake za mara kwa mara.
“Miaka Mitatu kasoro sasa tokea tumefunga ndoa, sijawahi kumuona Mama akija hapa, sipati mawasiliano naye. Napata wakati mgumu sana kujua kama yupo hai au amekufa” Nilisema ili tu kumhamisha kwenye kile alichokuwa anataka kuniambia maana nikitaka kumkera basi nimuulize kuhusu Mama
“Hicho sio nilicho kuitia hapa Veronica, usinihamishe kwenye reli”
“Kuna ubaya gani ukinijibu? sijatoka ndani kwa miaka hiyo yote, siwasiliani na yeyote kwa kipindi hicho chote zaidi ya Wewe”
“Sikia Veronica, nataka unipatie Mtoto wako nimpeleke kwa Bibi yake, siwezi kukaa na damu ya Mtu mwingine” Alisema huku akiweka sura ya Ukauzu, alikua ameniingizia kitu kipya kabisa kwenye kichwa changu.
“Umchukue Moyo?”
“Ndio!”
“Bado hujaongea sawa sawa! Nikupe binti yangu? hilo haliwezekani Sanga…nimefanya kila ulichotaka lakini kwa binti yangu unavuka mipaka kabisa, siwezi kukupa binti yangu hata siku moja na nisisikie unaongelea hilo jambo tena”
Nilijikuta nikimkalipia Anko Sanga, ndio ilikua ni mara yangu ya Kwanza kufanya hivyo, siku zote nilikuwa mtiifu kwake lakini alipomgusia Mtoto wangu alinigusa pabaya sana.
“Unanipandishia sauti mimi?”
“Sikupi Mtoto Sanga labda uniuwe kwanza ndipo umchukue lakini sio kwa hidhini yangu, hata Moyo akijua ulimchukua kutoka kwangu atanilaani sana” Nilipomaliza hii kauli nilikutana na kibao cha nguvu upande wa kushoto wa Shavu langu!
“Mpumbavu Mkubwa hivi unaniona mimi poyoyo kama huyo uliyezaa nae? sasa nisikilize kwa makini umetaka hujataka Mtoto ataondoka hapa full Stop”
“Endelea kunipiga hadi uniuwe lakini Kukupa Mtoto haiwezekani kabisa Sanga” niliongea nikiwa ninalia, alinipiga kibao kingine akanitupa chini kisha alianza kunikanyaga
“Shenzi taipu! Ujinga…wafanyie….wajinga wenzio…” alinipiga sana siku hiyo tena bila kupumzika akawa amenivimbisha jicho la upande wa kulia, alinisababishia maumivu makali kwenye kiuno changu kutokana na kunikanyaga!
Nililia sana, nikiwa kama Mama sikutaka kabisa kutengana na binti yangu alafu nisijuwe yuko wapi? Ushirikina wao sikutaka wamuingizie Mwanangu, japo alisema anampeleka kwa Mama lakini niliishiwa nguvu ya kuruhusu hilo kwanza Mama mwenyewe alishakuwa adui yangu, kingine sikujua anaishi wapi na sikupata kumuona kwa miaka hiyo yote. Alinipokonya funguo wa chumba ambacho Moyo alikuwa amelala, nilijitahidi sana kupambana na Sanga asimchukue Mtoto lakini sikuwa na mabavu ya kupimana nae.
Niliishia kulia kwa uchungu, hii nyumba ya Anko Sanga ilikuwa ya kifahari kubwa sana kiasi hata nifanyaje ilikuwa ni ngumu kutoa sauti nje, ilikuwa imejitenga nje ya mji wa Arusha ambako kulikuwa na mashamba yake. Usiku huo huo Anko Sanga alimchukua Moyo, alinifungia kule chumbani nilipiga sana kelele aniachie japo Binti yangu nipate kukaa nae lakini haikusaidia kwani alidhamiria kuniumiza, kunitia kovu ndani ya moyo wangu!
Nilimsikia Moyo akiwa analia ni wazi kuwa Sanga alimbeba vibaya Moyo bila hata kujali kama alikuwa Mtoto mdogo anayehitaji kunyenyekewa istoshe alikuwa usingizini, alilia huku akiita ‘Mamaa! ‘Mamaaa!’ Alinitia Uchungu sana, baadaye ukimya ulitawala nikaliona gari la Sanga likiwa linatoka maana nyumba ilikuwa ya ghorofa hivyo nilipata nafasi ya kuchunguza kutokea juu!
Sikupata Usingizi, nilikesha ninalia na kusali ili Mungu anitoe kwenye ile mitihani mizito iliyo migumu kwangu,
“Mungu nimekukosea nini mimi? kwanini unaniadhibu namna hii, kwanini yote ya kwangu mimi tuu?” Nilijikuta nikipaza sauti yangu ili kama Mungu amesinzia basi aamke aone jinsi ninavyoteseka, Maisha yangu yote niliishi kwa kumtegemea yeye na kuamiani lakini kwa kipindi kile niliona amenisahau kabisa.
Sanga hakurudi hadi kulipo pambazuka, nilikuwa nimesimama nikichungulia nje hadi jua lilipotoka, nilikuwa nikitazama geti pamoja na barabara ili kuona kama kuna Mtu au gari ilikuwa ikija, ndipo nilipoiona gari ndogo ya Anko Sanga aina ya Rav4 New Model, nikasema ni lazima nilipize kwa alichokifanya kwa binti yangu, kunitenga nae ni adhabu kubwa sana kwangu!
Nilipata wazo la kumpiga na kitu kizito kichwani ili nimuuwe kabisa maana nilikuwa nafanya kila kitu kwa ajili ya Mtoto wangu lakini walishamchukua, nilifunga dirisha baada ya kuona gari limeingia ndani, nilitafuta kitu kizito pale chumbani, niliiona chupa ya soda niliichukuwa na kujificha nyuma ya mlango ili akifungua tu nimtandike nayo, nilishajipanga kuwa liwalo na liwe siwezi kuendelea kuwa Mtumwa.
Nilijibanza vizuri sana huku nikiamini kuwa ilikuwa ndio nafasi yangu ya mwisho, nikiikosa hiyo nafasi naweza nisiipate tena maana nikimkosa hapo anaweza akanigeuza kuwa Mtumwa nisiye na uhuru tena, angeniona adui yake kwasababu ningemlipiza kwa kumchukua Mtoto wangu.
Nilikaa kwa kitambo kidogo kabla ya kuanza kusikia milango ikifunguliwa, kawaida alikuwa akitembea na rundo la funguo za milango, nilikuwa nikizisikia kila alipokuwa akitembea, nilisikia akija upande wangu ni wazi kuwa alikuwa akija chumbani, nilivuta pumzi za kutosha kisha nilijiweka sawa kumshambulia. Sikuwa na ujasiri wa kufanya hivyo lakini ilinibidi maana bila hivyo ningelikuwa kwenye wakati mgumu sana.
Vishindo vya miguu vilikoma kwenye mlango wa Chumba nilichopo kisha funguo ilianza kufungua kitasa taratibu, nilifumba macho yangu ili nisione kitakacho fanyika pale, niliivuta ile chupa sawa sawa, mlango ulipofunguliwa nikawa nyuma ya Mlango, niliposikia akitembea kuingia ndani basi nikaiachia ile chupa nikiwa nimefumba macho yangu ikatua kwenye kichwa chake, nikasikia sauti iliyoshindwa kutoka sawa sawa kisha nilisikia kitu kikianguka kama mzigo, Yes! nilikuwa nimelenga shabaha yangu vizuri, ikabidi sasa nifumbue macho yangu!
Nini Kitaendelea? Usikose SEHEMU YA NANE
JIUNGE NA KIJIWENI WHATSAPP CHANNEL Kwa Kugusa Hapa
Soma Riwaya Nyingine Za Kijiweni Kwa KUGUSA HAPA
Wewe kama MFANYABIASHARA.. Kuna wakati unatamani kuwafikia watu wengi zaidi na hujui wapi pa kuanzia , USIJALI kwani hapa ndipo ambapo MTAA UNAONGEA na tuko tayari kukusaidia kuwafikia watu wengi kwa BEI YA OFA
Njoo Utangaze Nasi Sasa Kwa Kutuambia Una TANGAZO Gani na unataka kutangaza kwa muda gani kwa kutuma ujumbe hapa WwhatsApp Kupitia Namba +255760871896
1 Comment
Sasa weka ya 8 tuendelee ma huondo