Ilipoishia Kimya (Nzena-Kijiji Kilicholaaniwa) – 04
“Nina amini, Mji wa Patiosa una majibu ya maswali mengi. Siri nyingi zitafunguka” alisema akimtazama Anna ambaye alianza kuonesha Mashaka huku akijiuliza kama Zahoro aliota jambo lingine aliloamua kulifanya Siri. Wakati wakiwa hapo wanazungumza, Alice alikua amesimama kwa mbali akiwatazama.
“Kuna jambo lingine uliliota?” akauliza Anna. Zahoro akamjibu
“Hakuna zaidi ya nilicho kusimulia. Lakini Nina uhakika na Mji wa Patiosa, utaenda kutegua kitendawili” Alisema Zahoro Kisha alimshika mkono Anna wakashuka taratibu Hadi chini, Zahoro alionekana kua makini sana, aliangaza huku na kule kabla ya kuanza kutafuta Mtumbwi.
SEHEMU YA TANO
Bahati nzuri walipata Mtumbwi mmoja ukielea, waliingia humo Kisha walianza safari ya kuelekea Mji wa Patiosa. Walikua kimya kama shimo tupu, akili zao zilikua zikiwaza safari hiyo na mambo mengi yasiyo na Majibu.
Anna alikua alijaribu kuisoma akili ya Zahoro lakini aliambulia patupu, Zahoro alionekana kuficha jambo huku akitazama mbele. Taratibu walipiga Kasia za Kimya kimya wakiliacha eneo waliloishi kwa Miaka Mingi.
“Hatimaye tunamwacha Adui Kimya nyuma yetu” alisema Zahoro, maneno yake yalikua mithiri ya Fumbo la Siri sana ambalo lilimfanya Anna awaze kwa kina zaidi. Anna aligeuka nyuma, alimwona Alice akiwa amesimama juu ya jiwe akiwatazama. Alishtuka na kuhisi huwenda Zahoro alianza kuitambua Siri yake na Adui Kimya aliyeuwa Watu wengi wa Kijiji Cha Nzena.
“Una maanisha nini?” aliuliza kwa wasiwasi Anna. Zahoro alishusha pumzi na kumuuliza Anna
“Ni Adui gani aliyetunyima Usingizi kwa Miaka yote kama siyo Kimya?. Basi ni yeye, tunamwacha, Nina hakika tunaenda kukutana na Adui mwingine” alisema huku akikata Kasia kwa mikono yake iliyojaa kwa mazoezi.
Anna alishusha pumzi Kisha aligeuka tena Nyuma, hakumwona Pacha wake Alice. Waliondoka pole pole kwa kutumia Mtumbwi kuelekea Patiosa. **
Patiosa, Mji wa Damu.
Huu ni Mji wa kale uliopotea kwa Miaka Mingi sana. Ni miongoni mwa Miji iliyopewa laana na kutoweka kwenye uso wa Dunia. Mji huu ni tofauti na Miji mingine iliyolaaniwa, Mji wa Patiosa haukukumbwa na vifo, waliishi huko wakitengwa na Dunia halisi.
Waliunda mifumo ya kiutawala, waliishi kwa amani japo walikua Kuzimu. Walitengeneza jeshi, walijenga Kuta ndefu za kuwakinga na Watu wengine kutoka kwenye Miji iliyo laaniwa. Baada ya kuangushwa kwa utawala wa Mfalme Munis ambaye ni Baba wa Anna na Alice, Mji huu ulibadilisha taswira yake.
Ulitawaliwa kwa kumwaga Damu na Mfalme katili Selasi, aliugeuza Mji wa Patiosa kua Mji wa Damu. Ni Mji ulioshamili Mauwaji ya kutisha sana. Mji uligeuza Wakazi kua Watumwa, Mfalme Selasi hakutaka Mtu yeyote mwenye nguvu aishi kwenye Ufalme wake, aliuwa Watu alioamini wangempindua na kuchukua madaraka.
Alilitumia jicho lake kama silaha ya kutisha ya kutawala, tofauti na Mfalme Munis aliyeitumia Pete ya ajabu kutawala.
Kila baada ya mwezi mmoja wanatumwa askari wa Mji wa Patiosa kufanya doria kuuzunguka Mji mzima kwa nje, sauti za farasi zilikua zikisikika. Kisha sauti ya kupulizwa kwa kitu mfano wa Pembe ya Myama ilisikika. Askari waliotumwa walikua wakirejea, mara Moja lango lilifunguliwa kisha Askari waliingia ndani ya Mji wa Patiosa kupitia lango refu sana lenye geti kubwa la Chuma.
Walikua wamekamata Watu watatu katika doria Yao, miongoni mwao walikua Wanaume wawili na Mtoto mmoja. Taarifa ilipelekwa Ikulu kwa Mfalme Selasi, akagiza Watu hao wapelekwe Ikulu.
Akiwa amesimama juu ya jengo la ghorofa Moja, alikua akitazama chini. Aliona Watu waliokua wamekamatwa, Walikua ni Wanaume wawili na Mtoto, Wanaume hao walijitambulisha kua walikua wametokea kwenye Kijiji kiitwacho Nzena, Naam‼ walikua ni wale waliondoka na Mtoto Moana waliyemfunga kitambaa usoni
Mfalme Selasi alinogewa na Hadithi hiyo, akaamua kushuka Hadi chini. Alivutiwa zaidi na Mtoto Moana, alichuchumaa Kisha akaondoa kitambaa usoni kwa Moana, akajikuta akitabasamu Kisha akamuuliza Mtoto.
“Unaitwa Nani?” Moana alimtazama Mfalme Selasi Kisha akamjibu bila hofu.
“Moana, Mtoto wa Zahoro” Basi, Mfalme Selasi akajikuta akicheka kidogo. Hakujua huyo Zahoro ni Nani na kwanini Mtoto alijiamini sana.
Mfalme Selasi, alisimama na kujipangusa mikono yake, alikua na jicho Moja. Akawageukia Wanaume wale Wawili, sura yake haikuonesha tabasamu kama alivyofanya kwa Moana, Kisha akawauliza
“Kipi kimewaleta hapa?” Wale Wanaume wakatazamana Kisha mmoja akajibu.
“Kutafuta mahali salama pa kuishi, Kuna kiumbe kimeuwa Watu wote katika Mji wetu” Mfalme Selasi akaachia tabasamu Kisha akawaambia walinzi.
“Hakikisheni mnawaua na kuwatupa mtoni, Mtoto akiwa miongoni mwao” alisema akiwa anaondoka eneo Hilo lakini kabla hata hajapandisha ngazi akasikia sauti ikimwita
“Mtukufu Mfalme” aliitambua sauti hii, ilitoka kwa mtabiri wa Ufalme wa Patiosa. Aligeuka akamwona Bibi mmoja
“Unasemaje Segebuka?” akamuuliza.
“Machoni mwa huyu Mtoto nimeona hatari, Si Mtoto wa kawaida, ametoka kwenye uzao wenye Kisasi na nguvu kubwa” alisema kwa heshima na adabu Kisha aligeuka chini. Kidogo sura ya Mfalme Selasi ilibadilika
Hakumtazama kwa tabasamu Moana, akamuuliza Mtabiri Segebuka. “Una hakika?”
“Hakika Mtukufu, ujio wake hapa Patiosa ni ishara ya mwisho wa enzi zako. Wazazi wake watakuangusha sababu wako njiani kuja hapa” alisema Mtabiri Segebuka, alimghadhabisha sana Mfalme Selasi, Kisha Mfalme akaagiza sasa Moana apelekwe mbele yake ndani ya chumba Cha Siri
Wale Wanaume wengine wakaenda kuuawa isipokua Moana pekee ambaye alihitajika na Mfalme Selasi, Kisha Mtabiri Segebuka akaungana na Mfalme pamoja na walinzi wa Mfalme Selasi. Tayari ujio wa Moana ulianza kubadilisha mambo kwenye Mji wa Patiosa.
Waliingia ndani kabisa kwenye chumba Cha Siri Cha Mfalme Selasi, akaketi kwenye kiti chake Kisha akamuuliza Moana.
“Umetumwa kuja hapa kwa lengo Fulani si Ndiyo?” Moana alikaa kimya, Segebuka akaingilia kati na kumwambia Mfalme.
“Hakuna alijualo, lakini hii ni ile Damu ya Munis. Naogopa kinachokuja mbele yetu” Mfalme alisimama kwa mshituko Mkubwa sana.
“Unasemaje, Munis?” aliuliza, yeye ndiye aliyerithi kiti Cha Mfalme Munis baada ya kuuawa na Mwanasayansi Steve Mbasa. Kisha aliwafukuza Watoto wa Mfalme na jamaa zake wengi aliwauwa kikatili, alimfunga Mama Yao Akina Anna kwenye Gerezani la Siri kwa Miaka Mingi sana Hadi umauti ulipomfika akiwa gerezani.
Haraka Mfalme alimsogelea Segebuka na kumshikaa shingoni Kisha akamwambia
“Unakumbuka ulisema kuwatenganisha ilikua ni njia sahihi ya kumaliza Ukoo wao, ulikua unasema uwongo si Ndiyo?” Kisha alimwacha akiwa anakohoa.
“Hapana Mtukufu, hatma imebadilika. Sikuoni ukiwa Mfalme wa Patiosa tena, huu Ndiyo ukweli Mfalme Wangu” alisema Segebuka Kisha alipiga goti, alikua amemtia hasira sana Mfalme Selasi. Kisha aliagiza askari kuzunguka Kila kona kutafuta Watu waliosalia hai na kuwaleta kwenye Ufalme.
Askari wa kutosha wakasambazwa Kila kona ya Mji ya Patiosa, nje na ndani ya Mji huo. Eneo lote la mto linaloingia katika Mji wa Patiosa lilizungukwa na askari, mitumbwi ikasambazwa kuhakikisha hakuna Mtu anayeingia Patiosa. Ulikua ni Mpango wa Mfalme Selasi kuzui jaribio la mapinduzi ambalo Mtabiri Segebuka alimweleza Mfalme.
**
Jioni iliingia, ikawakuta Anna na Zahoro wakielea taratibu majini, wakielekea Patiosa—bila kujua kwamba walikuwa wakisubiriwa ili wakamatwe na kuuawa mbele ya Mfalme Selasi. Palikuwa kimya; hakuna aliyeongea.
Hisia zao ndizo zilizokuwa zikizungumza—kila mmoja alijaribu kusoma mawazo ya mwenzake kwa macho. Midomo yao ilikuwa na mipauko kwa ukimya mrefu, mikono yao imechoka kwa kupiga kasia.
Zahoro alimwangalia Anna, na kila alipomtazama, alihisi kuna jambo alilokuwa akilificha.
“Nafikiria tunaweza kutafuta sehemu ya kupumzika sasa,” alisema kwa sauti ya upole. Safari ilikuwa ndefu na mikono yao ilihitaji pumziko. Anna alitikisa kichwa kukubaliana, kisha akajiegemeza kwenye ukingo wa mtumbwi. Macho yao yakatazama jua likizama taratibu.
“Tuna bahati kumpata Moana. Sisi ni wazazi wa kujivunia. Najua ni jasiri, na naamini hakuna baya lililomkuta,” alisema Anna, akishusha pumzi ndefu.
“Ndiyo,” alijibu Zahoro, “Mtoto wa simba ni simba pia. Tumelea askari imara.” Hali ya baridi ilikuwa inaanza kujitanda.
Mitumbwi ya askari kutoka Patiosa iliendelea kuzunguka mtoni, wakisaka manusura. Giza lilianza kuingia polepole hadi anga likawa jeusi.
Anna na Zahoro waliamua kutua kando ya mto, mahali penye miti mingi. Walikumbatiana mithili ya makinda ya ndege wakijilaza ardhini.
Wakiwa wamesinzia kwa uchovu, mitumbwi ya askari iliendelea kusogea. Hatimaye mtumbwi mmoja, ukiwa na askari watano, ulifanikiwa kuona kivuli cha mtumbwi wa Anna na Razaro ukielea pembezoni mwa ziwa. Moja ya tochi ilimulika moja kwa moja machoni mwa Anna.
Akastuka. Kwa haraka, aliketi kimya na kumtikisa Zahoro. Naye alishtuka na kuwa shahidi wa kilichoonekana.
“Hawa ni watu kutoka mji tunaoelekea?” Zahoro aliuliza kwa sauti ya chini. “Sina hakika. Lakini lazima tujiokoe,” Anna alijibu kwa tahadhari.
Akili yake ikaanza kufanya kazi ya haraka—alijua wazi kwamba huo haukuwa mtumbwi wa kawaida. Ulikuwa ni ujio wa askari waliotumwa kwa amri ya Mfalme Selasi.
Askari hao walivuka kuelekea upande walikokuwa wamejificha. Hatari ilikuwa hatua chache tu mbele yao…
Anna alichuchumaa taratibu, akashika kisu kidogo alichokuwa nacho kiunoni. Mikono yake haikutetemeka, lakini moyo wake ulikuwa ukipiga haraka kama
ngoma ya vita. Alimwangalia Zahoro, wakatizamana kwa muda mfupi kana kwamba walikuwa wakikubaliana bila maneno.
“Tochi yao ikipita tena, tusogee upande wa pili wa mti mkubwa pale,” alisema kwa sauti ya chini, akionyesha kwa kichwa.
Zahoro alikubali kwa kutikisa kichwa tu. Waliuvuta mtumbwi wao kidogo nyuma ya mawe yaliyokuwa karibu na miombo. Miti mirefu iliwasaidia kujificha vizuri zaidi.
Sauti ya maji ikichapwa kwa kasia za askari ilizidi kusikika karibu. Mmoja wao aliinua tochi juu na kusema kwa sauti ya amri:
“Panuka upande huu!”
Walikuwa karibu sana. Hatua chache tu.
Anna alimpapasa Zahoro begani na kumwambia, “Kama wakitukaribia zaidi, tupige mbizi upande wa kulia. Kuna kivuli cha majani, tutajificha huko.”
Zahoro akakubali tena kwa kichwa.
Ghafla, mmoja wa askari alisimama juu ya mtumbwi wao, akamulika upande wa Anna na kusema kwa ukali:
“Naona kivuli!”
Anna na Zahoro hawakusubiri tena. Kwa haraka, walijirusha majini na kupiga mbizi kwa kasi upande wa kulia kama walivyopanga. Maji yalikuwa baridi, lakini wakayavumilia.
Askari walipofika mahali walipokuwa wamejificha, hawakuwakuta. Moja ya tochi ikamulika juu ya maji, lakini ilionyesha tu mawimbi madogo yaliyosababishwa na mbizi yao.
“Walikuwa hapa! Haraka! Piga taa upande wa kulia!”
Anna na Razaro walikuwa tayari wamezamia chini ya kichaka kimoja kilichozama majini, wakivuta pumzi kwa taabu huku wakificha miili yao na vichwa vyao ndani ya majani makavu yaliyokuwa yakielea juu ya maji.
Mioyo yao ilipiga kwa nguvu, lakini hawakutikisa hata jani moja. Walijua— wakigundulika hapa, kifo kilikuwa hakiepukiki.
Upande mwingine wa mto, mbali kidogo, mlio wa miale ya moto ukapita hewani. Ilikuwa ni alama ya ishara—mmoja wa askari alikuwa ametuma ujumbe kwa njia ya moto—kuashiria kwamba wamepata alama za watu.
Anna na zahoro walitazamana tena. Macho yao yaliungana kwa matumaini moja tu—kupona.
Lakini walijua wazi… safari ya kuelekea Patiosa haikuwa tena ya kutafuta msaada. Ilikuwa safari ya maisha au kifo. Kutupwa kwa miale ya moto ni ishara ya Ujio wa askari zaidi eneo Hilo, palikua Giza huku taa kadhaa zilizobebwa na askari zikijitahidi kupambana na Hali hiyo ya Giza
Anna akamwambia Zahoro.
“Hatuwezi kufia hapa Zahoro, Moana anatusubiria. Hatma ya Maisha yetu Ipo hapa sasa hivi, ikiwa tutashindwa kujinasua hapa tutakua tumepoteza Kila kitu” alisema Anna huku akitetemeka kwa baridi.
Nini Kitaendelea? Usikose sehemu ya sita
JIUNGE NA KIJIWENI WHATSAPP CHANNEL Kwa Kugusa Hapa
Soma Riwaya Nyingine Za Kijiweni Kwa KUGUSA HAPA
Wewe kama MFANYABIASHARA.. Kuna wakati unatamani kuwafikia watu wengi zaidi na hujui wapi pa kuanzia , USIJALI kwani hapa ndipo ambapo MTAA UNAONGEA na tuko tayari kukusaidia kuwafikia watu wengi kwa BEI YA OFA
Njoo Utangaze Nasi Sasa Kwa Kutuambia Una TANGAZO Gani na unataka kutangaza kwa muda gani kwa kutuma ujumbe hapa WwhatsApp Kupitia Namba +255760871896
Nzena xx Nzena xx Nzena xx Nzena xx Nzena xx Nzena xx Nzena xx Nzena xx Nzena xx Nzena xx Nzena xx
1 Comment
Hadith ni nzur kinoma sema mnachelewa kutoa mwendelezi had mnatutoa kwenye leli dah…!