Ilipoishia sehemu ya Kumi ya In the name of LOVE
Nilimvuta na kumkumbatia huku nikikisikia kilio chake kwa karibu zaidi. Nililengwa na Mchozi lakini sikutaka utoke, niliuzuia huku nikimbembeleza
“Pole Mpenzi wangu, ukiwa katika Hali ya huzuni unanifanya naumia.” Nilisema kwa sauti ya utaratibu iliyojaa mapenzi, Zaylisa akajitoa mwilini Kisha akafuta chozi lake kwa kutumia mikono yake, akanitazama usoni akaniambia
“Samahani sana Jacob”
“Hata usijali Mpenzi, nimekuelewa” Endelea
SEHEMU YA KUMI NA MOJA
Zilipita siku mbili, hatimaye wiki nzima. Hakuna aliyejua Clara alikua wapi na kwanini simu yake ilikua haipatikani, kibaya zaidi hata Matilda hakua na mawasiliano ya Watu wa karibu wa Clara.
Tulisubiria Kila siku huwenda Clara angerejea lakini siku zilikua zinaenda mithiri ya Mshale wa saa. Kila dakika iliyoondoka iliondoka na tumaini, iliongeza wasiwasi mkubwa.
Tabia ya Zaylisa kuondoka na kutopatikana iliendelea, hata nilipoongea nae alinipa sababu dhaifu ambazo sikuzichuja ila nilimwamini sababu ya Mapenzi yangu kwake.
Siku Moja, alipoondoka asubuhi alisema anaenda kwao. Nilijaribu kumfuatilia maana alikua hataki Mimi niende kwao kumwona Baba yake Mgonjwa, japo nilichagua kumwamini lakini Kuna hisia Moja iliniambia napaswa kumfwatilia hata kama namwamini kiasi gani, kilichonifanya nipate wazo la kumfwatilia ni kitendo chake Cha kutopatikana kwenye simu anapoondoka nyumbani.
Yeye aliondoka kwa Bajaji, nyuma yake nilimfwatilia kwa kutumia Pikipiki ya kukodi, nilimwambia dereva aende pole pole nyuma ya Bajaji. Bajaji ilipofika Mwenge alishuka kisha akaelekea kwenye gari Moja iliyopanda iliyokua imesimama kando ya Barabara
Kisha baada ya dakika kama kumi hivi gari iliondoka na kuelekea barabara ya Ubungo. Baada ya mwendo kiasi gari ilikunja kushoto kama inaenda Sinza halafu ikasimama mbele ya Hoteli Moja, halafu Zaylisa alishuka kisha upande wa pili wa dereva alishuka Mwanaume mmoja aliyevalia ‘Superfly’ nyekundu.
Mwanaume huyo hakunipa nafasi ya kumwona sura yake maana muda wote alisimama akiwa amenipa mgongo, Mwanaume huyo alikua ni mfupi, ana kitambi pia.
Walizungumza hapo kwa dakika Moja Kisha waliongozana wakaelekea ndani ya Hoteli hiyo, sikujua alikua ni Nani na kwanini walienda hapo wakati Zaylisa aliniaga anaenda kumwangalia Baba yake.
Nilipata shahuku kubwa sana ya kutaka kujua walikua hapo kwa ajili gani, basi nilimlipa Bodaboda pesa yake halafu taratibu nikaelekea ndani ya
Hoteli hiyo, niliangaza huku na kule sikuwaona. Hapakua na dalili ya kuwaona japo nilikua na uhakika wapo ndani ya Hoteli hiyo
Nilikua nimesimama nje eneo la Bustani, palikua kimya sana. Iliniuma sana kuona Zaylisa alikua anasema uwongo, nusura chozi linidondoke lakini nilijikaza tu. Niliondoka pale mikono ikiwa nyuma, hasira ilinipanda.
Nilirudi nyumbani, nilihisi bugudha kubwa ndani ya nafsi yangu. Nilijiuliza mengi yasiyo na Majibu, sikujua yule Mwanaume ni Nani na Wana uhusiano gani, nilipitiliza Hadi sebleni nikiwa na hasira nikamkuta Matilda akiwa anaandaa chakula Mezani
Aliponiona alihisi kua sipo sawa, alinitazama kwa dakika kadhaa Kisha aliniuliza
“Upo sawa?” nilimtazama kidogo Kisha niliondoka zangu pale sebleni nikaelekea zangu chumbani.
Nilipofika chumbani nilichukua dawa zangu nilizokua nameza ili kutuliza maumivu ya kinywa nikameza, kichwa kilikua kinaniuma sana. Moyo Wangu ulivunjika kwa ajili ya Zaylisa, chozi lilinibubujika tu.
Nilihisi nahitaji kumjua zaidi Zaylisa, nilihisi hakuwa yule niliyempenda lakini nilijiuliza alipatwa na Nini kwa Kipindi kifupi au ndoa yake imembadilisha? Lakini Kila nilipoyakumbuka macho yake yalinianbia kua alikua akinipenda sana.
Niligonga kichwa changu ukutani huku nikitafuta majibu, mara Mlango uligongwa. Nilifuta chozi langu, nilienda taratibu kuufungua, Matilda alikua amesimama Mlangoni kama Mlinzi wa zamu, nilipomwona nilihisi siye niliyemtarajia
Sikua na chochote Cha kuzungumza na Matilda, nilivuta mlango ili niufunge lakini Matilda aliniambia
“Nimepokea ujumbe kutoka kwa Dada Clara” angalau hii ilikua taarifa niliyoisubiria, wazo la kuufunga mlango lilikoma. Nikamtazama Matilda, nilihitaji kujua ujumbe huo ulisemaje
“Unasema umepokea ujumbe kutoka kwa Clara?”
“Ndiyo”
Hamu na shahuku iliniingia kwa Kasi sana, sikuficha kua nilihitaji kujua Clara yupo wapi
“Amesema yupo wapi?”
“Hapana, amesema yupo salama wala tusihangaike atarudi akili yake ikiwa sawa” alisema Matilda, angalau nilishusha pumzi zangu. Nilijua tu kwa kile kilichotokea kati yake na Zaylisa ndicho kilichomfanya ahitaji kutuliza akili yake. Sura yangu ilipoa
“Basi sawa kama atakutafuta tena uniambie” niliongea kwa sauti ya Upole tofauti na mwanzo nilivyokua na hasira, niliufungua mlango kwa utaratibu Kisha nilitembea kidogo na Kuketi kwenye Kitanda. Suala la Clara nililiona lilikua limeshaeleweka ila sasa kuhusu Zaylisa ilikua kizungumkuti
“Kuna Siri gani hapa, yule Mwanaume ni Nani au Ndiyo yule anayempigiaga simu? Mh, Ndiyo kusema ndiye MZEE WA MIPANGO’? Sasa kama ni yeye Kuna mpango gani?” nilijiuliza maswali mengi bila kupata majibu ya maswali yangu. Mwisho nilipata wazo la kwenda nyumbani kwao Zaylisa
Nilitabasamu baada ya kupata wazo hili maana sikua na njia nyingine ya kujua ni kwanini Zaylisa anapoondoka anakua hapatikani kwenye simu, lakini pia nilipata Mashaka kua huwenda haendi nyumbani kwa Baba yake isipokua ni kwa yule Mwanaume mfupi nisiyemtambua.
Nilijifuta jasho Kisha nilielekea mlangoni nikaufungua na kuondoka, safari hii nilimuaga Matilda nikamwambia
“Natoka mara Moja, kama Zaylisa atarudi utamwambia kua sipo mbali” nilisema, kwa heshima Matilda aliitikia bila kuuliza chochote japo mdomo wake ulikua unataka kucheza lakini sikumpa nafasi nilimwacha kama samaki mwenye Maji mengi Mdomoni.
Nilitumia Bodaboda kuelekea Nyumbani kwa Wazazi wake, nilikua napafahamu ila Wazazi wake walikua hawanifahamu. Nilipofika nje ya nyumba Yao nilimlipa Bodaboda pesa yake Kisha nilisimama kwa sekunde kadhaa nikiiangalia nyumba ile, ilikua ni nyumba nzuri sana inayoonesha wakaazi walikua ni Watu wenye uwezo kifedha.
Huo ndio uhalisia, Wazazi wa Zaylisa walikua na uwezo kifedha, nyumba ilikua imetulia sana. Taratibu nilisogea na kubisha hodi getini, moyoni nilijiambia kua Liwalo na liwe nahitaji kufahamu mengi yaliyo gizani.
Nilisubiria pale kwa dakika Moja huku jua likiwa linanipiga. Mara alikuja Mdada mmoja mwenye umri sawa na Matilda, alipofika alinikaribisha
“Sijui nikusaidie nini Kaka?” aliniuliza, nilitabasamu kidogo Kisha nikamwambia
“Nimekuja kumjulia Hali Mzee Paulo” nilisema, Baba yake Zaylisa alikua akiitwa Mzee Paulo, alikuwa ni Bosi mstaafu wa mfuko wa akiba wa Taifa. Alikua ni Mzee mwenye hadhi na Maisha mazuri, yule Mdada alionesha kushangaa kanakwamba jina Hilo lilikua ngeni au hakujua kuhusu kuumwa kwa Mzee Paulo.
“Usijali Mimi ni rafiki wa Binti yake Zaylisa” nilijitambulisha, akazidi kushangaa Kisha akaniuliza
“Umetokea wapi?” aliniuliza huku akinitazama sana
“Mimi ninaishi Mbezi, usiwe na wasiwasi nataka kujua Hali yake tu” nilisema, yule Mdada akacheka kwa mtindo wa kuguna halafu akaniambia
“Unanishangaza sana, Mbona simfahamu huyo Mzee?” aliuliza. Sura yake ilikua ukimaanisha alichokisema na haikua utani.
“Humfahamu mwenye nyumba? Ni maajabu haya” nilisema huku nikicheka, nilikua na uhakika wala sikukosea nyumba. Mara nyuma yangu lilikuja gari ndogo nyekundu aina ya Alteza, Mwanaume mmoja mwenye asili ya kiarabu alitokeza kichwa chake akauliza
“Kuna nini hapo Sauda?” alikua akimtazama yule Mdada ambaye kwa hakika alikua ni Msichana wa kazi.
“Samahani Bosi, huyu Kaka anamuuliza Mzee Paulo. Mimi simfahamu lakini anadai anaishi humu” alisema yule Mdada, basi yule Muarabu akatabasamu tu Kisha akamwambia yule Mdada arudi ndani.
Kisha yule Muarabu akashuka kwenye gari akaja karibu yangu.
“Wewe ni Mtu wa pili unakuja kuulizia hapa baada ya Miaka minne kupita, alikuja Mwanamke anaitwa Clara kama sikosei alimuulizia Zaylisa. Nikamwambia kua Zaylisa haishi hapa, bahati nzuri nilikua na mawasiliano ya Zay nikampatia. Hata hivyo huyo Mzee alishafariki Miaka minne iliyopita baada ya kufilisika, nikainunua hii nyumba” alisema kwa kujiamini sana
“Unasemaje?” nilimuuliza kama Mtu aliyechanganyikiwa, yote niliyoyasikia yalikua yakinichanganya sana.
“Mzee Paulo alishafariki muda sana, Binti yake alishaolewa kitambo na Mafia mmoja hivi wa hapa Mjini, ulikua wapi Miaka yote hiyo usijue kua Mzee Paulo alishafariki? Hata Mke wake nasikia ni Mgonjwa sana yupo Kilimanjaro” swali lake lilikua sawa na kumwaga chumvi baharini, tayari
nilikua na maswali chungu mzima yaliyohitaji majibu lakini yeye alinipa mzigo mwingine mzito.
“Mzee Paulo amefariki?” niliuliza huku jasho likinitoka, nilihisi kukaribia kuujua ukweli Fulani mchungu sana.
“Muda sana. Wewe ni Nani yake?”
“Aah Usijali, Asante” nilisema Kisha niligeuka niondoke, ile napiga hatua nilihisi kizungu-zungu nikapepesuka nusura nianguke, yule Muarabu akataka kunisaidia lakini nilimpa ishara kua nitakua salama tu.
Niliondoka taratibu huku nikiwa na maswali mengi.
Nilitafuta Sehemu nikakaa ili nijiulize yote hata kama nitakosa majibu ya maswali yangu. Swali la kwanza nilijiuliza kama Mzee Paulo amefariki, Je Zaylisa alikua anaenda kumuuguza Baba yake gani? Kama Ndiyo hivyo maana yake alikua akiniongopea, sasa kama alikua akisema uwongo alikua akienda kwa yule Mzee Wa Mipango.
“Imepita Miaka Minne tangu kifo Cha Mzee Paulo, Miaka mitano baada ya Kifo Cha Melisa, sasa kwanini sikumbuki chochote kile. Mbona ile ajali ilitokea siku ya harusi ya Zaylisa na wala hakikua kipindi kirefu nilichokaa Hospitalini?” nilijiuliza, niliishia kutokwa na Machozi, sikua na Majibu ya maswali yangu.
Nilifuta chozi langu, nikapata wazo la kwenda kule Mgahawani ili nizungumze tena na yule Meneja wa Mgahawa, niliona ana mengi ya kunieleza. Nilitumia tena usafiri wa pikipiki kuelekea Mgahawani, nilipofika nilisimama kidogo huku nikihema
“Hapa ndipo mahali pekee palipojaa ukweli kuhusu Mimi” nilijisemea, Kisha pole pole nilitembea Hadi ofisini kwa Meneja. Mlangoni nilikutana na kufuri kubwa, nilisimama kidogo nilifikiria nifanyaje mara alipita Mhudumu mmoja wa kike
Aliponiona alikuja Hadi niliposimama Kisha alinisamilia na kuniuliza “Una shida gani?”
“Nilihitaji kuonana na Meneja lakini kwa bahati mbaya nimekuta pamefungwa, ametoka muda mrefu?” nilimuuliza.
“Alishaacha kazi mbona tokea juzi, Bosi anatafuta Meneja mpya ndio maana ofisi imefungwa” alisema Kisha aliondoka zake akionekana ni mwenye haraka sana, aliniacha na maswali, niliona tumaini Hilo lilikua hafifu sana. Kama ameacha kazi basi kumpata itakua shida sana
“Dada Samahani” nilimsimamisha kabla hajafika mbali, Kisha nilimfuata na kumuuliza
“Naweza kupata mawasiliano yake?”
“Sina hakika sababu inasemekana ameondoka Nchini, familia yake ipo Malawi. Sijui kama unaweza ukampata” alisema Kisha aliondoka, nilisimama huku nikijiuliza mengi yaliyopita kichwani kwangu. Mshumaa nilioutegemea ulikua umezimika ghafla, niliishiwa nguvu
Nikapata wazo jipya la kuelekea kule alikokua anaishi Sudi. Nilihitaji kuelewa kuhusu Miaka mitano iliyopita maana nilihisi huwenda jambo Hilo lilikua kweli japo sikua na kumbukumbu ya Miaka hiyo. Hadi kufikia hapo nilihisi uwepo wa Siri fulani nisiyoifahamu
Niliondoka pale Mgahawani nikaanza safari fupi ya kuelekea Nyumbani kwa Sudi, nilikatiza mitaa Hadi kufika huko. Jua lilikua Kali sana lakini halikuzuia dhamira yangu ya kufika alipokua anaishi Sudi.
Nilipofika niligonga geti kama kawaida ili nifunguliwe, bahati nzuri alikuja yule Mdada aliyenifungulia siku ile. Alinisalimia kwa Bashasha maana alinikumbuka, nami nilionesha Upendo kwake
“Karibu tena Kaka” alisema akiwa anatabasamu.
“Asante sana Dada yangu, nimerudi tena” nilisema, akanitazama Kisha akaguna na kuniambia
“Kuna jipya gani tena?”
“Aaah! Unajua Kuna mengi sana yanaumiza kichwa changu Dada yangu, nimetafuta sana Majibu ya maswali yangu nimeona hapa ndipo mahali pekee ninapoweza kupata majibu.” Nilisema.
“Sasa kaka yangu kama nilivyokwambia, Mimi ni mgeni hapa sijui mengi kukuhusu. Hata hivyo Leo Baba mwenye nyumba yupo” Mwili ulisisimka baada ya kusikia kua Baba mwenye nyumba yupo, angalau yeye angenipa mwanga zaidi.
“Yupo wapi?”
“Ingia tu” Niliingia Hadi Uwani, nilimwona Baba mwenye nyumba akiwa anatoka kwenye kile chumba ambacho Sudi alikua akiishi. Nilikua nikimfahamu juu juu tu, basi haraka nilisogea kabla hata hajakifunga kile chumba, nikamsalimia kwa heshima sana
“Marahaba” aliitikia akiniangalia kwa jicho la kutonikumbuka.
“Ni Mimi Jacob Baba” nilisema.
“Jacob?”
“Ndiyo, rafiki yake Sudi”
“Ahaaa‼ Sasa wewe Kijana ulipotelea wapi, tulifanya jitihada za kukutafuta lakini hatukukupata, ilikuaje ukamtelekeza Mdogo wako hapa?” alisema yule Baba mwenye Nyumba, Kisha akamwambia yule Mdada atupatie viti tukae, ilionekana alikua na mengi ya kuniambia
Moyo Wangu na akili yangu vilikua tayari kusikia chochote kile hata kama kitaniumiza kiasi gani lakini Ndiyo ukweli pekee niliouhitaji kuusikia ili nifahamu mengi yaliyokua yakinitatiza.
Nilikua kimya huku moyo Wangu ukinidunda, viti vilipoletwa tuliketi kando ya kile chumba Kisha yule Mzee alishusha pumzi zake akaniuliza
“Ulikua wapi Kijana?”
Nini Kitaendelea? Usikose sehemu ya KUMI NA MBILI
JIUNGE NA KIJIWENI WHATSAPP CHANNEL Kwa Kugusa Hapa
Soma Riwaya Nyingine Za Kijiweni Kwa KUGUSA HAPA
Wewe kama MFANYABIASHARA.. Kuna wakati unatamani kuwafikia watu wengi zaidi na hujui wapi pa kuanzia , USIJALI kwani hapa ndipo ambapo MTAA UNAONGEA na tuko tayari kukusaidia kuwafikia watu wengi kwa BEI YA OFA
Njoo Utangaze Nasi Sasa Kwa Kutuambia Una TANGAZO Gani na unataka kutangaza kwa muda gani kwa kutuma ujumbe hapa WwhatsApp Kupitia Namba +255760871896
Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love