Ilipoishia sehemu ya nane ya In the name of LOVE

Ghafla tu, wazo la kumpigia simu Zaylisa lilinijia, nilihitaji kujua kama  alikua amefika kwa Baba yake. Nilipopiga niliambiwa simu ya Zaylisa ilikua  haipatikani, nilipatwa na hasira sana 

Niliketi nikitafakari zaidi, hamu ya kuendelea kua ndani iliniisha. Niliona  ni Bora niende mgahawani ambako nilikua nikifanya kazi, japo nilikua  nimefukuzwa lakini niliamini huko ningepata mwanga zaidi wa Maisha  yangu  

Niliondoka, nikaita Taxi. Safari ya kuelekea mgahawani ilianza. Nafsi yangu  ilikua kwenye Giza nene, hapakua na mwanga mithiri ya Handaki. Endelea

SEHEMU YA TISA

Nilimkumbuka rafiki yangu Sudi, Nilitamani sana kuonana naye maana  tokea nilipofukuzwa kazi wiki chache zilizopita sikuonana naye tena,  nilikua na uhakika kua alishiriki mazishi ya Mdogo wangu Melisa. Nilitaka  kujua mengi sana kutoka kwake, basi Taxi ilitembea taratibu Hadi ilipofika  Mgahawani. 

Nilimlipa pesa dereva Kisha aliondoka zake, aliniacha nikiwa nimesimama  mbele ya Mgahawa. Nilikua nimevalia suruali ya kaki yenye mifuko  mikubwa, ilikua fupi, chini nilivalia sendozi nyeusi huku juu nikiwa na  tisheti nyeupe 

Nilitabasamu kidogo maana Mgahawa huo ulikua na kumbukumbu ya  safari ndefu ya Maisha yangu. Ilinijia kumbukumbu ya Siku ambayo  nilizungumza na Zaylisa Kuhusu kumuowa. Nilikumbuka siku hiyo Ndiyo  siku ambayo Mama yangu alifariki kwa kujinyonga, lile tabasamu liligeuka  kua huzuni nyepesi, chozi kidogo lilinilenga lakini sikuruhusu lidondoke 

Macho yangu yalikua yakichemka ukali wa fukuto la chozi huku kope zangu  zikicheza haraka haraka, nilivuta hewa nzito ili kufungua zaidi pua zangu. 

Muda huo jua lilikua likianza kua Kali kidogo, nilitoa kitambaa na kufuta  jasho pamoja na matone madogo ya machozi yaliyoganda kwenye kope  zangu. 

Halafu niliutazama zaidi Mgahawa, wakati huo Meneja alikua akikatiza  kwenye kiunga, aliniona nikiwa nimesimama. Taratibu alisogea Hadi  karibu na Mimi, nilipomwona nilitabasamu

Lakini yeye alitoa tabasamu la Mshangao kama vile alikua akijiuliza  maswali mengi yasiyo na Majibu.  

“Ooh Jacob” aliita kwa sauti ya Wasiwasi kidogo. Kisha alisogea zaidi “Ni Mimi hapa Meneja wangu” nilisema, nilizidi kumfanya anishangae. 

“Karibu tu” alinikaribisha huku akinipa ishara kua niingie Mgahawani,  tuliongozana huku nikiangalia huku na kule lakini sikufanikiwa kumwona  hata Mfanyakazi mmoja niliyemfahamu, Kila Mfanyakazi alikua mpya  machoni pangu kitu ambacho kilinishangaza 

Nilihisi kutembea kwenye sakafu isiyonifahamu Mimi, niliona wakiwa  wanahudumia Wateja tofauti tofauti, hata mpangilio wa meza, pazia na  mapambo ulikua wa tofauti sana kama vile ulipitia muda mrefu  nisioukumbuka 

Nilitembea nyuma ya Meneja huku nikiwa na maswali mengi sana, macho  yangu yalikua yakishuhudia vitu vingi vilivyonipa maswali mengi.  

Tulielekea Moja kwa moja kwenye ofisi ya Meneja, alinikaribisha tena  Kisha aliketi kitini huku akinitazama kwa Udadisi sana. Nilitabasamu  kidogo huku nikiyapa nafasi macho yangu kubarizi ofisi ya Meneja, ilikua ni  ofisi tofauti na ofisi niliyoifahamu 

“Karibu sana Jacob” alinikaribisha tena, alikua ni Mtu wa kurudia maneno. 

“Nimesha karibia Meneja wangu, wiki chache tu Kila kitu kimebadilika.  Naona una sura ngeni Kila Kona ya Mgahawa, sioni wale Watu  niliowafahamu” nilisema, Kauli hii ilimfanya anitazame kwa jicho la tofauti  kidogo, alizidi kuonekana ni mwenye maswali mengi ya kuniuliza. 

“Aah! Kwani Jacob…” alisema kwa kusitasita, nikamwahi 

“Bosi usijali, najua ulinifukuza. Nimekuja hapa Nina maswali kadhaa, hata  hivyo sikupanga kuonana nawe, nilikuja kwa ajili ya Sudi. Unajua nilipata  ajali siku Moja baada ya kunifukuza hapa, angalau sasa najisikia nafuu”  nilisema, niliuwona Msongo wa maswali ambao Meneja alikua akipambana  nao 

“Jacob upo sawa?” aliniuliza. 

“Ndiyo Meneja wangu, vipi Sudi amefika kazini Leo?” niliuliza. “Sudi?” 

“Ndiyo, maana sikumwona baada ya ajali. Hata hivyo nimempoteza Mdogo  wangu Melisa sijui kama unalifahamu Hilo?” nilimuuliza, akameza funda 

zito la mate huku akiniangalia kwa jicho la wasiwasi. Alianza kuwa mwoga  na wala sikujua ni kwanini  

Nilijitazama labda nilikua na kitu kilichoanza kumpa hofu lakini sikuona. “Aah Unajua Sudi….aaah‼” alijiuma uma, nikamuuliza tena “Au naye ulimfukuza?” 

“Aaah‼ Ndiyo, aliacha kazi mwenyewe hivyo sikujua hata alielekea wapi”  alinijibu, nilishusha pumzi zangu 

“Basi sawa, nilikuja kumtazama yeye tu. Maana nimeshauriwa na Daktari  kua siruhusiwi kutumia simu hivyo nimeshindwa kufanya mawasiliano  naye” nilisema Kisha nilinyanyuka, naye alinyanyuka huku akinitazama  sana 

“Jacob, upo sawa?” aliniuliza swali lile lile, nilijua pengine alisikia kua  nilipata ajali na labda alikua akijali kuhusu afya yangu.  

“Usijali nipo sawa, Wacha nikamwangalie anapoishi” nilisema Kisha  niliondoka pale ofisini, kitu pekee nilichotaka ni kuonana na Sudi maana ni  Mtu pekee ambaye angeliweza kuniambia mambo mengi nisiyoyaelewa  katika Maisha yangu baada ya ile ajali. 

Kutoka pale Mgahawani Hadi anapoishi Sudi palikua na Umbali kiasi,  wastani wa dakika kama ishirini na tano kwa usafiri. Nilitumia usafiri wa  Bajaji, kichwa kilianza kuniuma kwa mbali lakini niliona ni Bora niende  kwa Sudi ili kufahamu mengi nisiyoyajua kuhusu Mimi. 

Nilijiona ni Mtu niliye gizani, wiki chache za ajali zilibadilisha mambo  mengi sana. Sikua na tofauti na kitabu kilichopoteza baadhi ya kurasa kwa  kuungua na Moto, tumaini pekee lilikua ni Sudi.  

Tulipofika, nilimpa hela dereva Kisha pole pole nilitembea kutoka  Barabarani kuelekea mtaani, ndani huko ambako hata Bajaji lisingeliweza  kupita kirahisi. Mitaa ile haikua mipya kwangu, nilikua naifahamu vizuri  sana.  

Basi nilitembea kwa dakika kama mbili hivi, nilihisi kiu ya Maji tena ya  Baridi, niliona Duka nikaingia nikanunua Maji Kisha nikanywa na kusonga  mbele Hadi nilipofika anapoishi Sudi. Ilikua ni nyumba ya uswahilini yenye  geti dogo Jekundu, niligonga na kusubiria lifunguliwe 

Mara nilisikia sauti ya kufunguliwa Kisha nilimwona Mwanamke mmoja  mfupi mweusi, aliyejifunga kilemba chekundu, alivalia Dera la rangi ya  kahawia

“Karibu” alisema, sura yake ilikua ngeni machoni pangu ila sikutaka  kulijadili Hilo sababu wapangaji hasa nyumba za Mijini huama Kila  kukicha. Nilitabasamu kidogo maana Ndiyo ilikua Haiba yangu kubwa 

“Ahsante, samahani. Namuulizia Sudi, sijui nimemkuta?” alistaajabu kwa  kuguna kidogo Kisha akaniambia 

“Mh! Kaka yangu Mimi ni mgeni tu hapa, nimehamia juzi. Simjui huyo Sudi  labda uingie kama unakifahamu chumba chake” alisema, basi niliingia  nikiwa nyuma yake Hadi eneo la Uwani, maana Sudi alikua akiishi chumba  Cha Uwani. 

Chumba chake kilikua kimefungwa kufuli kubwa, nilishusha pumzi maana  nilijua atakua ametoka na kwa jinsi alivyofunga basi alikua mbali na  nyumbani. 

“Chumba chake ni kile pale lakini kimefungwa” nilimwonesha yule  Mwanamke.  

“Kwani mbona nilisikia kua kile chumba kina Siri” alisema, kidogo  nilishtuka. 

“Siri, una maanisha nini?”  

“Mh! Samahani , nimesikia kile chumba hakipangishwi. Huu ni mwaka wa  Tano sasa” alisema, nilijikuta nikicheka maana kwa ninavyofahamu nilikua  nikiishi mle Mimi, Sudi na Mdogo wangu Melisa tena ni wiki kadhaa tu  zilizopita. 

“Hebu acha utani Bwana, kile chumba anaishi rafiki yangu Sudi. Labda tu  ulisikia vibaya” nilisema lakini sura ya yule Mwanamke haikubadilika Bali  iliendelea kuonesha kua alichokisema alikimaanisha 

“Kaka yangu, Mimi nimeelezwa na Mwenye nyumba maana lengo langu  lilikua nipange kile chumba. Niliambiwa kua ndani ya kile chumba alifia  Msichana tena aliuawa na huyo unayemsema sijui ni Sudi kama sikosei  

Kisha akakimbia, tangu hapo hakuna aliyeishi tena hivyo mwenye nyumba  aliamua kukifunga.” Alisema kwa sauti ya Msistizo, nilijikuta nikiishiwa  nguvu Hadi nilipepesuka. Kizungu-zungu kiliniandama Hadi Niliketi juu ya ndoo 

“Kwani huyo Sudi wewe ni Nani Yako?” aliniuliza, nilimeza funda zito la  mate. Nilihisi kuzidi kupagawa, nilichokisikia ni kama kilikua kwenye  filamu au vitabu vya Riwaya. Ingewezekana vipi kifungwe kwa Miaka  mitano kisa Sudi alifanya Mauwaji wakati Meneja aliniambia aliacha kazi,  kama angelikua amefanya tukio Hilo ningejua sababu Mimi ni rafiki yake.

Jasho lilikua likinitoka, nilimuuliza yule Mwanamke aliyekua mbele yangu “Huyo Msichana aliyemuuwa alikua ni Nani?”  

“Nitajuaje Mimi, hata hivyo sikupaswa kuyasema yote haya. Hujajibu, huyo  Sudi ni Nani Yako?” 

“Rafiki yangu, Ona Dada yangu. Mimi nilipata ajali wiki chache zilizopita,  nilimwacha Mdogo wangu na Sudi, unaposema chumba hakitumiki kwa  Miaka mitano sasa nastaajabu. Ni ndoto ya aina gani hii?” nilisema, mara  Simu ya yule Mwanamke iliita. 

“Mume wangu ananipigia, hicho ndicho nilichokisikia na wala Sina Cha  ziada” aliondoka akiwa anaongea na simu, aliniacha nikiwa nimekaa juu ya  ndoo, nilitamani kuamini lakini uhalisia ulinikataza.  

Nilipata wazo la kurudi Mgahawani kwa meneja, niliamini sasa ni yeye  ndiye anayeweza kufumbua Fumbo hili, nilinyanyuka taratibu kama  Mgonjwa. Nilitembea kwa kujiburuza huku jasho likinitoka, nilikua  nimechanganyikiwa sana. Kila kitabu nilichofungua ili nifahamu mengi  kilikua na mapungufu ya kurasa muhimu, sasa nilirudi Mgahawani 

Nilielekea Moja kwa moja Hadi ofisini kwa Meneja, nilimkuta akiwa  anaendelea na majukimu yake. Aliponiona alinyanyuka kitini na  kunitazama kwa Mshangao, alionekana kama Mtu aliyetarajia kua  ningerudi kwake 

Nilikua navuja jasho, nilichoka sana. Nikaketi nikiwa kimya sana, shingo  yangu ilikua ikiangalia chini, Jasho lilidondokea kwenye Suruali yangu 

“Jacob” aliita Meneja, taratibu nilinyanyuka kichwa changu nilimtazama,  alinitazama bila kusema chochote kile. 

“Naishi Dunia ipi?” nilimuuliza, aliinamia chini. Alionesha kujutia kwa  jambo Fulani ambalo hakuniambia nilipofika kwa mara ya kwanza  kumuulizia Sudi.  

“Jacob, samahani” 

“Samahani ya Nini?” nilimuuliza, alipoanza kunyanyuka Mdomo wake  ghafla alikatishwa na sauti ya kufunguliwa kwa Mlango, Nami nilishtuka.  

Niligeuka haraka kutazama mlangoni, Zaylisa alikua mbele ya macho  yangu. Nilimtazama kwa kustaajabu sana, aliwezaje kujua nilipo?  

“Jacob” aliniita kwa sauti ya taratibu, Kisha alimtazama Meneja.

“Nitakueleza Kila kitu, naomba turudi nyumbani” alisema, nilijawa na  tumaini  

Kitu pekee nilichohitaji ni kujua mengi yaliyokua yakizunguka kichwani  kwangu, Basi. Mimi na Zaylisa tuliondoka pale Ofisini kwa meneja bila  kusikia chochote Cha umuhimu kutoka kwa Meneja, ni kama Zaylisa alikua  amekatisha mazungumzo yetu lakini kwakua alikua ameniambia atanieleza  Kila kitu ilikua rahisi kwangu kukubali. 

Tulitumia usafiri wa Taxi Hadi nyumbani kwa Clara, palikua kimya sana  hakuna aliyezungumza na mwenzake. Palitulia kimya mithiri ya Usiku wa  Giza nene, nilitembea taratibu huku kichwa changu kikiwa kimejaa maswali  mengi, nyuma yangu nilikua nikizisikia hatua za Zaylisa, kiatu chake kirefu  Cha kuchongoka kilikua kinamtoka sauti ya ‘KO! KO!’  

Nilitekenya kitasa huku mkono mmoja ukiwa nyuma ya kiuno changu,  nilielekea Kuketi kwenye sofa kama Mtu aliyepoteza tumaini, Zaylisa naye  aliingia Kisha aliufunga mlango. Pole pole naye alisogea kando yangu Kisha  akafungua kinywa chake kwa sauti ya utulivu sana 

“Jacob” aliniita, niligeuza shingo nikamtazama. Alikua amebana midomo  yake Kisha akanishika bega taratibu, mguso wa kunituliza 

“Pole, najua una maswali mengi lakini nitayajibu” alisema Kisha  alinyanyuka, nilikua namtazama kama Mtu aliyekua na mengi niliyokua  nikiyatafuta. Kisha aliekea kwenye friji, akatoa Maji ya baridi akayamimina  kwenye glasi, akarudisha jicho kwangu 

Halafu pole pole akaja nilipokua nimekaa, naye akakaa na kuniambia 

“Tafadhali kunywa kwanza haya Maji Mpenzi wangu Kisha nitazungumza  nawe” nilimtazama nikiwa kimya, sura yangu ilikua na uchovu mwingi.  Akanipatia glasi, nikatumia mkono Wangu wa kushoto kupeleka glasi  kinywani Kisha nikaruhusu koo langu kupitisha Maji ya baridi 

Nilipiga funda Nne za nguvu, kweli nilijisikia utulivu. Zaylisa akaichukua  glasi kutoka kwangu na kuiweka juu ya meza ya halafu akanitazama huku  akitabasamu. 

“Ulijuaje kama nilikua pale?” nilimuuliza kwa sauti ya umakini, Kisha  nilimtumbulia macho. 

“Jacob, najua una maswali mengi sana. Nitajibu Moja baada ya jingine”  alisema Zaylisa

“Nataka kujua, Mimi ni Nani Zaylisa? Kwanini Kila kitu kimebadilika ndani  ya wiki chache tu?” nilimuuliza maswali mawili yaliyomfanya apumue kwa  kina kabla ya kuitumia sauti yake tulivu kunijibu.  

“Wewe ni Jacob wangu, yule yule niliyempenda na ninayempenda. Jacob,  baada ya ajali Kuna kitu hakipo sawa kwako” alisema Kisha alisita  kuendelea, nikamuuliza 

“Hicho kimefanya Kila kitu kibadilike? Sudi alimuuwa Mdogo wangu na  siyo kama ulivyoniambia kua Melisa alikufa kwa mshituko?” 

“Hapana, Melisa alikufa kwa Mshituko Jacob. Nilikuwepo kwenye Mazishi,  Jacob Bado haujapona vizuri unapaswa kutuliza akili Kisha Kila kitu  kitakua sawa. Kila unachokiona hakipo kama unavyofikiria, jipe muda  Kisha ukipona utaona mambo yanaenda inavyotakiwa” alisema Zaylisa,  hakukata kiu ya maswali yangu. Ni kweli nilipata mtikisiko wa Ubongo  kidogo kutokana na ajali lakini Bado akili yangu ilikua sawa Kwani nilikua  natambua lakini nilihisi Kuna Sehemu ya Maisha yangu ilikua imerukwa. 

Chozi lilinidondoka taratibu, upande mmoja wa akili yangu uliniambia kua  nilikua ninaishi kwenye Dunia iliyojaa siri na Giza lakini upande mwingine  uliniambia kua nilikua Pengine akili yangu ilikua inapitia changamoto  kidogo 

“Lakini Zaylisa, ni kwanini Watu huniita Bosi? Mimi ni Nani hasa, kitu gani  sikijui kuhusu Mimi?” nilimuuliza, hakunipa jibu, alinisogeza na kunilaza  kifuani pake huku akipapasa nywele zangu taratibu.  

** 

 SURA YA 8 

(Mpango wa Siri) 

Jioni ilipoingia ilinikuta nikiwa nimeketi valandani, nilikua nabarizi kidogo  huku nikipigwa na jua jepesi lililokua likielekea kuzama. Kila nilichokiona  mbele yangu kilikua kina rangi nyekundu ya jua, upepo ulikua ukivuma  taratibu sana 

Palikua kimya, nilihitaji ukimya huo ili kunituliza akili yangu iliyokua  ikipotea mara kwa mara. Nilikua nimekunja Nne nikiwa nimeketi kwenye  kiti Cha nyavu kilichonipa utulivu, nilivalia singlendi nyeupe na Suruali  nyepesi

Alikuja Zaylisa, alikua ameshikilia sahani yenye matunda. Nilipomwona  nilimwonesha tabasamu, naye alinirudishia tabasamu  

Zaylisa ni Mwanamke mzuri sana ambaye Kila Mwanaume alihitaji kua  naye, tabasamu lake lilikua tiba isiyoonekana ya Moyo Wangu.  Nilimtazama kidogo Kisha alisema 

“Usiwaze sana kuhusu Dunia Yako Jacob. Kila kitu kitakua sawa” alisema  huku akivuta kiti na Kuketi. 

“Karibu matunda Mpenzi” alisema tena, alinipatia sahani yenye matunda  pamoja na Uma. Nilichoma kipande Cha tiki Maji Kisha nilikitia Mdomoni  na kukitafuna pole pole 

“Asante My love. Uwepo wako ni tulizo tosha kwangu” nilisema huku  nikimalizia kutafuna, akanishika mkono akaniambia 

“Nitakua na wewe Maisha yangu yote Jacob, sitakuachilia hata kama penzi  letu litapitia njia yenye Milima na mabonde” maneno yake yalinifanya  nitabasamu tu, Kila Mwanaume hutulizwa kwa Maneno mazuri na matamu  kama haya  

“Lakini Zay, Bado nahisi Kuna kurasa ya Maisha yangu imeondolewa  kwenye kitabu changu” nilisema, Zaylisa alinisugua mkono Wangu taratibu  akaniambia 

“Najua na ninakuelewa, unavyojihisi kwasasa hata Mimi najisikia vibaya  Jacob. Kamwe sitakua sawa Hadi pale nitakapo hakikisha upo sawa”  

Licha ya maneno mazuri na ya matumaini kutoka kwa Zaylisa Bado nilikua  na wasiwasi kuhusu Mimi. Nilifikiria kuhusu ile Bahasha, sikujua ilikua  imepotelea wapi?  

Kama Matilda hakuichukua sasa Nani mwingine aichukue, kwanini ipotee  ina nini ndani yake? Nilijiuliza yote lakini mwisho nilijiuliza kuhusu Mtu  ambaye Zaylisa alikua amempigia simu asubuhi ‘MZEE WA MIPANGO’  

“Babe” nilishtuliwa na Zaylisa baada ya kuona nilikua nimezama mawazoni,  nilishtuka Kisha niliigiza kama vile nilikua sawa tu. Kabla hajasema neno  lingine mara Simu yake iliita, haraka aliangalia ni Nani alikua akimpigia  

Ghafla sura yake ilipoteza uchangamfu, akaonekana kua na wasiwasi. 

“Samahani naongea Na simu” alisema Kisha aliondoka pale akaelekea  ndani, sikutaka kujishughulisha sana. Niliendelea kula matunda 

Haikuchukua muda mrefu, Zaylisa alirudi akiwa na furaha.

“Kulikoni mbona unafurahia sana, halafu hujanambia kuhusu Hali ya Baba  Yako” nilimuuliza. 

“Kumbe haikua inshu kubwa sana Mpenzi, Presha ilipanda kidogo. Ah!  Mama yangu naye akalikuza sana” alisema huku naye akichukua kipande  Cha tunda kwa kutumia mkono wake Kisha akaliweka Mdomoni. 

“Na vipi kuhusu hiyo simu, una furaha sana”  

“Eeh! Mama alikua akinipa mrejesho kuhusu Hali Baba” alisema Zaylisa.  Niliguna tu Kisha niliendelea kula matunda. 

Siku iliyofuata asubuhi mapema, Zaylisa aliniaga kua anaenda kumjulia  Hali Baba yake, tukakumbushana kua ilikua ni siku ya Clara kurudi kutoka  Arusha. 

Nini Kitaendelea? Usikose sehemu ya KUMI

JIUNGE NA KIJIWENI WHATSAPP CHANNEL Kwa Kugusa Hapa 

Soma Riwaya Nyingine Za Kijiweni Kwa KUGUSA HAPA

Wewe kama MFANYABIASHARA.. Kuna wakati unatamani kuwafikia watu wengi zaidi na hujui wapi pa kuanzia , USIJALI kwani hapa ndipo ambapo MTAA UNAONGEA na tuko tayari kukusaidia kuwafikia watu wengi kwa BEI YA OFA

Njoo Utangaze Nasi Sasa Kwa Kutuambia Una TANGAZO Gani na unataka kutangaza kwa muda gani kwa kutuma ujumbe hapa WwhatsApp Kupitia Namba +255760871896 

Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love 

Exit mobile version