Ilipoishia sehemu ya tano ya In the name of LOVE

Upepo ulikua ukisukuma nywele zake, nilipata shahuku ya kutaka kuongea  naye. Nilielekea mlangoni nikafungua mlango taratibu, sauti ya mlango  ilimfanya ashtuke na kugeuka. Aliniona nikiwa nimesimama mlangoni  nikimtazama, alikua akidondosha chozi bila kuficha. 

Tulitazamana bila kusemeshana kwa sekunde kadhaa huku nikitafakari  nini maana ya chozi lake, mbona Kila niwapo karibu naye hua nahisi Hali  isiyo ya kawaida. Nilisogea taratibu nikimtazama, macho yetu yalikua  thabiti yasiyo kwepana  

Hadi namfikia hakuna aliyeongea na mwenzake, nilijikuta nikimweka vizuri  nywele zake.  Endelea

SEHEMU YA SITA

“Clara, Kwanini unalia, muda huu nilitegemea ungekua chumbani kwako”  nilimuuliza, swali langu liliamsha chozi lake zaidi. Alidondosha chozi 

“Nafikiria kuhusu Melisa, alichokisema wakati wa chakula” alisema Clara,  nilikumbuka alichokisema Melisa. Ni kuhusu kunitia Mimi ‘Baba’ 

“Hilo halina shida, Mimi ni sawa na Baba yake. Au naweza kua Baba yake  pale anapohisi anahitaji faraja ya Baba” nilisema, sikujua Masikini Kila  neno lilikua kama mwiba kwake, alinitazama kwa jicho la maumivu zaidi 

“Natamani Baba yake Angekua Hapa Jacob, Angekua anajua kua Melisa ni  Binti yake” alisema. 

“Kwani Baba yake yupo wapi?”  

“Baba yake hamkumbuki tena Melisa, ameenda mbali na kumbukumbu  zake nzuri. Mara ya mwisho ilikua ni siku ya Kumbukumbu ya Kuzaliwa  kwa Melisa, tangu hapo hamkumbuki tena” alisema akiwa anamwaga chozi. 

“Amemkimbia Mtoto au kimetokea nini?” 

Akatikisa kichwa chake, akaniambia 

“Asingeliweza kumkimbia, anampenda sana. Naamini ipo siku  atamkumbuka Binti yake Melisa” alisema Kisha aliondoka mbele ya macho  yangu mithiri ya nyoya la Kuku, upepo ulinipitia akinipita ubavuni na  kurejea ndani, aliniacha na maswali mengi yasiyo na Majibu. 

Upepo wa baridi ulinisindikiza nikiwa kama nimemwagiwa na Maji ya  baridi.  

“Jacob” Sauti ya Zaylisa ilisikika nyuma yangu, nilipogeuka nilimwona yeye  akiwa anatabasamu.

“Umeniacha chumbani peke yangu Mpenzi, umekuja kupigwa na Baridi  huku kweli?” nilitabasamu bila kua muwazi. 

“Nilikua…” kabla sijamaliza alinikatisha, akaniambia 

“Ulikua unapunga upepo, Mpenzi naumia ukiwa hivi. Kama Kuna chochote  unanificha siwezi kujisikia vizuri Jacob, nimeachana na Mwanaume yule  kwasababu niliolewa naye kwa shinikizo la Wazazi tu lakini siyo Upendo”  alisema, sikutaka ajisikie vibaya. Nilimvuta na kumkumbatia kwa Huba  liwakalo moto. 

*** 

Siku iliyofuata, asubuhi ilianza kwa baridi Kali. Nilishtuka na kutoka  kitandani, nilitikisa kichwa changu, kidogo nilihisi maumivu ya kichwa  hasa upande wa Kushoto.  

Nilijikuta nikiwa mwenyewe pale kitandani, Zaylisa hakuwepo.  

“Aaah, Aaah” niligugumia kidogo sababu ya maumivu ya Kichwani,  nilishusha pumzi nzito huku swali pekee nililojiuliza lilikua 

“Zaylisa yupo wapi?” basi nilishusha miguu yangu pole pole, nikaikanyaga  sakafu Iliyo baridi. Sakafu Iliyo Kimya isiyonikumbuka, nilitembea taratibu  nikafungua mlango pole pole, nikaangaza eneo la Korido. Eneo lote lilikua  kimya kama Chumba kilicho tupu. 

Kabla sijafanya maamuzi ya kwenda popote nilianza kusikia sauti mbili  zikiongea, zilikua ni sauti zenye kumbukumbu ndani yangu. Moja  niliitambua kua ni ya Mpenzi wangu Zaylisa, nyingine ilikua ya Clara. Sauti  zao hazikuashiria amani, walikua wakiongea kwa mafumbo sana  

“Mh‼” niliguna, nikapikicha macho yangu katika Hali ya kuondoa uzito  machoni, nikahisi wepesi machoni lakini uzito masikioni niliposikia Clara  akisema 

“Huu haukua mpango wetu Zaylisa, wewe ni Mke wa Mtu. Kilichokuleta  hapa ni nini?” lilikua ni swali dogo lakini lilibeba hatma ya Maisha yangu,  hapo hapo nilihisi Ubaridi puani. 

Nilivuta tena hewa Kisha niliitoa pole pole, nilikua nimesimama mlangoni  Bado. 

“Clara, ukitaka kua salama usiyaguse Maisha yangu. Nina ufunguo,  nikiamua nafungua popote. Muda wowote ninaoutaka” alisema Zaylisa,  sikuelewa walikua wakibishania kitu gani ambacho Kila mmoja alikua 

akiongea kwa mafumbo. Basi, niliamua kuzifuata sauti zao nikipita Korido  Iliyo Kimya 

Baada ya hatua mbili nilijikuta nikisimama taratibu, miguu yangu iligoma  kufanya safari. Nilihisi palikua na Mtu nyuma yangu, Mtu huyo alikua  kimya lakini alikua na hisia iliyounganishwa na Mimi 

Taratibu niligeuka kuangalia nyuma, chumba Cha Mwisho kabisa Mlangoni  alikua amesimama Melisa. Huyu siyo Melisa Mtoto, Bali ni Mdogo wangu  Melisa, alikua amevalia nguo nyeupe mithiri ya Malaika. 

Tabasamu lake lilikua linanipa ujumbe wa Siri niliokua nashindwa  kuufungua. Jicho langu Moja lilianza kudondosha chozi, pole pole midomo  yangu ilianza kutetemeka 

Tabasamu la Melisa lilikua thabiti machoni pangu, lilikua ni tabasamu lile  lile lililofanana na Marehemu Mama. Jicho lingine likadondosha chozi la  Hisia Kali ya maumivu, nilinyoosha Mkono ili Melisa aje kwangu 

Alikua ameshafariki lakini kwanini nilikua namwona, sikuweza kupata  Majibu.  

“Melisa” niliita, aliendelea kutabasamu tu. Kisha alisema 

“Kumbuka Kaka, usijipoteze kamwe, kumbuka wewe ni Nani. Wewe ni  Jacob, Ndiyo jikumbuke Kaka….” Alisema huku akinitazama Usoni, nilikua  na maswali mengi lakini mdomo Wangu uligoma kuuliza chochote. 

Nilianza kutembea kuelekea alipokua amesimama, sikutaka kuchelewa  nilitaka kumkumbatia Melisa, nilikua nimemkumbuka sana. Nilisogea na  kumkumbatia kwa hisia Kali sana, nililipata joto lake, nilihisi kua Sehemu  salama sana Maishani mwangu 

“Melisa, nimekukumbuka sana. Usiondoke ukaniacha tena” nilisema huku  chozi langu likimdondoka mabegani kwa Melisa 

“Usiniache tena, Baki na Mimi. Nakuahidi sitaondoka tena, sitakuacha peke  Yako…..nitakulinda Maisha yangu yote, nitatimiza ahadi zangu..” nililia  sana, sikutegemea kama ningemwona tena Mdogo wangu Melisa 

Nilikaa kimya kusubiria aseme chochote, nilipepesa macho yangu pole  pole.  

Japo nilizungumza sana lakini kwa Melisa ilikua kimya, palikua kimya zaidi  ya kimya nilichowahi kukisikia. Kama vile Dunia ilikua ikisimama na Kila  Mtu akiwa anasubiria jambo Fulani, ghafla nikaisikia sauti kutoka kwa  Melisa

“Babaa” ilikua ni sauti ya Mtoto mdogo, nilihisi kurukwa na akili yangu.  Nilijikuta nikiwa nimechuchumaa nikiwa nimemkumbatia Mtoto Melisa,  sikuamini kua ilikua ni ndoto ya kutisha iliyokua ikitembea. 

Niliinua uso wangu, Ndiyo‼ Melisa Alikua mbele yangu, aliniita tena 

“Babaa‼” huku chozi likiwa linamtiririka, nilihisi kuvuta hewa nzito yenye  joto, halafu kabla hata sijafikiria zaidi nilisikia sauti ya kugombana. Clara  na Zaylisa walikua wakigombana Sebleni 

Haraka nilikimbilia Sebleni, nilimkuta Msichana wa kazi akiwa anaamua  ugomvi wao, sikujua walikua wakigombana nini lakini Zaylisa alikua akilia  baada ya kuniona Kisha alinifuata na kunikumbatia akiniambia 

“Jacob, Clara hataki niishi hapa” alisema huku chozi likiwa linamvuja,  nilinyanyua uso na kumtazama Clara, niliona jinsi alivyopata Kigugumizi  kusema. Lakini nilihisi alikua anataka kujitetea, nilimkagua na Msichana  wa kazi. Naye alinitazama kidogo kwa aibu halafu akamtazama Clara 

Pale pale Melisa aliingia na kwenda Moja kwa moja kwa Mama yake Kisha  akamkumbatia huku naye chozi likimbubujika, hata sura yake ilionesha  huzuni sana. Nilijihisi kutoelewa Kila kitu nilichokiona na kukisikia 

Chembe chembe ya maumivu iliniingia ghafla, macho yangu yakachemka  chem chem ya Machozi mithiri ya Mtu aliyewekwa pilipili machoni,  nilimkubatia zaidi Zaylisa. 

Sikujua walikua wakigombana nini lakini nilichagua kua Upande wa  Zaylisa, hisia ziliniambia alikua akionewa na Clara. 

Nilimtazama tena Clara, niliona akinyanyua midomo yake ili aongee lakini  nilitikisa kichwa changu kuashiria kua asiongee chochote sababu nilielewa. 

Niliondoka na Zaylisa, tukaelekea chumbani taratibu huku Zaylisa akilia  kwa sauti ya chini, Melisa alinitazama, nilihisi alihitaji sana kuniambia kitu  Fulani muhimu lakini alikua amefungwa minyororo ndani ya akili yake . 

Miguu yangu ilihesabu hatua pole pole Hadi tulipozama na kufunga  Mlango. Nilimtazama Zaylisa, macho yake yalikua mekundu kwasababu ya  kulia, nilimketisha kitandani Kisha nilitumia kitambaa kumfuta chozi lake  taratibu kama Daktari wa Macho.  

“Asante..” alisema. Nilimshika mikono yake huku uso wangu ukiwa na  Upole usio mithirika.  

“Mpenzi wangu” hatimaye nilisema. Alinitazama zaidi, sikuona hata  chembe ya Uwongo machoni pake

“Pole kwa kilichotokea, sijui ilianzaje lakini….”  

“Jacob, hauniamini?”  

“Hapana Mpenzi sijasema sikuamini, lakini haikua njia nzuri kulumbana  naye kiasi kile. Nafikiria ingekua busara zaidi ungenieleza bila kubishana  naye” nilisema kwa sauti ya Upole, Mungu alinijaalia sauti nzuri na nzito  iliyotoka kwa mpangilio 

“Kilichomiuma, aliniita Masikini pia changudoa. Tokea umenijua umewahi  kuniona Mimi nikiwa changudoa Jacob? Hilo la Umasikini halina shida  kwangu kwasababu pesa zinatafutwa” nilishusha pumzi zangu Kisha  nilipepesa macho yangu huku feni ya juu ikiendelea kuzunguka na  kutupatia Upepo 

“Wacha nikazungumze naye, nimkanye asirudie kukuita hivyo na kama  atarudia basi tutaondoka hapa” 

“Jacob….Haina haja, sitaki uende mbali Mpenzi wangu, kaa kando yangu”  alisema Zaylisa Kisha alijilaza mapajani mwangu, aliizuia rasmi nia yangu  ya kwenda kwa Clara. Nilitabasamu na kuanza kuchezea nywele zake 

“Itakuaje akitufukuza?” aliniuliza Zaylisa. 

“Tutatafuta Sehemu ya kuishi Zaylisa.” 

“Jacob, hauna kazi upo hapa tu unafikiria itakua rahisi?” 

“Sasa nifanye nini au nikueleze nini Mpenzi, nimefukuzwa kazi kule  Mgahawani. Nimewapoteza Mama na Mdogo wangu Melisa, ndani ya  kipindi kifupi Kila jambo limebadilika, nikuonapo nahisi tumaini kubwa  likichipua ndani yangu, sitaacha nitapambana” 

“Siku Moja ntakuambia nini Cha Kufanya Jacob, ukifanya hicho utakua na  pesa nyingi na hakuna Mtu atakaye thubutu kucheza na Utu wako” alisema  Zaylisa, aliniacha na mzigo mzito wa maswali yasiyo na Majibu, nilijiuliza  ataniambia nifanye nini ili nipate pesa nyingi kiasi hicho 

Niliendelea kumbembeleza taratibu huku tukiuruhusu ukimya utawale.  Nywele za Zaylisa zilikua laini, zilinipa Raha kuzipapasa 

Mara mlango uligongwa, Zaylisa aliinuka Kisha alinitazama. Sote tulijiuliza  ni Nani aliyekua anaugonga mlango, Mimi nilinyanyuka na kuelekea  Mlangoni, nilipofungua nilikutana na sura ya Msichana wa kazi, alianza  kunitazama kwa jicho la Upole sana Kisha akaniambia

“Dada anakuita” niligeuka kumwangalia Zaylisa, hakusema chochote ila  alinitazama kwa jicho la kuniambia kua nitakacho kiamua kitakua sawa  kwake. Nilishusha pumzi kidogo halafu nikamjibu 

“Sawa, nakuja” sauti ya taratibu iliyojaa uzito ilinitoka. Yule Msichana  aliondoka zake, nilifunga mlango. Nikamwangalia tena Zaylisa, nilishusha  pumzi Kisha nikafungua tena mlango nikatoka kwa ajili ya kwenda  kuonana na Clara. 

Nini Kitaendelea? Usikose sehemu ya SABA

JIUNGE NA KIJIWENI WHATSAPP CHANNEL Kwa Kugusa Hapa 

Soma Riwaya Nyingine Za Kijiweni Kwa KUGUSA HAPA

Wewe kama MFANYABIASHARA.. Kuna wakati unatamani kuwafikia watu wengi zaidi na hujui wapi pa kuanzia , USIJALI kwani hapa ndipo ambapo MTAA UNAONGEA na tuko tayari kukusaidia kuwafikia watu wengi kwa BEI YA OFA

Njoo Utangaze Nasi Sasa Kwa Kutuambia Una TANGAZO Gani na unataka kutangaza kwa muda gani kwa kutuma ujumbe hapa WwhatsApp Kupitia Namba +255760871896 

Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love xx Love 

 

Leave A Reply

Exit mobile version