Ilipoishia Return of Faudhia sehemu ya saba 

“Naomba niongee na Shayo haraka” Alisema Rais, mara moja  Waziri Mkuu alipiga simu kwa mkuu wa kitengo cha Usalama wa  Taifa ambaye hadi kufikia wakati huo hakujuwa Faudhia alikuwa  wapi, ni mzima au amekufa ila Faudhia alikuwa barabarani  kuelekea Dar kwa ajili ya kuzuia mpango wa Mzee Shomari. 

Mara moja simu ya Mzee Shayo ilipokelewa na maongezi kati ya  Mzee Shayo na Rais yalianza, Rais alisikika kwa kupoa sana  tofauti na mwanzo ambapo alionesha hasira sana kwa Mzee Shayo 

“Shayo!!” Aliita Rais 

“Naam Mkuu” Aliitika Mzee Shayo . ENDELEA 

SEHEMU YA NANE 

“Wewe ni Mtu pekee ambaye unaweza ukadhibiti kila kitu na  kuleta sifa kwa Taifa hili, ruhusu Vijana wako waishambulie  Benki sasa hivi” Alisema Rais kisha mwisho alisema kwa kukaza  sauti tofauti na mwanzo alivyoanza. 

“Mkuu, ndani ya Benki kuna Raia wasio na hatia, shambulio  lolote lile tutakalo lifanya litasababisha madhara makubwa  sana. Hiyo siyo suluhu ya jambo hili Mkuu, busara ni  kuhakikisha Mateka wote wanatoka salama” Alijibu Mzee Shayo 

“Mimi ndiye Rais wa Nchi hii nataka uamrishe walengaji wako  waishambulie Benki haraka iwezekanavyo” Alisema tena Rais kwa  sauti ya kufoka huku akijuwa fika kuwa Mzee Shayo hawezi  kukubaliana na wazo hilo.

  

“Hilo haliwezekani Mkuu, tuvute subra kwa masaa kadhaa  nitakuja na mpango wa nini tufanye” Alisema tena Mzee Shayo 

“Shayo! Narudia tena Mimi ndiye Rais wa hii Nchi, hakuna Rais  mwingine wala amiri jeshi Mkuu. Kama utashindwa kufanya hivyo  nitatengua uteuzi wako haraka sana” Alisema Rais kwa sauti  ile ile ya kufoka 

“Mkuu siwezi kutoa amri hiyo kwa vijana wangu, hii kazi  inahitaji…” 

“Shayo siwezi kukubembeleza” Alisema Rais kisha simu  ilikatika, Mzee Shayo alibakia akiwa njia panda, alijaribu  tena kuipiga simu ya Faudhia lakini haikuita kabisa,  alijiuliza kama Faudhia atakuwa ameshakufa basi hakutokuwa na  jambo lolote la kuzuia amri ya Rais huyo, alichoka na  kujitupa Kitini huku akitafakari afanye kitu gani. 

Mwendo wa Bakora huko Bagamoyo Road, Matilda aliendesha gari  kama dereva wa mshindano ya Formula one, ilikuwa ni safari  yenye matumaini, Bado Mzee Shayo aliendelea kumtafuta Faudhia  huku Mzee Shomari akipewa taarifa kuwa Diana alikuwa  ameshauawa na mzigo ulikuwa umechukuliwa, taarifa hiyo ilimpa  wazimu sana Mzee Shomari, alimpigia tena Chogo na kumwambia  kuwa wana chini ya masaa mawili kuhakikisha wanachomoka ndani  ya Benki hiyo haraka sana, wakati huo huo baada ya kumaliza  kuongea na Chogo alipiga simu na kuagiza Helkopta isogee  lilipo jengo la China plaza ili aweze kuondoka baada ya  kuhakikisha akina Chogo wanatoka salama. 

Akiwa ofisini Mzee Shayo, ilikuwa ni baada ya saa moja kupita  aliingia Mwanaume mmoja aliyejulikana kama Samuel Dinonga,  alikuwa ni Mkuu wa jeshi la polisi, iliwapasa kumpa salamu  aliyostahili kisha Dinonga alimueleza Mzee Shayo kuwa yeye  ndiye aliyepewa jukumu la kuongoza idara ya Usalama wa Taifa  kwa wakati huo, Mzee Shayo alipaswa kukiacha kitengo haraka  sana. Yalikuwa ndiyo maamuzi ya Rais, hakukuwa na namna, Mzee  Shayo aliacha kila kitu na kuondoka ofisini hapo. 

Lengo la Rais lilikuwa ni kuishanbulia Benki hiyo bila kujali  kuwa kulikuwa na Gavana na Mke wake pia kilikuwa na  wafanykazi wa Benki na wateja wa Benki hiyo ambao hawakuwa na  hatia yoyote ile, muda huo alilielekea gari lake ili aweze  kutimka eneo hilo la Makao makuu ya Kitengo cha Usalama wa  Taifa, alipofika ndani ya gari simu yake iliita. 

Aliitilia mashaka kidogo simu hiyo sababu ilipigwa kwa namba  ambayo hakuifahamu kabisa, alisubiria kidogo kisha aliipokea 

“Hello!” Alisema Mzee Shayo kwa umakini wa hali ya juu sana.

“Baba!!” Alisikia sauti ya Faudhia ikimuita, hakuamini  masikio yake ni kama vile alisikia kitu kisichomuingia  akilini 

“Faudhia uko wapi?” Alihoji Mzee Shayo 

“Nipo Barabarani nakuja huko Baba, naomba unisikilize kwa  makini sana” Alisema Faudhia 

“Ndio ndio” 

“Ndani ya jengo la China plaza ndimo alipo Mkuu wa kikosi  hicho, si mwingine ni Mzee Shomari! Chukua askari nenda  kamdhibiti haraka sana mimi muda siyo mrefu nitakuwa Dar”  Alisema Faudhia kwa umakini sana 

“Kwasasa mimi siyo Mkuu wa Kitengo Faudhia, sina mamlaka ya  kuamrisha askari wa kitengo tena” Alisema Mzee Shayo 

“Oooh! Shit, basi jitahidi uwende mwenyewe maana ndani ya  hicho kitengo kuna Watu wanafanya kazi ya kukwamisha juhudi”  Alisema Faudhia 

“Sawa ngoja nisogee huko” alisema Mzee Shayo kisha simu  ilikatika, aliangalia kwenye gari yake aliona silaha aina ya  Bastola, hakujuwa uzito wa ulinzi wa huko ndani ya jengo la  china plaza ila aliamini Bastola hiyo itamsaidia, aliondoa  gari kitengo na kuelekea China plaza. 

Mkuu mpya wa kitengo Bwana Dinonga alifuata maagizo ya Rais  wa Nchi, ilikuwa ni lazima aunganishe jeshi la polisi na  askari wa kitengo ambao walikuwa eneo la tukio kuifanya kazi  kwa pamoja. Aliondoa idadi kubwa ya Askari pale makao makuu  kwa ajili ya kuelekea Benki ili kuishambulia benki hiyo,  lengo likiwa kuuwa kila aliye ndani ya jengo hilo ili siri ya  pesa zile iendelee kubakia wakiamini kuwa Chemba haikuweza  kuonekana wakati chemba ya siri ilikuwa imeshafunguliwa. 

Upande wa pili, Helkopta iliyoitwa kwa ajili ya kumchukua  Mzee Shomari ilikuwa ikijongea taratibu kuelekea hapo, Mzee  Shayo naye akiwa ndani ya gari lake alikuwa akifikiria ni  jinsi gani ataweza kukabiliana na Magaidi hao ndani ya jengo  la China plaza, safari ya kutoka Kigamboni hadi Mjini ilikuwa  fupi tu ukizingatia hakukuwa na shughuli zozote zilizokuwa  zikifanyika ndani ya Jiji hili la kibiashara, muda huo  Faudhia alikuwa akiingia Dar, mwendo wao haukuwa wa kawaida,  walipofika Tegeta Matilda alimwambia Faudhia kuwa anahisi  kizunguzungu kutokana na spidi ya gari aliyokuwa nayo,  ilimlazimu Faudhia amwambia Matilda kuwa asimamishe gari 

  

haraka, Basi Matilda alifanya hivyo wakiwa maeneo ya kwa  Ndevu – Tegeta 

“Pole sana, Asante pia” Alisema Faudhia, Matilda alishindwa  hata kumjibu Faudhia alipoteza fahamu akiwa ameshikilia  usukani. Faudhia alishuka na kuielekea pikipiki iliyokuwa  imesimama kando ya Barabara, aliiwasha na kuondoka eneo hilo. 

Ukimya ulikuwa mkubwa sana alipofika maeneo ya Mnazi mmoja,  alilazimika kushuka na kutembea kwa mguu kuelekea China  plaza, japo alikuwa Mzee lakini hakusahau mbinu zake  zilizompa umaarufu miaka ya 90, Mzee Shayo alikuwa ni zaidi  ya komando wa vita, alisogea kwa kasi ya ajabu kwa kutumia  njia za ndani kama anaelekea Shimoni kariakoo, alijuwa fika  kuwa kama ni kweli magaidi hapo ndipo walipoweka kambi yao  basi ulinzi wake utakuwa mkubwa sana. Alikuwa ndani ya suti  ya kijivu iliyomkaa vizuri, alivua koti akabakiwa na shati  jeupe litakaloweza kumpa urahisi wa kuifanya kazi yake.  Alikuwa akitembea huku akiangalia saa yake aliyoweka muda  maalum wa kufika eneo husika kabla kitengo cha Usalama wa  Taifa hakijashambulia Benki na kuuwa Watu wasio na hatia,  alikuwa na nusu saa tuu iliyobakia, muda huu alikuwa  ameshazunguka hadi Msimbazi polisi, alikuwa sasa eneo la  Msikiti wa Shekh Idrisa, alikuwa makini kuliko wakati wowote  katika Maisha yake, alijuwa hiyo ndiyo nafasi pekee na  pengine ingelikuwa kazi yake ya mwisho kutokana na umri wake  na pia kuondolewa kwake kwenye kitengo na Rais. 

Kwa mbali asikia sauti ya Helkopta ambayo ilikuwa ikielekea  China plaza kwa ajili ya kumchukua Mzee Shomari, muda huo  Faudhia alikuwa ameshafika upanga kwenye msikiti wa Maamur  ili kuingia kwenye hiyo chemba itakayotumika kutorosha pesa  kutoka Benki kuu. Alipofika hapo aliona Watu watatu wenye  asili ya kiarabu wakiwa wamekaa kwa nje, aliwatazama kwa  jicho la kijasusi aligundua Watu hao ambao ni wanaume  walikuwa na silaha walizozificha kwenye viuno vyao, Faudhia  alifikiria atumie njia gani kufika pale, alifikiria kwa zaidi  ya dakika mbili huku ile presha kuwa muda unaisha ilizidi  kumjaa aliona ni bora aamuwe kufanya kitu kimoja. 

Alisogea hadi kwenye ukuta kimya kimya pasipo wale Wanaume  kushtuka huku wanaume hao wakionekana kusoma vitabu ya dini,  alijuwa ulikuwa mtego ili watu wasishtuke chochote, aliona  pia baadhi ya Watu wakitoka na kuingia Msikitini hapo,  ilikuwa ngumu kwake kujuwa kuwa Watu hao walikuwa wema au  maadui. Pembezoni aliona nguo zilizokuwa zinetundikwa na  zilikuwa ni za kiume, haraka Faudhia alizichukua na kuzivaa.

Alihakikisha anaonekana kama Mwanaume, na kweli alifanikiwa  kwenye hilo, alivuta pumzi zake ili kujiondoa wasiwasi kisha  aliitoa bastola aliyoichukua baada ya kumuuwa Diana,  aliangalia Bastola hiyo yenye risasi tatu pekee aliona  isingeliweza kumfaa ila ingelimsaidia kwa kiasi fulani,  aliiweka sawa Bastola yake kisha aliingia barabara ya lami  akawa anasogea, Wale Wanaume walipomuona Faudhia walionekana  kumkagua kwa kutumia macho yao yaliyojaa wizi huku  wakijifanya wengine kusoma na mwingine kuchezea tasbihi.  Walipeana isharaka kisha mmoja akaingia ndani wawili  wakabakia pale, Faudhia alisogea hadi lango la Msikiti.  Mwanaume mmoja aliyekaa alimsalia Faudhia kwa Salam ya  Kiislam 

“Asalaam Alaykum?” Alisalimia huku akimtazama Faudhia ambaye  alikuwa amevalia kiremba na kuificha sura yake kwa kuangalia  pembeni, yule Mwanaume alimsalimia tena Faudhia 

“Asalam Alaykum Shekh” Alisalimia bila wasiwasi, Faudhia  alihema sana akijuwa kuwa jamaa huyu alikuwa ameshamshtukia,  kisha Mwanaume huyo aliinuka na kumsogelea Faudhia ambaye  hakutaka kuonesha sura yake. 

Sura ya Mwanaume huyo ilianza kubadilika na kuwa ya hasira,  alikuwa tayari ameshamtilia Mashaka Faudhia. Alizidi kusogea  kisha alimuuliza Faudhia 

“Wewe ni nani?” Aliuliza kwa rafudhi ambayo ilionesha wazi  kuwa Mwanaume huyo alijifunza kiswahili siku si nyingi,  mapigo ya moyo ya Faudhia yalizidi kwenda mbio. Yule Mwanaume  akawa anasogea kuitazama sura ya Faudhia, endapo atagundua  kuwa Faudhia si Mwanaume itakuwa shida kwa Faudhia 

Yule Mwanaume alisogeza mkono ili amshike Faudhia amgeuze,  Faudhia alifumba macho yake kuwa asingeliweza kufurukuta  hapo, ghafla kabla hata hajamgusa Faudhia liliingia gari la  kubebea maiti lililoleta maiti kwa ajili ya kuswaliwa.  Purukushani za watu zikawa nyingi na kwakuwa walisimama  katikati ya lango iliwapasa kulipisha gari hilo, Faudhia  alibakia upande wa kulia na yule Mwanaume alirudi upande wa  kushoto kisha gari ikapita katikati yao. Fumba na kufumbua  Macho yule Mwanaume aligundua kuwa Faudhia ameshatoweka pale,  haraka alipiga simu kwa wenzake kuwa eneo hilo si salama  tena, aliwavuka Watu na kuelekea kwenye mlango wa kuzidi  kuzama ndani ya Msikiti huo. 

Naam!! Sasa, Mzee Shayo alikuwa ameshafika chini ya Jengo la  China plaza, jengo hilo lilikuwa refu lenye vioo, Mzee Shayo  alipochungulia kwa mbele aliona kuna Watu waliokuwa 

wamesimama pembezoni, alijuwa tu Watu hao siyo watu salama  kwake, muda huo Helkopta ilikuwa hewani juu ya Ghorofa hilo,  alijuwa ndiyo wakati sahihi wa kuanza kukiwasha ili kuzuia  Mzee huyo asitoweke eneo la tukio. Haraka alisogea mbele ya  jengo, alimvizia mlinzi wakwanza kisha alimnyonga kwa kutumia  kamba ya kiatu chake, alimvuta hadi mahali ambako kulikuwa na  jenereta kubwa la kuzalisha umeme, huyu wa pili alikuwa  amempa mgongo Mzee Shayo hivyo ilikuwa ni rahisi kumalizana  naye, alimpiga kiwiko eneo la shingo, alifanya kimya kimya  kisha alimvuta na kumsogeza pembeni, alihakikisha anawasachi  na kuchukua silaha zao. Alikuwa ni Mtu makini sana ambaye  aliijuwa thamani ya kazi aliyokuwa akiifanya, alisogea hadi  mlango wa kuingilia, jengo lilikuwa kimya sana na hakukuwa na  dalili kuwa Kulikuwa na mitembeo ya Mtu zaidi ya sauti ya  Helkopta iliyokuwa juu ya Jengo, humo ndani Mzee Shomari  alidhamiria kuhakikisha kuwa anachukua kila kitu kabla ya  kutimka, alichotaka ni kuhakikisha Chogo anatoroka na pesa  hizo ndani ya benki kwanza kabla yeye hajaondoka sababu  alishajuwa ni wapi watakutana kwa ajili ya kugawana kiasi  hicho 

Alimpigia Chogo na kumwambia kuwa ni muda wa kuondoka, upande  huo wa Benki tayari Chogo alikuwa na kiasi hicho cha pesa  ndani ya mabegi kilichobakia kilikuwa ni kuondoka tuu,  aliwaambia vijana wake kuwa 

“Tunaenda kuwa Mamilionea leo” Alisema Chogo kwa tabasamu,  aliamuru waifuate Chemba kwa ajili ya kuondoka, tayari  alikuwa ameshawaweka vijana huko wakawa wanachimba na  kuunganisha chemba hiyo ambayo hadi kufikia muda huo ilikuwa  tayari kilichobakia kilikuwa wao kuondoka tuu. Alipofika  kwenye Korido alikumbuka kuna kitu amesahau kisha aliwaambia  vijana wake kuwa wamsumbirie kwenye chemba, Chogo alienda  kwenye Chumba ambacho alimuacha Selina. Huwezi amini Chogo  alikuwa ameshampenda Selina, alipofika alimtazama Selina  ambaye alikuwa analia akiwa amekaa juu ya meza, chogo alijawa  na huruma huku simu yake ikiwa inazidi kuita, alikuwa ni Mzee  Shomari ndiye aliyekuwa akimpigia simu. 

Upande mwingine ndani ya Msikitini, Mtafutano ulikuwa mkubwa  mno, Faudhia aliijuwa ramani ya ilipo chemba hiyo ya  utoroshwaji wa pesa ndani ya Benki, alijificha mahali ambapo  aliamini ingelikuwa rahisi kuwaona Wanaume hao, wanaume  walipofika ndani waliufunga mlango huo ili kisisikike  chochote kutokea humo na kwenda kule Msikitini ambako  kulikuwa na harakati za kuanza ibada ya kuisalia Maiti. 

Walifunga viwanbo vya kuzuia sauti kwenye Bastola zao ili  kuhakikisha hakuna kitakachosikika ili wasije haribu mpango wao. Faudhia alikuwa kwenye moja ya vyumba ambavyo vilikuwa  ndani ya Eneo hilo, wale wanaume waligawana Majukumu ya  kumsaka Faudhia. 

Chumba alichojificha Faudhia kilikuwa kina dirisha la Kioo  hivyo ilimpa urahisi wa kuona na kuonwa pia endapo adui yake  atatazama kwenye kioo, mlango ulitekenywa huku Faudhia akiwa  amjibanza ukutani, bastola yake ilikuwa kiunoni sababu  aliamini matumizi ya Bastola yangelimfanya agundulike. Wale  magaidi waliambiana kuwa wanapaswa kuingia kwa pamoja kwenye  vyumba na kutoka pamoja hivyo endapo mmoja hatotoka basi  chumba hicho ndicho ambacho adui yao atakuwa yumo. 

Wakati kitasa kinatekenywa, Faudhia aliona Upanga kwenye kona  ya Chumba hicho, aliuchukua taratibu bila kupiga kelele ya  aina yoyote ile, alijiweka sana huku kioo kikiwa ndio msaada  pekee kwake, yule Mwanaume alivyotokeza kichwa alikutana na  upanga ambao ulizama kichwani, haraka Faudhia alimvuta  Mwanaume huyo ndani kisha alichukua Bastola ya Mwanaume huyo  alafu akasikia sauti ya kwanza ikisema 

“Safi” sauti ya pili nayo ilisema kutokea chumba kingine  ikisema 

“Safi” wakimaanisha kuwa vyumba vyao vipo salama hapo ndipo  Faudhia aliposhtuka kuwa anapaswa kuwa nje ya chumba haraka  sana ili awawahi Wanaume hao, alifanya hivyo upesi sana huku  akiwa ameelekeza Bastola yake mbele mahali ambako sauti hizo  zilitoka, wale wanaume hawakuisikia sauti ya tatu ya mwenzao  ndipo walipotoka nje haraka ila walikuwa wamechelewa,  walikutana na mishale ya risasi kutoka kwa Faudhia, Msichana  kutoka Mbeya, aliwamaliza kimya kimya bila kusikika popote  sababu bastola ilikuwa na kiwambo cha kuzuia sauti . 

Nini Kitaendelea USIKOSE SEHEMU YA TISA

JIUNGE NA KIJIWENI WHATSAPP CHANNEL Kwa Kugusa Hapa 

Soma Riwaya Nyingine Za Kijiweni Kwa KUGUSA HAPA

Wewe kama MFANYABIASHARA.. Kuna wakati unatamani kuwafikia watu wengi zaidi na hujui wapi pa kuanzia , USIJALI kwani hapa ndipo ambapo MTAA UNAONGEA na tuko tayari kukusaidia kuwafikia watu wengi kwa BEI YA OFA

Njoo Utangaze Nasi Sasa Kwa Kutuambia Una TANGAZO Gani na unataka kutangaza kwa muda gani kwa kutuma ujumbe hapa WwhatsApp Kupitia Namba +255760871896 

9 Comments

  1. Thanks alot kijiwen
    But mnafanya niunge megabyte zangu always ili tyu kupata hii zaid ya story
    Kubali Sanaa faudhia people ya green city

Leave A Reply

Exit mobile version