Ratiba ya Hatua ya 16 Bora ya michuano ya TotalEnergies CAF AFCON Morocco 2025 imekamilika baada ya hatua ya makundi iliyojaa ushindani mkali na kuonyesha ubora wa soka barani Afrika.
Hatua ya kwanza ya mtoano itachezwa kuanzia Jumamosi, tarehe 3 hadi Jumanne, tarehe 6 Januari 2026, kwa michezo miwili kila siku. Timu zitachuana kuwania tiketi ya kufuzu kwenda robo fainali.
Mabingwa wa zamani Senegal watafungua hatua hii kwa kumenyana na Sudan katika Uwanja wa Grand Stade de Tangier, huku Mali wakipimana nguvu na Tunisia jijini Casablanca.
Siku ya Jumapili, wenyeji Morocco watavaana na Tanzania katika Uwanja wa Stade Prince Moulay Abdellah, Rabat, wakisaka taji lao la kwanza la AFCON baada ya zaidi ya miaka 50. Tanzania imeingia 16 Bora kama moja ya timu bora zilizomaliza nafasi ya tatu. Baadaye siku hiyo, Afrika Kusini itakutana na Cameroon katika pambano la kuvutia.
Jumatatu, Misri itakabiliana na Benin mjini Agadir, huku Nigeria wakicheza na Msumbiji jijini Fès.
Hatua ya 16 Bora itahitimishwa Jumanne kwa mechi kati ya Algeria dhidi ya DR Congo, kabla ya mabingwa watetezi Côte d’Ivoire kumenyana na Burkina Faso mjini Marrakech.
Michuano ya robo fainali itachezwa tarehe 9–10 Januari, huku fainali ikipangwa kuchezwa tarehe 18 Januari 2026 katika Uwanja wa Stade Prince Moulay Abdellah, Rabat.
SOMA PIA : Barua Ya Wazi Kwenda Kwa Kocha Miguel Gamondi



