Ilipoishia Nzena (Kijiji Kilicholaaniwa) sehemu ya kwanza
“Baba” aliita Zahoro, Mzee Miroshi alimtazama Zahoro bila kusema chochote huku sura yake ikionesha utayari wa kumsikia.
“Naogopa Mimi” alisema Zahoro, alijisogeza mwilini mwa Baba yake na kumkumbatia, haikua hali ya kawaida kwa Mzee Miroshi. Alijua ni kitu gani alichokua akikiota Mwanaye sababu alimsikia akiweweseka.
Alimeza tena funda zito la mate huku akimpiga piga Zahoro Mgongoni katika hali ya kumfanya ajisikie kupoa.
SEHEMU YA PILI
Zahoro alilala mwilini mwa Baba yake hadi kulipopambazuka, alipoamka alikutana na sura ya Baba yake. Uso wa Zahoro bado ulikosa nuru kabisa, aliketi vizuri huku akiwa amejiinamia kimya.
Mzee Miroshi hakusema chochote alinyanyuka na kuelekea chumbani kwake, kisha baada ya dakika mbili alirejea chumbani kwa Zahoro na Kuketi kitandani.
“Zahoro” alimwita
“Baba”
“Usije ukazungumzia kuhusu ndoto yako kwa Mtu yeyote yule, jiandae tunaondoka Kijijini sasa hivi” alisema kisha alihitaji kunyanyuka lakini Zahoro alisema na kumfanya asite kunyanyuka
“Umeijuaje ndoto yangu Baba?” aliuliza huku akimtazama Baba yake, alikaza macho huku akisubiria jibu. Mzee Miroshi alinywea, akatazama chini huku akiwa amejiinamia
“Baba” baada ya kitambo Zahoro alimkumbusha Baba yake. Mzee Miroshi akainua kichwa chake akamtazama Zahoro kisha akamshika mkono na kumwambia
“Ulichokiota nakijua, hii ni siri nzito sana ambayo inakuja kuharibu Kijiji cha Nzena. Ulikua mdogo Zahoro wakati laana inatolewa na Bibi Lugumi kutokana na kifo cha Masumbuko, niliamini laana ile haiwezi kupita bure ni lazima ingerudi na kukitesa Kijiji. Miaka kumi na tatu imepita sasa, ile Laana imeanza kufanya kazi, naamini kuanzia sasa Nzena itakua sehemu mbaya zaidi Duniani” alisema kwa utulivu Mzee Miroshi, wakati huo ilikua kama hadithi ya kusadikika kwa Zahoro.
Masikio yake yalisikia, akili yake ikamuuliza, Baba yake aliwezaje kujua alichokiota. Alishusha pumzi kisha akamwuliza Baba yake
“Kwani Masumbuko aliuawa?” Kabla Mzee Miroshi hajajibu, ilisikika sauti ya kuita huko nje. Mzee Miroshi akamwambia Zahoro
“Andaa mizigo michache tunaondoka sasa hivi, ngoja niitike wito nje” alisema kisha taratibu aliondoka chumbani kwa Zahoro. Alipofika nje, alikutana na Mzee mwingine aliyeegemea ukuta mbovu, akamwambia
“Kwanini unataka kuangukia ukuta wangu Mzee Kisugu?” Mzee huyo aliyeitwa kwa jina Kisugu, alinyanyua macho yake. Alikua amevalia shati jeusi lenye makunyazi, suruali iliyopasuka kidogo. Juu alikua na baraghashia iliyopoteza rangi yake ya kahawia
Alimtazama Mzee Miroshi kwa macho yaliyobeba Ujumbe fulani mzito, walisogeleana. Tahadhari ilianza kumwingia Mzee Miroshi, aliona uso mfupi wa Mzee Kisugu ukiwa na Ujumbe wa kutatanisha, akamwuliza tena
“Kimetokea nini Kijijini?” Kisha Mzee Kisugu akashusha pumzi, akasema “Msiba Mzee Miroshi”
“Msiba?”
“Siyo mdogo, Kijiji kina Msiba mzito sana”
“Upi huo?”
“Watu watatu wamekutwa wakiwa wamejinyonga wenyewe kwenye Majumba yao, wote ni viongozi wa Kijiji akiwemo mwenyekiti, Makamu wake pamoja na Mzee Ushirika” Mwili wa Mzee Miroshi ulikua kama umemwagiwa maji, alipoa mwili na roho yake, hata mdomo wake ulikataa kutoa neno akabakia akiwa amemtazama tu.
“Jiandae uje Mzee Mwenzangu” alimaliza Mzee Kisugu kisha akageuka na kuondoka hapo kwa hatua fupi fupi huku mikono ikiwa nyuma, chozi lilianza kumbubujika Mzee Miroshi, nyuma yake alitokea Zahoro, alikua amesikia kila kitu.
Zahoro alisogea hadi mbele kwa Baba yake, akashuhudia chozi likimbubujika Baba yake. “Baba” akaita.
“Hupaswi kua hapa Zahoro, Ondoka haraka sana. Mungu akipenda tutaonana wakati mwingine” alisema Mzee Miroshi, bado masikio ya Zahoro yalikua yakipokea kauli tata ambazo hakuweza kuzichambua na kuzielewa kabisa.
“Baba”
“Nimesema ondoka Kijijini hapa, Nenda mbali, hii adhabu isikukute Zahoro.” Mzee Miroshi alipaza sauti yake, Zahoro hakuwahi kuisikia sauti ya namna hii kutoka kwa Baba yake hivyo alijua kuna jambo lisilo la kawaida limeanza kutokea Kijijini hapo, haraka akaingia ndani kisha akatoka akiwa amebeba begi dogo Jeusi
Alimtazama Baba yake.
“Usiseme chochote, nenda na Usigeuke nyuma. Nenda mbali Zahoro, hii laana isikukute popote. Kuanzia Sasa usizungumze chochote kile hadi utakapofika mbali na Kijiji hiki” alisema Mzee Miroshi huku chozi likiendelea kumbubujika.
Macho ya Zahoro yalidondosha chozi, hakutegemea kama siku moja angetengana na Baba yake. Ghafla palitokea wingu la ajabu lililoanza kukifanya kijiji kua giza, Zahoro akamwambia Baba yake
“Kama ninaikimbia laana ziwezi kukuacha hapa Baba yangu. Twende” alisema kisha alimshika mkono Baba yake, Mzee Miroshi akamwambia Zahoro.
“Nenda ndani, kwenye begi langu kuna kitabu. Niletee haraka sana” alisema, haraka Zahoro alikimbilia ndani huku giza likianza kukizingira Kijiji chote. Ilikua ni hali ya ajabu ambayo ilishtua wengi, ghafla Asubuhi iligeuka kuwa Giza tupu.
Zahoro alipotoka ndani hakumwona Baba yake, alijaribu kuizunguka nyumba kwa kuamini pengine angekua nyuma ya nyumba lakini haikuwa hivyo, hapakua na dalili ya uwepo wa Mzee Miroshi popote pale. Hali ya taharuki ilianza pale Kijijini Nzena, watu walitoka ndani ili kujionea kwa macho namna ambavyo Giza lilikua likiingia kwa kasi ya ajabu sana.
“Babaaa‼ Babaaaa‼” aliita Zahoro huku chozi likimtoka, alimjua Baba yake na misimamo yake. Hakutaka kuongozana na Zahoro, alihitaji Zahoro pekee aondoke Kijijini hapo haraka zaidi. Zahoro hakua na chaguo, alianza kukimbia kuondoka kijijini hapo.
Mzee Miroshi alikua amejificha nyuma ya Mti mkubwa akimtazama Zahoro akiwa anakimbia, akajisemea
“Nenda, hukuhusika na chochote Zahoro. Mimi nitawajibika sababu sikupinga mauwaji ya Masumbuko, hii laana itatumaliza na kulipa kisasi kwa Kifo cha yule Kijana na Bibi yake” alipomaliza kujisemea aliishika njia ya kuelekea kwenye Msiba.
Baada ya Masaa matatu, giza liliondoka ghafla sana. Anga likatawaliwa na mwanga wa jua. Simulizi za hapa na pale zilianza, kila mmoja alielezea namna ambavyo giza lile liliweza kumwogopesha.
Mkaguzi wa Kijiji aliyetumwa na Wazee wa Kijiji aliagizwa kuzunguka kila nyumba ili kubaini kama giza lile lilileta madhara, alipomaliza kuzunguka alirudisha jibu kua hali ilikua shwari kabisa Kijiji chote.
Mzee mmoja akamtazama Mzee Miroshi kisha akamwuliza
“Una hakika?” alikua amemkazia macho, kilikua ni kikao cha dharura huku taarifa ya Mzee Miroshi kua Kijiji kimepokea laana ikijadiliwa. Mzee Miroshi akatazama chini, alipoinua kichwa akapepesa kidogo kope zake huku upepo wa wastani ukiendelea kuvuma
“Ndiyo, si habari ya kusadikika bali ni habari ya kweli” alijibu kwa sauti ya utii kwa Mzee huyo wa Kijiji cha Nzena aliyekua amekunja uso wake, wengi walikua wakimwogopa kutokana na Uchawi alionao. Yeye ndiye aliyetoa amri ya Masumbuko kuuawa kwa kile alichokiita kuondoa laana.
Kisha akamsogelea Mzee Miroshi, Mzee huyu Mchawi na katili aliitwa Mzee Kova. Alikua na macho mekundu, alikua amevalia msuli na tisheti nyeusi, akamtazama sana Mzee Miroshi kisha akamwambia
“Namwona Zahoro akikimbia Kijiji, hakuna atakayeondoka hapa Nzena.” Alisema kwa kujiamini, kikao hiki kilikua kikifanyika nyumbani kwa Mzee Kova. Akaagiza Zahoro akamatwe haraka sana
Askari wa Kijiji walitawanyika kila kona kumtafuta Zahoro. Mzee Miroshi alimwomba Mzee Kova kwa kupiga magoti kua amwache Zahoro aondoke Kijijini lakini amri hiyo haikubadilika, yeye pia alikamatwa na kufungiwa kwenye moja ya chumba cha Mzee huyo hapo nyumbani kwake.
Hakuna aliyejaribu kufungua mdomo kuhoji, wala kutetea. Wote walikua kimya akiwemo Mzee Kisugu.
**
Upande wa pili, Zahoro alikua amekimbia umbali mrefu hadi alichoka. Bado alikua ndani ya Kijiji lakini angalau alikua amefika mbali. Aliamua kupumzika chini ya Mti mmoja mkubwa, akafungua begi lake dogo akatoa kopo la maji na kuanza kugida ili kuusaidia mwili kukaa vizuri.
Sauti ya Bi Lugumi ilikua ikijirudia masikioni mwake, ilikua ni sauti kali iliyokua ikimwambia kua Laana ya Kijiji ilikua imeshafika, hakuna Mtu atakayeingia wala kutoka ndani ya Kijiji hicho, Watu watakufa kwa mpigo, wataandamwa na laana ya vizazi na vizazi.
Sauti hii ilikua ikimfanya Zahoro akimbie zaidi, alinyanyuka na kuongeza mbio akiamini alikua akikaribia Kijiji jirani, alikua Msituni. Alizidi kukimbia hadi alipoanza kusikia sauti ya vilio vya Watu. Alisimama kwa mshituko na Mshangao mkubwa.
“Kwanini wanalia?” alijiuliza Zahoro, alikua akitokwa na jasho. Alimeza funda zito la mate kisha alianza kutembea huku akiishuhudia njia mbele yake kitu ambacho kilianza kumshangaza Wakati alikua kwenye Msitu mnene. Aliamua kuifuata huku sauti ya vilio ikizidi kupaa kuonesha kua alikua ameshafika eneo hilo.
Cha ajabu alianza kusikia sauti ya Baba yake Mzee Miroshi, alisimama huku akijiuliza alikua akiisikia kweli au lilikua wenge lake tu, masikio na akili yake vikamwambia alikua akiisikia kweli sauti ya Baba yake Mzee Miroshi akiwa anagugumia kwa maumivu. Hakutaka kuamini kua sauti hiyo ilikua ya Baba yake kwani alikua ameenda mbali zaidi na Kijiji
“Sasa kama ni Baba yangu, amefika saa ngapi huku?” alijiuliza, akili yake ikakumbuka kua alipotezana na Baba yake wakati giza linaingia, akajipa tumaini huwenda Baba yake alikua wa kwanza kufika.
Kadili alivyokua akipiga hatua alizidi kushangaa Zahoro, alikua akiingia Kijijini kwao, Ndiyo! Kijiji cha Nzena ambacho alikua amekikimbia kwa zaidi ya Masaa matatu, nguvu zilimwisha Zahoro. Mbele yake alikua akiitazama nyumba ya Mzee Kova, ndimo sauti ya Baba yake ilimokua ikisikika.
Nguvu zilizidi kumwisha Zahoro, chozi lilianza kumbubujika huku yale maneno ya Bibi Lugumi yakianza kutimia, akayasikia tena kua
“Laana imeshaingia Kijiji cha Nzena, Hakuna atakayeingia wala kutoka. Watu watakufa kwa Mpigo, laana itadumu vizazi kwa vizazi” sauti hii ilimfanya aamini kua ndoto yake ilikua ya ukweli ndiyo maana hata alipojaribu kukikimbia Kijiji alijikuta akirejea tena Kijijini.
**
Kijiji cha Nzena kilipotea, hakuna aliyekiona tena. Wageni waliotarajia kuingia Kijiji hicho siku hiyo walipigwa na Butwaa. Hapakua na Kijiji isipokua pori lenye nyasi fupi, ndege na Wadudu wadogo wadogo. Mwanzo ilikua kama taarifa ya kuchekesha ilipofika kwa baadhi ya Watu wakiwemo matajiri wanao miliki migodi ndani ya Kijiji hicho.
Masaa mawili baadaye taarifa ilienea Duniani, kauli ya Bibi Lugumi ilizidi kutimia. Taarifa kila ilipofika ilishangaza sana, haikua rahisi kuamini eti Kijiji kimepotea hakionekani. Wataalam wa masuala ya Uchunguzi, maafisa wa ardhi, viongozi wa Vijiji jirani wote walikubaliana kua Kijiji hicho kilikua kimetoweka na kubakia Pori dogo, eneo hilo ndilo hasa kilipokua Kijiji cha Nzena.
**
Kijijini Nzena.
Zahoro aliendelea kushangaa, Sauti ya Baba yake kuomba msaada ilizidi kumduwaza. Hakujua aamini au akatae lakini tayari alikua ameingia tena Kijiji kilicholaaniwa cha Nzena.
Alipiga magoti na kujiinamia huku chozi likimtoka Zahoro, yeye na Baba yake pekee ndiyo ambao walikua wa kwanza kutambua kua laana ya Kifo cha Masumbuko iliyotolewa na Bibi Lugumi ilikua imeanza kufanya kazi, lakini ni yeye pekee ndiye
aliyegundua kua hakuna anayeweza kuondoka hapo Kijijini kuanzia muda ambao aliiota Laana ile na kuisikia sauti ya laana ya Bibi Lugumi
Akiwa hapo anatokwa na mchozi, mara alivamiwa na walinzi wa Kijiji waliotumwa na Mzee Kova kumkamata. Dunia yake ilijaa mishangao sana, akawauliza kwa sauti ya upole huku chozi likimtoka.
Nini Kitaendelea? Usikose SEHEMU YA TATU Hapa Hapa Kijiweni
JIUNGE NA KIJIWENI WHATSAPP CHANNEL Kwa Kugusa Hapa
Soma Riwaya Nyingine Za Kijiweni Kwa KUGUSA HAPA
Wewe kama MFANYABIASHARA.. Kuna wakati unatamani kuwafikia watu wengi zaidi na hujui wapi pa kuanzia , USIJALI kwani hapa ndipo ambapo MTAA UNAONGEA na tuko tayari kukusaidia kuwafikia watu wengi kwa BEI YA OFA
Njoo Utangaze Nasi Sasa Kwa Kutuambia Una TANGAZO Gani na unataka kutangaza kwa muda gani kwa kutuma ujumbe hapa WwhatsApp Kupitia Namba +255760871896
2 Comments
Duh angetoka hata zahoro tu sio mbaya asa mbona balaa hili
Fantastic story 👏