Ilipoishia Nyumba Juu Ya Kaburi 06

Nilikua nikihema, Wazazi wangu walikua wamesimama vile vile kama Watu wasiojitambua.  Yule Bibi aliendelea kunisogelea huku mguu wake mmoja akiwa anauburuza. Ulikua kama una  dosari ya ukilema hivi, nilikua kwenye butwaa ambayo ilihitaji Mtu anitingishe ndiyo nitoke  katika ile hali tata. 

Fumba na kufumbua Macho yule Bibi Kizee alikua amejaa machoni pangu akinimulika na  macho yake makali, nilishtuka na kutoka katika ile hali ya Butwaa. Nilipohitaji kukimbia  alinishika mkono na kunivuta kwake lakini alipigwa na shoti kali, niliona moto mkali  uliomsukuma na kumtupa chini.  Endelea

SEHEMU YA SABA

Alinitazama kwa Mshangao kisha aliniuliza kwa sauti yake kali. 

“Wewe ni Nani?” aliongea huku akitokwa na moshi mdomoni, bado mvua ilikua ikichapa.  Niliuangalia mkono wangu, niliiuona ule ushanga, ndio ulionisaidia. Sasa kilichobakia kwangu  kilikua ni kuokoa Uhai wangu, nilirudi nyuma nyuma tayari kukimbia, yule Jini aliwaamrisha  Wazazi wangu wanifukuze. 

Niliipa miguu yangu mamlaka ya kukimbia, lakini sikufikiria kwenda mbali isipokua kurudi  nyumbani mara moja, nilijigonga getini eneo la mguu lakini halikuninyima mwendo, nilijivuta  haraka na kukimbilia ndani kisha nilifunga mlango.  

Nilifika ndani nikiwa nimechoka, nimelowa na pia nimetawaliwa na hofu. Haikua hali ya  kawaida niwakimbie Wazazi wangu niliowapenda, radi zilikua zikipasua anga halafu sauti ya  kucheka ya yule jini ilikua ikisambaa kila kona. 

Nilisimama nikiwa nina bubujikwa na machozi, Wazazi wangu walikua kama mazombi  yasiyoelewa Mimi ni Nani kwao, sijui aliwafanyia nini hadi wakaanza kuniwinda kiasi hiki. Basi  nilikua nikiwaona Wazazi wangu kupitia kioo cha mlangoni jinsi walivyokua wamebadilika.

Macho yao yalikuwa hayana kiini cheusi, meupe kama karatasi, walikua wakitokwa na udenda. Niliumia ndani ya moyo wangu kuwaona Wazazi wangu katika hali ile ya ajabu, walikua na  nguvu za ajabu kiasi kwamba walikua wakivunja kioo waingie ndani. 

Nilitamani sana kuwasihi Wazazi wangu wanitambue lakini niliona isingelikua rahisi,  nikapandisha ngazi huku nikisikia namna walivyokua wakivunja kioo, nilikimbia kwa spidi sana  hadi chumbani kwangu, nikawa naitafuta simu yangu ili niombe Msaada nje. 

Sijui simu nilikua nimeiweka wapi, niliitafuta kila kona. Nilianza kusikia sauti ya kusukumwa  kwa mlango wangu kwa nguvu, walikua wameshafika mlangoni kwangu. 

Nilikua natetemeka sana maana nafsi yangu ilikosa utetezi tena. Kwa bahati nzuri niliisikia simu  yangu ikiita. Sijui ni saa ngapi iliingia uvunguni mwa kitanda, niliinama, ilikua mbali kidogo  hivyo ni lazima nikivute kitanda kwanza, nilijivuta nikakisukuma kitanda nikaipata simu yangu.  

Nilikua natetemeka sana, mwili ulikua ukichuruzika maji. Mapigo yangu ya moyo yalikua  yakienda sambamba na pumzi zangu. Mate yalinikauka, kutoa nywira ya simu yangu ilinichukua  dakika nyingi kutokana na wasiwasi uliokua umenivaa. Nilishindwa hata kuifungua simu yangu,  mlango ulikua katika nyakati za mwisho kufunguka. 

Nilidondosha simu yangu huku nikiwa nimeutolea macho mlango ukiwa unatikiswa haswa,  nilihisi harufu ya kifo. Taratibu nilianza kurudi nyuma nikitamani nipate msaada usiotarajiwa.  Hamad‼! Mlango ulifunguka, Baba na Mama yangu walikua mbele yangu  

Walikua katika fahamu zisizo zao, walisimama wakinitazama. Niliona huo ni muda wa  kuzungumza nao pengine ningeweza kuwashawishi wakarudi katika hali zao, chozi lilinitoka.  Sikuwahi kuwaza wala kuota kua siku moja Baba na Mama yangu wangekuwa katika hali kama  hiyo, hali ambayo wasingeliweza kunitambua Mimi binti yao wa pekee Celin. 

“Mama‼ Babaa‼” nilianza kwa sauti ya kilio cha maumivu sana, niliishiwa nguvu hata maneno  niliyohitaji kuyatoa yalikua mazito kutoka mdomoni mwangu. Nilikua na maumivu makali sana  ndani yangu, udenda ulikua ukiwatoka Wazazi wangu. 

“Ni Mimi Celin, najua hamnitambui kama ambavyo ninyi hamjitambui Wazazi wangu. Mimi ni  Binti yenu, hampaswi kunidhuru” walikua wametulia kimya wakati naongea, nilihisi walikua  wanaanza kunisikiliza. 

“Ona, furaha yenu ni Mimi hapa, furaha yangu ni ninyi hapo. Hayo siyo Maisha yenu, sijawahi  kuwaona mkiwa hivyo naomba wazazi wangu rudini katika halo zenu. Mna mengi ya kuyajuwa  kuhusu hii nyumba” Nilisema, hapa sasa ndipo nilipoiona dhamira ya yule jini kwangu,  alichotaka ni kuhakikisha Wazazi wangu wananimaliza. 

Walinifuata kwa spidi ya ajabu ili wanishambulie lakini kwa bahati nzuri niliweza kuwakwepa  nikajigonga ukutani, Mama alikua kama Mbogo kwa jinsi alivyokua akitoa sauti ya hasira kama  Mnyama vile.

“Mama ni Mimi Celin” nilisema, angalau Baba yangu alikua hana hasira kama ambayo Mama  yangu alikua nayo, alinivamia tena kunishambulia. Alinijeruhi kwa kucha ndefu, kisha  nilimsukuma nikapata nafasi ya kuondoka pale chumbani, nikashusha ngazi haraka huku Mama  akiendelea kunikimbiza. 

Nilifika hadi chini, nilipogeuka Mama yangu alinirukia mithiri ya Ndege tai, alinidondosha chini  kama mzigo halafu akawa ananishambulia vibaya sana usoni kwa kucha, nilijitahidi sana  kupambana naye ili niinuke, nilifanikiwa kumsukuma lakini alikua amenikwaruza usoni vya  kutosha.  

Nilisimama huku Mama akijiandaa tena kunishambulia, nilishaona kua kama sitakua ngangali  basi Mama angeweza kunimaliza, maana alinishambulia usoni bila huruma halafu alinikwangua  shingoni na kuniacha na maumivu makali sana. Nilipaswa kupambana naye bila kujali kua  hayupo katika fahamu zake. 

Alikua akiunguruma kama Simba mwenye njaa, nilikimbilia jikoni lakini kabla hata sijafunga  mlango aliusukuma kwa nguvu, alikua akinifuata taratibu baada ya kuingia jikoni, nilirudi  nyuma nyuma nikifikiria nifanye jambo gani. Mama alinisogelea bila haraka, alijua  nisingeliweza kukimbilia popote tena. Nilifika mwisho wa jiko, nikakutakana na meza na ukuta  nyuma yangu. 

Upande wa kushoto palikua na kisu, nilisogea taratibu huku nikiiambia nafsi yangu kuwa  nisipojiokoa sitaweza kupona, nilimpenda Mama yangu lakini aligeuka kua adui yangu. Nilipaswa kumshambulia kama alivyokua akinishambulia 

Nilipapasa na kukishika kisu. 

“Mama, ni Mimi Celin, Mwanao hupaswi kunitendea hivi” nilisema kwa mara ya mwisho, kama  atanisikia na kuacha kunishambulia kwa maelekezo ya yule jini mbaya. Haikusaidia, Mama  alikuja tena mithiri ya ndege tai ili anishambulie 

Sikujiuliza mara mbili nilipaswa kufanya nini, nilimkita kisu Cha shingo Mama yangu. Kilizama  upande mmoja na kutokea upande mwingine. Mama aligugumia kwa mumivu mkali, ile hali ya  ushetani ilimtoka ghafla tu akawa Yule Mama niliyempenda kisha alidondoka chini akihema kwa  shida. 

“Mamaa‼” nilimwita kwa sauti iliyojaa mashaka, kisha nilikaa chini na kukipakata kichwa  chake. Mama alikua akitapatapa kwa maumivu, alikua hawezi kusema chochote kutokana na kile  kisu nilicho mchoma nacho. 

Alianza kukosa hewa, nilikua ninalia na kumwomba msamaha Mama yangu. Baba alikuja jikoni  akiwa katika hali ya kujitambua kabisa, alikua ameloa nguo zake. Alipotuona alishangaa sana  kisha alikuja haraka pale chini na kuniuliza kilichompata Mama.

Niliishia kulia nikimtazama Mama, Baba akaniambia tumpeleke Hospitali Mama akapate  huduma ya kwanza, sikuwa na chaguo isipokua kumsikiliza, sote tulikua tumechanganikiwa ila  Baba alichanganikiwa zaidi maana alionekana kutojua chochote kilichotokea. Muda huo mvua  ilikua imeacha kunyesha, palikua tulivu na wala hapakua na hali yoyote yenye kutia wasiwasi. 

Baba alimbeba Mama hadi nje, bahati nzuri palikua na Taxi moja iliyokua ikipita.  Tuliisimamisha kisha tulimpakiza Mama, tulianza safari ya kuelekea Hospitali. Tulipofika,  Mama alipokelewa kama mgonjwa mahututi anayehitaji huduma haraka sana bila maelezo  yoyote yale, aliingizwa chumba cha Upasuaji mara moja. 

Mimi na Baba tulikaa kwenye Benchi, uso wa Baba yangu uliniambia vingi, kimoja  kilichotawala zaidi ni swali la nini kilichotokea hadi Mama akawa katika hali ile, Mimi ndiye  niliyepaswa kumpa majibu Baba lakini atanielewa?  

“Celin” Baba aliniita, alikua amevalia shati la Mistari myeupe na suruali nyeusi na kiatu cheusi  chini. Niligeuka kumtazama maana nilikua nimejiinamia nikilia, chochote kitakachotokea basi  Mimi ndiye niliyesababisha. Chozi lilikua linanivuja 

Baba alipepesa macho yake akanitazama mara moja kisha akaangalia chini na kuniuliza kwa  sauti ya taratibu sana. 

“Mama yako amefikwa na nini, kile kisu Nani amemchoma?” aliuliza Baba, nilibana midomo  yangu. Kila jibu nililo lifikiria kua lingekua jibu kwa Baba lingezua maswali zaidi, nilimtazama  Baba ili kusoma sura yake alikua akifikiria nini. 

Kisha nilimwambia Baba “Sijui Baba, sijui nini kimetokea. Nimemkuta Mama katika hali ile”  Nililazimika kusema uwongo, Baba alishusha pumzi ndefu. Mtu mzima yeye, alihitaji ushawishi  zaidi kuamini nilikua sijui chochote kuhusu Mama. 

“Polisi watakuja, tutawajibu hatujui?” aliniuliza. Nilizidi kudondosha chozi. 

“Baba, niamini sijui chochote. Nilimkuta akiwa katika hali ile Mimi” nikizidi kujitetea mbele ya  Baba. Chozi lilikua likinibubujika huku nafsi yangu ikinisuta. Chochote kitakachomkuta Mama,  wa kulaumiwa ni Mimi hapa Celin. 

Basi Baba aliniegemeza kwenye bega lake ili kunipa faraja, niliendelea kulia huku tukisubiria  taarifa kutoka chumba cha Upasuaji. Tulikaa kwa zaidi ya masaa mawili, jua lilikua likikimbia  kwa kasi kuelekea kuzama, jioni ilikua imeshaingia, taa ziliwashwa kuonesha kua giza lilikua  linajiandaa kuingia. 

Nilikua na uchovu wa kukimbizana huku na kule, mwili ulikua na maumivu pia nilikua na  majeraha kadhaa ya kucha za Mama. Baada ya dakika kumi kupita, Daktari mmoja alitoka  chumba cha Upasuaji, tulikua tunasubiria kwa muda mrefu, tuliposikia mlango ukifunguliwa  tulisimama mara moja na kutazama.

Tulipomwona Daktari tulisogea aliposimama akituangalia, alikua akitokwa na jasho, alivua  Barakoa kisha akajishika kiuno. Sura yake ilikosa tumaini, nilijikuta nikilegea mwili mzima.  Baba akamuuliza 

“Hali ya mgonjwa inaendeleaje?” aliulza Baba kwa shahuku sana, yule Daktari akamtazama  Baba, akashusha pumzi kidogo akasema 

“Tumejitahidi sana” kisha akatikisa kichwa halafu akaendelea 

“Jitihada zimezidi kudra, amefariki” sauti ya yule Dakati siwezi kuisahau, yaani ndani ya wiki  moja nilipoteza Watu watatu muhimu sana Maishani mwangu. Nilianza kumpoteza Zena, kisha  Caren, leo nampoteza Mama yangu Mzazi tena kwa mikono yangu Mimi mwenyewe, niliangua  kilio cha Mtu mzima, nilihitaji nilie kwa uchungu tena kwa sauti kubwa kabisa. 

Baba alinishikilia maana nilikua ninalia kwa kusaga meno, kilichoniliza zaidi ni kwamba  Mikono yangu ndiyo iliyoondoa Uhai wa Mama yangu, nilimuuwa mwenyewe katika hali ya  kujiokoa. Baba alitokwa na machozi huku akiwa ameufunga mdomo wake, aliitumia mikono yake kunibembeleza lakini haikusaidia. 

Daktari akamwomesha Baba chumba kitupu ili tukakae huko kwa muda, Baba alinipeleka huko  na kufunga mlango ili nilie hadi maumivu yaishe, palikua na viti viwili. Baba aliketi na kuniacha  sakafuni nilie hadi nimalize, nililia sana Mimi. Hakuna siku nililia sana kwenye Maisha yangu  kama siku hii, maneno ya yule Jini Bibi kizee yalitimia, nilitambaa hadi miguuni kwa Baba  nikamwambia 

“Nisamehe Baba” nilisema nikiwa ninalia, japo nilikua ninalia lakini niliona maumivu hayawezi  kwisha kama sitasema ukweli mbele ya Baba yangu aliyekua hajui nini kilitokea, alikua  akinitazama tu.  

“Nisamehe Mimi Baba , ni makosa yangu” niliendelea kusema, Baba alishangaa inawezekanaje  yakawa ni makosa yangu. Aliniyanyua na kuniuliza 

“Inawezekanaje ukasema ni makosa yako Celin?” nilifuta chozi, nilihitaji ujasiri sasa kumweleza  ukweli Baba. Nilianza kusema “Kifo cha Mama ni Makosa yangu, mikono yangu niliyoipenda  imeondoa uhai wa Mtu ninayempenda” Baba alihamaki akaniuliza kwa sauti kavu 

“Unasemaje?” 

“Baba, sikukusudia. Nimemuuwa Mama kwa bahati mbaya Mimi, nisamehe Baba Aaaah‼”  niliendelea kulia, nilimweleza Baba ukweli lakini hakuonekana kuukubali kabisa. Alinilea na  kunifundisha tabia njema, akasema 

“Sikukuzaa Muuwaji Celin, sitaki kuyaamini maneno yako” alisema Baba kwa uchungu sana  kisha alipiga hatua za haraka na kwenda kujiinamia ukutani. Nilisikia kilio cha chinichini cha  Baba na manung’uniko, nilielewa ni vita ya ndani kwa ndani ndiyo iliyokua ikiendelea kwake.

Nilijiuliza nimwambie nini Baba yangu aniamini, nilimfuata alipo, hali ilibadilika na mimi ndiye  niliyekua namtuliza Baba baada ya Baba kunituliza Mimi 

“Baba‼” nilimwita, alikua amejiinamia. Hakutaka nilione chozi lake kabisa. Nilimwita tena  akaniambia 

“Celin, wewe siyo Muuwaji Mwanangu tena huwezi kumuuwa Mama yako Mzazi. Sitaki kusikia  hizo hadithi, niambie nini kimemkuta Mama yako?” alisema Baba akiwa ameuficha uso wake  ukutani, macho yangu yalikua hayakauki chozi hata kidogo, niliendelea kububujisha chozi  

“Baba, Mwanao nimepitia Mazingira magumu sana tena kwa siri msijue nyinyi” nilisema, kilio  kilianza upya. Baba aligeuka kunitazama. Macho yake yalikua yamejawa na chozi, alihitaji  kusikia nilichotaka kukisema. Nilimtazama. 

“Chanzo cha yote ni ile nyumba Baba, ina majini na kaburi ambalo ndugu wawili wamezikwa  mle. Hakuna aliyeweza kuishi ndani ya ile nyumba salama, hata kifo cha Mama ni matokeo ya  usiri wangu” Nilisema jambo ambalo lilimfanya Baba ashangae sana 

“Umetoa wapi hayo unayoyasema Celin?” aliniuliza Baba kwa Mshangao mkubwa sana, nilifuta  chozi langu nikaivaa roho ya Ujasiri ili nimsimulie Baba kila kitu. Nilimsimulia kila hatua, kila  jambo. Hadi namaliza kumweleza Baba alikua ameketi kitini akinitazama kwa uzito sana. Sura  ya majonzi ilimtawala Baba yangu 

“Kwanini ulificha jambo kubwa namna hiyo Celin, siri yako imeharibu Maisha yetu, siri yako  imeondoa uhai wa Mama yako Celin” alinilaumu Baba, nilikua tayari kupokea lawama zote  maana tayari maji yalinifika shingoni, nilikua naangamia. 

“Unafikiria Polisi wataelewa haya?” aliniuliza Baba, tayari kitengo cha Polisi kilipokea taarifa  ya shambulio la Mama yangu. Walikua wameshafika, mlango ulikua ukigongwa 

Baba alinisogelea akaniambia 

“Kama unaweza kumaliza kila kitu basi maliza Celin” alisema, kabla hata sijamjibu chochote Baba alielekea mlangoni na kufungua mlango, polisi walikua wamesimama mlangoni. 

Baba aligeuka na kunitazama kisha alinipa ishara ya tumaini kwa kuniachia tabasamu. 

“Sisi ni maafisa wa Polisi, tunahitaji kuondoka na ninyi kwa ajili ya mahojiano” alisema Polisi  mmoja, Baba akasema 

“Haina haja ya kuondoka na sisi, peke yangu nitathibitisha kila kitu. Binti yangu hakuwepo eneo  la tukio” alisema Baba, kauli yake ya ghafla ilionesha kua alikua ameubeba msalaba wangu.  Polisi walinitazama kwa sekunde kadhaa huku nikiwa mwoga maana Mimi ndiye Muuwaji,  kisha waliondoka na Baba yangu. Nililia sana, sikuwa na Mtu karibu yangu wa kuniambia  maneno ya faraja.

Mama yangu alikua amefariki, Baba alikua mikononi mwa Polisi kwa makosa yangu Mimi. Nilijiinamia baada ya kulia kwa muda mrefu, baadaye nilitoka kwenye kile chumba. Nilipata  Ujasiri wa kuuliza namna ya kuipata Maiti ya Mama kwa ajili ya Maziko. Utaratibu ulikua ni  lazima tulipie pesa kidogo ndipo watupatie maiti, sikua na pesa nilimwambia Daktari natakiwa  kurudi nyumbani kuchukua pesa. Akaniangalia kisha akaniambia 

“Usijali Msichana, tayari maiti imelipiwa” nilishangaa sana, ni Nani anayeweza kuilipia maiti ya  Mama yangu ili itoke Hospitalini. Nilimtazama kwa Mshangao halafu nikamuuliza 

“Hivi nimekusikia ipasavyo?”  

“Ndiyo, Mjomba wako amelipia” alipomaliza kusema nikamwona Mjomba Mgina akiwa  anakuja tulipokua tumesimama na Daktari. Huzuni iliniingia Upya kabisa, nilimkimbilia  Mjomba na Kumkumbatia kwa Uchungu sana. 

“Pole Celin, pole sana Mjomba” alisema huku akinipiga piga taratibu mgongoni katika hali ya  kunipoza machungu. Chozi lilinibubujika tena, kwakua tayari nilikua nimemueleza kila kitu  Baba yangu sikutaka kuleta tena Mkanganyiko. 

“Inaniuma Mjomba, Mama amekufa kikatili sana” nilisema, maumivu yaliyokua yamejaa  moyoni mwangu yalikua yakinichoma mithiri ya sidano. 

Basi, tuliitoa Maiti Hospitalini na kuipeleka nyumbani kwa Mjomba Mgina. Palitawala Majonzi  na vilio, maswali yasiyo na Majibu. Uvumi kua Baba yangu alikua amemuuwa Mama yangu  ulianza kusambaa miongoni mwa waombolezaji, kila Mtu alimwita jina baya Baba yangu. 

Nilizidi kuumia ndani ya Nafsi yangu, Baba yangu aliitwa Muuwaji kwa sababu ya kunisaidia  Mimi. Alijivesha ngozi yangu kunificha Muuwaji halisi, nililia kwa mambo mengi yasiyo na  Majibu. Macho yalinivimba, kesho yake tulimzika Mama kwenye Makaburi ya Jiji. 

Hatimaye Mama yangu aliungana na Zena na Caren kwenye makazi ya milele. Kilichokua  kimebakia kwangu kilikua fumbo kubwa, hakuna aliyejua kuhusu ile nyumba yenye kaburi na  jini anayeuwa. 

Sikutaka kumwambia yeyote, moyo wangu ulijawa na kisasi. Sikuuona umuhimu wa kuendelea  kuishi ikiwa nimepoteza Wapendwa wangu kwa usiri wangu. Baba alifikishwa Mahakamani siku  Nne baada ya kumzika Mama, alikiri mbele ya Mahakama kua alitenda Mauwaji hayo kwa  mikono yake kwa kile alichokiita wivu wa Mapenzi. 

Nini Kitaendelea? Usikose Sehemu Ya NANE

COMMENTS ZIWE NYINGI SASA 

JIUNGE NA KIJIWENI WHATSAPP CHANNEL Kwa Kugusa Hapa 

Soma Riwaya Nyingine Za Kijiweni Kwa KUGUSA HAPA

Wewe kama MFANYABIASHARA.. Kuna wakati unatamani kuwafikia watu wengi zaidi na hujui wapi pa kuanzia , USIJALI kwani hapa ndipo ambapo MTAA UNAONGEA na tuko tayari kukusaidia kuwafikia watu wengi kwa BEI YA OFA

Njoo Utangaze Nasi Sasa Kwa Kutuambia Una TANGAZO Gani na unataka kutangaza kwa muda gani kwa kutuma ujumbe hapa WwhatsApp Kupitia Namba +255760871896 

Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx

3 Comments

Leave A Reply

Exit mobile version