Ilipoishia Nyumba Juu Ya Kaburi 06
Nilikua nikihema, Wazazi wangu walikua wamesimama vile vile kama Watu wasiojitambua. Yule Bibi aliendelea kunisogelea huku mguu wake mmoja akiwa anauburuza. Ulikua kama una dosari ya ukilema hivi, nilikua kwenye butwaa ambayo ilihitaji Mtu anitingishe ndiyo nitoke katika ile hali tata.
Fumba na kufumbua Macho yule Bibi Kizee alikua amejaa machoni pangu akinimulika na macho yake makali, nilishtuka na kutoka katika ile hali ya Butwaa. Nilipohitaji kukimbia alinishika mkono na kunivuta kwake lakini alipigwa na shoti kali, niliona moto mkali uliomsukuma na kumtupa chini. Endelea
SEHEMU YA SABA
Alinitazama kwa Mshangao kisha aliniuliza kwa sauti yake kali.
“Wewe ni Nani?” aliongea huku akitokwa na moshi mdomoni, bado mvua ilikua ikichapa. Niliuangalia mkono wangu, niliiuona ule ushanga, ndio ulionisaidia. Sasa kilichobakia kwangu kilikua ni kuokoa Uhai wangu, nilirudi nyuma nyuma tayari kukimbia, yule Jini aliwaamrisha Wazazi wangu wanifukuze.
Niliipa miguu yangu mamlaka ya kukimbia, lakini sikufikiria kwenda mbali isipokua kurudi nyumbani mara moja, nilijigonga getini eneo la mguu lakini halikuninyima mwendo, nilijivuta haraka na kukimbilia ndani kisha nilifunga mlango.
Nilifika ndani nikiwa nimechoka, nimelowa na pia nimetawaliwa na hofu. Haikua hali ya kawaida niwakimbie Wazazi wangu niliowapenda, radi zilikua zikipasua anga halafu sauti ya kucheka ya yule jini ilikua ikisambaa kila kona.
Nilisimama nikiwa nina bubujikwa na machozi, Wazazi wangu walikua kama mazombi yasiyoelewa Mimi ni Nani kwao, sijui aliwafanyia nini hadi wakaanza kuniwinda kiasi hiki. Basi nilikua nikiwaona Wazazi wangu kupitia kioo cha mlangoni jinsi walivyokua wamebadilika.
Macho yao yalikuwa hayana kiini cheusi, meupe kama karatasi, walikua wakitokwa na udenda. Niliumia ndani ya moyo wangu kuwaona Wazazi wangu katika hali ile ya ajabu, walikua na nguvu za ajabu kiasi kwamba walikua wakivunja kioo waingie ndani.
Nilitamani sana kuwasihi Wazazi wangu wanitambue lakini niliona isingelikua rahisi, nikapandisha ngazi huku nikisikia namna walivyokua wakivunja kioo, nilikimbia kwa spidi sana hadi chumbani kwangu, nikawa naitafuta simu yangu ili niombe Msaada nje.
Sijui simu nilikua nimeiweka wapi, niliitafuta kila kona. Nilianza kusikia sauti ya kusukumwa kwa mlango wangu kwa nguvu, walikua wameshafika mlangoni kwangu.
Nilikua natetemeka sana maana nafsi yangu ilikosa utetezi tena. Kwa bahati nzuri niliisikia simu yangu ikiita. Sijui ni saa ngapi iliingia uvunguni mwa kitanda, niliinama, ilikua mbali kidogo hivyo ni lazima nikivute kitanda kwanza, nilijivuta nikakisukuma kitanda nikaipata simu yangu.
Nilikua natetemeka sana, mwili ulikua ukichuruzika maji. Mapigo yangu ya moyo yalikua yakienda sambamba na pumzi zangu. Mate yalinikauka, kutoa nywira ya simu yangu ilinichukua dakika nyingi kutokana na wasiwasi uliokua umenivaa. Nilishindwa hata kuifungua simu yangu, mlango ulikua katika nyakati za mwisho kufunguka.
Nilidondosha simu yangu huku nikiwa nimeutolea macho mlango ukiwa unatikiswa haswa, nilihisi harufu ya kifo. Taratibu nilianza kurudi nyuma nikitamani nipate msaada usiotarajiwa. Hamad‼! Mlango ulifunguka, Baba na Mama yangu walikua mbele yangu
Walikua katika fahamu zisizo zao, walisimama wakinitazama. Niliona huo ni muda wa kuzungumza nao pengine ningeweza kuwashawishi wakarudi katika hali zao, chozi lilinitoka. Sikuwahi kuwaza wala kuota kua siku moja Baba na Mama yangu wangekuwa katika hali kama hiyo, hali ambayo wasingeliweza kunitambua Mimi binti yao wa pekee Celin.
“Mama‼ Babaa‼” nilianza kwa sauti ya kilio cha maumivu sana, niliishiwa nguvu hata maneno niliyohitaji kuyatoa yalikua mazito kutoka mdomoni mwangu. Nilikua na maumivu makali sana ndani yangu, udenda ulikua ukiwatoka Wazazi wangu.
“Ni Mimi Celin, najua hamnitambui kama ambavyo ninyi hamjitambui Wazazi wangu. Mimi ni Binti yenu, hampaswi kunidhuru” walikua wametulia kimya wakati naongea, nilihisi walikua wanaanza kunisikiliza.
“Ona, furaha yenu ni Mimi hapa, furaha yangu ni ninyi hapo. Hayo siyo Maisha yenu, sijawahi kuwaona mkiwa hivyo naomba wazazi wangu rudini katika halo zenu. Mna mengi ya kuyajuwa kuhusu hii nyumba” Nilisema, hapa sasa ndipo nilipoiona dhamira ya yule jini kwangu, alichotaka ni kuhakikisha Wazazi wangu wananimaliza.
Walinifuata kwa spidi ya ajabu ili wanishambulie lakini kwa bahati nzuri niliweza kuwakwepa nikajigonga ukutani, Mama alikua kama Mbogo kwa jinsi alivyokua akitoa sauti ya hasira kama Mnyama vile.
“Mama ni Mimi Celin” nilisema, angalau Baba yangu alikua hana hasira kama ambayo Mama yangu alikua nayo, alinivamia tena kunishambulia. Alinijeruhi kwa kucha ndefu, kisha nilimsukuma nikapata nafasi ya kuondoka pale chumbani, nikashusha ngazi haraka huku Mama akiendelea kunikimbiza.
Nilifika hadi chini, nilipogeuka Mama yangu alinirukia mithiri ya Ndege tai, alinidondosha chini kama mzigo halafu akawa ananishambulia vibaya sana usoni kwa kucha, nilijitahidi sana kupambana naye ili niinuke, nilifanikiwa kumsukuma lakini alikua amenikwaruza usoni vya kutosha.
Nilisimama huku Mama akijiandaa tena kunishambulia, nilishaona kua kama sitakua ngangali basi Mama angeweza kunimaliza, maana alinishambulia usoni bila huruma halafu alinikwangua shingoni na kuniacha na maumivu makali sana. Nilipaswa kupambana naye bila kujali kua hayupo katika fahamu zake.
Alikua akiunguruma kama Simba mwenye njaa, nilikimbilia jikoni lakini kabla hata sijafunga mlango aliusukuma kwa nguvu, alikua akinifuata taratibu baada ya kuingia jikoni, nilirudi nyuma nyuma nikifikiria nifanye jambo gani. Mama alinisogelea bila haraka, alijua nisingeliweza kukimbilia popote tena. Nilifika mwisho wa jiko, nikakutakana na meza na ukuta nyuma yangu.
Upande wa kushoto palikua na kisu, nilisogea taratibu huku nikiiambia nafsi yangu kuwa nisipojiokoa sitaweza kupona, nilimpenda Mama yangu lakini aligeuka kua adui yangu. Nilipaswa kumshambulia kama alivyokua akinishambulia
Nilipapasa na kukishika kisu.
“Mama, ni Mimi Celin, Mwanao hupaswi kunitendea hivi” nilisema kwa mara ya mwisho, kama atanisikia na kuacha kunishambulia kwa maelekezo ya yule jini mbaya. Haikusaidia, Mama alikuja tena mithiri ya ndege tai ili anishambulie
Sikujiuliza mara mbili nilipaswa kufanya nini, nilimkita kisu Cha shingo Mama yangu. Kilizama upande mmoja na kutokea upande mwingine. Mama aligugumia kwa mumivu mkali, ile hali ya ushetani ilimtoka ghafla tu akawa Yule Mama niliyempenda kisha alidondoka chini akihema kwa shida.
“Mamaa‼” nilimwita kwa sauti iliyojaa mashaka, kisha nilikaa chini na kukipakata kichwa chake. Mama alikua akitapatapa kwa maumivu, alikua hawezi kusema chochote kutokana na kile kisu nilicho mchoma nacho.
Alianza kukosa hewa, nilikua ninalia na kumwomba msamaha Mama yangu. Baba alikuja jikoni akiwa katika hali ya kujitambua kabisa, alikua ameloa nguo zake. Alipotuona alishangaa sana kisha alikuja haraka pale chini na kuniuliza kilichompata Mama.
Niliishia kulia nikimtazama Mama, Baba akaniambia tumpeleke Hospitali Mama akapate huduma ya kwanza, sikuwa na chaguo isipokua kumsikiliza, sote tulikua tumechanganikiwa ila Baba alichanganikiwa zaidi maana alionekana kutojua chochote kilichotokea. Muda huo mvua ilikua imeacha kunyesha, palikua tulivu na wala hapakua na hali yoyote yenye kutia wasiwasi.
Baba alimbeba Mama hadi nje, bahati nzuri palikua na Taxi moja iliyokua ikipita. Tuliisimamisha kisha tulimpakiza Mama, tulianza safari ya kuelekea Hospitali. Tulipofika, Mama alipokelewa kama mgonjwa mahututi anayehitaji huduma haraka sana bila maelezo yoyote yale, aliingizwa chumba cha Upasuaji mara moja.
Mimi na Baba tulikaa kwenye Benchi, uso wa Baba yangu uliniambia vingi, kimoja kilichotawala zaidi ni swali la nini kilichotokea hadi Mama akawa katika hali ile, Mimi ndiye niliyepaswa kumpa majibu Baba lakini atanielewa?
“Celin” Baba aliniita, alikua amevalia shati la Mistari myeupe na suruali nyeusi na kiatu cheusi chini. Niligeuka kumtazama maana nilikua nimejiinamia nikilia, chochote kitakachotokea basi Mimi ndiye niliyesababisha. Chozi lilikua linanivuja
Baba alipepesa macho yake akanitazama mara moja kisha akaangalia chini na kuniuliza kwa sauti ya taratibu sana.
“Mama yako amefikwa na nini, kile kisu Nani amemchoma?” aliuliza Baba, nilibana midomo yangu. Kila jibu nililo lifikiria kua lingekua jibu kwa Baba lingezua maswali zaidi, nilimtazama Baba ili kusoma sura yake alikua akifikiria nini.
Kisha nilimwambia Baba “Sijui Baba, sijui nini kimetokea. Nimemkuta Mama katika hali ile” Nililazimika kusema uwongo, Baba alishusha pumzi ndefu. Mtu mzima yeye, alihitaji ushawishi zaidi kuamini nilikua sijui chochote kuhusu Mama.
“Polisi watakuja, tutawajibu hatujui?” aliniuliza. Nilizidi kudondosha chozi.
“Baba, niamini sijui chochote. Nilimkuta akiwa katika hali ile Mimi” nikizidi kujitetea mbele ya Baba. Chozi lilikua likinibubujika huku nafsi yangu ikinisuta. Chochote kitakachomkuta Mama, wa kulaumiwa ni Mimi hapa Celin.
Basi Baba aliniegemeza kwenye bega lake ili kunipa faraja, niliendelea kulia huku tukisubiria taarifa kutoka chumba cha Upasuaji. Tulikaa kwa zaidi ya masaa mawili, jua lilikua likikimbia kwa kasi kuelekea kuzama, jioni ilikua imeshaingia, taa ziliwashwa kuonesha kua giza lilikua linajiandaa kuingia.
Nilikua na uchovu wa kukimbizana huku na kule, mwili ulikua na maumivu pia nilikua na majeraha kadhaa ya kucha za Mama. Baada ya dakika kumi kupita, Daktari mmoja alitoka chumba cha Upasuaji, tulikua tunasubiria kwa muda mrefu, tuliposikia mlango ukifunguliwa tulisimama mara moja na kutazama.
Tulipomwona Daktari tulisogea aliposimama akituangalia, alikua akitokwa na jasho, alivua Barakoa kisha akajishika kiuno. Sura yake ilikosa tumaini, nilijikuta nikilegea mwili mzima. Baba akamuuliza
“Hali ya mgonjwa inaendeleaje?” aliulza Baba kwa shahuku sana, yule Daktari akamtazama Baba, akashusha pumzi kidogo akasema
“Tumejitahidi sana” kisha akatikisa kichwa halafu akaendelea
“Jitihada zimezidi kudra, amefariki” sauti ya yule Dakati siwezi kuisahau, yaani ndani ya wiki moja nilipoteza Watu watatu muhimu sana Maishani mwangu. Nilianza kumpoteza Zena, kisha Caren, leo nampoteza Mama yangu Mzazi tena kwa mikono yangu Mimi mwenyewe, niliangua kilio cha Mtu mzima, nilihitaji nilie kwa uchungu tena kwa sauti kubwa kabisa.
Baba alinishikilia maana nilikua ninalia kwa kusaga meno, kilichoniliza zaidi ni kwamba Mikono yangu ndiyo iliyoondoa Uhai wa Mama yangu, nilimuuwa mwenyewe katika hali ya kujiokoa. Baba alitokwa na machozi huku akiwa ameufunga mdomo wake, aliitumia mikono yake kunibembeleza lakini haikusaidia.
Daktari akamwomesha Baba chumba kitupu ili tukakae huko kwa muda, Baba alinipeleka huko na kufunga mlango ili nilie hadi maumivu yaishe, palikua na viti viwili. Baba aliketi na kuniacha sakafuni nilie hadi nimalize, nililia sana Mimi. Hakuna siku nililia sana kwenye Maisha yangu kama siku hii, maneno ya yule Jini Bibi kizee yalitimia, nilitambaa hadi miguuni kwa Baba nikamwambia
“Nisamehe Baba” nilisema nikiwa ninalia, japo nilikua ninalia lakini niliona maumivu hayawezi kwisha kama sitasema ukweli mbele ya Baba yangu aliyekua hajui nini kilitokea, alikua akinitazama tu.
“Nisamehe Mimi Baba , ni makosa yangu” niliendelea kusema, Baba alishangaa inawezekanaje yakawa ni makosa yangu. Aliniyanyua na kuniuliza
“Inawezekanaje ukasema ni makosa yako Celin?” nilifuta chozi, nilihitaji ujasiri sasa kumweleza ukweli Baba. Nilianza kusema “Kifo cha Mama ni Makosa yangu, mikono yangu niliyoipenda imeondoa uhai wa Mtu ninayempenda” Baba alihamaki akaniuliza kwa sauti kavu
“Unasemaje?”
“Baba, sikukusudia. Nimemuuwa Mama kwa bahati mbaya Mimi, nisamehe Baba Aaaah‼” niliendelea kulia, nilimweleza Baba ukweli lakini hakuonekana kuukubali kabisa. Alinilea na kunifundisha tabia njema, akasema
“Sikukuzaa Muuwaji Celin, sitaki kuyaamini maneno yako” alisema Baba kwa uchungu sana kisha alipiga hatua za haraka na kwenda kujiinamia ukutani. Nilisikia kilio cha chinichini cha Baba na manung’uniko, nilielewa ni vita ya ndani kwa ndani ndiyo iliyokua ikiendelea kwake.
Nilijiuliza nimwambie nini Baba yangu aniamini, nilimfuata alipo, hali ilibadilika na mimi ndiye niliyekua namtuliza Baba baada ya Baba kunituliza Mimi
“Baba‼” nilimwita, alikua amejiinamia. Hakutaka nilione chozi lake kabisa. Nilimwita tena akaniambia
“Celin, wewe siyo Muuwaji Mwanangu tena huwezi kumuuwa Mama yako Mzazi. Sitaki kusikia hizo hadithi, niambie nini kimemkuta Mama yako?” alisema Baba akiwa ameuficha uso wake ukutani, macho yangu yalikua hayakauki chozi hata kidogo, niliendelea kububujisha chozi
“Baba, Mwanao nimepitia Mazingira magumu sana tena kwa siri msijue nyinyi” nilisema, kilio kilianza upya. Baba aligeuka kunitazama. Macho yake yalikua yamejawa na chozi, alihitaji kusikia nilichotaka kukisema. Nilimtazama.
“Chanzo cha yote ni ile nyumba Baba, ina majini na kaburi ambalo ndugu wawili wamezikwa mle. Hakuna aliyeweza kuishi ndani ya ile nyumba salama, hata kifo cha Mama ni matokeo ya usiri wangu” Nilisema jambo ambalo lilimfanya Baba ashangae sana
“Umetoa wapi hayo unayoyasema Celin?” aliniuliza Baba kwa Mshangao mkubwa sana, nilifuta chozi langu nikaivaa roho ya Ujasiri ili nimsimulie Baba kila kitu. Nilimsimulia kila hatua, kila jambo. Hadi namaliza kumweleza Baba alikua ameketi kitini akinitazama kwa uzito sana. Sura ya majonzi ilimtawala Baba yangu
“Kwanini ulificha jambo kubwa namna hiyo Celin, siri yako imeharibu Maisha yetu, siri yako imeondoa uhai wa Mama yako Celin” alinilaumu Baba, nilikua tayari kupokea lawama zote maana tayari maji yalinifika shingoni, nilikua naangamia.
“Unafikiria Polisi wataelewa haya?” aliniuliza Baba, tayari kitengo cha Polisi kilipokea taarifa ya shambulio la Mama yangu. Walikua wameshafika, mlango ulikua ukigongwa
Baba alinisogelea akaniambia
“Kama unaweza kumaliza kila kitu basi maliza Celin” alisema, kabla hata sijamjibu chochote Baba alielekea mlangoni na kufungua mlango, polisi walikua wamesimama mlangoni.
Baba aligeuka na kunitazama kisha alinipa ishara ya tumaini kwa kuniachia tabasamu.
“Sisi ni maafisa wa Polisi, tunahitaji kuondoka na ninyi kwa ajili ya mahojiano” alisema Polisi mmoja, Baba akasema
“Haina haja ya kuondoka na sisi, peke yangu nitathibitisha kila kitu. Binti yangu hakuwepo eneo la tukio” alisema Baba, kauli yake ya ghafla ilionesha kua alikua ameubeba msalaba wangu. Polisi walinitazama kwa sekunde kadhaa huku nikiwa mwoga maana Mimi ndiye Muuwaji, kisha waliondoka na Baba yangu. Nililia sana, sikuwa na Mtu karibu yangu wa kuniambia maneno ya faraja.
Mama yangu alikua amefariki, Baba alikua mikononi mwa Polisi kwa makosa yangu Mimi. Nilijiinamia baada ya kulia kwa muda mrefu, baadaye nilitoka kwenye kile chumba. Nilipata Ujasiri wa kuuliza namna ya kuipata Maiti ya Mama kwa ajili ya Maziko. Utaratibu ulikua ni lazima tulipie pesa kidogo ndipo watupatie maiti, sikua na pesa nilimwambia Daktari natakiwa kurudi nyumbani kuchukua pesa. Akaniangalia kisha akaniambia
“Usijali Msichana, tayari maiti imelipiwa” nilishangaa sana, ni Nani anayeweza kuilipia maiti ya Mama yangu ili itoke Hospitalini. Nilimtazama kwa Mshangao halafu nikamuuliza
“Hivi nimekusikia ipasavyo?”
“Ndiyo, Mjomba wako amelipia” alipomaliza kusema nikamwona Mjomba Mgina akiwa anakuja tulipokua tumesimama na Daktari. Huzuni iliniingia Upya kabisa, nilimkimbilia Mjomba na Kumkumbatia kwa Uchungu sana.
“Pole Celin, pole sana Mjomba” alisema huku akinipiga piga taratibu mgongoni katika hali ya kunipoza machungu. Chozi lilinibubujika tena, kwakua tayari nilikua nimemueleza kila kitu Baba yangu sikutaka kuleta tena Mkanganyiko.
“Inaniuma Mjomba, Mama amekufa kikatili sana” nilisema, maumivu yaliyokua yamejaa moyoni mwangu yalikua yakinichoma mithiri ya sidano.
Basi, tuliitoa Maiti Hospitalini na kuipeleka nyumbani kwa Mjomba Mgina. Palitawala Majonzi na vilio, maswali yasiyo na Majibu. Uvumi kua Baba yangu alikua amemuuwa Mama yangu ulianza kusambaa miongoni mwa waombolezaji, kila Mtu alimwita jina baya Baba yangu.
Nilizidi kuumia ndani ya Nafsi yangu, Baba yangu aliitwa Muuwaji kwa sababu ya kunisaidia Mimi. Alijivesha ngozi yangu kunificha Muuwaji halisi, nililia kwa mambo mengi yasiyo na Majibu. Macho yalinivimba, kesho yake tulimzika Mama kwenye Makaburi ya Jiji.
Hatimaye Mama yangu aliungana na Zena na Caren kwenye makazi ya milele. Kilichokua kimebakia kwangu kilikua fumbo kubwa, hakuna aliyejua kuhusu ile nyumba yenye kaburi na jini anayeuwa.
Sikutaka kumwambia yeyote, moyo wangu ulijawa na kisasi. Sikuuona umuhimu wa kuendelea kuishi ikiwa nimepoteza Wapendwa wangu kwa usiri wangu. Baba alifikishwa Mahakamani siku Nne baada ya kumzika Mama, alikiri mbele ya Mahakama kua alitenda Mauwaji hayo kwa mikono yake kwa kile alichokiita wivu wa Mapenzi.
Nini Kitaendelea? Usikose Sehemu Ya NANE
COMMENTS ZIWE NYINGI SASA
JIUNGE NA KIJIWENI WHATSAPP CHANNEL Kwa Kugusa Hapa
Soma Riwaya Nyingine Za Kijiweni Kwa KUGUSA HAPA
Wewe kama MFANYABIASHARA.. Kuna wakati unatamani kuwafikia watu wengi zaidi na hujui wapi pa kuanzia , USIJALI kwani hapa ndipo ambapo MTAA UNAONGEA na tuko tayari kukusaidia kuwafikia watu wengi kwa BEI YA OFA
Njoo Utangaze Nasi Sasa Kwa Kutuambia Una TANGAZO Gani na unataka kutangaza kwa muda gani kwa kutuma ujumbe hapa WwhatsApp Kupitia Namba +255760871896
Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx
3 Comments
Good https://is.gd/N1ikS2
Awesome https://is.gd/N1ikS2
Good https://is.gd/N1ikS2