Ilipoishia Kimya (Nzena-Kijiji Kilicholaaniwa) – 02
Walibana pumzi zao vizuri, walianza kuisikia sauti ya Mwanamke. Sauti iliyowauliza
“Mko wapi?” ilikua ni ile sauti ya ajabu ya kunong’ona. Ikiambatana na Kicheko Cha chini chini.
“Nawaona” iliendelea sauti hiyo huku Zahoro akiwa amejikausha kimya, ile sauti Ikawa inakuja karibu na walipo kwa juu, Zahoro akampa ishara Anna kua wanapaswa kutengana kwa muda ikiwezekana wakutane pangoni. Mwanga ulizidi kusogea huku Upepo ukiwa unakaribia walipokua wamejificha. Endelea
SEHEMU YA TATU
Haraka Kila mmoja akatoa kitambaa usoni na kuanza kukimbia kwa kutawanyika, Anna akielekea kushoto, Zahoro akielekea Kulia katika Hali ya kuchanganya. Walikua wakiufahamu vyema Msitu huo hivyo walijua ni kitu gani wanapaswa kufanya.
Kicheko kilisikika kwa nguvu sana, baadhi ya ndege wabishi waliosalia Msituni walianza kuruka, sauti hii waliisikia wale Wanaume kwenye ule Mtumbwi pamoja na Moana ambaye alipata hisia ya hatari kwa wazazi wake. Alipaza sauti kwa kilio akiwaita Wazazi wake lakini Mwanaume mmoja alimziba mdomo, walikua wamefika mbali sana. Waligeuka kuutazama ule Msitu waliona ndege wakiruka kwa purukushani, sauti ya Kicheko ilizidi kupaa huku Zahoro na Anna wakiendelea kukimbia kwa Kasi bila kugeuka nyuma
Ule mwanga wenye jicho uliamua kumfuata Zahoro kwa Kasi sana, Anna aliligundua Hilo baada ya kukimbia kwa muda huku akihisi Hali ya usalama, akalazikika kupanda juu ya Mlima eneo ambalo chini yake kuna Pango ambalo walikua wakiishi hapo kwa muda mrefu, eneo Hilo pekee ndilo eneo salama. Aliuwona ule mwanga namna ulivyokua ukisambaa kwa Kasi. Hakujua ni namna gani angeweza kumsaidia Zahoro, aliishi kupiga goti na kuanza kulia.
Alijua fika kua Zahoro asingeliweza kukiepuka kifo safari hii, kingine kilichomliza ni kutekwa kwa Mtoto wao Moana. Hakujua angeweza kumpata wapi
Kwa Upande wa Zahoro aliendelea kukimbia kwa Kasi mithiri ya Ngiri pori, alikua akizifahamu njia za Siri hapo Msituni, alijua apite wapi ili akatokee pangoni lakini mwanga ulizidi kumfukuza kwa Kasi sana.
Alikimbia kwa kujitahidi angali alikua ameshaanza kuchoka, mara akajikwaa kwenye kisiki na kuanguka. Damu ilianza kumvuja eneo la Mguu wa kulia Sehemu ya Ugoko wake, akajivuta taratibu na kuketi nyuma ya jiwe kwa utulivu sana huku akihisi maumivu makali sana. Giza lilikua limeshatanda Msituni kutokana na namna miti ilivyokua imefungamana
Alikua akihema lakini hakuruhusu kuendelea kuhema kwa Kasi, alihitaji kua makini zaidi huku sasa akiitwa Kwa jina lake, alikua akiisikia sauti ya Baba yake ikimwita na kumwambia
“Toa kitambaa Zahoro nataka nikutazame” sauti hii ilikua na nguvu ya kumuumiza moyo wake na kumlazimisha sana. Alijitahidi kuikataa huku akiweka vizuri kitambaa Chake usoni, haikua sauti ya kawaida. Sauti ilisikika mbele ya macho yake, ilikua dhahiri kabisa palikua na kiumbe Cha ajabu mbele yake.
“Aaaah! Aaaaaah!” aligugumia kwa sauti kubwa Zahoro, maumivu ya Mguu yalikua juu sana lakini pia alishajua ilikua ni ngumu kujiokoa hapo.
“Unataka nini?” aliuliza Zahoro, alikua na uhakika palikua na kiumbe mbele yake.
“Nataka Maisha Yako na kizazi chako” ilisema hiyo sauti. Ilikua sauti ya kutisha, nzito sana.
Zahoro alikua akihema kwa hofu na maumivu, aliona hapakua na dalili ya uhai kwa Upande wake.
“Wewe ni Nani?” akauliza Zahoro kwa sauti ya Ujasiri sasa, aliongea kama Mtu aliyekwisha kata tamaa.
“Mimi ni ile laana mliyopewa, sitamwacha hata Mmoja kutoka kwenu. Nitawaangamiza nyote” ilisema hiyo sauti, Zahoro akaangua Kicheko Cha dhihaka na huzuni ndani yake Kisha akamwambia
“Umechelewa, kutoka kwenye kizazi changu huwezi kukimaliza chote. Yupo atakayeishi” kile kiumbe Cha ajabu ambacho Zahoro hakukiona kilianza kupiga yowe za hasira kutokana na Kauli ya Zahoro Kisha kikasena kwa sauti nzito
“Toa kitambaa usoni” alihimiza, kwakua Zahoro alikua tayari ameshakata tamaa hakuona kama alikua na sababu ya kuendelea kuficha macho yake. Alionesha kiburi, aliondoa kitambaa na kuyaacha macho yake yakiwa Bado yamefumba.
“Nitazame” alisema kiumbe huyo, Taratibu Zahoro alifungua macho yake Kisha akamtazama. Alijikuta akiduwaa alipokiona kiumbe Cha ajabu chenye kichwa kikubwa, macho madogo na meno marefu sana. Kilikua kinavuja Ute mwili mzima. Kiumbe hicho kilikua Uchi wa Mnyama.
Kisha kikatoa Kicheko Cha dhihaka kabisa huku akimtazama Zahoro, kilikua ni kiumbe Cha ajabu ambacho kilisisimua mwili wa Zahoro.
Chozi lilimtoka Zahoro Kisha kwa hisia ya maumivu ya moyo na hasira akasema
“Wewe ndiye uliyeuwa familia yangu, umeuwa Kila Mtu hata asiye na makosa. Nakuapia, mwisho wa mwanzo wako umefika na hiyo laana itafutika” alisema Zahoro. Kile kiumbe kiliongeza Kicheko chake, kilicheka kwa sauti ya Juu zaidi na zaidi. Sauti ambayo ilisambaa Kila mahali.
Kisha ghafla akabakia kimya, akasema “Hakuna atakayeweza kuifuata laana kwasababu imeandikwa kwenye ardhi hii Hadi pale Kila Mtu atakapokua amekufa”
“Unataka kuiona Siri ya Kifo?” aliuliza. Zahoro akamtazama Kisha akamwambia
“Hata wewe umelaaniwa” Kile kiumbe kikapata hasira Kisha kikamkaba shingoni Zahoro na kumwambia
“Laana haiwezi kulaaniwa, Kila aitamkaye anaunda kiumbe kama Mimi lakini wewe huwezi kwasababu Mimi ni laana iliyotamkwa” Kisha akamwachilia Zahoro akiwa anakohoa kwa kukosa hewa.
Ghafla wote walisikia sauti ya Ngoma ikiwa inapigwa kutokea mbali kidogo, sauti hiyo iliwafanya wote wawe kimya kuisikiliza. Siyo Ngoma pekee Bali palikua na sauti ikiwa inaimba. Kile kiumbe kikapata hasira sababu hakipendi kelele, kikageuka kumtazama Zahoro, alimwona ni Mtu dhahifu aliyeumia hivyo angeweza kumrudia na Kummaliza.
Aliondoka hapo mithiri ya Upepo huku mwanga mwekundu ukitangulia mbele yake. Ghafla lile Giza la asili likarejea, Zahoro aligundua Ngoma hiyo ilikua ikipigwa na Anna, ilikua ni Moja ya mbinu zao za kukabiliana na kiumbe hicho kwa Miaka Mingi.
Kilichobakia kwa Zahoro kilikua ni kujivuta na kuelekea pangoni mahali ambako palikua pa Siri na Usalama kwake. Alijaribu kujivuta kwa nguvu Hadi aliposinama kwa kujishikiza kwenye miti, Kisha alianza kujiburuza taratibu huku ile sauti ya Ngoma ikiendelea kurindima.
Maumivu makali ya Mguu yalimfanya Zahoro atembee taratibu sana, aliendelea kujiburuza hivyo hivyo huku akiugulia maumivu, Damu ilikua ikichuruzika Kila alipopiga hatua zake.
**
Upande wa Pili, Anna aliendelea kupiga Ngoma huku akiimba, alijua nini Maana ya anachokifanya na alikua na uhakika kua kiumbe kingemfuata yeye. Hakuogopa Bali aliuvaa Ujasiri, alikua hajafunika macho yake. Alikua akipiga na kuimba huku akiangalia chini.
Alianza kuhisi Upepo wa ajabu, alijua sasa kile kiumbe kilikua kimeshafika alipo. Alikua juu ya jiwe Moja kubwa eneo la Wazi kabisa. Alipojua kua Kiumbe kilikua mbele yake aliacha kuimba na kupiga Ngoma.
Alisimama na kukabiliana kwa macho makavu na kile kiumbe. Kile kiumbe kilijitokeza kwa umbo lake la asili ambalo Zahoro aliliona. Ilikua tofauti kwa Anna, hakuogopa wala hakushangaa isipokua alitabasamu tu.
Kile kiumbe kilikasirika sana baada ya kumwona Anna, Kisha kikamuuliza “Ni wewe?” aliuliza kwa sauti ya kumfahamu Anna. Kisha Anna akamjibu
“Nataka kwenda Duniani, kuishi kama wao, kuwa kama wao na kulipa Kisasi Cha kifo Cha Wazazi wangu” alisema Anna. Mara kile kiumbe kikabadilika ghafla na kua Binadamu wa kike mzuri sana, Anayefanana na Anna kwa Kila kitu kasoro mavazi Yao. Anna alivalia mavazi ya kuchakaa wakati huo yule Mwingine alivalia nguo ghali zaidi za kifalme.
“Anna, huwezi kwenda Duniani. Wewe ni mali ya Kuzimu, hapa Ndiyo kwako. Wewe si Binadamu Bali ni kiumbe Cha ajabu tu kama Mimi. Sikiliza Anna, kilichotokea kwa Wazazi wetu kimetokea Miaka Mingi, hakuna kitu tutafanya tena” alisema Kisha Anna akamsogelea na kumwambia
“Alice, sitakubali kamwe Hadi nihakikishe namsambaratisha yule Mwanasayansi aliyeuwa Wazazi wetu.”
“Na huyu unayemlinda?”
“Yeye ni njia ya Mimi kufika Duniani, anayajua mafumbo yote ya Wapi ilipo njia ya kutoka kuzimu. Ni suala la muda tu” alisema Anna.
“Una hakika? Nilijua umeshakufa Anna” alisema Alice Kisha alimkumbatia Anna huku chozi likimbubujika, wao ni mapacha kwa kuzaliwa. Ni Watoto wa mfalme wa zamani wa Mji mmoja uliopotelea Kuzimu uitwao Patiosa.
Wazazi wao waliuawa na Mwana Sayansi ambaye yeye na Mwenzake walifanikiwa kuingia Kuzimu na Kuwauwa Wazazi wao Kisha kuondoka na kitu muhimu na kurejea nacho Dunia halisi. Tangu hapo Familia Yao ilipoteza nguvu Kisha utawala ukachukuliwa kimabavu na Mfalme mwingine ambaye anaitawala Patiosa Kisha aliwafukuza Anna na Alice, ukawa Ndiyo mwanzo wa kutengana kwao.
Katika makuzi ya Alice alijikuta anapata nguvu za ajabu zilizomwezesha kuishi Kuzimu kama Fumbo la Laana nyingi zilizotamkwa Duniani. Hubeba laana na kuzifanyia kazi ili aendelee kua na nguvu za kuishi Kuzimu huku akiwa anawindwa sana na Mfalme wa Patiosa aitwaye Mfalme Selasi.
“Sikufa ile siku nilipoanguka kutoka Mlimani, niliishi kama Mwindaji. Niliishi na hasira, nilisaidia wengi waliopotelea Kuzimu huku nikiwa na Imani siku Moja nitapata njia ya kufika Duniani na kulipa Kisasi kwa kifo Cha Wazazi wetu. Nimejikuta nimenasa hapa kwa Miaka Miaka mingi bila kuzeeka wala kufa kama ulivyo wewe, niliitafuta nafasi ya kukutana na huyo Mtu. Mtu mwenyewe ni Zahoro”
“Niligundua uwepo wako muda mrefu sana Alice lakini nilikuacha ufanye kazi Yako, wakati mwingine nilipambana nawe kuokoa Watu wasio na hatia ambao wamepotelea huku. Unajua nini, Wengi wamepotelea huku kwasababu ya laana, wengi hawana hatia. Ni lazima tutafute njia ya kuwarejesha Duniani.” Alisema Anna, maneno ya Anna yalimtoa machozi Alice.
Kisha walitazamana. Alice akamwambia Anna.
“Bila kufanya hii kazi nitapoteza nguvu zangu Anna. Japo najutia kwasababu nimemwaga Damu za Watu wengi bila kujali. Nilihitaji kua na nguvu nyingi zaidi ili siku Moja nirejeshe kiti Cha Enzi Cha Ufalme wa Patiosa” Anna akamshika mkono Alice akamwambia
“Najua, Nina Uhakika pia kua Binti yangu wa pekee ameelekea Patiosa pamoja na Wanaume wawili. Nahitaji kumwokoa, lakini najua ni ngumu sana kwetu kuingia Patiosa kutokana na mhuri wa Kichawi tuliopigwa wakati tunafukuzwa.” Alisema Anna, Alice alishangaa sana akamwuliza
“Una Mtoto?”
“Ndiyo, ni Mtoto wetu pamoja na Zahoro.”
“Hongera Anna.” Alisema Alice huku chozi likiendelea kumbubujika Kisha akamkumbatia tena Anna. Kisha akamuuliza
“Una mpango gani sasa?”
“Kumwambia Ukweli Zahoro kua Adui Kimya ni wewe, kilicho mbele ni kumpata Binti yetu Moana Kisha kutafuta njia ya kuelekea Duniani. Baada ya Kisasi sitawalazimiaha Zahoro na Moana kuishi Kuzimu. Watachagua wapi wanataka kuishi” Alisema Anna, Alice alifuta chozi lake Kisha akamwambia Anna
“Kama ni hivyo basi tunaweza kua kitu kimoja lakini sitakusaidia kuelekea Duniani ikiwa Kuna njia, Mimi nitaitawala Patiosa Milele kuenzi Wazazi wetu. Kwasasa nitaungana nawe kurejea Patiosa kwa ajili ya kumpata Mtoto na kupambana Mfalme Selasi. Wote wakatabasamu
JIUNGE NA KIJIWENI WHATSAPP CHANNEL Kwa Kugusa Hapa
Soma Riwaya Nyingine Za Kijiweni Kwa KUGUSA HAPA
Wewe kama MFANYABIASHARA.. Kuna wakati unatamani kuwafikia watu wengi zaidi na hujui wapi pa kuanzia , USIJALI kwani hapa ndipo ambapo MTAA UNAONGEA na tuko tayari kukusaidia kuwafikia watu wengi kwa BEI YA OFA
Njoo Utangaze Nasi Sasa Kwa Kutuambia Una TANGAZO Gani na unataka kutangaza kwa muda gani kwa kutuma ujumbe hapa WwhatsApp Kupitia Namba +255760871896
Nzena xx Nzena xx Nzena xx Nzena xx Nzena xx Nzena xx Nzena xx Nzena xx Nzena xx Nzena xx Nzena xx