Ilipoishia Return of Faudhia sehemu ya sita

“Kama lilivyo tamu penzi lako, basi nahitaji uniambie wapi  ilipo chemba ya siri iliyohifadhi pesa za Kimarekani” Alisema  Chogo akiwa anavaa nguo zake, alipomaliza alikuwa bado  hajapata jibu kutoka kwa Selina ambaye alikuwa akitetemeka  kwa woga 

“Ukimya wako unaashiria kuwa ni bora ufe kuliko kusema ilipo  Chemba si ndiyo?” Aliuliza tena Chogo, safari hii  alibadilisha sura yake na kujaza hasira

“Tafadhali usiniuwe, ipo chumba namba 43” Alisema Selina  . Endelea

SEHEMU YA SITA

“Hebu twende huko” Alisema Chogo kisha aliongozana na Selina,  waliingia ndani ya Lift kisha safari ilianza kuelekea juu ya  Ghorofa hilo la Benki, walipofika huko Selina alimuonesha  ilipo chemba, ilikuwa imefichwa nyuma ya Kioo kikubwa ambacho  kwa Mtu mwingine ni ngumu kujuwa kuwa eneo hilo kulikuwa  kumehifadhiwa Mabilioni ya Dola za Kimarekani ambazo  zilitokana na mauzo ya Siri ya Madini ambayo Rais na Waziri  Mkuu walifanya Biashara hiyo kisiri 

“Fungua” Alisema Chogo, Selina alibonyeza mahali kisha kioo  kilijivuta pembeni, kulikuwa na mlango wa Umeme eneo hilo,  palitakiwa kuingizwa namba za siri, Selina aliingiza namba za  siri na Mlango huo ulifunguka, Chogo hakuamini macho yake,  kwa mara ya kwanza katika Maisha yake alishuhudia kiasi  kikubwa cha pesa, chumba kilijaa pesa nyingi za kimarekani 

“Woww!!” Alisema Chogo akionesha kufurahi sana, alimfuata  Selina na kumpiga busu kama ishara ya furaha baada ya  kukutana na kiasi hicho ambacho ndicho kilichowafanya waiteke  Benki hiyo na baadhi ya Miji na kambi za Jeshi. 

“Nakuwa Bilionea muda siyo mrefu Selina, ilikuwa ni ndoto ya  Maisha yangu kuja kuwa Bilionea mkubwa Afrika” Alisema Chogo  huku akiruka kwa furaha kisha aliendelea kusema 

“Hatimaye Baba yangu atalala kwa amani baada ya kuhakikisha  nasomba kiasi hiki cha pesa” Aliposema hivi Selina alipata  shahuku ya Kumuuliza Chogo 

“Baba yako atalala kwa amani? Anahusiana vipi na pesa hizi?”  Alihoji huku akiwa anautazama mgongo wa Chogo, alipogeuka  alimpa jibu Selina 

“Miaka mingi nikiwa na umri wa miaka 10, Baba yangu alikuwa  akifanya kazi kwenye mgodi wa Melerani, alipokuwa akichimba  alikutana na Jiwe kubwa sana la dini, alienda kuwaambia  viongozi wa mgodi huo ambao walielekea pamoja chini  kuliangalia, walipothibitisha kuwa Jiwe hilo lilikuwa ni dini  lenye thamani kubwa sana walimuuwa Baba yangu kisha walitoa  taarifa kuwa amefukiwa na kifusi, niliishi maisha magumu  sana. Nilimuaga Mama kuwa naenda Mjini , bahati mbaya  nilipata ajali ya gari, kitu pekee kilichonisaidia nilirushwa  dirishani na kutumbukia kwenye maporomoko, wengine wote  walikufa kwenye ajali hiyo, aliyenisaidia alikuwa ni rafiki  wa Baba yangu ambaye alinieleza kila kilichotokea, Mama yangu  pia alikufa kwa presha baada ya kusikia kuwa nimepata ajali.  Sikuwa na sababu ya kurudi Arusha, yule rafiki wa Baba aliniambia napaswa kulipa kisasi kwa kila kilichomfika Baba  yangu” 

“Alinisafirisha na kunipeleka Colombia, niliishi huko na  kufundishwa biashara ya uuzaji wa madawa ya kulevya, jinsi ya  kutumia silaha na mapigano, baadaye nilirudi Tanzania na  kutengeneza kundi la ESS, lengo ni kusomba pesa zote  zilizotokana na Mauzo ya Madini ambazo Rais na Waziri Mkuu  waliifanya Biashara kwa siri sana, wewe ukiwa unalifahamu  hilo Selina.” aliposema hivi Selina aliinamia Chini, Chogo  alikuwa akiongea kwa Uchungu sana lakini kwa namna  alivyoelezea ilionesha wazi kuwa Chogo alidanganywa na Mzee  Shomari ili Mzee Shomari afanikishe lengo fulani, kupitia  ugaidi huo tayari alishasomba madini kwenye migodi mingi Na  kilichokuwa kimebakia ni hicho kiasi kikubwa cha pesa ambacho  endapo kitachukuliwa basi alipanga kuwauwa Diana na Chogo  kisha atimke zake Uholanzi kwa rafiki yake. 

“Pole sana, lakini kufanya hivi huoni kama unahatarisha  Maisha yako zaidi?” Aliuliza Selina 

“Maisha yangu yalishakuwa kwenye hatari baada ya Baba yangu  kufariki huko Mgodini, nilifanya kazi za hatari pale Arusha  nikiwa bado shule, nani alijali?” Alisema Chogo kisha alikaa  juu ya pesa 

“Unahisi unaweza ukatoka hapa ukiwa salama?” Aliuliza Selina 

“Baada ya Masaa 24 nitatoka hapa nikiwa na kiasi hiki cha  pesa” Alisema Chogo. 

Ndani ya Makao makuu ya Kitengo cha Usalama wa Taifa huko  Kigamboni, Mzee Shayo alikuwa ameketi akisubiria simu ya  Faudhia, hakuwa na taarifa yoyote iliyomhusu Faudhia maana  mara ya mwisho walipeana majukumu ya kufanya kwa kila mmoja  wakati Faudhia akirudi Arusha Mzee Shayo akienda gereza la  Segerea huko Tabata. 

Wakati Mzee Shayo anamtafakari Faudhia, huyo Faudhia alikuwa  akihangaika namna ya kulifungua Brifkesi lile, kila namba  waliyoingiza haikufungua Brifkesi hilo, Faudhia alimtaka yule  Mdada kusimamisha gari, kisha alishuka na kutafuta jiwe  kubwa, alipasua ile Brifkesi, ndani yake kulikuwa na karatasi  zilizoandikwa ” MPANGO ESS” 

Haraka Faudhia alichukua kila kitu na kurudi ndani ya gari,  alimwambia yule Mdada kuwa aendeshe mwendo wa kasi huku yeye  akisoma karatasi hizo ambazo zilionesha kuwa mpango wote wa  Ugaidi ulisukwa humo ndiyo maana ulienda kufukiwa ndani ya shimo walilodai kuwa ni kaburi la Martin Gimbo, hivyo basi  mpango wa kundi la ESS ulipangwa muda mrefu hata kabla Ya  hiyo ajali ya kutengenezwa ya Martin Gimbo. 

Karatasi hizo zilikuwa na siri nzito za mipango yote ya Mzee  Shomari Nchini Tanzania, kwanza karatasi hizo zilisema ni  wapi Mzee Shomari ataweka kambi yaani kule kwenye jengo la  China Plaza, pili jinsi madini yatakavyokuwa yanaibwa na  kupelekwa Nje ya Nchi, tatu jinsi watavyokiondoa kiasi  kikubwa cha pesa ndani ya Benki kuu, Nne jinsi alivyowatumia  askari jeshi kupandikiza mabomu katika kambi zote Tanzania  kisha akawa na rimoti ya kuongoza mabomu hayo ndiyo maana  jeshi hawakuweza kutoka na kwenda kuzuia Ugaidi kwa hofu ya  kambi zao kulipuliwa, Tano jinsi alivyo tengeneza ajali ya  Basi na kumpata Chogo kisha kumjaza chuki na maneno ya  kupandikiza ili aichukie Nchi yake, lengo likiwa kumsadia  yeye Mzee Shomari kufanya Ugaidi na kuiba alivyokusudia  Tanzania. 

Karatasi hiyo ilikuwa na michoro ya namna walivyotengeneza  njia ya Chini kwa chini kutokea Msikiti wa Maamur Upanga hadi  Benki Kuu, hivyo wangeitumia njia hiyo kuondoka na pesa bila  askari kujuwa kuwa walikuwa wameshatimka, Faudhia aliendelea  kusoma na kuujuwa mpango wa Mzee Shomari kuanzia A hadi Z,  ghafla gari yao iligongwa kwa nyuma na gari moja aina ya  Toyota Mkonga nje 

Alipochungulia alimuona Diana akiwa ndani ya gari hilo 

“Shit!!” Alisema Faudhia akiwa tayari ameshafahamu kila kitu,  Diana alijitahdi kutaka kuwasiliana na Mzee Shomari na  kumwambia kuwa mpango wao unaweza kwenda songombingo sababu  Faudhia ameshajuwa kila kitu lakini mawasiliano yalikuwa  yamekata, alichotaka kufanya Diana ni kumzuia kwanza Faudhia  asifanye chochote hata kulisogelea Jiji la Dar-es-salaam  sababu yalibakia masaa chini ya 24 ili wamalize kazi yao. 

Yule Mdada aliendesha kwa woga sana huku akijitahidi kukwepa  risasi ambazo Diana alikuwa anazimimina kwa lengo la  kuwazuia, Mdada alijikuta akigonga Mti baada ya kuondolewa  barabarani na Diana, Ukimya ulitawala sana kwenye gari ya  akina Faudhia 

Diana alishuka kwenye gari akiwa na Bastola yake, alisogea  kwa tahadhari sana kuelekea lilipo gari la akina Faudhia huku  akijuwa fika kuwa haitokuwa rahisi kumnasa Faudhia kutokana  na mafunzo aliyonayo. Alipofika alimkuta Yule Mdada pekee,  hakumuona Faudhia

“Fauhdia yupo wapi?” Alihoji Diana, yule Mdada alionekana  kujawa na woga, ilibidi aoneshe mahali ambapo Faudhia  alikuwepo, Naam! Alikuwa nyuma ya Mti mkubwa ulio jirani na  eneo walilopata Ajali. Baada ya kuona ameshajulikana alipo,  haraka Faudhia aliuwahi mkono wa Diana ambao ulikuwa  umeshikilia Bastola, wakawa wananyang’anyana Bastola mkononi  mwa Diana, hatimaye iliangukia pembeni. 

“Diana hupaswi kufanya hivi, ningekuwa nataka kukuuwa  ningekuuwa tokea kule tulipokuacha, ila nilikuacha ili  utafakari maneno yangu!! Mzee Shomari ndiye aliyemuuwa Mama  yako siyo Mimi” Alisema Faudhia akiwa anamtazama Diana kwa  jicho lililojaa umakini sana 

“Ni bora ungeniuwa pale pale Faudhia ila kuniacha hai ni kosa  kubwa sana, unafikiri nitapotea kwa maneno yako? Lazima  nilipe kisasi cha kifo cha Mama yangu” Alisema Diana kisha  alikaa mkao wake kwa ajili ya kupambana na Faudhia. 

Kama kawaida yake alijirusha sambasoti na kutua karibu zaidi  na Faudhia, aliona pigo la ngumi lililotumwa na Faudhia,  alikwepa kisha aliinuka na teke la mkunjo na kumpiga Faudhia  begani, kisha alijifytua na kumkata ngwara Faudhia ambaye  alinguka chini hata hivyo haraka alijiokota. Faudhia aliona  ni bora apambane na rafiki yake huyo ili kuliokoa Taifa. 

Alivuta taswira fupi ya mafunzo aliyoyapata Mexico kisha  alimtazama Diana ambaye alionekana dhahiri kuwa alijawa na  hasira sana, alifanya kama anamfuata hivi kisha alijifyetua  na kutua pembeni akajikuta anautazama mgongo wa Diana,  alimsindikiza na teka kali ambalo lilimsomba Diana hadi  kwenye mti, alichukia sana Diana aliokota gongo la mti kisha  alilitumia kama silaha kupambana na Faudhia ambaye alikuwa  tayari amedhamiria kama kufa yeye au kufa Diana maana  alijaribu sana kumueleza ukweli wa kilichotokea hadi Mama  yake akafa. 

Faudhia alirusha ngumi mfululizo bila kupumzika, Diana  alijitahidi kuzizuia lakini hakufanikiwa kuzuia zote  alijikuta akiruhusu ngumi kadhaa kwenye kifua chake, pale  pale alikohoa damu. Faudhia hakuhitaji maongezi tena bali  alichotaka ni kuhakikisha anatembea ndani ya muda ili awahi  kuzuia mpango wa Mzee Shomari. Diana kila alipojaribu  kumsogelea Faudhia alikunbana na kadhia ya mapigo matakatifu  yaliyozidi kumfanya ateme damu, Faudhia hakuwa na huruma tena  na rafiki yake alijirusha na kutua mbele ya Diana kisha  akafanya kama anataka kukimbia alafu akajikunja na kumvaa  Diana eneo la shingo kisha akampa kabali ya miguu shingoni.

Hali ilianza kuwa ngumu kwa Diana alijikuta akianza kukosa  hewa, alipiga miguu ya Faudhia akiomba aachwe lakini tayari  mzimu wa kazi ulikuwa umempanda sana Faudhia, alihakikisha  anambana hadi alipokatisha uhai wa Diana, alipohakikisha kuwa  Diana ameshakufa alimuacha kisha alimwambia yule Mdada kuwa  wanapaswa kuondoka haraka sana, walirudi nyuma wakachukua  gari ya Diana kisha waliingia Barabarani kwa ajili ya  kuelekea Dar-es-salaam. 

Mdada alikuwa akiendesha gari kwa hofu huku akijikuta akiwa  na maswali mengi ya kumuuliza Faudhia, alianza kumuuliza 

“Wewe ni nani na kwanini unafuatiliwa?” Faudhia alimtazama  yule Mdada kisha alimwambia 

“Naitwa Faudhia, mimi ni undercover wa kitengo cha Usalama wa  Taifa” Alijibu Faudhia kisha alionekana kusahau jambo 

“Wewe unaitwa Nani?” Aliuliza Faudhia 

“Naitwa Matilda” 

“Ooh!! Sawa Matilda nashukuru kukufahamu pia nashukuru kwa  msaada wako, kama si wewe ningelikuwa nimeshakufa” Alisema  Faudhia, Matilda aliuliza tena. 

“Na yule ni nani? Inaonekana mlikuwa mnafahamiana, kwani  ulimuuwa Mama yake?” Alihoji tena Huyo Mdada  

aliyejitambulisha kama Matilda 

“Hapana!! Sikumuuwa Mama yake, yule anaitwa Diana ni rafiki  niliyesoma naye huko Mbeya, sijui hata alijiingiza vipi  kwenye ugaidi” Alisema Faudhia kisha alirudisha macho yake  mbele, safari yao ilizidi kusonga mbele 

  • ••••••••••••••••• 

Ndani ya Jengo la China plaza, Mzee Shomari alikuwa bize  kumtafuta Diana kwa njia ya simu lakini simu ya Diana  haikupokelewa, alimtafuta kwa zaidi ya masaa mawili jambo  ambalo lilianza kumpa wasiwasi, alipoona simu zake  hazipokelewi alimpigia Chogo ndani ya Benki kuu kisha  akamwambia 

“Diana hapatikani kwa zaidi ya masaa mawili, maliza mchakato  haraka iwezekanavyo” Alipomaliza kumpa maelekezo Chogo,  alipiga simu Arusha kwa Mtu mwingine wa kazi kisha alimuagiza  kuelekea kwenye kaburi kuangalia kama mzigo utakuwa  umechukuliwa

Chogo alipopata maelekezo ya kuendelea na mchakato aliita  vijana wake kisha aliwaambia 

“Weka pesa zote ndani ya mabegi” Aliposema hivi vijana wake  haraka walifungua mfuko mmoja mkubwa sana ambao ulikuwa na  mabegi mengi kisha zoezi la kuweka pesa lilianza mara moja. 

Zilikuwa ni pesa nyingi mno, walishindilia kwenye mabegi hayo  ambayo yalikuwa makubwa na meusi, tayali gari lilikuwa  limeshaandaliwa ndani ya Msikiti wa Maamur kwa ajili ya  kubeba pesa hizo ambazo watapita nazo chini kwa chini kutokea  Posta hadi Upanga. 

Kule Ikulu, Rais alikuwa katika hali ya wasiwasi mno endapo  chemba ya siri ingefahamika kupitia kwa mdada ambaye  anajulikana kama Selina, lakini tayari Selina alikuwa  ameshaonesha ilipo chemba ya siri na tayari pesa zilishaanza  kuchotwa huko, yeye na Waziri Mkuu walionekana kuficha kuhusu  biashara hiyo ya madini ambayo waliifanya kwa siri sana ili  baadaye pesa hizo zihamishwe kwa siri kwenda Marekani. 

“Naomba niongee na Shayo haraka” Alisema Rais, mara moja  Waziri Mkuu alipiga simu kwa mkuu wa kitengo cha Usalama wa  Taifa ambaye hadi kufikia wakati huo hakujuwa Faudhia alikuwa  wapi, ni mzima au amekufa ila Faudhia alikuwa barabarani  kuelekea Dar kwa ajili ya kuzuia mpango wa Mzee Shomari. 

Mara moja simu ya Mzee Shayo ilipokelewa na maongezi kati ya  Mzee Shayo na Rais yalianza, Rais alisikika kwa kupoa sana  tofauti na mwanzo ambapo alionesha hasira sana kwa Mzee Shayo 

“Shayo!!” Aliita Rais 

“Naam Mkuu” Aliitika Mzee Shayo 

Nini Kitaendelea USIKOSE SEHEMU YA NANE

JIUNGE NA KIJIWENI WHATSAPP CHANNEL Kwa Kugusa Hapa 

Soma Riwaya Nyingine Za Kijiweni Kwa KUGUSA HAPA

Wewe kama MFANYABIASHARA.. Kuna wakati unatamani kuwafikia watu wengi zaidi na hujui wapi pa kuanzia , USIJALI kwani hapa ndipo ambapo MTAA UNAONGEA na tuko tayari kukusaidia kuwafikia watu wengi kwa BEI YA OFA

Njoo Utangaze Nasi Sasa Kwa Kutuambia Una TANGAZO Gani na unataka kutangaza kwa muda gani kwa kutuma ujumbe hapa WwhatsApp Kupitia Namba +255760871896 

16 Comments

  1. Admin kwan unatumia mfumo gan kutumia na mdaga maana cjajua kila ck kila baada ya mda gan na mda gan unatuma uwe na utalatibu ili tujue maana husomek story ni nzul ila utoaji wako haupo sawa nilipenda jinsi ulivyo kuwa unatoa simuliz ya mama niachie mume wangu nikajua itakayo kuja utaweka mfumo mzuli zaid lakin apa ume long kuliko iliyo pita

Leave A Reply

Exit mobile version